Ni nchi gani zinazofanya biashara na Iran na ushuru wa Trump unamaanisha nini?

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock
- Author, Jemma Crewand & Faarea Masud,
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Rais wa Marekani Donald Trump amesema nchi zinazofanya biashara na Iran, zitawekewa ushuru wa 25% kwa biashara wanazofanya na Marekani.
Hilo linakuja huku Iran ikikabiliana na maandamano ya kuipinga serikali, na maelfu ya watu wakihofiwa kufariki.
Trump ana historia ya kutumia ushuru kuweka shinikizo kwa nchi.
Siku ya Jumatatu Trump alichapisha taarifa kwenye Truth Social: "Kuanzia hivi punde, nchi yoyote inayofanya biashara na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran italipa ushuru wa 25% kwa biashara yoyote inayofanya na Marekani."
Rais huyo hajaeleza kwa undani juu ya agizo hilo.
Nchi gani hufanya biashara na Iran?
Kati ya nchi zaidi ya 100 zinazofanya biashara na Iran, China ndiyo mshirika wake mkubwa wa mauzo ya nje.
Katika mwaka 2025 hadi Oktoba mwaka huo, ilitumia zaidi ya dola bilioni 14 (£10.4bn) kwa bidhaa kutoka Iran, kulingana na Trade Data Monitor kutokana na takwimu za Mamlaka ya Forodha ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
China inafuatiwa na Iraq, ambayo ilipokea bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 10.5 kutoka kwa jirani yake. Iran pia inafanya Biashara na Falme za Kiarabu na Uturuki, miongoni mwa wateja wake wakubwa.
Mauzo ya nje kutoka Iran hadi Uturuki yaliongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka dola bilioni 4.7 mwaka 2024 hadi dola bilioni 7.3 mwaka jana.
Karibu bidhaa zote 10 bora za Iran zinazouzwa nje nchi, zinahusiana na mafuta - ni mojawapo ya wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani.
Pia husafirisha chakula kwa mataifa mengine, ikiwa ni pamoja na fistiki (pistachio) na nyanya.
Hata hivyo, Iran hununua bidhaa muhimu zaidi kutoka kwa washirika wake wa biashara kuliko inavyouza nje.
Chakula kinachangia takriban theluthi moja ya bidhaa inazoagiza, hasa mahindi, mchele, mbegu za alizeti na mafuta pamoja na soya.
Lakini bidhaa muhimu zaidi zinazoagizwa na Iran ni dhahabu.
Katika miezi 12 hadi Oktoba 2025, iliagiza dhahabu yenye thamani ya dola bilioni 6.7 ikilinganishwa na dola bilioni 4.8 mwaka uliotangulia.
Ushuru huu utatekelezwaje?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Taarifa ya Trump inasema ushuru wa 25% "utaanza kutumika mara moja."
Hata hivyo, bado hakuna maelezo kutoka Ikulu kuhusu jinsi ushuru huo utakavyo fanya kazi kivitendo, au ni nchi zipi hasa ambazo zitawekewa ushuru huo.
Hatujui kama utahusisha nchi zote zinazofanya biashara na Iran au washirika wake wakubwa tu wa kibiashara.
Pia haijulikani ikiwa ushuru wa 25% utawekwa juu ya ushuru uliopo ambao utawala wa Trump tayari umeuweka.
Marekani pia haijabainisha chini ya sheria gani ushuru huu mpya utaanzishwa. Ushuru mkubwa uliotangazwa Aprili iliyopita uliwekwa chini ya Sheria ya Kimataifa ya Mamlaka ya Kiuchumi ya Dharura.
Lakini ushuru huu wa sasa unakabiliwa na changamoto ya kisheria - Mahakama Kuu ya Marekani inatarajiwa kutoa uamuzi wake siku ya Jumatano. Siku ya Jumatatu Trump alisema Marekani itapoteza ikiwa ushuru huu hautoungwa mkono.
Kutekeleza ushuru uliopendekezwa kunaweza kuwa vigumu. Iran inakadiriwa kupata mabilioni ya pesa kutokana na mauzo ya nje ya mafuta mwaka 2024 kwa kutumia meli za magendo ambazo ni vigumu kuzifuatilia na huuza mafuta yake kwa sarafu ya Yuan ya China badala ya dola za Marekani.
Uhusiano wa Marekani na China

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa mtazamo wa juu juu, tangazo la Trump lina hatari ya kufufua tena mzozo wa kibiashara kati ya Marekani na China.
Kama rais atatekeleza alichoandika, inamaanisha bidhaa za China zinazopelekwa Marekani zinapaswa kutozwa ushuru mpya wa asilimia 25 mara moja.
Hata hivyo, bidhaa hizo tayari zinakabiliwa na kiwango cha ushuru cha 30.8% cha awali, kulingana na Bloomberg Economics.
China imeonyesha kuwa ina uwezo wa kupambana na kile inachokiona kama hatua isiyo na usawa ya Marekani.
Imefanya hivyo kwa kuanzisha ushuru wake dhidi ya Marekani, lakini muhimu zaidi kwa kutangaza vikwazo kwa mauzo ya nje ya madini adimu, ambayo Marekani inayahitaji sana kwa ajili ya viwanda vyake vya teknolojia.
Kwa sasa China inatawala usambazaji wa kimataifa wa madini hayo, na hilo linaipa nguvu muhimu, jambo ambalo liliisaidia Beijing kufikia makubaliano ya muda ya kibiashara na Marekani mwezi Novemba ambayo yalipunguza mvutano.
Kwa hivyo kuanzisha ushuru mpya wa 25% kwa China kutaleta mvutano, na Beijing tayari imeonya kuwa "itachukua hatua zote muhimu kulinda haki na maslahi yake halali."
Uchumi wa Iran

Chanzo cha picha, Getty Images
Akiba kubwa ya mafuta ya Iran inaifanya kuwa moja ya wazalishaji 10 wakubwa wa mafuta duniani na inapaswa kuwa chanzo cha utajiri.
Hata hivyo, uchumi wake umedhoofika kutokana na miaka mingi ya usimamizi mbaya wa fedha za umma, kushuka kwa mauzo ya mafuta na vikwazo vikali vya kimataifa.
Wengi kati ya watu milioni 92 nchini humo wanapambana kupata mahitaji ya msingi kama vile chakula na huduma za umma, na gharama ya maisha ndiyo kiini cha maandamano yanayoonekana katika wiki za hivi karibuni.
Wakati huo huo bidhaa zimekuwa ghali zaidi kutokana na mfumuko wa bei, ambao ulifikia 48.4% mwezi Oktoba huku kukiwa na mabadiliko ya sera za serikali ambayo yamesababisha thamani ya rial kushuka dhidi ya dola ya Marekani.
Hilo hufanya uagizaji kuwa ghali zaidi na kufanya uwekezaji katika mifumo ya umeme na maji kuwa mgumu na hivyo kukwamisha ahadi za serikali za kuongeza uzalishaji wa ndani wa kila kitu kuanzia chakula hadi bidhaa za watumiaji.
Kupunguzwa kwa ruzuku za mafuta mwezi Desemba na kupungua kwa biashara ya nje kutokana na ushuru huu wa hivi karibuni kunamaanisha mfumuko wa bei bado unaweza kupanda juu na kuusukuma uchumi kuelekea kuanguka.















