Ujue mfumo unaotumiwa na meli kusafirisha biashara haramu kwa bendera ya Tanzania

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Rashid Abdallah
- Nafasi, BBC Swahili
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Si mara ya kwanza kwa meli zenye bendera ya Tanzania kukamatwa katika matukio mbalimbali ya uhalifu. Ikiwemo usafirishaji wa madawa ya kulevya, hadi usafirishaji wa vilipuzi.
Tanzania imesema meli iliyokamatwa nchini El Salvador wiki hii ikiwa na shehena ya dawa za kulevya huku ikipeperusha bendera ya nchi hiyo, ilisajiliwa visiwani Zanzibar.
Msemaji wa serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa amesema serikali ya Zanzibar imechukua hatua kadhaa ikiwemo kufuta usajili wa meli. Meli hiyo ya FMS Eagle ilikamatwa na maafisa wa kupambana na dawa za kulevya ikiwa na mzigo wa tani 6.6 wa dawa hizo haramu.
Swali ambalo mtu anaweza kujiuliza. Ni kwa vipi bendera ya nchi, mfano Tanzania, inaweza kutumika na meli ili kusafirisha tani ya mzigo wa biashara haramu?
Sheria zinasemaje?

Chanzo cha picha, AFP
Tuanze na sheria kwanza: Katika muktadha wa sheria ya kimataifa inataka kila meli ya biashara isajiliwe katika nchi. Nchi ambayo meli imesajiliwa huipa meli haki ya kupeperusha bendera yake ya kiraia. Meli inafanya kazi chini ya sheria za nchi iliyosajiliwa, na sheria hizi hutumika ikiwa meli inahusika katika kesi za baharini.
Nchi ambayo meli imesajiliwa ndio husimamia sheria za udhibiti juu ya meli hiyo na kuikagua meli mara kwa mara, kuthibitisha vifaa na wafanyakazi wa meli, na kutoa hati za usalama na kuzuia uchafuzi wa mazingira.
Usajili wa meli uko wa aina mbili; usajili uliofungwa (closed registry) na usajili wa wazi (open registry). Usajili uliofungwa kwa kawaida huhitaji mmiliki wa meli au wafanya kazi kuwa ni wakaazi au raia wa nchi wanayo sajili. Na usajili wa wazi ni ule ambao wageni huruhusiwa kusajili umiliki wa meli zao katika nchi wasizo na uraia nazo.
Nchini Tanzania kuna taasisi mbili zinazoshughulikia usajili wa meli. Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC), na Mamlaka ya Usafiri wa Baharini ya Zanzibar (ZMA). TASAC ambalo linasimamia masuala ya baharini Tanzania bara, linaendesha shughuli zake kwa mfumo wa usajili uliofungwa tangu 2018 – hutoa usajili kwa raia wa Tanzania, wakazi, au mashirika yaliyosajiliwa nchini Tanzania.
Kwa upande wa ZMA, hutumia usajili wazi pia, ambao unaruhusu raia wa kigeni na makampuni ya kigeni kusajili meli chini ya bendera ya Tanzania.
Tatizo liko wapi?

Chanzo cha picha, DAILY NEWS
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa sehemu kubwa, tatizo liko katika mfumo huu mfumo wa usajili wa wazi, ambao pia huitwa Flags of convenience {FoC). Wasafirishaji wa madawa ya kulevya katika bahari, mara nyingi hutumia meli zilizosajiliwa katika mfumo huu.
Ni utaratibu wa baharini wa kusajili meli katika nchi nyingine isiyokuwa ile ambayo mmiliki wa meli anatokea. Kwa wasiokuwa na nia njema, hutumia utaratibu huu kuepuka kanuni kali za usajili wa meli katika nchi zao, kulipa kodi za chini, kutumia vibaya usimamizi mdogo wa meli katika nchi wanazo sajili, na pia huutumia mfumo huu ili kujificha.
Ripoti zinaeleza kuwa, kufikia mwaka 2024, Panama, Liberia, na Visiwa vya Marshall ndizo nchi tatu zinazoongoza katika kusajili asilimia kubwa ya meli za kimataifa kupitia mfumo huu.
Mfumo huu wa usajili wa wazi, ulianza miaka ya 1920 huko Marekani wakati wamiliki wa meli walipotaka kuwapa abiria wao pombe wakati kukiwa na katazo.
Ili kufanikisha azma yao wamiliki hao wakafanya usajili wa meli zao huko Panama. Walipoona kuna faida katika kukwepa kanuni za nchi zao, waliendelea kusajili meli zao huko Panama hata baada ya marufuku ya pombe kuondolewa.
Ni muhimu kuelewa kuwa usajili wa meli wa namna hii sio usajili haramu. Licha ya kuwepo kwa ukosoaji lakini ni usajili unaokubalika kisheria.
Wanaounga mkono mfumo huu, husema kuna faida za kiuchumi za kuongezeka kwa uhuru katika kuchagua wapi mtu anataka meli yake isajiliwe kwa ajili ya biashara za kimataifa. Na wamiliki wa meli kutoka nchi zinazoendelea hutumia mfumo huu ili kuingia katika ushindani wa kibiashara katika mazingira ya kimataifa.
Moja ya sababu ya Zanzibar kubaki na mfumo huu wa usajili, ni kwa lengo la kuongeza ajira kwa vijana ambao huajiriwa katika meli hizi zinazomilikiwa na raia wa nchi nyingine lakini kwa usajili wa Zanzibar.
Wanaopinga mfumo huui, likiwemo Shirikisho la Wafanyakazi wa Uchukuzi wa Kimataifa (ITF) na mashirika mengine yanafanya kampeni dhidi ya mfumo huu kwa sababu mara nyingi haufuati viwango vya kimataifa na huzingatia faida bila kujali usalama wa wafanyakazi na mazingira.
Si mara ya kwanza

Chanzo cha picha, SMZ
Mwaka 2018, Alieyekua rais wa Tanzania John Magufuli alisimamisha usajili wa wazi wa meli baada ya matukio ya kukamatwa kwa meli tano zinazopeperusha bendera Tanzania zikiwa zimebeba bidhaa haramu, na kutaka mfumo mzima wa ujasili kuangaliwa upya.
Mapema Januari 2018 serikali ya Ugiriki ilikamata meli yenye bendera ya Tanzania karibu na kisiwa cha Crete ikiwa njiani kuelekea Libya huku ikiwa imebeba vilipuzi. Libya ilikuwa chini ya vikwazo vya silaha ilivyowekewa na Umoja wa Mataifa kutoka mwaka 2011.
Wiki chache kabla ya hapo, meli nyingine yenye bendera ya Tanzania ilikamatwa katika bahari ya Atlantic ikiwa imebeba tani 1.6 za madawa ya kulevya.
Akizungumza na BBC, Hamza Hassan Juma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa pili wa rais Zanzibar, amesema, “hakukuwa na raia wa Tanzania katika meli iliyokamatwa El Salvador, wala sio meli ya Tanzania, na haimilikiwi na Tanzania na Tanzania haihusiki na biashara na madawa ya kulevya.”
Wakati Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ikisikitika na kulaani kilichotokea, kwa bendera ya Tanzania chini ya usajili wa Zanzibar kutumika vibaya, swali linabaki: Je, lipi litafanyika kuzuia matukio ya namna hii yanayojirudia rudia?
na je mfumo wa usajili wa meli za nje (Open) wa kujitegemea kwa upande wa Zanzibar unapaswa kuangaliwa upya?















