Kwanini mwanasayansi huyu wa Pakistani anahusishwa na mpango wa nyuklia wa Iran?

Dr. Abdul Qadeer Khan

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 6

Mnamo Februari 4, 2004, tukio ambalo Wapakistani waliona kwenye skrini zao za televisheni lilikuwa la mlipuko, na mwangwi wake ulisikika kote ulimwenguni, ikiwemo Pakistani.

Hadithi ilikuwa kwamba Dk Abdul Qadeer Khan, mhusika mkuu katika programu ya nyuklia ya Pakistan, alikiri kwenye televisheni ya serikali kwamba aliuza siri za nyuklia kwa nchi zingine kinyume cha sheria na bila ya serikali ya Pakistani kujua.

"Uchunguzi umethibitisha kwamba shughuli nyingi zilizoripotiwa zilifanyika na kwamba hatua hizi zilianza kwa amri yangu," alisema Dk Abdul Qadeer Khan, aliyevalia suti na tai, katika taarifa ya kukiri kwake.

"Katika majadiliano yangu na viongozi husika wa serikali, nyaraka na matokeo yaliwekwa mbele yangu na nilikubali kwa hiari kwamba mengi kati ya hayo yalikuwa ya kweli na sahihi."

"Ndugu zangu wapendwa, nimeamua kufika mbele yenu ili kuwaeleza masikitiko yangu makubwa na kuomba radhi. Pia nataka kufafanua kuwa serikali haikuwahi kunipa kibali chochote kwa shughuli hizi."

Rais wa wakati huo Pervez Musharraf alimweka Dk. Abdul Qadeer Khan katika kizuizi cha nyumbani na kukata mawasiliano yake na ulimwengu wa nje, lakini Pakistan na Dk. Qadeer walibaki kwenye habari za ulimwengu.

Jarida la Time liliangazia picha yake kwenye jalada lake katika toleo lake la Februari 14, 2004 likiwa na nukuu: "The Merchant of Danger."

Chanzo cha picha, TIME MAGAZINE

Lakini nchini Pakistan, maswali yameibuka kuhusu kauli zake, na maswali haya yamekuwa yakiulizwa mara kwa mara: Inawezekanaje mwanasayansi huyo muhimu awe anauza siri na teknolojia ya nyuklia kwa muda mrefu na hakuna mtu nchini humo, hasa jeshi la Pakistani na mashirika yake ya kijasusi, anayejua kuhusu hilo?

Miaka minne baadaye, Dk. Abdul Qadeer Khan, katika mahojiano na gazeti la The Guardian kuhusu kukiri kwake, alisema kwamba alikuwa amesoma yote haya kutoka kwenye kipande cha karatasi ambacho "amekabidhiwa."

Dk. Qadir alishutumiwa kwa kuuza siri za nyuklia kwa Iran, Korea Kaskazini, na Libya kupitia mtandao wa siri na kusaidia mipango yao ya nyuklia.

Iran, Korea Kaskazini na Libya

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hadithi ilianza miaka ya 1990. Kulingana na ripoti iliyochapishwa na BBC mnamo Desemba 2004, Shirika la huduma za siri Uingereza na CIA ya Marekani walipata waliufikia mtandao wa siri wa Dk. Abdul Qadeer Khan mwishoni mwa miaka ya 1990. Mashirika haya yalifanya shughuli kadhaa na kumtambulisha mmoja wa mawakala wao kama mpenyezaji taarifa kwenye mtandao.

Kwa mujibu wa habari hizo hizo, kwa msaada wa vyanzo vingine na Kituo cha Ujasusi cha Uingereza, walifanikiwa kubaini wanunuzi, makampuni feki, vyanzo vya fedha, na mtandao wa maabara unaohusishwa na Dk Abdul Qadeer Khan.

Ilipodhihirika kuwa Dk. Abdul Qadeer Khan alikuwa ameunda mtandao wa kimataifa ambao ulisambaza vifaa vinavyohitajika kwaajili ya silaha za nyuklia, Kamati ya Ujasusi ya Pamoja ya Uingereza ilielezea wasiwasi wake kuhusu suala hili tangu mwanzoni mwa 2000.

Lakini kiungo muhimu zaidi katika hadithi hiyo kilikuja mnamo Desemba 2003, wakati maajenti kutoka Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na Huduma ya Ujasusi ya Siri ya Uingereza (MI6) walipopata taarifa kutoka kwa maafisa wa Libya kwamba Libya ilikuwa imekabidhi mipango ya silaha za nyuklia katika bahasha za kahawia ilipoachana na mpango wake wa nyuklia.

Kwa mujibu wa habari hii, pamoja na mipango hiyo, sehemu zinazohusiana na mpango wa nyuklia zilitolewa na Dk Abdul Qadeer Khan, na hii iliipa Marekani kisingizio kikubwa cha kuishinikiza Pakistan kuchukua hatua dhidi yake.

"Kukiri" kwa serikali ya Pakistan

Mnamo Machi 2005, Sheikh Rashid Ahmed, aliyekuwa waziri wa habari wa Pakistan wakati huo, alikiri kwamba Dk Abdul Qadeer Khan alitoa teknolojia ya nyuklia kwa Iran, lakini serikali haikujua kuhusu mpango huo. Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa mwakilishi wa serikali ya Pakistani kufanya uandikishaji kama huo.

Sheikh Rashid Ahmed alisema katika mahojiano kwa njia ya simu na Shirika la Habari la Associated Press: "Daktari Abdul Qadeer ameipatia Iran vituo kadhaa" na "yeye binafsi aliisaidia Iran na serikali ya Pakistani haikuwa na jukumu lolote katika suala hili."

Kulingana na ripoti ya BBC iliyochapishwa mnamo Oktoba 2021, inaonekana kwamba mpango wa Iran wa kituo cha Natanz cha centrifuge uliegemea zaidi miundo na malighafi ambayo hapo awali ilitolewa kwa Irani kupitia mtandao wa Dk. Abdul Qadeer Khan.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika moja ya mikutano hiyo, wawakilishi wa Dk Abdul Qadeer Khan waliikabidhi Iran orodha ya vifaa na sehemu zinazotumika katika mpango wa nyuklia, ambayo pia ilijumuisha bei, na Wairani wanaweza kuagiza bidhaa kwa kuzingatia hilo.

Jenerali Pervez Musharraf, Rais wa Pakistan wa wakati huo, alimweka Dk. Abdul Qadeer Khan katika kizuizi cha nyumbani na kukata mawasiliano yake na ulimwengu wa nje.

Chanzo cha picha, Getty Images

Katika ripoti iliyochapishwa na Al Jazeera mnamo Desemba 22, 2004, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilijibu madai hayo kwa kusema kwamba walikuwa wamenunua vifaa kutoka kwa baadhi ya wachuuzi, lakini "hatujui vifaa hivi vilitoka wapi." Taarifa hiyo pia ilisema kuwa mpango wa nyuklia wa Iran ulikuwa wa amani na kwamba hauna nia ya kuunda bomu la nyuklia.

Picha za satelaiti za vituo vya nyuklia vya Iran huko Natanz

Chanzo cha picha, MAXAR TECHNOLOGIES

Dk Abdul Qadeer Khan alikana kuisaidia Iran

Dk. Abdul Qadeer Khan alikuwa chini ya kizuizi cha nyumbani kwa kipindi kifupi sana. Mnamo mwaka wa 2012, Dk. Qadeer pia aliunda chama cha kisiasa kilichoitwa Pakistan Tehreek-e-Tahafuz, ambacho kilipata kushindwa vibaya katika uchaguzi huo, na kushindwa kupata kiti kimoja.

Wakati huo huo, baada ya muda mrefu, alifanya mahojiano na baadhi ya waandishi wa habari ambapo alikanusha taarifa yake ya kukiri kwenye televisheni na kukana shughuli yoyote haramu.

Katika mahojiano na jarida moja la kimataifa, alisema kwa uwazi kwamba yeye hana uhusiano wowote na mpango wa nyuklia wa nchi yoyote isipokuwa Pakistan, na haswa kuhusiana na Iran, alisema: "Inawezekanaje kwamba nchi kama Iran, ambayo ni mwanachama wa Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Nyuklia (NPT) na imekuwa ikisema kwamba haitaki kutengeneza bomu, inaweza kutengeneza bomu kwa msaada wa mtu?

Aliyachukulia madai hayo kuwa sawa na propaganda zilizokuwa zimetolewa dhidi ya Iraq: "Kwa sababu Iran ni mwanachama wa Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Nyuklia (NPT) na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ina uwezo wa kukagua mpango wake wa nyuklia mahali popote wakati wowote. Kwa hivyo, madai kwamba Iran inaunda bomu ni ya uwongo kabisa."

Kuhusu uwezo wa nyuklia wa Korea Kaskazini, alisema kuwa nchi hiyo imekuwa ikiungwa mkono na China na Urusi kwa miaka mingi na "haihitaji msaada wa nchi nyingine kutengeneza bomu."

Akijibu shutuma kwamba Libya inajaribu kutengeneza bomu la nyuklia kwa kutumia teknolojia iliyonunuliwa kutoka kwake, Dk Qadir alisema: "Inawezekanaje nchi ambayo haina hata uwezo wa kutengeneza baiskeli kutengeneza bomu la nyuklia?"

"Hatua za kutowajibika"

Mohammad Ali, mtaalamu wa masuala ya ulinzi na nyuklia ameiambia BBC: "Msimamo thabiti wa nchi na serikali ya Pakistan umekuwa kwamba Dkt. Abdul Qadeer Khan amejaribu binafsi kuisaidia Iran, ambayo haikuwajibika na nje ya sera rasmi za serikali ya Pakistan."

"Kwa takribani miaka 25, Pakistan imedumisha msimamo kwamba mpango wa nyuklia wa Pakistani na teknolojia ya makombora ni kwa ajili ya ulinzi wa Pakistani yenyewe, kuzuia, na usalama wa kikanda na haitatolewa kwa nchi nyingine yoyote."

Muhammad Ali pia alisema: "Msimamo huu unaungwa mkono na wasiwasi uliofichika na tamaa kwamba Pakistan haitaki tuhuma zinazohusiana na kuenea kwa nyuklia ziwe maarufu kupita kiasi na kwamba tuhuma kama hizo hazina maslahi kwa nchi."

Kuna tofauti gani kati ya programu za nyuklia za Pakistan na Iran?

Silaha

Chanzo cha picha, Getty Images

Dk. Mansoor, mtaalamu wa masuala ya nyuklia na ulinzi katika Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Australia huko Canberra, amefanya utafiti wa kina kuhusu mipango ya nyuklia ya Pakistan, India, na Iran.

Akielezea tofauti kati ya mipango ya nyuklia ya Pakistan na Iran anasema: "Pakistani haijawahi kutia saini NPT, wakati Iran imetia saini, na hiyo ni tofauti kubwa kwa sababu Iran imetia saini, hivyo kidole cha lawama kinaelekezwa kwake, na wanasema, ikiwa una mpango wa amani, kwa nini unahitaji kurutubisha uranium nyingi?"

"Kwa kuwa Pakistan imeendeleza mzunguko wake wa nishati ya nyuklia ndani na nje ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, hakuna nchi inayoweza kuishutumu Pakistan kwa jambo kama hilo, kwa sababu Pakistan sio saini ya NPT na imepata uwezo huu ndani ya nchi. Kwa upande wa Iran, hata hivyo, shughuli zote ziko chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, na ndio maana ukosoaji unaelekezwa kwake."

Anaongeza: "Lakini Iran inafanya kila kitu ambacho Pakistan au nchi yoyote imefanya kwa mpango wake wa nyuklia, sehemu muhimu zaidi ikiwa ni kuunda mzunguko wa nishati ya nyuklia."