Lesotho yatangaza hali ya janga huku kukiwa na mashaka ya ushuru wa Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images
Lesotho imetangaza hali ya janga la kitaifa kutokana na "kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira kwa vijana na watu kupoteza kazi" huku kukiwa na mashaka kutokana na ushuru wa Marekani.
Lesotho ilikumbwa na ushuru wa juu kuliko nchi nyingine yoyote wa 50% kutoka kwa Rais Donald Trump wa Marekani mwezi Aprili, ingawa ushuru huo umesitishwa kwa sasa.
Naibu Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Nthomeng Majara amesema hali ya janga itaanza kutumika hadi tarehe 30 Juni 2027.
Ukosefu wa ajira nchini Lesotho umefikia 30% lakini kwa vijana kiwango hicho ni karibu 50%, kulingana na takwimu rasmi.
Tamko hilo, kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti Majanga, inaruhusu serikali "kuchukua hatua zote muhimu ili... kupunguza madhara ya maafa" miongoni mwa mengine.
Maafisa nchini Lesotho - nchi yenye zaidi ya watu milioni mbili - wanasema hatua hiyo itaruhusu serikali kuelekeza fedha haraka kwenye programu zinazolenga kuwafanya vijana kufanya kazi na kusaidia uchumi kuimarika.
Idara kadhaa tayari zimetangaza hatua za awali, ikiwa ni pamoja na kufuta ada ya usajili wa biashara kwa waanzishaji wadogo wa biashara na wa kati.
Uchumi wa nchi hiyo unaotegemea nguo ulikuwa unakabiliwa na ukosefu wa ajira uliokithiri, hasa miongoni mwa vijana, hata kabla ya Trump kupunguza misaada na kuweka vikwazo vya kibiashara vya ushuru, kulingana na ripoti ya AFP.
Lesotho ilikuwa ni mojawapo ya wanufaika wakubwa wa Sheria ya Ukuaji na Fursa ya Afrika na Marekani (Agoa), ambayo inatoa fursa nzuri ya kibiashara kwa baadhi ya nchi ili kukuza uchumi wao.
Kulingana na serikali ya Marekani, nchi hizo mbili zilifanya biashara ya bidhaa zenye thamani ya dola milioni 240 (£187m) mwaka 2024, nyingi ya bidhaa hizo zikiwa ni mauzo ya nje kutoka Lesotho kwenda Marekani, hasa nguo.
Ingawa ushuru wa asilimia 50 ulisitishwa, mauzo ya nje ya Lesotho kwenda Marekani bado yanakabiliwa na ushuru wa 10%, kama nchi nyinginezo.
Serikali ya Lesotho imeonya kuwa inaweza kupoteza hadi ajira 40,000 ikiwa Agoa haitarudishwa hadi mwishoni mwa mwezi Septemba, kulingana na AFP.
Waziri wa Biashara wa Lesotho Mokhethi Shelile aliiambia tovuti ya habari ya biashara ya Afrika Kusini, Moneyweb mwezi uliopita kwamba wanunuzi kutoka Marekani "hawafanyi manunuzi kwa sababu hawaelewi kitakachotokea."
Nchi hiyo pia iliathirika pakubwa na kusitishwa kwa programu za Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) duniani kote. Lesotho ni miongoni mwa nchi zilizonufaika na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Ukimwi (Pepfar), uliozinduliwa mwaka 2003.
Wakosoaji wanasema mgogoro huu ulikuwa unatarajiwa, kwani hadi mwezi Machi, Lesotho ilikuwa katika hali ya janga ya miezi minane kutokana na uhaba mkubwa wa chakula.
Wakati huo, Waziri Mkuu Sam Matekane alisema karibu raia 700,000 walikuwa wanakabiliwa na njaa kali, iliyosababishwa na ukame wa muda mrefu.
Unaweza kusoma;












