Jinsi mabaharia wanavyosema walidanganywa na kusafirisha Cocaine na Muingereza

gh

Chanzo cha picha, Daniel Guerra

Muda wa kusoma: Dakika 7

Kwa Mbrazili Daniel Guerra aliyetamani kuwa baharia ili kusafiri ulimwenguni, tangazo la kazi lilikuwa ni kutimia kwa ndoto yake.

Mmiliki wa boti la kifahari wa Uingereza alikuwa akitafuta watu wawili wa kumsaidia kusafiri kutoka Brazili kupitia Bahari ya Atlantiki, mojawapo ya safari kuu za baharini.

Hakutakuwa na mshahara, lakini gharama zote zililipwa - na, muhimu zaidi, Bw Guerra angepata uzoefu wa baharini aliouhitaji ili afuzu kama nahodha wa baharini.

"Ndoto yangu ilikuwa kuwa nahodha na kwenda kufanya kazi Ulaya," anakumbuka kijana huyo mwenye umri wa miaka 43, ambaye aliona tangazo hilo kutoka kwa wakala wa ajira za mabaharia mtandaoni.

"Kwa hivyo nilifurahi sana, nikijua ndoto yangu ilikuwa inaanza."

Mambo yalionekana kuwa mazuri zaidi wakati Bw Guerra na muajiriwa mwenzake, Rodrigo Dantas, 32, walipokutana na mwajiri wao mpya Muingereza.

Walikuwa na hofu kwamba anaweza kuwa mmiliki mwenye majivuno au mwenye maringo, ambaye angehakikisha kuwa wanajua yeye ndiye bosi.

Lakini haikuwa hivyo, George Saul alikuwa mtu mwenye tabasamu, alionekana kuwa rafiki , ambaye hakuweka masharti ya kufuata utaratibu. Mabaharia, alisema, wanaweza hata kumuita kwa jina lake la utani - "Fox".

"Nilikuwa nikifanya kazi kwenye baadhi ya boti nyingine na wamiliki wazee, wakorofi sana na walinidharau," anaongeza Bw Dantas. Lakini yeye "alikuwa mzuri, na rafiki sana."

Unaweza pia kusoma:
f

Chanzo cha picha, Daniel Guerra

Maelezo ya picha, George Saul (katikati) aliwaomba mabaharia - Daniel Guerra (kushoto) na Rodrigo Dantas (kulia) - wamuite kwa jina lake la utani "Fox" na walivutiwa na urafiki wake.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Fox hata alikubalika kwa wazazi wa Bw Dantas, ambao walikuwa na wasiwasi kuhusu mtoto wao kufanya safari ndefu kwenye boti la kifahari linalomilikiwa na mtu wasiyemfahamu kabisa, na wakaomba wakutane naye.

Walifahamu kwamba Fox alikuwa ameleta boti lake la kifahari linalofahamika kama Rich Harvest nchini Brazili kwa ajili ya ukarabati, na walitaka wafanyakazi wenye uwezo wa kuirejesha Ulaya kwa niaba yake.

Pamoja na mabaharia Bw Dantas na Bw Guerra, kungekuwa na watu wengine wawili, akiwemo nahodha aliyehitimu.

"Nilisema: 'Angalia, muangalie mwanangu'," anakumbuka baba yake Bw Dantas, João. "Alisema: 'Usijali, nitamtunza Rodrigo.'

Ilionekana kwamba si wazazi wake pekee waliotaka kujua kama kila kitu kiko sawa ndani ya boti la Rich Harvest.

Kabla ya kuondoka nchini Brazil, polisi wa eneo hilo walitumia takriban saa sita kupekua boti kutafuta dawa, kwa usaidizi wa mbwa wa kunusa.

Hawakupata walichokuwa wakitafuta, hata hivyo, na mabaharia walidhani ulikuwa ukaguzi wa kawaida tu.

Walikuwa wamesikia hadithi kuhusu cocaine kupandwa kwenye boti, na sasa angalau walijua dawa hiyo haimo.

"Unaposafiri kupitia uwanja wa ndege... begi yako hupitia uchunguzi wa mashine ya X-ray," asema Bw Dantas. "Kwa hivyo nilifahamu vizuri ni safari ya kimataifa na wanakuja kuikagua boti."

b

Chanzo cha picha, Brazil police

Maelezo ya picha, The Rich Harvest ilisakwa na polisi kwa saa sita kabla ya kuondoka Brazil

Wasiwasi kama huo ulikuwa mbali na mawazo yao hadi hatimaye walipoanza safari yao kuu mnamo tarehe 4 Agosti 2017, wakiiacha pwani ya Brazil taratibu nyuma yao.

Pamoja nao walikuwemo na wahudumu wa ziada, Daniel Dantas (hakuna uhusiano wowote na Rodrigo Dantas) na nahodha mpya aliyeajiriwa wa boti, Mfaransa Olivier Thomas, 56, badala ya nahodha wa awali wa Uingereza ambaye ujuzi wake wa meli haukuwa umethibitishwa.

Mmiliki ‘‘Fox’’, wakati huo huo, alikuwa amerejea Ulaya kwa ndege siku mbili zilizopita.

"Ilikuwa siku nzuri, hali ya hewa nzuri, jua," anakumbuka Bw Guerra, ambaye alichapisha ujumbe wa shukrani kwa Fox kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Ulisomeka: "Ninashukuru sana, Fox, kwa hili... nafasi ya kujifunza na kwa uhusiano wetu ambao umenifanya kuwa na nguvu zaidi. Asante mwenzangu."

Baada ya majuma mawili ya kusafiri kwa meli, boti hiyo ilipata matatizo ya injini, na kuilazimu kusimama katika Cape Verde, visiwani vilivyopo karibu na pwani ya Afrika Magharibi.

Kwa mara nyingine tena, Bw Guerra na Bw Dantas walipata sababu za kujione eneo zuri. Visiwa hivyo ni paradiso ya watalii, na Fox alisema angewatumia pesa ili wafurahie wakati matengenezo yakifanywa kwenye ndani ya boti.

Na polisi zaidi walipokuja kupekua meli, Bw Guerra hakuwa na wasiwasi.

"Hawakupata chochote huko Brazil," aliwaza. "Hawatapata chochote huko Cape Verde pia."

Polisi wa Cape Verde walikuwa waangalifu zaidi kuliko wenzao wa Brazil, wakitumia vifaa maalum vya kukata ili kufungua sehemu za ndani za boti.

Chini ya sakafu ya bandia iliyojificha, walipata karibu tani 1.2 za cocaine- yenye thamani ya takriban £100m ($134m) iwapo itauzwa katika mitaa ya Ulaya.

"Nilihisi kwamba uhuru wangu wote umetoweka," alisema Bw Guerra. "Nilikuwa na hasira, sikuweza kukubali kilichokuwa kikitendeka, unafahamu? Nilijiona kupumbazwa sana.”

Mnamo mwezi Machi 2018, wafanyakazi hao walifunguliwa mashtaka huko Cape Verde, wakipinga kutokuwa na hatia.

Walisistiza kuwa hawakuwahi kusikia kuhusu boti ya Rich Harvest au mmiliki wake hadi walipoona tangazo la kazi, walisisitiza.

Walihukumiwa, hata hivyo, kifungo cha miaka 10 jela kila mmoja - katika kile kilichotajwa kama moja ya ugunduzi ukamataji mkubwa wa Cocaine.

Lakini licha ya kufurahishwa na kukamatwa kwa dawa hizo , mwanamume ambaye polisi wa Brazili walimtaja kama mshukiwa mkuu alitoroka.

Waliamini kuwa mpangaji mkuu wa operesheni hiyo alikuwa Fox, mmiliki wa boti ambaye kwa mara ya kwanza taarifa zake walizipata kutoka Shirika la kitaifa la uhalifu la Uingereza (NCA).

Polisi wa Brazil wanaamini kuwa alikuwa kiongozi wa operesheni ya kusafirisha dawa hizo.

g

Chanzo cha picha, Cape Verde police

Maelezo ya picha, Hizi ni baadhi tu ya pakiti za kokeini zilizokamatwa na maafisa huko Cape Verde zilizogunduliwa zikiwa zimefichwa chini ya sakafu ya bandia ya Rich Harvest na kwenye matanki bandia ya maji

Mnamo Agosti 2018, Fox alikamatwa nchini Italia, ambapo polisi wa Brazil walifungua kesi ya kumrudisha nyumbani. Walitaka arejeshwe Brazil kujibu tuhuma zinazomkabili.

Lakini nyaraka za mashtaka zilichelewa kufika, na akaachiliwa – jambo lililomsikitisha Inspekta wa polisi wa Brazil Andre Gonçalves.

Alihofia kwamba baadaye Fox alijificha.

"Tulibaki na hisia kwamba baada ya kazi yetu yote, hatutaweza kufikia mwisho wake," aliiambia BBC. "Ilikuwa inasikitisha sana."

Bwana Gonçalves alisema timu yake imeweka Fox na boti chini ya uangalizi nchini Brazil. Wanaamini kwamba "ukarabati" kwenye boti hiyo kwa kiasi fulani ulilenga kutengeneza sehemu za siri ndani yake, na kwamba dawa hizo zilipakiwa kwenye chombo hicho kabla ya mabaharia kuajiriwa.

Bw Gonçalves anakiri kwamba mwanzoni, alidhani mabaharia hao wanne walihusika pia.

“Mtu anapokuwa kwenye boti iliyojaa dawa za kulevya, unafikiria mtu huyo lazima awe na uhusiano nayo,” alisema.

Lakini alipochunguza asili zao, hakuweza kupata chochote kilichowaunganisha hapo awali na ulimwengu wa dawa za kulevya au Fox.

"Kadiri nilivyoenda ndani zaidi bado sikuweza kupata uhusiano ... lakini wakati huo huo uchunguzi uliimarisha ushahidi tuliokuwa nao dhidi ya Fox."

Maombi ya mabaharia hao ya kutokuwa na hatia pia yalipata kuungwa mkono na chanzo kisichotarajiwa - Muingereza mwenzake Robert Delbos, mwanamume ambaye alidaiwa kuwa mshirika wa Fox.

.

Chanzo cha picha, Police

Maelezo ya picha, ''Badala ya kuwalipa wafanyakazi ipasavyo na kujipatia mtaalamu wa kusafirisha watu kwa umwagaji damu - aliajiri watu wanne wasio na hatia." Robert Delbos, ambaye alifanya kazi katika hatua ya kwanza ya ukarabati wa mashua ya Fox

Delbos, 71, ni mlanguzi wa dawa za kulevya aliyepatikana na hatia, akiwa amefungwa jela miaka 12 mwaka 1988 kwa kujaribu kusafirisha tani 1.5 za bangi nchini Uingereza.

Kabla ya Rich Harvest kuondoka Brazil, timu ya Bw Gonçalves ilioilimuona Delbos ikisimamia hatua za kwanza za ukarabati wa boti.

Hapo awali walishuku kuwa alikuwa aakiweka vyumba vya siri, na walimfungulia kesi zilizofaulu za kumrejesha wakati huo huo kama zile zilizofunguliwa dhidi ya Fox.

Delbos alikaa kwa miezi kadhaa katika gereza la supermax la Brazil akisubiri kesi, lakini pia alisema dawa hizo ziliwekwa ndani ya boti baadaye bila yeye kujua.

Aliachiliwa baada ya hakimu katika kesi yake kuamua kuwa hawakuweza kuthibitisha kuwa anajua kuhusu mpango huo wa magendo.

Katika mahojiano na BBC, alidai kuwa hata walanguzi wa dawa za kulevya walikuwa na kanuni za maadili, na Fox alizivunja kwa kutumia mabaharia wasio na hatia badala ya kuajiri wafanyabiashara wa magendo.

"Hili ni kosa kabisa. Namaanisha, hufanyi hivi," alisema.

"Alikuwa mtu mjinga ambaye alikuwa mchoyo. Badala ya kuwalipa wafanyakazi ipasavyo na kuwapata walanguzi sugu - aliawajiri watu wanne wasio na hatia."

Mashaka kuhusu hatia ya mabaharia yalipoongezeka, familia zao zilianza kampeni kwa niaba yao.

Mnamo 2019, hukumu yao huko Cape Verde ilibatilishwa, na wakaruhusiwa kurudi nyumbani.

Fox, wakati huo huo, hajawahi kukabiliwa na kesi, na akarudi Uingereza.

f

Chanzo cha picha, Getty Images/BBC

Maelezo ya picha, Picha ya selfie ya George Saul, AKA Fox, ilitumwa kwenye Instagram yake

Bw Dantas anasema alihangaika kutafuta kazi ya meli aliporejea nyumbani, huku baadhi ya waajiri wakidhania kuwa lazima alikuwa na hatia.

Shauku ya Bw Guerra ya kusafiri kwa meli duniani kote "iliishia Cape Verde".

Anasema alipoteza uwezo wake wa kumuamini watu, muhimu wakati wa changamoto katika safari yoyote ndefu ya boti ya kifahari.

Hata sasa, bado anajiuliza Fox alikuwa nani hasa - yule jamaa "mzuri" wa Uingereza ambaye aliwahi kumshukuru sana, ambaye tangazo la kazi liligeuza maisha yake juu chini.

Anasema kwamba "angependa sana kuona haki ikitendeka", lakini hana hamu ya kukutana na Fox tena.

"Nikikutana naye sio mimi nitaongea, itakuwa Daniel mwingine. Hisia mbaya zote nilizokuwa nazo gerezani zitakuja na sitaweza kuwa mtu mstaarabu."

Wizara ya sheria ya Brazili ilisema haikuzungumzia kesi za mtu binafsi.

Wakati huo huo, Rodrigo Dantas na Daniel Guerra wanajaribu kujenga upya maisha yao nchini Brazil, ndoto zao za kuwa manahodha wa mashua zimetelekezwa.

Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi