Wairani kumgeuka Khamenei? Wahoji ukimya wake wakati Iran ikishambuliwa

Ayatollah Khamenei

Chanzo cha picha, leader.ir

    • Author, Monitoring section
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Wakati serikali ya Iran tangu ianze kukabiliwa na moja ya mapigano yake makubwa na hatari zaidi ya kijeshi dhidi ya Israel, Ayatollah Ali Khamenei, kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu, hajaonekana hadharani kwa muda sasa.

Kutoonekana kwake hadharani na kuwa mstari wa mbele kwenye mgogoro dhidi ya Israel umewafanya raia na viongozi kuhoji nafasi yake kama Kiongozi Mkuu wa taifa na Amiri Jeshi Mkuu.

Japo kuna usitishwaji wa mapigano kwa siku kadhaa sas akama ilivyotangazwa na Rais wa Marekani Donald Trump, bado hajaonekana hadharani zaidi ya video na sauti tu.

Ujumbe wake wa kwanza kupitia video baada ya kutangazwa kwa usitishaji mapigano na Israel uliotolewa baada ya siku kadhaa za ukimya haukufuta mashaka, bali uliibua maswali mapya zaidi.

Ukimya wakati wa vita na usitishaji mapigano

Tarehe 18 Juni, alitoa ujumbe mkali kwa Marekani akimjibu Donald Trump. Ujumbe huo uliambatana na picha moja tu na sauti ambayo inasemekana kuwa na marudio ya maneno, ishara kwamba huenda uliandaliwa katika mazingira ya kutatanisha au ya siri.

Baada ya hapo, Marekani ilishambulia vinu vya nyuklia vya Iran, huku Iran ikijibu kwa makombora dhidi ya kambi ya kijeshi ya Marekani huko Qatar.

Licha ya maendeleo hayo makubwa, hakukuwa na tamko lolote kutoka kwa Khamenei. Hata Baraza Kuu la Usalama wa Taifa lilitoa taarifa ya usitishaji mapigano bila kumtaja kiongozi huyo, jambo lisilo la kawaida kwa mujibu wa Ibara ya 110 ya Katiba ya Iran inayompa mamlaka kamili ya vita na amri ya mwisho ya kijeshi.

Mnamo Juni 26, baada ya wiki ya ukimya, Ayatollah Khamenei alijitokeza tena katika video nyingine, safari hii akionekana kutoka upande mmoja tu, na akizungumzia "ushindi dhidi ya Israel", akiepuka kabisa maneno kama "usitishaji mapigano" au "makubaliano".

Falanqe

Chanzo cha picha, Getty Images

Mazingira ya kisiasa, kiusalama na vyombo vya habari

Ripoti mbalimbali zimeeleza kuwa Khamenei alijificha na kukata mawasiliano ya kielektroniki ili asifuatiliwe. Msaidizi wake, Mehdi Fazaeli, alithibitisha kwa njia isiyo ya moja kwa moja kuwa yuko "mahali salama".

Hata hivyo, viongozi wa serikali wameendelea kukwepa kueleza afya yake, alipo, na jinsi maamuzi makubwa yanavyofanyika bila yeye kuonekana.

Wachambuzi wengine wanaona ukimya huu kama mkakati wa kisiasa akijiepusha kuhusishwa moja kwa moja na usitishaji mapigano ambao unaweza kuonekana kama kushindwa.

Wanadai kuwa Khamenei ana historia ya kukaa kimya wakati wa majaribu makubwa.

Mitandao ya kijamii imejaa kejeli na uvumi wengine wakisema "amejificha kitaifa", au hata kufa, huku wengine wakitaja kuwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) limechukua nafasi yake.

Sawirka Khamenei

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Vyombo vya habari vya Israel na nadharia za mwisho wa utawala wake

Wakati huo huo, vyombo vya habari vya Israel viliripoti kuhusu mshangao wa watu wa karibu na Khamenei.

Ripoti nyingine zilisema anahofiwa kuwindwa na Israel kwa lengo la kumuua.

Channel 14 ya Israel iliuliza, "Je, kiongozi amekimbia?" huku wengine wakihusisha hali hiyo na mipango ya kumpeleka Urusi.

Wachambuzi walidai kuwa kuna wasiwasi kuhusu afya ya akili ya Khamenei na mjadala umeanza kuhusu mrithi wake anayesemekana kuwa kijana na mkali zaidi.

Kutoonekana hadharani kwa Khamenei katikati ya vita hii ni ujumbe unaoweza kuashiria hali ya sintofahamu juu ya mamlaka yake.