Diogo Jota na André Silva wazikwa

Chanzo cha picha, Reuters
Wachezaji kandanda Diogo Jota na André Silva wamepewa heshima zao za mwisho na familia zao, marafiki na wachezaji wenzao kwenye mazishi ya pamoja nchini Ureno.
Jota, 28, alizikwa pamoja na kaka yake, Silva, 25, baada ya kufariki kwenye ajali ya gari siku ya Alhamisi.
Maafisa wanasema gari lao lilitoka nje ya barabara kutokana na tairi kupasuka huku likipita gari jingine.
Habari hizo ziliuacha ulimwengu wa soka katika mshtuko huku wengi wakiacha risala zao za rambirambi katika vilabu ambavyo alikuwa amecheza.
Jota alikuwa njiani kurejea Liverpool kwa ajili ya mazoezi ya kabla ya msimu mpya, akisafiri kwa gari na feri kwa sababu alikuwa amefanyiwa upasuaji mdogo hivyo madaktari walimshauri asisafiri kwa ndege.
Alikuwa ameoa mpenzi wake wa muda mrefu Rute Cardoso, ambaye alizaa naye watoto watatu, siku 11 tu zilizopita.

Chanzo cha picha, Getty Images
Waombolezaji walihudhuria mazishi ya ndugu hao katika mji wa kwao Gondomar siku ya Jumamosi huku wachezaji wa Diogo Jota wakiungana na jamaa zake kuomboleza nyota huyo wa Liverpool na mamia ya wengine wakikusanyika nje ya Igreja Matriz kumuaga.
Watu walisimama kimya barabarani walipokuwa wakisikiliza matangazo ya sauti ya ibada ya mazishi, aliandika ripota wa michezo Matt Graveling.
Wakati huo huo, mashabiki waliokuwa na huzuni walimweleza ripota wetu Sofia Ferreira Santos kwamba kushuhudia ibada hiyo ilikuwa jambo gumu sana kwao lakini muhimu kuhudhuria.
Kwa meneja wa Liverpool Arne Slot, "Diogo hakuwa mchezaji wetu pekee. Alikuwa mpendwa wetu sote. Alikuwa mchezaji mwenzetu, mfanyakazi mwenza, mshirika mwenzetu na katika majukumu yote hayo alikuwa wa pekee sana" - hisia zilizorudiwa na wengine wengi waliojitokeza katika siku chache zilizopita.

Chanzo cha picha, Getty Images
Hata baada ya ibada ya Gondomar kukamilika watu waliendelea kuingia katika makaburi ya kanisa hilo ambako awali kulifanyika ibada ya faragha ya maziko ya ndugu wawili.
Katika lango la kuingia eneo hilo, kuna mfano wa fulana mbili nyekundu zilizotengenezwa kwa maua – ikiwa ni ishara ya heshima zilizoletwa kanisani hapo awali na wachezaji wa Liverpool Virgil Van Dijk na Andy Robertson.
Zinaonyesha nambari 20 na 30, zinazovaliwa na Diogo na André.
Kuna kadi ndogo, iliyo na ujumbe kutoka kwa Klabu ya Soka ya Liverpool, ambayo inaisha kwa maneno: "Hautawahi Kutembea Peke Yako."
Huku barabara za Gondomar zikiwa hazina tena wageni na kurejea tena kwa hali yake ya kawaida, hilo linatokea bila wanawe wawili mashuhuri.
Kipindi kifupi na cha kusisimua akiichezea Liverpool

Chanzo cha picha, Getty Images
Ndani ya miaka mitano ya kujiunga na Reds, Jota, ambaye anacheza nafasi ya winga na mshambuliaji, amejidhihirisha kuwa mchezaji muhimu wa Liverpool, chini ya kocha Mjerumani Jürgen Klopp na kisha Mholanzi Arne Slot.
Alichukua jukumu muhimu katika mafanikio ya Wekundu hao katika miaka ya hivi karibuni, haswa katika safari yao ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita.
Alifunga mabao tisa katika michuano yote msimu uliopita, huku Liverpool ikitwaa taji lao la 20.
Alifunga mabao 65 katika maisha yake ya soka akiwa na Liverpool, akishinda taji la Premier League mwaka 2025, Kombe la FA na Kombe la EFL msimu wa 2022, na kumaliza mshindi wa pili katika Ligi ya Mabingwa 2022.
Akiwa na timu ya taifa ya Ureno
Jota ameichezea Ureno katika viwango vya chini ya miaka 19, 21 na chini ya miaka 23.
Alionekana kwa mara ya kwanza akiwa na timu ya kikosi cha kwanza mnamo 2019.
Ureno pia ilishinda UEFA Nations League kwa mara ya pili, ikiishinda Uhispania kwa mikwaju ya penalti baada ya sare ya kusisimua kwenye fainali Jumapili, Juni 8, 2025.
Alitwaa ubingwa akiwa na timu ya taifa ya nchi yake kwa mara ya kwanza msimu wa 2018/19.
Jota alicheza kama mshambuliaji wa Ureno na alicheza karibu mechi 50 katika timu ya taifa. Takwimu zinaonyesha kuwa aliifungia nchi yake mabao 14 wakati wa maisha yake mafupi.
Alishinda taji la Ubingwa wa Uingereza akiwa na Wolverhampton Wanderers msimu wa 2017/18, ambapo ilikuwa daraja la pili la soka la Uingereza.










