'Tutaishi vipi?': Ushuru wa Trump unavyowaathiri masikini

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Khanyisile Ngcobo & Shingai Nyoka
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Kiwanda cha nguo nchini Lesotho, ambacho kimetengeneza mashati ya gofu yenye nembo ya Trump, huenda kikalazimika kufungwa hivi karibuni kufuatia ushuru mkubwa uliowekwa na serikali ya Marekani mapema mwaka huu.
Nchi hiyo ndogo ya kifalme kusini mwa Afrika iliwekewa ushuru wa 50% - kiwango cha juu kuliko nchi nyingine yoyote - na Rais wa Marekani Donald Trump mwezi Aprili.
Ingawa ushuru huo umesitishwa tangu wakati huo, Trump anasema utarejea Ijumaa ijayo, Agosti 1, pamoja na nchi zingine ulimwenguni, isipokuwa kama kuna makubaliano yatafikiwa.
"Hatujui jinsi tutakavyo ishi katika maisha haya. Tutakufa," Aletta Seleso aliambia BBC kwa sauti ya huzuni akiwa amesimama nje ya kiwanda cha Precious Garments, ambapo mashati ya gofu ya Trump yametengenezwa.
Mama wa mtoto mmoja mdogo amefanya kazi huko kwa karibu muongo mmoja, pia akisaidia familia yake kubwa kwa mshahara wake wa kila mwezi wa dola $160 (£120).
Viwanda vya nguo katika nchi hiyo pia vinazalisha dangirizi za kampuni za Marekani kama vile Levi's na Wrangler.
Lakini mashaka juu ya mustakabali wa sekta ya nguo nchini humo ni sababu moja kwa nini Lesotho imetangaza "hali ya maafa" ya kitaifa mapema mwezi huu ili kuharakisha uundaji wa ajira.

BBC inakutana na Bi Seleso, anasema wafanyakazi wameambiwa kampuni hiyo "inaweza kufunga wakati wowote kuanzia sasa. Wanasema ni juu ya ushuru."
Wakati huo huo, Bi Seleso na wenzake wameambiwa wafanye kazi kwa wiki mbili kwa mwezi, ikimaanisha wanapata nusu tu ya malipo.
Anasema kwa sasa ni "vigumu sana" kwake kumsaidia mtoto wake, mama na watoto wawili wa marehemu dadake mdogo, ambao wote wako chini ya uangalizi wake.
Lakini Sam Mokhele, katibu mkuu wa moja ya vyama vya wafanyakazi vinavyowakilisha wafanyakazi 150 katika kampuni hiyo, anasema kampuni hiyo "haijaonyesha dalili zozote za kutaka kufungua kazi" kwa sasa.
"Lakini walichosema [wanaweza] kufunga ikiwa mambo hayatabadilika," anasema.
Sekta ya Nguo

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ingawa ushuru wa 50% umesitishwa, mauzo ya Lesotho kwenda Marekani bado yanatozwa ushuru wa 10%, kama nchi nyingine.
Hadi mwaka huu, mauzo yake ya nje hayakuwa chini ya ushuru wowote wa Marekani chini ya Sheria ya Ukuaji na Fursa ya Afrika (Agoa) - sheria iliyopitishwa mjini Washington mwaka 2000 kuruhusu uuzaji katika soko la Marekani bila ushuru wa bidhaa kutoka baadhi ya nchi ili kupunguza umaskini na kuunda nafasi za kazi.
Sekta ya nguo ndiyo mwajiri mkubwa zaidi miogoni mwa sekta binafsi Lesotho. Inatoa karibu ajira 50,000, kati ya wakazi zaidi ya milioni mbili.
Idadi ya ajira kwa sasa ni 36,000 kulingana na serikali, na kazi 12,000 zimeathiriwa moja kwa moja na ushuru wa Marekani. Ukuaji wa mauzo ya nguo ya Lesotho uliochochewa na mpango wa Agoa.
Na ndio maana Trump aliiwekea nchi hiyo ushuru wa juu, jambo ambalo lilikuwa na lengo la kukomesha mapango wa Agoa, na kutatiza mustakabali wa sekta moja muhimu katika uchumi wa nchi hiyo.
Ukosefu wa ajira

Ukosefu wa ajira umefikia 30% lakini kwa vijana kiwango ni karibu 50%, kulingana na takwimu rasmi.
Mwanaharakati wa vijana Tšolo Thakeli anaiambia BBC hata bila tishio hili kwa sekta ya nguo, hali ni "ya kusikitisha" kwani "hakuna kazi, haswa kwa vijana".
"Tuna wahitimu kutoka kila ngazi... hawana ajira. Kuna hali mbaya ya kukosa matumaini miongoni mwa vijana," anasema.
Ingawa kuna sababu nyingi, Bw Thakeli analaumu "upendeleo wa ajira na ufisadi" wengi wanadai umekithiri nchini.
Mjasiriamali huyo mwenye umri wa miaka 31 na mwanasheria aliyehitimu ni mkosoaji mkubwa wa serikali ya Lesotho na alikamatwa baada ya kutuma video kwenye mitandao ya kijamii akihoji iwapo ahadi ya Waziri Mkuu Sam Matekane ya kuunda nafasi za kazi 70,000 ndani ya wiki mbili ilikuwa na uhalisia.
Anaiambia BBC kuwa waziri mkuu hana mpango mzuri wa kukabiliana na mzozo huo.
"Hakuna kitu kinachoonekana ambacho serikali imefanya au kushughulikia tatizo hili. [Ni] ahadi tupu," anasema.
Hili linakanushwa na Waziri wa Biashara Mokhethi Shelile, ambaye anasisitiza kuwa serikali inafanya kazi kujaribu kutatua suala hilo.
"Tayari tulikuwa na suluhu, hata kabla ya ushuru kutangazwa, kwa sababu soko la Marekani lilikuwa tayari limeanza kuwa soko gumu kwetu," anaiambia BBC.
Anasema nchi "tayari inahamia katika uzalishaji kwa ajili ya Afrika Kusini" na mambo yalivyo sasa, ni "20% tu ya sekta ya nguo inapeleka katika soko la Marekani."
Kiwanda cha TZICC, kinachomilikiwa na raia wa Taiwan, kimekuwa kikifanya kazi nchini Lesotho tangu 1999, kikitengeneza nguo za michezo kama JC Penney, Walmart na Costco.
Kiwanda hicho kimekuwa kikizalisha nguo 400,000 kwa mwezi lakini wakati BBC inakitembelea, mamia ya mashine za cherehani zinakusanya vumbi katika moja ya ghala.
Meneja katika kampuni hiyo, Rahila Omar, anasema wafanyakazi 1,000 wa kampuni hiyo, wengi wao wakiwa wanawake, wameachishwa kazi kwa muda wa miezi minne ijayo kutokana na agizo la ushuru.
"Kwa sababu ya... shinikizo la ushuru, wanunuzi wetu walitaka tumalize nguo zilizopo haraka iwezekanavyo. Tulipewa tarehe ya mwisho Juni 30, lakini tulimaliza kabla ya Juni 30, na ndiyo sababu tunaachishwa kazi," anasema.
Wakati kiwanda hicho pia kinasambaza nguo kwa wauzaji wa reja reja wa Afrika Kusini, Bi Omar anasema mapato yanayotokana na ununuaji huo ni madogo ikilinganishwa na kile ambacho kampuni hiyo inapata kutoka soko la Marekani.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












