Jinsi ghasia za magenge zilivyoteka ‘Paradiso’ ya utalii

f
Maelezo ya picha, Paul amekuwa katika genge tangu alipokuwa na umri wa miaka 15 karibu nusu ya maisha yake

Na Ana María Roura, Daniel Wittenbeg & Blanca Moncada,

BBC News Mundo, Guayaquil

"Mambo ni hatari hivi sasa. Kifo kinaweza kutoka popote," Paul anatuambia. Paul ambaye ni mwanaume mwembamba, mwenye umbo dogo mwenye umri wa miaka takriban 30 ni mwanachana wa genge la uhalifu lenye vurugu zaidi nchini Ecuador

Anaamini amekuwa kwenye orodha ya kundi hasimu ya watu wanaotakiwa kuuawa kwa mwaka mmoja na nusu na sababu pekee ya yeye kuwa bado kuwa hai ni kutokana na maombi ya mama yake: "Ni kama Mungu hanitaki huko juu , na shetani hatanipeleka chini kaburini."

Paul (sio jina lake halisi) anaeleza kwamba ameishi karibu nusu ya maisha yake katika genge katika jiji kubwa zaidi la Equador, Guayaquil.

Kama watu wengine wengi, alijiunga akiwa kijana , alipokuwa na umri wa miaka 15. Alifikiri angeishi maisha ya "sherehe na kupata wasichana ".

Paul anaogopa kwamba ikiwa atendelea kuwa katika genge hilo kwa muda mrefu, maadui zake kutoka kwa magenge hasimu - ambayo yanaendesha vita vya umwagaji damu – watamuua.

Kwa hivyo tunaendelea kuzunguka jiji ili kufanya iwe vigumu kwa mtu yeyote kutufuata.

"Nilitaka heshima," anasema kuhusu sababu zake za kujiunga na moja ya magenge hadi 20 ambayo yamechangia ghasia ambazo zimebadilisha sura ya Ecuador.

Hadi hivi majuzi nchi ya Ecuador ambayo inafahamika kwa kuwa moja ya nchi salama zaidi katika eneo hilo, ikiwa pia ni lango la Visiwa vya Galapagos na eneo lenye msitu mkubwa na ilikuwa kivutio cha watalii wengi.

Lakini sasa ina kiwango cha juu zaidi cha mauaji kilichorekodiwa katika Amerika ya Kusini.

Mnamo 2023, polisi walirekodi takriban vifo 8,000 vilivyotokana na ghasia. Kiwango hiki ni mara nane zaidi ya kile cha mwaka wa 2018 na kinaiweka Ecuador juu ya nchi kama Mexico na Colombia.

g
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mnamo mwezi Januari, Ecuador iligonga vichwa vya habari kote ulimwenguni wakati kituo cha Televisheni kilipotekwa na watu waliojifunika nyuso waliojihami wakati wa matangazo ya moja kwa moja .

Wakati huohuo, magenge yalitekeleza utekaji nyara na kuanzisha mashambulio ya milipuko katika miji mingi, na wafungwa walifanya ghasia katika magereza.

Rais Daniel Noboa, ambaye alikuwa ameapishwa miezi miwili tu iliyotangulia alitangaza hali ya hatari. Tangu wakati huo, polisi wamewakamata zaidi ya watu 16,000.

Hali ya hatari ilimalizika siku ya Jumatatu, lakini rais alidumisha hali ya "mgogoro wa ndani unaohusisha silaja", huku jeshi likiwa na mamlaka ya kipekee.

Anataka kuanzisha hatua zaidi kama vile udhibiti mkali wa bunduki na hukumu kali za kifungo cha gerezani. Hatua hizo zitapigiwa kura katika kura ya maoni tarehe 21 Aprili.

Hakuna shaka kwamba maisha ya watu wengi wa Ecuador yamebadilika kutokana na kuongezeka kwa ghasia za magenge.

w
Maelezo ya picha, Polisi wenye silaha wakiwa katika shughuli ya ulinzi wakati wa operesheni ya usalama huko Guayaquil

Dk Gabriela Almeida anasema anaona "wagonjwa wengi walio na matatizo ya wasiwasi, na watu wanaosumbuliwa na mashambulizi ya hofu".

Dk Almeida mwenyewe anaepuka kutoka nje wakati wa usiku. "Kulikuwa na utekaji nyara karibu na hapa," anaelezea.

"Nilipokuwa kijana mdogo, nakumbuka niliona kile kilichokuwa kikiendelea nchini Colombia," anasema kuhusu uhalifu unaohusiana na dawa za kulevya katika nchi hiyo jirani.

"Hatukuwahi kufikiria jambo kama hilo linaweza kutokea katika nchi yetu," anasema, na kuongeza kuwa anafikiria kuhamia Uhispania kwa sababu Ecuador "tunaishi katika jinamizi".

Guayaquil,ngome ya dawa za kulevya Equador

Mengi ya masaibu hayo yamechochewa na kukua kwa biashara ya dawa za kulevya.

Uzalishaji na utumiaji wa kokeini kote ulimwenguni umefikia viwango vya rekodi ya juu , kulingana na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa za Kulevya na Uhalifu.

Kati ya mwaka wa 2020 na 2021 pekee, uzalishaji wa kokeini uliongezeka kwa karibu theluthi moja na magenge ya mihadarati yalianza a kutafuta njia mpya za kusafirisha kokeini inayozalishwa katika nchi za Colombia na Peru.

Ecuador, ambayo iko kati ya Peru na Colombia na ambayo uongozi wake hauna ujuzi wa kutosha kupambana na ulanguzi wa dawa za kulevya ilionekana kuwa sehemu mwafaka

f

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Polisi wanaonyesha dawa za kulevya, silaha na simu zilizokamatwa huko Guayaquil mnamo Machi 2024

Matokeo yake, Ecuador imebadilishwa kuwa kitovu cha usambazaji wa kimataifa, ambapo dawa huhifadhiwa, kutayarishwa kwa usafirishaji - mara nyingi hufichwa ndani ya makontena ya usafirishaji - na kutumwa hadi mahali inapotakikana.

Magenge kama yale ambayo Paul ni mwanachama yana jukumu kubwa katika mchakato huu mzima .

Paul anatuambia kwamba aliacha kushughulikana kiasi kidogo cha dawa za kulevya kulevya na kuingia katika usafirishaji wa kilogramu nyingi za kokeini.

Anasema jukumu lake jipya lilikuwa kuficha dawa haramu miongoni mwa bidhaa zingine ndani ya makontena ya usafirishaji.

Asilimia tisini ya dawa haramu zinazoondoka Ecuador zimefichwa ndani ya makontena ya usafirishaji yanayoondoka kwenye bandari ya Guayaquil, kulingana na walinzi wa pwani wa Ecuador.

Walinzi wa pwani wameongeza uchunguzi na ufuatiliaji lakini wanasema hatari kwa wafanyikazi wake imeongezeka pia.

"Hapo zamani, tulikuwa tukishughulika na wahalifu wa kawaida. Sasa, mtu yeyote tunayemwona anaweza kuwa na silaha za hali ya juu," mmoja wa makamanda wa walinzi wa pwani anatuambia, tunapoungana na timu yake kwenye boti inayoshika doria bandarini na maeneo jirani.

b
Maelezo ya picha, Walinzi wa pwani wanasema ufisadi umefanya kazi yake kuwa ngumu zaidi

Hataki tufichue jina lake kwa kuhofia kulengwa na magenge na amevaa barakoa ya kijivu kuficha uso wake.

Timu yake yenye silaha hufanya doria hadi mara nne kwa siku, kutafuta wanachama wa genge wanaotumia boti ndogo kujaribu kuficha dawa kwenye makontena yaliyowekwa kwenye meli kubwa.

Kamanda huyo anasema wamekuwa wakiathiriwa na ufisadi siku za nyuma na Paul anathibitisha kuwa genge hilo lilikuwa likimlipa mtu aliyekuwa bandarini kuzima kamera za ulinzi nyakati muhimu ili wanachama wa magenge hayo wafanye shughuli zao haramu bila kutambuliwa.

g
Maelezo ya picha, Walinzi wa pwani hufanya doria za mara kwa mara kuzunguka bandari na maeneo ya jirani

'Kila mtu anataka eneo…'

Kwa Paul, ulanguzi zaidi wa dawa za kulevya unamaanisha "fedha zaidi, silaha bora". Lakini pia ulizua vita vya umwagaji damu kati ya magenge hasimu.

"Kila mtu anataka eneo. Eneo la kuuza dawa za kulevya, eneo la biashara haramu - hata kwa kunyang'anya pesa kutoka kwa watu na kuwateka nyara," Paul anaelezea.

Tunapomuuliza kwa nini anakataa kuondoka kwenye genge hilo, anadai hajahusika sana tangu aende mafichoni, lakini wanachama wa magenge wanaomtafuta 'wapo kila mahali'

Anatuambia anadumisha uhusiano na genge lake ili wampige jeki ikihitajika na silaha zaidi za kujilinda.

Angeweza kujisalimisha kwa mamlaka, lakini anadai kwamba "njia pekee ya kuacha genge itakuwa kuondoka nchini" kwani magenge yanafanya kazi magerezani.

Baada ya kumbana zaidi kwa maswali kuhusu uhusiani wake na magenge anakiri bila kusita kuwa ameua watu lakini anasema anajuta kuharibu familia.

"Ninajuta kwa kuchukua maisha ya watu. Natatizika kulala kwa sababu nimeumiza watu wengi."

Kupigania haki, kuteseka kwa sababu ya dhuluma

Tulipoiuliza serikali kuhusu masuala haya , tuliambiwa "imepunguza kwa kiasi kikubwa" idadi ya vifo vinavyotokana na ghasia , "imemaliza nguvu za magenge yaliyopangwa" magerezani, kuchunguza kesi za rushwa, na ikasema inashinda vita dhidi ya " mafia".

Lakini watu waliopewa jukumu la kuwafikisha mbele ya sheria wanachama wa magenge wamekuwa walengwa.

Waendesha mashtaka sita wameuawa katika kipindi cha miaka miwili.

Mmoja wao alikuwa César Suárez, ambaye alikuwa akiongoza uchunguzi wa shambulio la kituo cha televisheni na pia katika visa kadhaa vya ufisadi. Aliuawa kwa kupigwa risasi mjini Guayaquil mnamo Januari .

f
Maelezo ya picha, Mwendesha mashtaka wa umma Michelle Luna anataka ulinzi bora kwa watu wanaojaribu kuwafikisha wahalifu mbele ya sheria

Mwendesha mashtaka mwenzake wa umma Michelle Luna anamkumbuka kama "mtu mchangamfu sana" ambaye alipenda kazi yake.

Yeye na wenzake wanahofia kwamba mtu yeyote anayejaribu kukabiliana na magengeya uhalifu ya ghasia ya Ecuador sasa analengwa na uhalifu uliopangwa na anadai hatua za ziada za usalama zinahitajika .

Anataka utambulisho wa waendesha mashtaka usifichuliwe na kesi za mahakamani zinazofanyika mbali ziletwe karibu ili kuepuka hatari ya kusafiri hadi katika chumba kimoja cha mahakama ambapo washukiwa wanashtakiwa.

Ingawa yeye binafsi hajapokea vitisho , Luna ana wasiwasi kwamba hilo litafanyika muda sio mrefu na pia atashambuliwa na anafikiria kubadilisha kazi.

"Ikiwa hatutapata hakikisho zaidi kuhusu usalama wetu, itabidi nijiuzulu," anasema. "Mawakili hawajasoma na kufanya mazoezi kwa miaka mingi kufanya kazi ambayo ni kama ya kujiua."

Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Yusuf Jumah