Fordo yaanza kujengwa, kuanzisha vita mpya Iran?

Sawiro Dayax Gacmeed

Chanzo cha picha, Maxar

Muda wa kusoma: Dakika 3

Picha za satelaiti zilizopigwa Juni 29 zinaonyesha vifaa na mashine nzito za ujenzi vikifanya kazi katika kituo cha nyuklia cha Fordo nchini Iran, ambacho hivi karibuni kililengwa na mashambulizi ya Marekani.

Huku kazi ya ujenzi ikiendelea, maswali mazito yameibuka kuhusu hatima ya akiba ya uranium iliyorutubishwa sana na kukataliwa kwa wakaguzi wa kimataifa.

Je, ujenzi huu unaweza kuichochea Marekani kushambulia tena na kuibua vita vipya, vikali zaidi katika Mashariki ya Kati?

Picha hizo zinaonyesha magreda yakiendelea na shughuli kwenye barabara mpya ya kuingilia kituo hicho, karibu na eneo lililoshambuliwa na mabomu yenye uwezo wa kupenya ardhini ya Marekani (GBU-57). Chini zaidi mlimani, tingatinga na lori pia vinaonekana vikifanya kazi.

Magari ya ujenzi yameonekana pia kwenye lango la kinu hicho na kwenye jengo lililobomolewa upande wa mashariki wa jengo hilo, ambazo zote ziliharibiwa katika mashambulizi ya Israel siku moja baada ya yale ya Marekani.

Kwa mujibu wa David Albright, mtaalamu wa silaha za nyuklia aliyefanya uchambuzi wa picha za eneo hilo zilizopigwa Juni 28, shughuli hizi za ujenzi zinaweza kujumuisha kuziba mashimo, kufanya tathmini ya uharibifu wa uhandisi, na kuchukua sampuli za mionzi. Hata hivyo, Rais wa Marekani Donald Trump alidai baada ya mashambulizi hayo kwamba vituo muhimu vya urutubishaji nyuklia vya Iran "vimeangamizwa kabisa."

Kauli hii inapingana na maelezo ya Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA), ambaye alibainisha Ijumaa kuwa "baadhi" ya vituo vya nyuklia vya Iran "bado vipo," na kwamba Iran inaweza kuanza tena urutubishaji wa urani "ndani ya miezi michache au hata chini ya hapo." Ingawa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imekiri uharibifu mkubwa, maelezo kamili bado hayajulikani.

Nini hatma ya akiba ya uranium iliyorutubishwa?

s
Maelezo ya picha, Magari ya ujenzi yakiendelea na ukarabati wa kasi kinu cha Fordo, moja ya maeneo muhimu ya kurutubisha nyuklia Iran, yaliyoshambuliwa na Marekani

Swali jingine muhimu ni hali ya takriban kilogramu 408 za akiba ya uranium iliyorutubishwa sana ambayo serikali ya Marekani inadai imezikwa ndani ya kituo cha Fordo.

Ingawa Iran, katika barua kwa IAEA siku ya kwanza ya shambulio la Israel, ilisema imechukua hatua "maalum" kulinda nyenzo hii, Bw. Grossi ameeleza kutojua mahali ilipo. "Hatujui vifaa hivi vinaweza kuwa wapi," Bw. Grossi aliiambia CBS, akiongeza, "Baadhi yake yanaweza kuwa yameharibiwa katika shambulio, lakini baadhi yake yanaweza kuwa yamehamishwa kwenda eneo jingine. Kwa hivyo hatimaye, hilo linapaswa kubainishwa."

Hali inazidi kuwa tata kutokana na hatua ya serikali ya Iran kusitisha kisheria ushirikiano na IAEA. Tehran imekataa ombi la Bw. Grossi kutembelea maeneo yaliyoathirika, hasa Fordo. "Tunahitaji kuweza kuelewa kinachoendelea, viko wapi na nini kilitokea," Bw. Grossi alisisitiza.

Licha ya hayo, Donald Trump anasisitiza kuwa vituo vya nyuklia vya Iran vimeharibiwa, na kwamba kuhamisha vifaa hivi ni kazi ngumu sana, na Iran haikupata muda wa kutosha.

Kinu ama Kituo cha Fordo kina sifa gani?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kituo cha urutubishaji uranium cha Fordo kiko kilomita 96 kusini mwa Tehran, katika eneo la milima karibu na mji wa Qom. Kilijengwa ndani ya mapango marefu katika milima ya kaskazini mwa Iran isiyofikika kwa urahisi, Fordo awali ilikuwa safu ya vichuguu vya chini ya ardhi vilivyotumiwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Baada ya kufichuliwa na mashirika ya kijasusi ya Magharibi, Iran ilithibitisha rasmi kuwepo kwa kituo hicho cha urutubishaji mwaka 2009. Fordo imeundwa kuhifadhi takriban centrifuges 3,000 ambazo zinastahimili mashambulizi ya anga.

Chini ya Mkataba wa Pamoja wa Mpango Kazi Kamili (JCPOA), Iran ilikubali kubadili Fordo kuwa kituo cha utafiti na kusitisha shughuli za urutubishaji uranium kwa miaka 15.

Hata hivyo, baada ya Marekani kujiondoa kwenye mkataba huo, Iran ilianza tena shughuli za urutubishaji uranium katika kituo hicho, ikiongeza hadi asilimia 20 kufikia mwaka 2021, na mnamo Novemba 2022, iliongeza kiwango cha urutubishaji hadi 60%, ikitangaza nia yake ya kuongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wake wa urutubishaji.

Kituo cha Fordo pia kinajulikana kama "Shahidi Alimohammadi," kwa heshima ya Masoud Alimohammadi, profesa wa fizikia katika Chuo Kikuu cha Tehran na, kwa mujibu wa maafisa na vyombo vya habari vya Iran, mmoja wa "wanasayansi wa nyuklia" waliouawa Januari 2009 kaskazini mwa Tehran.

Marekani na Israel hawataki kiwepo, Je kuibua mgogro mwingine?