Ushuru mpya wa Trump unamaanisha nini kwa Tanzania na nchi zingine za Afrika Mashariki?

Chanzo cha picha, Getty Images
Na Yusuph Mazimu
Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza viwango vipya vya ushuru kwa bidhaa zinazoingizwa nchini humo, viwango ambavyo havijaonekana tangu mwanzoni mwa karne iliyopita.
"Leo ni Siku ya Ukombozi," Trump alisema. "Ni moja ya siku muhimu katika historia ya Marekani, na ni tangazo la uhuru wa kiuchumi wa Marekani."
"Tutaifanya Marekani kuwa kubwa na tajiri tena. Nchi yetu imenyang'anywa kwa zaidi ya miaka 50. Hilo halitafanyika tena."
Kwa ujumla, hakuna nchi itakayoepuka ushuru wa Wamarekani kwa ununuzi wa bidhaa zao ambapo "kiwango cha chini cha ushuru" kitakuwa 10%.
Kwa idadi yake ya watu zaidi ya 340mil na nguvu za uchumi wake, Marekani ni nchi yenye washirika wengi wa kibiashara, ikifanya biashara na karibu nchi zote duniani. Lakini kutangazwa kwa ushuru mpya sasa kunakwenda kubadili kwa kiwango kikubwa namna dunia itakavyofanya biashara na kuathiri karibu ulimwengu mzima. Viwango vipya vinagusa mataifa yote tajiri na maskini, na hicho ndicho kinachozua mijadala na kuleta hofu ya kiuchumi kila kona ya dunia.
Nchi maskini zaidi kama za Afrika Mashariki kwa kawaida hutegemea zaidi ushuru wa forodha kuliko kodi ili kuongeza mapato. Je hatua ya sasa ina maana gani kwa uchumi wa Tanzania na nchi za Afrika Mashariki?
Viwango vipya vya Ushuru kwa Afrika Mashariki
Trump ametangaza ongezeko la ushuru kwa bidhaa mbalimbali kutoka Afrika Mashariki. Ushuru huu mpya unalenga sekta mbalimbali, hasa kilimo na viwanda, ambazo zinategemewa na mataifa haya ya afrika Mashariki kwa mapato ya kigeni. Anchokifanya Trump ni kuhakikisha nchi hiyo inanufaika zaidi, kwa sababu zipo nchi zinazoitoza bidhaa za Marekani kiwango kikubwa zaidi cha ushuru. Trump anasema 'hilo linakoma". ingawa kwa Afrika Mashariki ni DRC pekee yenye kutoza 22% bidhaa zinazoingia nchini humo kutoka Marekani, nchi nyingi ziko kwenye kiwango cha 10%. Viwango vipya vya Trump ni kama vinavyoonekana hapa chini.

Chanzo cha picha, Getty Images
Tanzania, Kenya, Rwanda, Burundi, na Ethiopia
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa nchi hizi, ushuru wa bidhaa zote zinazozalishwa na kuingizwa Marekani kutoka Afrika Mashariki umewekwa kwa kiwango cha asilimia 10%. Hii inajumuisha bidhaa kama Chai, kahawa, na maua kutoka Kenya na Rwanda. Samaki, mbegu za korosho, na bidhaa za ngozi kutoka Tanzania.
Bidhaa za Kakao na vanila kutoka Uganda na Rwanda na bidhaa za viwanda kutoka Kenya na Ethiopia.
Kwa mfano, mwaka 2024, Kenya iliuza tani 58,000 za chai na tani 23,000 za kahawa kwenye soko la Marekani, kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Biashara Duniani (WTO). Tanzania yenyewe iliuza tani 12,000 za samaki na tani 8,500 za mbegu za korosho kwa Marekani, kulingana na ripoti ya FAO. Kwa vyovyote vile ushuru huu wa 10% utaendelea kuongeza gharama za bidhaa zinazozalishwa katika nchi hizi na kutishia biashara ya bidhaa zinazoingizwa Marekani.
"Asilimia 10% ni kubwa sana kibiashara, hasa kwa jiografia yetu na umbali wetu na Marekani, unaoongeza gharama, uhifadhi na ushindani, haitakuwa rahisi sana kwa wafanyabisahara wengi", anasema Beatrice Kimaro, Mchumi kutoka Tanzania
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC)
Hali ya ushuru kwa DRC ni tofauti kidogo na nchi tajwa hapo juu. Kwa viwangp vya sasa, DRC inatoza 22% kwa bidhaa zinazozalishwa nchini kwake na kuingizwa Marekani, huku Marekani ikitoza 11% kwa bidhaa zinazozalishwa DRC. Hii ina maana kwamba bidhaa kutoka DRC zitakutana na kiwango kikubwa cha ushuru kilicho juu kuliko kile cha nchi nyingine za Afrika Mashariki, cha tofauti ya asilimia 1% na hii inaweza kudhoofisha ushindani wa bidhaa za DRC kwenye soko la Marekani.
Kwenye viwango vya sasa, DRC ataathirika zaidi tofauti na Tanzania, Kenya na nchi zingine zenye viwango vya 10%. Lakini kwa upande mwingine ushuru wake wa 22% kwa bidhaa za Marekani zinazoingia DRC ni mkubwa mara mbili zaidi ya nchi zingine. Hilo linaweza kufidia, lakini je ni soko pekee kwa bidhaa za Marekani? kwa sababu ya Marekani kuwa na washirika wengi kibiashara na masoko mengi, viwango vya sasa vinaweza kuiweka DRC jia panda.
Uganda
Uganda pia ina hali tofauti, kwani inatoza 20% kwa bidhaa zinazozalishwa nchini Uganda na kuingizwa Marekani, wakati Marekani inatoza 10% kwa bidhaa zinazozalishwa Uganda. Hii inamaanisha kuwa Uganda itakutana na ushuru wa juu kwa bidhaa zake zinazozalishwa na kuingizwa Marekani, lakini pia itafaidika na kiwango kidogo cha ushuru kutoka kwa Marekani kwa bidhaa zake zinazohitajika Marekani.
Lakini kiwango hicho kidogo, kinatozwa na nchi zingine za ukanda huu za Tanzania, Kenya, Burundi, Rwanda ana Ethipia. Hilo linaongeza ushindani.
"Kitu cha kuzingatia ni nchi kuuza bidhaa nyingi kuliko kuagiza, hapo utatengeneza uchumi na kuimarisha sarafu yako, kupewa viwango vidogo vya ushuru kwa bidhaa zinazouzwa Marekani ni jambo la msingi kwa ukuaji wa uchumi wa mmataifaya Afrika Mashariki, anasema Beatrice.
Athari kwa Uchumi wa Afrika Mashariki
Ushuru mpya alioanzisha Rais Trump, kwa bidhaa zinazoingizwa nchini humo kutoka Afrika Mashariki, unatarajiwa kuwa na athari kubwa kwa sekta mbalimbali za uchumi. Ushuru huu, unaolenga sekta za kilimo, viwanda, na usafirishaji, unahatarisha uchumi wa mataifa kama Kenya, Tanzania, Uganda, na Ethiopia, ambazo zote zinategemea sana biashara ya nje, hasa soko la Marekani.
Athari hizi zitakuwa na madhara mbalimbali kwa nchi hizi, ambazo tayari zinakumbwa na changamoto za uchumi na biashara. Wakati huu, matokeo ya ushuru huu yatakuwa na nguvu kubwa kutokana na uhusiano wa kibiashara kati ya Marekani na Afrika Mashariki kupitia Programu ya Upendeleo ya Biashara ya Afrika (AGOA), ambayo iliwapa nchi za Afrika Mashariki fursa ya kuuza bidhaa zao kwa Marekani bila ya kulipa ushuru na mipango mingine kwa kuuza kwa ushuru wa chini zaidi. Lakini sasa kila bidhaa itatozwa 10%. Ongezeko la ushuru wa Trump linaweza kutishia manufaa ya AGOA, jambo ambalo litahitaji marekebisho katika mikakati ya biashara ya nchi hizi.
"Kwa ufupi maeneo matatu yataathirika zaidi, gharama za biashara, sekta za uzalishaji kama kilimo, viwanda, usafirishaji, na ajira pamoja na hali ya kifedha', anasema Kimaro, Mchumi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Sekta ya kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi nyingi za Afrika Mashariki, na bidhaa nyingi zinazozalishwa kanda hii hutegemea masoko ya nje kama Marekani. Bidhaa kama chai, kahawa, samaki, mbegu za korosho, na kakao ni baadhi ya mazao makuu yanayouzwa kwa wingi kwa soko la Marekani. Hata hivyo, ongezeko la ushuru linaweza kupunguza ushindani wa bidhaa hizi na kuongeza gharama za uzalishaji.
Kenya ambaye ni mzalishaji mkubwa wa chai na kahawa, na soko la Marekani linachangia kwa kiasi kikubwa mapato ya nchi hii. Ushuru wa 10% utaongeza gharama za bidhaa hizi, na hii inaweza kuwa na athari kwa wakulima wa chai na kahawa ambao tayari wanakabiliwa na changamoto za mfumuko wa bei wa ndani. Wakulima wa chai na kahawa wa Kenya wanakumbana na changamoto kubwa za kiuchumi ambazo zinaweza kuzidishwa na ushuru huu mpya.
Uganda yenyewe inauza zaidi kakao na vanila kwa soko la Marekani. Ushuru mpya wa sasa unaweza kupunguza ushindani wa bidhaa hizi, kwani bidhaa za Afrika Mashariki zitakuwa na gharama zaidi ikilinganishwa na bidhaa kutoka maeneo mengine ya dunia, kwa sasabu za kijiografia. Hii itapunguza mapato ya wakulima na wafanyabiashara, hasa wale wa kakao na vanila, ambao wanategemea soko la Marekani kwa sehemu kubwa.
Tanzania inategemea sana samaki waliohifadhiwa na korosho. Ushuru wa 10% kwa samaki kutoka Tanzania utaathiri biashara na kupunguza faida kwa wakulima na wafanyabiashara katika sekta hizi. Hali hii inaweza kupunguza fursa za ajira kwa wananchi wa Tanzania, ambao wengi wao wanategemea kilimo kwa maisha yao.
Nini nchi za Afrika Mashariki zinaweza kufanya nini kwa sasa?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa vyovyote vileu ushuru huu mpya huu unatahitaji hatua za haraka kutoka kwa serikali za Afrika Mashariki ili kupunguza madhara ya ushuru huu mpya. Na hii ni kwa sababu ya kuweka viwango sawia vya 10% kwa nchi zote duniani zinazofanya biashara na Marekani.
Ingawa Rais Trump mwenyewe ametoa nafasi ya mazungumzo kwa nchi zinazodhani zinaweza kufikia makubaliano mapya na kurekebisha ushuru huu, ikisalia ilivyo wachumi wanaonya kwamba hatua hii itaathiri si tu watu wa afrika mashariki, bali nchi karibu zote na wakiwemo wamarekani wenyewe, watakaolazimika kulipia ushuru kwa kila bidhaa inayoagizwa kuingia nchini humo.
"Hiii ni zaidi ya vita, itabadili mambo mengi ya kibiashara, ni lazima kutafuta masoko mengine kwa sasa, Afrika mashariki zikiendelea kutafuta suluhu nyingine na Marekani kwenye ushuru huu mpya', anasema Beatrice.
Ili kupunguza athari za ushuru huu mpya, mataifa ya Afrika Mashariki yanaweza kuchukua hatua kadhaa Kutafuta masoko mbadala, kwa kuimarisha biashara na mataifa ya Asia, Ulaya, na Afrika yenyewe ili kupunguza utegemezi wa soko la Marekani.
Pili, kuboresha viwango vya uzalishaji kwa kuwekeza katika teknolojia za kisasa ili kuboresha ubora wa bidhaa na kuongeza thamani ya mauzo. Tatu, kuwekeza katika iiwanda vya ndani hasa sekta za ndani za uchakataji wa malighafi ili kuongeza ajira na kupunguza utegemezi wa masoko ya nje.
Lakini Serikali za Afrika Mashariki pia zinaweza kufanya mazungumzo ya kibiashara na Marekani kutafuta suluhisho kama vile makubaliano ya ushuru nafuu au kuingia katika mikataba mipya ya biashara.
Dunia inasemaje kwa viwango vya ushuru vya Trump?

Chanzo cha picha, getty
Kila pembe ya dunia imeonekana kupinga hatua hii ya Trump ya kuweka angalau kiwango cha 10% kuendelea mbele kwa bidhaa zote zinazoingia nchini Marekani. Umoja wa Ulaya (EU) na Uingereza zimesema hatua hii kuathiri uchumi wa dunia.
Mkuu wa Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen anasema "matokeo yatakuwa mabaya kwa mamilioni ya watu duniani kote" na anaongeza kuwa Ulaya inakamilisha mpango wake wa kwanza wa kukabiliana na ushuru wa chuma (Marekani tayari ilikuwa imeweka ushuru wa 25% kwa chuma na aluminiamu ya EU, kabla ya tangazo la sasa).
China yenyewe imeahidi "hatua madhubuti za kukabiliana" dhidi ya hatua hiyo.
Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney yeye anasema ni "muhimu kuchukua hatua kwa makusudi na kwa nguvu".
Giorgia Meloni, Waziri Mkuu wa Italia amezitaja ushuru wa Marekani kuwa "mbaya" na kuonya kuwa zinaweza kuzua vita kubwa vya kibiashara.
Waziri mkuu wa Australia, Anthony Albanese anasema "hiki si kitendo cha rafiki".
Kaimu rais wa Korea Kusini Han Duck-Soo anasema "vita vya biashara duniani vimekuwa ukweli".
Dunia imeshtuka, kila mtu anazungumzia hatua za kuchukua za haraka. Bila shaka na mataifa ya Afrika Mashariki na yenyewe yatachukua hatua za haraka.














