Ushuru ni nini na kwa nini Trump anautumia?

j

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais wa Marekani Donald Trump
    • Author, Jennifer Clarke
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Rais wa Marekani Donald Trump anatazamiwa kutangaza ushuru zaidi tarehe 2 Aprili, 2025 ambao utazikumba nchi zote.

Kabla ya hapo, tayari ameanzisha mfululizo wa ushuru kwa uagizaji wa chuma, alumini, magari pamoja na bidhaa zote kutoka China.

Trump anasema – kwa hatua hizi ambazo zinazifanya bidhaa za kigeni kuwa ghali zaidi - zitasaidia wazalishaji wa Marekani na kulinda kazi zao.

Pia unaweza kusoma

Ushuru ni nini?

Ushuru ni kodi inayotozwa kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nchi nyingine.

Kwa mfano, ushuru wa 25% kwa bidhaa ya thamani ya dola za kimarekani $10 (£7.76) itamaanisha malipo ya ushuru ni dola $2.50. Kampuni zinazoleta bidhaa za kigeni nchini zinapaswa kulipa ushuru huu kwa serikali.

Ushuru ni sehemu ya dira ya kiuchumi ya Trump. Anasema "ushuru" ndilo neno analolipenda zaidi. Anasema kodi hizo zitawahimiza watumiaji wa Marekani kununua bidhaa zaidi zinazotengenezwa Marekani, kukuza uchumi wa nchi na kuongeza kiwango cha kodi.

Trump anataka kupunguza pengo kati ya bidhaa ambazo Marekani inaagiza na zile inazosafirisha kwenda nchi nyingine.

Rais wa Merika pia amesema ushuru unakusudiwa kuilazimisha China, Mexico na Canada - kufanya zaidi katika kukomesha wahamiaji na dawa za kulevya kuingia Marekani.

Trump amekiri uwezekano wa kudorora kwa uchumi kutokana na sera zake za kibiashara.

Bidhaa zitapanda bei?

k

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wachambuzi wameonya ushuru huo mpya utavuruga kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa magari ya Marekani
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wanauchumi wanatarajia ushuru kuongeza bei za bidhaa kwa wateja wa Marekani katika bidhaa nyingi zinazoagizwa kutoka nje.

Bidhaa zilizoathiriwa na ushuru zinajumuisha kila bidhaa kuanzia bia, mafuta hadi maparachichi. Kwa sababu ya ushuru, Makampuni yanaweza kuamua kuagiza bidhaa chache za kigeni, jambo ambalo linaweza kufanya zile zinazopatikana kuwa ghali zaidi.

Miongoni mwa makampuni yanayowekewa ushuru, ni yale ya magari kutoka nje ya nchi. Marekani iliagiza takribani magari milioni nane mwaka jana - yakigharimu takribani dola bilioni 240 (£186bn), ni takribani nusu ya mauzo ya jumla.

Ushuru mpya wa 25% kwa uagizaji wa magari kutoka nje na vipuri vya gari utaanza kutekelezwa tarehe 2 Aprili, na malipo ya ushuru huo yataanza siku inayofuata. Ushuru kwa vipuri utaanza kulipwa mwezi Mei.

Bei za magari tayari zimeanza kupanda kutokana na ushuru kwa bidhaa kutoka Canada na Mexico. Vipuri kwa kawaida huvuka mipaka ya Marekani, Mexico na Canada kabla ya gari kutengenezwa kamili.

Ushuru aliotangaza Trump katika muhula wake wa kwanza kama rais ulipandisha wastani wa bei ya chuma na alumini nchini Marekani kwa 2.4% na 1.6%, kulingana na Tume ya Biashara ya Kimataifa ya Marekani.

Ushuru kwa mashine za kufulia zilizoagizwa kutoka nje kati ya 2018 na 2023 uliongeza bei ya mashine hizo kwa 34%, kwa mujibu wa takwimu rasmi.

Bei zilishuka mara tu ushuru ulipoondoshwa.

Trump ametangaza ushuru gani?

  • Aprili 2:

Ushuru wa 25% kwa magari yanayoingia Marekani. Ushuru wa 25% kwa vipuri vya magari vinavyoagizwa kutoka nje kuanzia mwezi wa Mei.

Machi 12:

25% ya ushuru kwa bidhaa zote za chuma na alumini

  • Machi 6:

Msamaha wa ushuru kwa bidhaa zinazotoka katika chini zenye makubaliano ya biashara huria za Amerika Kaskazini, kama vile televisheni, viyoyozi, maparachichi na nyama ya ng'ombe.

Ushuru wa kemikali ya potashi – inayotumiwa katika mbolea na wakulima wa Marekani - ilipunguzwa kutoka 25% hadi 10%

  • Machi 5:

Msamaha wa ushuru kwa mwezi mzima kwa magari yanayotengenezwa Amerika Kaskazini ambayo yanatii makubaliano ya biashara huria.

  • Machi 4:

10% ya ushuru kwa bidhaa za China iliongezeka mara mbili hadi 20%

25% ya ushuru dhidi ya bidhaa kutoka Mexico na Canada, na ushuru wa 10% kwa uagizaji wa nishati ya Canada

  • Februari 4:

10% ushuru kwa bidhaa kutoka China

Nchi nyingine zimejibu nini?

k

Chanzo cha picha, PA Media

Maelezo ya picha, Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer

Uingereza imeathirika na ushuru wa magari na chuma - na inatarajiwa itaathirika tena kwa ushuru wa Aprili 2. Lakini serikali ya nchi hiyo haijatangaza ushuru wowote kwa bidhaa kutoka Marekani kama njia ya kujibu ushuru wa Trump.

Katibu wa Biashara Jonathan Reynolds anasisitiza kuwa mazungumzo ya kibiashara yanayoendelea na utawala wa Trump yanamaanisha kuwa Uingereza iko katika "nafasi bora zaidi ya nchi yoyote" kufanya ushuru upunguzwe au kuondoshwa.

Nchi nyingine zimeanzisha ushuru kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka Marekani. Hilo litazifanya bidhaa za Marekani kuwa ghali, na kuongeza hofu ya vita vya kimataifa vya biashara ambavyo vinaweza kuleta matatizo kwa uchumi duniani kote.

China imeanzisha ushuru wa 10-15% kwa baadhi za kilimo za Marekani. Pia imelenga makampuni ya anga ya Marekani, ulinzi na teknolojia.

Ushuru wa Umoja wa Ulaya unaolenga bidhaa za Marekani zenye thamani ya Euro bilioni 26 (£22bn) utaanza tarehe1 Aprili na kutekelezwa kikamilifu tarehe 13 April. Utalenga bidhaa nyingi ikiwemo boti, bia, pikipiki, pamoja na bidhaa za chuma na alumini.

Canada imeweka ushuru wa 25% kwa chuma kutoka Marekani, alumini na bidhaa zingine. Ushuru zaidi unaweza kuletwa tarehe 2 Aprili.

Mexico imechelewa kuanzisha ushuru wake wa kulipiza kisasi huku mazungumzo na Marekani yakiendelea.