Mzozo wa kibiashara kati ya Marekani na China: Afrika itaathirika vipi?

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 6

Rais wa Marekani Donald Trump amechukua hatua ya kwanza katika kile ambacho wengi wanakielezea kama vita vya kibiashara na baadhi ya washirika wakubwa wa kiuchumi nchini humo.

Ingawa Rais Trump alisitisha tisho lake la kuongeza ushuru kwa Mexico na Canada siku ya Jumatatu, akikubali kusitisha kwa siku wa 30 kwa ajili ya makubaliano na nchi hizo mbili jirani ya kuimarisha ulinzi wa mipaka na kukomesha uhalifu, Marekani imeanza kuweka ushuru wa asilimia 10 kwa bidhaa zote zinazoingizwa kutoka China.

Huku wengi wakiamini kuwa hatua hizo za Marekani zinaweza kuwa ni hatua za kuanzisha vita vya kibiashara, wachambuzi kote barani Afrika wamekuwa wakitathmini ni wapi hatari hizo zinaweza kuwa katika bara la Afrika kwa kile kinachoweza kuwa kipindi cha msukosuko kwa uchumi wa dunia.

Nigeria, Kenya, Ghana, Angola na Afrika Kusini ni miongoni mwa washirika wakuu wa kibiashara wa Marekani barani Afrika zikiwa na biashara kubwa za bidhaa na huduma za pande mbili.

Kwamujibu wa Ofisi ya Muwakilishi wa biashara wa Marekani, mnamo 2022, uagizaji wa bidhaa kutoka Afrika Kusini ulifikia thamani ya dola bilioni 14.6, na bidhaa ikiwa ni pamoja na lulu, mawe ya thamani, na chuma kutoka Afrika Kusini. Bidhaa nyingine kama dhahabu, kakao, uranium, aluminium, chuma na bidhaa nyingine zilitoka nchi nyingine za Afrika ikiwa ni pamoja na Ghana, Ivory Coast, Gambia na Senegal.

Katika mwaka huo huo, nchi yenye idadi kubwa ya watu barani Afrika, ilisafirisha bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 4.8 kwenda Marekani, ambazo ni mafuta ghafi, kakao, chakula cha kilimo miongoni mwa mengine, wakati ikiagiza magari, mashine, na mafuta yaliyosafishwa kutoka kwa kampuni kubwa ya kiuchumi.

Kiasi hiki cha biashara kinaweza kushuka kwa kiasi kikubwa ikiwa Rais Trump hatasitisha ushuru wa biashara kwa washirika wake wa biashara wa Afrika.

Nchi za Afrika kwa sasa zinafurahia faida za sheria ya ukuaji na fursa za Afrika (AGOA); Sheria ya biashara ya Marekani ambayo inaziruhusu nchi za kusini kwa Jangwa la Sahara kusafirisha bidhaa kwenda Marekani bila kulipa ushuru.

Sheria hiyo iliyosainiwa mwaka 2000 na Rais Bill Clinton imefanyiwa marekebisho, hivi karibuni mwaka 2015. Kwasababu ya kumalizika Septemba 2025, Sheria ya Uboreshaji wa AGOA ya 2024 inayopendekeza kuongezwa kwa ushirikiano huo hadi 2041 haikupitishwa na Rais Joe Biden kabla ya kuondoka madarakani.

Kuna hofu miongoni mwa baadhi ya watu barani Afrika kwamba huenda Rais Trump asiunge mkono kurefushwa kwa muswada huo kama sehemu ya sera zake za kiuchumi za 'Marekani Kwanza'.

"Mara tu ushuru unapoanzishwa baada ya kumalizika kwa sheria ya AGOA, biashara za Afrika (SMEs) zitaathirika." Obiora Madu, Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Afrika cha Ugavi aliiambia BBC.

h

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

AGOA kwasasa inaruhusu nchi 32 za Afrika zinazostahiki kuuza bidhaa nyingi za kilimo, ngozi, vipuli vya magari, kemikali, divai, chuma na nyinginezo.

Kuanguka kwa uchumi kunakotarajiwa kutokana na hili kunaweza kusababisha kupungua kwa Pato la Taifa (GDP) - kipimo cha kitengo cha mapato ya nchi, miongoni mwa nchi za Afrika. Umoja wa Mataifa ulikadiria ukuaji wa pato la taifa la asilimia 3.7 mwaka 2025, kutoka asilimia 3.4 mwaka 2024 wakati Benki ya Maendeleo ya Afrika ikikadiria ukuaji wa asilimia 4.2 mwaka huu, kutoka asilimia 3.8 mwaka jana. Kupungua kwa biashara kunaweza kusababisha kushuka kwa ukuaji.

Wachambuzi pia wanatathmini athari zinazoweza kutokea kwa Afrika kutokana na ushuru ushuru wa juu wa Trump kwa chumi wa China.

China imetangaza hatua za kulipiza kisasi dhidi ya hatua ya Rais Trump, ambapo ushuru wa asilimia 15 utatozwa kwa makaa ya mawe ya Marekani, gesi asilia na magari. Beijing pia imedokeza nia yake ya kuwasilisha malalamiko katika Shirika la Biashara Duniani.

Katika miaka ya hivi karibuni, China imeongeza uwepo wake wa kibiashara barani Afrika, na kuwa mshirika mkubwa wa kibiashara wa bara hilo hadi kufikia rekodi ya juu ya biashara ya thamani ya dola bilioni 282 mwaka 2023.

Nchi hiyo inaagiza malighafi kama madini na mafuta ya visukuku kutoka Afrika huku ikipekeka bidhaa zake za viwandani katika bara hilo.

Nigeria bado ni soko kubwa la bidhaa za China barani Afrika ambapo kuna hofu kuwa kikwazo katika soko la Marekani huenda kikailazimisha China kulijaza soko la Afrika kwa bidhaa zake.

"China inaweza kuanza kufurika bara la Afrika (Afrika) na bidhaa za China haraka na kuifanya Afrika kuwa eneo la kutupa bidhaa zake, na kuhatarisha kiuchumi wazalishaji wetu wa ndani." Dele Ayemibo, mtaalamu wa masuala ya biashara ameiambia BBC.

Baadhi ya nchi za Afrika kwa muda mrefu zimekuwa zikipambana na uingiaji wa bidhaa za kiwango cha chini zinazoingia katika masoko yake kutoka Asia, licha ya juhudi za mifumo ya udhibiti wa ndani ili kuzuia tabia ya kutupa bidhaa za viwango vya chini barani, bara hilo linaendelea kupata hasara kubwa kutokana na tabia hiyo.

Makundi kadhaa ya sekta binafsi yamezitaka serikali za Afrika kujikita katika vita vya kibiashara vinavyoendelea na kuangalia ndani ya bara hilo kwa kuwawezesha wazalishaji wa ndani, kuhamasisha kuongeza thamani kwa malighafi na kukuza biashara miongoni mwao.

Mkataba wa biashara huria wa bara la Afrika, AfCFTA haujatekelezwa kikamilifu tangu ulipoanzishwa takriban miaka mitano iliyopita. Upungufu wa miundombinu, vikwazo vya kibiashara, mitandao duni ya usafirishaji, na vituo vya mipakani vimezuia utekelezaji wa AfCFTA, ikihitaji mabilioni ya dola ya uwekezaji kuwa yenye ufanisi.

"Uchumi wa Afrika unapaswa kuongeza utekelezaji wa makataba wa AfCFTA. Wanahitaji kukuza kiwango cha biashara na kuifanya ifanye kazi." Obiora Madu aliongeza.

Muungano wa nchi kadhaa zilizoanzishwa na Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini unaofahamika kama BRICS wenye lengo la kukuza uhusiano wa kiuchumi kati ya wanachama na kupunguza ushawishi wa dola ya Marekani kama biashara kubwa na sarafu ya akiba. Mataifa mengine ya Afrika ambayo yamesajiliwa ni pamoja na Misri, Ethiopia, Nigeria, Algeria na Uganda.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Wiki iliyopita, Rais Donald Trump alizionya nchi wanachama wa BRICS dhidi ya kuchukua nafasi ya dola ya Marekani kama sarafu ya akiba kwa kurudia tishio la ushuru wa asilimia 100 alilololitoa wiki kadhaa baada ya kushinda uchaguzi wa rais wa Novemba.

"Tutahitaji ahadi kutoka kwa nchi hizi zinazoonekana kuwa na uhasama kwamba hazitaunda sarafu mpya ya BRICS, wala kurudisha sarafu nyingine yoyote kuchukua nafasi ya dola ya Marekani yenye nguvu au, watakabiliwa na ushuru wa 100%," Rais Trump alisema katika taarifa.

"Hakuna nafasi kwamba BRICS itachukua nafasi ya dola ya Marekani katika biashara ya kimataifa, au mahali pengine popote, na nchi yoyote inayojaribu kusema hello kwa Ushuru, na kwaheri kwa Amerika!," aliongeza.

Nchi za Afrika zina hatari ya kurekodi mapato ya chini ya mtaji kutokana na viwango vya juu vya riba vilivyoletwa na Marekani, kama njia ya kupunguza mfumuko wa bei.

Sarafu za ndani ikiwa ni pamoja na Naira ya Nigeria, Rand ya Afrika Kusini na Shilingi ya Kenya zinaweza kuwekwa chini ya shinikizo, na kudhoofisha nguvu ya sarafu hizo za ununuzi wa bidhaa za kigeni.

Vita vya kibiashara pia vinatoa fursa kwa nchi za Afrika. Kutokana na kuvurugika kwa biashara , nchi zenye chumi zinazoongoza zinaweza kugeuza njia yake ya usafirishaji wa bidhaa zake kupitia Afrika kuelekea Marekani na kinyume chake, na hivyo kutoa fursa kwa kutoa kuunda ushirikiano mpya na kuongeza mauzo yake ya nje.

Hata hivyo, mapambano yanayoendelea yanayozikabili nchi hizi zinazoendelea ni kizuizi kinachoziba mwanga wa fursa katikati ya vita vya biashara kati ya wakubwa, kuwazuia kuvuna tuzo ambazo zinaweza kuwa zao.

"Afrika itafaidika tu na vita hii ya kibiashara ikiwa wataamka na kurekebisha mifumo yao." Bwana Ayemibo alisema.

g

Chanzo cha picha, Getty Images

g

Chanzo cha picha, Getty Images

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi