‘Dawa za kulevya zilinisababishia kukojoa damu na kuleta shida kwenye ubongo’

Na Dinah Gahamanyi

BBC News Swahili

TH
Maelezo ya video, Arsene Ndikumana: Mraibu wa madawa ya kulevya

Ndikumana ni mmoja wa vijana wengi nchini Burundi wanaokabiliwa na uraibu wa dawa za kulevya, wengi wao wakiishi katika maeneo ya madangulo ya taka na mitaani baada ya kuzikimbia familia zao.

Unapotembea katika baadhi ya mitaa ya mji mkuu wa Burundi unaweza kuwaona baadhi ya vijana wenye uraibu wa dawa za kulevya, wakirandaranda mitaani, na baadhi wakisogelea magari kuomba pesa.

Licha ya kwamba hakuna takwimu rasmi kuhusu idadi ya vijana wanaotumia mihadarati nchi Burundi, mashirika ya kupambana na dawa za kulevya yanasema matumizi ya mihadarati hasa miongoni mwa vijana nchini Burundi yanaendelea kuongezeka.

w
Maelezo ya picha, Mashirika ya kupambana na matumizi ya dawa za kurevya nchini Burundi yanasema kuwa idadi ya vijana wanaotumia mihadarati inaongezeka hasa maeneo ya mijini

Mojawapo ya mashirika hayo ni Association Burundaise pour un Monde de paix san drogue (ABMPD), ambalo kupitia kituo chake kilichopo jijini Bujumbura, limekuwa likiwafuata mitaani ya vijana wanaotumia mihadarati, na kuwaelimisha kuhusu umuhimu wa kuachana na mihadarati , kuwapatia ushauri wa nasaha na wa kisaikolojia na kutoa matibabu kwa wale wanaoyahitaji.

Shirika hili ambalo lilianzishwa mwaka 2021, huwapokea vijana wenye uraibu wa mihadarati walau 11 hadi 15 kwa siku na imeweza kuwaokoa vijana 40, 18 kati yao wakiwa ni wa kike. Baadhi ya wanawake wanaoweza kufika kwenye kituo hiki , huwa wamebakwa kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.

Unapotembelea kituo cha ABMPD unawapata vijana wa rika tofauti kuanzia umri wenye umri wa miaka 15 na 25 hivi, wanaotumia mihadarati, walio katika mchakato wa kuiacha, pamoja na wale ambao wameweza kuacha kabisa matumizi ya dawa za kulevya, na kuwahamasisha wenzao kuacha kuzitumia.

‘’Mimi kusema kweli bado ninatumia mihadarati ya aina nyingi, lakini Cocaine ndio ninayotumia zaidi, maana nikiibugia inaniliwaza sana…sipati msongo wowote wa mawazo, ninatulia’’, anasema , Ntamavugiro Pascar - mraibu mwingine wa dawa za kulevya, ambaye anasema ana matumaini ya kuacha kutumia dawa hizo.

‘’Nimepunguza kutumia kiasi, niko katika juhudi za kuacha, lakini kusema kweli bado natumia… tatizo ni kwamba nisipotumia mwili unaniuma, nahisi baridi kali na ninatetemeka , ninakosa amani kabisa, inanifanya nitumie tena.’’ aliongeza.

w
Maelezo ya picha, Arsene Ndikumana, mraibu wa mihadarati ambaye ameazimia kuachana nayo, anasema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni maumivu makali ya mwili, na baridi kali wanapoacha kutumia.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kama Ntamavugiro Pascar, Arsene Ndikumana pia amekuwa akitumia bangi na Cocaine, lakini pia yeye hutumia Heroine inayofahamika zaidi miongoni mwa watumiaji kama Booster , pamoja na kile wanachoita Cocktail - mchanganyiko wa bangi, tumbaku, heroinę na tumbaku ‘kali ya wazee’,

‘’Dawa za kulevya zilinisababishia kukojoa damu, nilikuwa situlii, nazunguka huku na kule kuzitafuta, nikokosa inakuwa shida’’, Arsene Ndikumana aliiambia BBC.

Niliambatana na marafiki wabaya. ‘’Wanatuingiza katika mambo mabaya sana’’, anasema Ndikumana, ambaye sasa anakiri kuwa yalikuwa makosa kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya na kwa sasa yuko katika mchakato wa kutafuta usaidizi ili aache uraibu huo.

‘’Wajumbe wa shirika hili, walitupata kwenye majaa ya taka wakija kutuambia ubaya wa dawa za kulevya, mara ya kwanza tukawapiga mawe, lakini baadaye tukawasikiliza, na kilichotuvutia ni kwamba baadhi yao walikuwa wakitumia dawa za kulevya kama sisi na kuacha, kwa hiyo tuliona ni wenzetu', alisema Emery Ngarambe, ambaye aliacha kutumia mihadarati na sasa ni mtoa ushauri nasaha kwa wenzake ambao bado wanatumia dawa hizo.

g
Maelezo ya picha, Emery Ngarambe, kijana aliayeacha kutumia mihadarati na sasa ni mtoa ushauri nasaha kwa vijana wenzake ambao bado wanatumia, akiwahamasisha kuachana na mihadarati.

Jambo moja ambalo vijana hawa wanakubaliano nalo wote ni kwamba unapotumia dawa za kulevya kila mtumiaji hutumia mbinu ziwezekanazo, hata ziwe hatari ili kuipata pesa za kununulia dawa hizo. Wengi wao huiba mali na pesa hasa za familia na jamaa zao na kuziuza ili kupata pesa za mihadarati.

‘’Kusema kweli ukiwa mtumiaji wa mihadarati huwezi kukubali kukosa kuitumia, utatumia njia zote uipate …hauwezi kutulia kwasababu, kabla haujatumia, unahisi maumivu makali ya mwili na kibaridi ambacho kitakusumbua’’, anasema Emery.

‘’Mimi nyumbani nilikuwa ninawalaghai mara kwa mara wazazi wangu, ndugu, marafiki na jamaa na hata watu wengine wananipa pesa- kwa mfano niliwadanganya wazazi wangu wanipe pesa nikawanunulie shamba, hilo halikuwa kweli, niliichukua pesa yote nikapotea nayo tukagawana na wenzangu, tukanunua mihadarati na kuitumia’’.

Ulaghai na wizi wa mali na pesa ni mambo ambayo wengi wa vijana hawa wakikiri kuyafanya kama chanzo cha pesa za kununuliaa madawa ya kulevya.

‘’Mimi nilishirikiana na vijana watumiaji wenzangu wa mihadarati, kuvusha mali za wazazi wangu, ikiwa ni pamoja na televisheni, viti na masufuria…ili tupate pesa za kununulia mihadarati, watumiaji huwa tunakuwa na urafiki mkubwa’’, aliniambia Nsabimana Methode ambaye alikuwa mtumiaji wa madawa ya kulevya, lakini sasa ameacha kwa mwaka wa nne sasa.

‘Ushauri kwa mfano’

Bi Emmeliene Harushamagara alikuwa mtumiaji sugu wa mihadarati nchini Kenya ambako alikuwa amekwenda kusoma - lakini kwa sasa ni afisa anayehusika na mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa vijana wa Burundi katika taasisi ya MBMPD:

‘’Binafsi mimi nilitumia mihadarati kwa muda mrefu, nilipokwenda kusoma Kenya, kwasababu ya kuwa na upweke wa kuwa mbali na wazazi na familia yangu , pamoja matatizo mengine mbali mbali nilijipata katika matumizi ya dawa za kulevya. Nilitumia karibu aina zote za dawa za kulevya, nililala nje, na baadaye nikakatiza masomo na kuwa kondakta [makanga] wa mabasi ya abiria ili kupata pesa za kukidhi kiu ya mihadarati. Katika kipindi hiki chote nilikuwa pia mwizi wa mabavu hasa nikiwaibia wanawake na wanaume ambao niliona ningeweza kuwaibia’’ anasema, Bi Harushamagara.

Anasema kutokana na matumizi ya mihadarati, alifungwa mara kwa mara katika magereza mbali mbali nchini Kenya na kuachiliwa na baadaye alikata shauri na kuamua kurudi nyumbani kwao Burundi baada ya maisha kuwa magumu.

h
Maelezo ya picha, Emelliene Harushamagara afisa wa shirika la kupambana na matumizi ya dawa za kulevya, MBMPD, ambaye pia alikuwa mraibu wa dawa za kulevya anasema uzoefu wake umemsaidia kuwasaidia vijana waraibu wa mihadarati

Lakini kabla ya kurudi Burundi alipata usaidizi katika kituo kimoja cha kuwasaidia watumiaji wa dawa za kulevya ambapo alipewa Medhodine - dawa inayosaidia kupunguza maumivu kwa watumiaji wa mihadarati na baada ya miezi sita ya kupokea ushauri nasaha na matibabu, alirejea Burundi.

Alipofika Burundi alipobaini kuwa kuna tatizo kubwa la matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa vijana ndipo alipojiunga na taasisi ya Shirika la ABMPD, ili kuwasaidia vijana kuacha kutumia mihadarati.

Ari ya kutaka kuacha kutumia dawa za kulevya

Watumiaji wa dawa za kulevya wanasema sio rahisi kuachana na matumizi yake. Lakini Emery Ngarambe ana mtazamo tofauti kuhusu hilo.

‘’Uamuzi na utashi wa mtu binafsi ni muhimu sana iwapo mtu anataka kuachana na matumizi ya dawa za kulevya. Kwa mfano mimi nilihisi kuwa ninataka kuachana na mihadarati, lakini sikujua niache vipi, lakini tulipofundishwa athari zake na maafisa wa kupambana na dawa za kulevya, tuliamua kuachana nayo’’ alisema Emery.

‘Aliongeza kuwa: ‘Ukiwa na utashi wa kibinafsi na kujiambia kwamba nataka kuachana na dawa za kulevya , uchukua uamuzi na upate usaidizi kama tuliopata hapa inawezekana kabisa kuachana na mihadarati…sisemi utaacha siku moja, ni mchakato wa taratibu, kwa mfano kama ulikuwa unatumia misokoto mitatu ya bangi, utaanza kutumia miwili, kisha mmoja na baadaye utaacha kabisa.’’

‘Wazazi wenye watoto wanaotumia mihadarati wasiwalaani’

Emery anawasihi wazazi watambue kwamba mtu anayetumia dawa za kulevya sio mwendawazimu bali ni mgonjwa.

‘’Wazazi wenye watoto wanaotumia mihadarati msiwalaani!,kwani kwa mtu kufikia hatua ya kutumia dawa za kulevya, huwa inatokana na sababu mbali mbali,inaweza kuwa ni kutokana na wewe mzazi hasa mnapokuwa na matatizo ya kifamilia’’alisisitiza Emery.

Anaisihi jamii pia kuacha kuwatesa watumiaji wa mihadarati: ‘’Ukimuona mtu yeyote anayetumia mihadarati usimpige na kumvunja, sio suluhu, kama ni mzazi ongea naye ujue ni kitu gani kilimfanya ajiingize katika mihadarati na kuitumia…pole pole utajua ni hatua gani unaweza kuchukua ili kumsaidia kuacha kutumia dawa za kulevya’’, alishauri Emery .

‘’Mtumiaji ana nguvu na anaweza kubadilika, la muhimu tumjali, tuwe naye karibu na tuwapeleka katika mashirika yanayoweza kuwasaidia kuachana na matumizi ya dawa za kulevya’’ anaongeza.

Emery na wenzake waliiambia BBC kuwa, baada ya kupokelewa na kituo cha kupambana na matumizi ya dawa za kulevya, na kupewa ushauri nasaha, na hata baadhi kupokelewa na familia zao, wana matumaini kuwa siku za usoni wataweza kuwa watu wa maana katika maisha yao , familia na jamii yao.