Kwa nini mbu huuma baadhi ya watu zaidi kuliko wengine?

Chanzo cha picha, WIKIMEDIA COMMONS/CDC/JAMES GATHAN
Mbu na magonjwa wanayobeba yameua watu wengi zaidi katika historia ya binadamu.
Takwimu zinaonyesha kuwa mbu ndiye kiumbe hatari zaidi kwa binadamu ulimwenguni. Mwaka 2018 pekee, wadudu hao walisababisha vifo karibu 725,000.
Hali hii inatia wasiwasi na ilisababisha Baraza la Afya Ulimwenguni katika hafla ya kila mwaka ya kufanya maamuzi la Shirika la Afya Duniani (WHO) kuidhinisha mwaka Mwitikio wa Kimataifa wa Udhibiti wa Vekta (GVCR) 2017-2030. Hii ni hatua inayolenga kuelekeza nchi kimkakati ili kuimarisha udhibiti wa wadudu, miongoni mwao mbu wakiwemo.
Maamuzi hayo ni muhimu kwa kuzuia magonjwa na kukabiliana na milipuko ya kuambukiza inayoibuka. Baada ya yote, mbu wanaweza kusambaza magonjwa mengi, kama vile West Nile fever, Zika, dengue, homa ya manjano, chikungunya, maambukizi ya virusi vya Semliki, homa ya Sindbis, na malaria ambayo ilisababisha vifo 627,000 kwa mwaka 2020 pekee
Lakini unafahamu ni kwanini mbu huamua kuuma watu fulani na na sio mtu aliye karibu nawe.
Carbon dioxide na harufu ya mwili
Mbu, dume na jike, wanaweza kuishi bila kuuma wanyama wengine. Lakini wanawake wanahitaji damu ili kukamilisha mzunguko wao wa uzazi.
Karibu karne moja iliyopita, hewa ya kaboni (CO2) ilitambuliwa kuwa ni ya kuvutia kwa mbu. Na gesi hiyo ilitumiwa kukamata mbu jike ambao hutafuta damu inayohitajika kupata virutubisho kwa oogenesis yaani kizazi cha mayai.
Lakini hakuna ushahidi unaonesha kuwa CO2 hutumiwa kama kipimo cha tofauti cha kivutio. Pia, viwango vya utoaji wa kaboni havielezi kwa nini mbu hupendelea mtu mmoja kuliko mwingine. Sababu ni nini basi?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kuna ishara nyingine za kemikali zinazoathiri mvuto wa mbu kwa watu fulani, hasa joto, mvuke wa maji, unyevunyevu, ishara za mwanga na muhimu zaidi harufu zinazotolewa kupitia ngozi ya binadamu.
Bado haijajulikana kwa uhakika ni harufu zipi zinazovutia mbu zaidi, lakini tafiti kadhaa zinaonyesha molekuli kama vile indole (harufu iliyopo kwenye lami ya makaa ya mawe na kwenye kinyesi), nonanol, octenol na lactic asidi kama washukiwa wakuu.
Watafiti wanaoongozwa na Matthew DeGennaro wa Chuo Kikuu cha Florida nchini Marekani kimetambua kipokezi cha kipekee cha harufu kinachojulikana kama kipokezi cha ionotropic 8a (IR8a), ambacho humruhusu mbu aina ya Aedes aegypti kutambua lactic acid Kama inavyojulikana, mbu huyu ndiye msambazaji wa dengue, chikungunya na zika.
Wanasayansi walipobadilisha kipokezi cha IR8a, kilichopatikana kwenye antena za wadudu, waligundua kuwa mbu hawakuweza kutambua asidi ya lactic na harufu zingine za asidi zinazotolewa na binadamu.

Chanzo cha picha, SHUTTERSTOCK/KHLUNGCENTER
Acetophenone: 'manukato' ambayo huvutia mbu
Utafiti wa hivi karibuni umeonyesha kuwa virusi vya dengue na zika hubadilisha harufu ya panya walioambukizwa na binadamu ili kuwavutia zaidi mbu. Ni mkakati wa kuvutia, kwani umesaidia wadudu kuuma mtu husika, kutoa damu yao iliyoambukizwa na kusafirisha virusi kwa mtu mwingine.
Virusi vinaweza kufanya hivyo kwa kurekebisha utoaji wa ketone yenye harufu nzuri - acetophenone ambayo inavutia sana mbu.
Kwa kawaida, ngozi ya binadamu na panya hutoa mfumo wa kinga ya asili ambayo hupunguza idadi ya bakteria. Lakini imeonyeshwa kuwa, katika panya walioambukizwa dengue au zika, mkusanyiko wa peptidi hupunguzwa na bakteria ya jenasi Bacillus huongezeka ambayo huamsha uzalishaji wa acetophenone.
Kwa binadamu, Uhalisia sawa ulitokea: harufu zilizokusanywa kutoka kwa makwapa ya wagonjwa wa dengue zilikuwa na acetophenone zaidi kuliko za watu wenye afya.
Jambo la kuvutia ni kwamba hii inaweza kurekebishwa. Baadhi ya panya walioambukizwa dengue walitibiwa na dawa ya isotretinoin, ambayo ilipunguza utoaji wa acetophenone. Matokeo yake, panya hawakuvutia wadudu.
Viini vinavyobadilisha harufu
Hii sio kesi pekee ambayo viumbe vidogo wanabadili fiziolojia ya mbu na binadamu ili kupata maambukizi yao.
Watu walioambukizwa na vimelea vinavyosababisha malaria, Plasmodium falciparum, kwa mfano, wanavutia zaidi kuliko watu wenye afya nzuri kwa mbu Anopheles ambao ni waenezaji wa ugonjwa huo.
Sababu bado haijulikani, lakini inaweza kuhusishwa na ukweli kwamba Plasmodium falciparum hutoa kitangulizi cha isoprenoid inayoitwa (E) -4-hydroxy-3-methylbut-2-enyl pyrophosphate (HMBPP). Kitangulizi hiki huathiri tabia ya mbu ya kutafuta damu na kulisha pamoja na uwezekano wake wa kuambukizwa.
Kwa hakika, HMBPP inawasha seli nyekundu za damu za binadamu ili kuongeza kutolewa kwa CO2, aldehydes na monoterpenes, ambayo kwa pamoja huvutia mbu kwa nguvu zaidi na kuja "kunyonya damu yetu".
Kuelewa ni mambo gani yanayosababisha mbu kuuma mtu fulani na kumuacha mwingine itasaidia kuamua na kupunguza hatari ya kueneza magonjwa ya kuambukiza yanayoambukizwa na wadudu















