Mfahamu mtu aliyefichua siri za mpango wa nyuklia wa Israel

Chanzo cha picha, Reuters
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema baada ya shambulio dhidi ya Iran: "Tumefanya shambulizi katika moyo wa mpango wa silaha wa Iran."
Shambulio hilo liliacha shaka kidogo kuhusu nia ya vita ya Israeli.
Iran inasisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa amani, lakini Israel kwa miaka mingi imekuwa ikidai kuwa Iran inafuatilia kwa siri mpango wa silaha za nyuklia.
Israel yenyewe inafuata sera ya kutothibitisha wala kukanusha silaha zake za nyuklia, lakini ulimwengu unaamini kuwa Israel inamiliki silaha za nyuklia.
Sababu ya ufichuzi huu inaweza kuhusishwa na mtu mmoja: mtu ambaye ufichuzi wake ulifichua oparesheni za siri za Israeli kuwa nguvu ya nyuklia.
Hatua hii nusura impokonye uhuru wake kwa takriban miongo miwili

Chanzo cha picha, AFP
Vanunu alikuwa mfanyakazi wa zamani wa Kituo cha Utafiti wa Nyuklia cha Dimona, akifanya kazi katika kituo hicho kwa miaka tisa hadi 1985.
Lakini kabla ya kuacha kazi yake, alipiga kwa siri picha za kituo hicho.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Picha zilionyesha vifaa vya kuchimba nyenzo za mionzi kwa utengenezaji wa silaha na maabara ya mfano wa kituo cha nyuklia.
Mnamo 1986, alijiunga na kikundi cha kupinga nyuklia huko Sydney, Australia, ambapo alikutana na mwandishi wa habari wa kujitegemea wa Colombia aitwaye Oscar Guerrero na kumshawishi kuchapisha picha hizo.
Kwa hiyo aliwasiliana na Peter Hunnam, mwandishi wa habari wa gazeti la kila wiki la Uingereza The Sunday Times.
Mnamo Oktoba 1986, gazeti la The Sunday Times lilichapisha makala ambayo ilisifiwa kuwa mojawapo ya sehemu bora zaidi za uandishi wa habari wa Uingereza. Kichwa cha habari kilikuwa: "Imefichuliwa: Siri ya silaha za Nyuklia za Israel."
Chanzo cha makala hiyo ilikuwa fundi wa nyuklia wa Israel Mordechai Vanunu. Ufichuzi wake ulithibitisha shaka juu ya uwezo wa nyuklia wa nchi yake na kuonyesha kuwa mpango wao wa silaha za nyuklia ulikuwa mkubwa na wa juu zaidi kuliko ilivyofikiriwa hapo awali.
Alifanya kazi katika Kituo cha Utafiti wa Nyuklia cha Dimona katika Jangwa la Negev, karibu kilomita 150 kusini mwa Yerusalemu.
Gazeti la kila wiki lilihitimisha kuwa Israel imekuwa nchi ya sita duniani yenye nguvu za nyuklia na inaweza kuwa na hadi vichwa 200 vya nyuklia.
"Tulikuwa na wasiwasi, tulikuwa tumechoka, watu wengi hawakuwahi kuandika habari kubwa kama hiyo hapo awali," ripota wa Sunday Times Peter Hunnam aliambia BBC.
Lakini kufikia siku ambayo Sunday Times ilichapisha habari hiyo - Oktoba 5 - chanzo chao cha asili kilikuwa kimetoweka
Msaliti au mfichuzi?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanahabari wa Sunday Times Peter Hunnam alikutana kwa mara ya kwanza na Mordechai Vanunu huko Sydney, Australia, mwezi wa Agosti mwaka huo na akavutiwa na sura yake.
"Nilipomwona Vanunu, alikuwa mtu mdogo, mwembamba, mwenye upara kiasi, asiyejiamini, aliyevalia kwa njia isiyo rasmi, na kwa hakika si kama mwanasayansi wa nyuklia," Hunnam alisema.
"Lakini alidhamiria kuujulisha ulimwengu kile alichokiona Dimona," aliongeza.
Mwishoni mwa 1985, Vanunu aliamua kuacha kazi yake na kuzuru bara Asia , akiwa amekatishwa tamaa na jinsi Israeli inavyowatendea Wapalestina na kutengeneza silaha za nyuklia.
Kabla ya kuondoka Israel, alipiga picha kutoka ndani ya kituo cha nyuklia, picha zinazoonyesha mashine za kuchimba vifaa vya mionzi kwa ajili ya utengenezaji wa silaha na mifano ya maabara ya vifaa vya thermoelectric.
Uamuzi huu ulimpeleka kwanza London na Sunday Times, kisha Roma na kutekwa nyara na shirika la ujasusi la Mossad, na kisha kurudi Israeli na kifungo cha muda mrefu gerezani.
"Alianza kusimulia kisa chake cha kuvutia sana cha jinsi alivyoleta kwanza kamera bila filamu, kisha baadaye akaficha filamu kwenye soksi yake na kupiga picha kwa siri usiku na mapema asubuhi," alisema ripota wa Sunday Times Peter Hunnam.
Wahariri wa Sunday Times walimhimiza Hunnam kumleta Vanunu London ili kuangalia usahihi wa hadithi yake.
Licha ya wasiwasi, Vanunu alikubali kusafiri kwa ndege hadi Uingereza. Gazeti la Sunday Times lilimweka katika hoteli ya siri nje ya London.
Lakini alihangaika na kuhamishiwa hoteli moja katikati mwa London, ambako jambo ambalo hakulitarajia lilitokea.
"Wikendi hiyo, alikuwa amekutana na mwanamke mmoja mtaani, aliwahi kumuona mara kadhaa na kwenda naye kwenye sinema, nikauliza, 'Una uhakika kuwa huyu mwanamke ni yule unayesema kuwa ndiye?'" Hunnam alisema.
Wakati wa kukaa kwake London, Hunnam alizidi kuwa na wasiwasi kuhusu usalama wa Vanunu na mara kwa mara aliuliza kuhusu ustawi wake.
"Mara ya mwisho Vanunu alisema, 'Nitaenda kaskazini mwa Uingereza kwa siku chache tu, usijali,' na nikasema, 'Chochote utakachofanya, nipigie mara mbili kwa siku ili nihakikishe uko sawa," alisema.
Mwezi mmoja baadaye, serikali ya Israeli ilifichua kwamba Vanunu alikuwa amekamatwa.
Alikuwa amenaswa na mtego wa kutongozwa huko Roma na alichukuliwa na fahamu kwa mashua hadi Israeli.

Chanzo cha picha, Reuters
Akiwa anasafirishwa kutoka gerezani kwa gari la mizigo, aliandika maelezo fulani ya jinsi alivyotekwa nyara kwenye kiganja cha mkono wake na kukishika nyuma ya kioo ili waandishi wa habari waliokuwa wakisubiri waweze kuona taarifa hiyo.
Alisema kuwa huko London, alikuwa na urafiki na wakala wa Mossad mzaliwa wa Amerika aitwaye Cheryl Bentoff, ambaye alijifanya kama mtalii.
Wakala wa Mossad alimdanganya aende Roma kwa siku chache mnamo Septemba 30. Alipofika huko, alitekwa nyara na kupoteza fahamu.
Vanunu alishtakiwa Machi 1987 kwa makosa ya uhaini na ujasusi na akahukumiwa kifungo cha miaka 18 jela. Alitumia zaidi ya nusu ya muda huu katika kifungo cha upweke.
"Nilitaka ulimwengu ujue kinachoendelea… Huu sio uhaini, huu ni kuufahamisha ulimwengu, kinyume na sera za Israel," alisema katika mahojiano yaliyorekodiwa kutoka gerezani.
Aliachiliwa mnamo Aprili 21, 2004, lakini hakuruhusiwa kuondoka Israeli.
Tangu wakati huo, amekamatwa tena mara kadhaa kwa kukiuka masharti ya msamaha wake au kuachiliwa.
"Hujachukua chochote kutoka kwangu kwa miaka 18; hutachukua chochote kutoka kwangu kwa muda wa miezi mitatu! Israel! Aibu kwako," Vanunu alifoka kabla ya kukamatwa tena mwaka wa 2009.
Siri iliofichwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Kabla ya ufichuzi wa Vanunu, kulikuwepo na taarifa kuhusu uwezo wa nyuklia wa Israel, hata miongoni mwa washirika wake wa karibu.
Israel inaaminika kuanza mpango wake wa nyuklia muda mfupi baada ya nchi hiyo kuanzishwa mwaka 1948.
David Ben-Gurion, waziri mkuu wa kwanza wa nchi hiyo, alielewa thamani ya kuzuia nyuklia, lakini hakutaka kuhatarisha uhusiano wa kirafiki na nchi za Magharibi kutokana na kuenea kwa silaha zisizo za kawaida katika eneo lisilo na utulivu.
Hivyo Israel ilifikia makubaliano ya siri na Ufaransa kujenga Dimona, mtambo wa kuzalisha umeme unaoaminika kuwa na ulizalisha wa nyenzo za silaha za nyuklia katika miaka ya 1960. Kwa miaka mingi, Israel ilidai kuwa Dimona ilikuwa kiwanda cha nguo.
Wakaguzi wa Marekani walitembelea kituo hicho mara kadhaa katika miaka ya 1960, lakini waliripotiwa kutofahamu kuwepo kwa vituo vya chini ya ardhi kwa sababu viingilio vya lifti na mahandaki vilifunikwa kwa matofali na plasta.
Kulingana na makadirio ya Kituo cha Kudhibiti Silaha na Kuzuia Kuenea kwa Silaha, Israeli kwa sasa ina vichwa 90 vya nyuklia.
Hata hivyo, nchi hiyo imedumisha sera rasmi ya utata kuhusu uwezo wake wa nyuklia, na viongozi wa Israel wamerudia kusema kwa miaka mingi kwamba "Israel haitakuwa nchi ya kwanza kuanzisha silaha za nyuklia katika Mashariki ya Kati."
Tangu mwaka wa 1970, nchi 191 zimejiunga na Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia, makubaliano ya kuzuia kuenea kwa nyuklia na kuhimiza upokonyaji silaha.
Nchi tano - Marekani, Urusi, Uingereza, Ufaransa na China - zinaruhusiwa kumiliki silaha kwa sababu zilijenga na kufanya majaribio ya mabomu ya atomiki kabla ya Januari 1, 1967.
Israel haijajiunga na mkataba huu.
Huko Israeli, Vanunu anachukuliwa kuwa msaliti, lakini wafuasi wake walimwita "shujaa wa amani" alipoachiliwa mnamo 2004.
Katika mahojiano yake ya kwanza na BBC baada ya kuachiliwa kwake, alisema "hakuwa na majuto."
Aliendelea, "Nilichofanya ni kuujulisha ulimwengu kinachoendelea kwa siri, sikusema tuiangamize Israeli au tuiangamize Dimona, niliwaambia waangalie walichonacho wajihukumu wenyewe.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla












