Maswali matano kuhusu uchumi wa China yajibiwa

Three cargo ships sail on Huangpu River in China's financial centre Shanghai

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Soko la hisa la China limeshuka chini zaidi mwaka huu kwa kipindi cha miaka mitano
    • Author, Yan Chen
    • Nafasi, BBC

Tangu China ilipoanza kufungua na kurekebisha uchumi wake mwaka 1978, ukuaji wa Pato la Taifa umekuwa wastani wa 9% kwa mwaka.

Wakati janga la Covid-19 liliposababisha uharibifu wa uchumi wa kimataifa, China ilirikodi ukuaji wa chini zaidi wa 2.2% mwaka 2020.

Ukuaji uliongezeka mwaka uliofuata kwa 8%, lakini mwaka 2022 ulishuka na kukuwa kwa 3%.

Pia unaweza kusoma

Kupanda na kushuka kwa uchumi wa China

China ilitangaza mwezi Januari uchumi wake umekuwa kwa 5.2% mwaka 2023. Lakini ndani ya nchi, watu wana maoni tofauti; ukosefu wa ajira kwa vijana ulifikia rekodi ya juu zaidi ya 20% mwezi Juni mwaka jana na soko la hisa lilipungua chini zaidi kwa miaka mitano mapema mwaka huu.

Idadi ndogo ya Wachina waliokuwa na hasira walieleza kuhusu kudorora kwa uchumi wa nchi yao kwenye akaunti zao za Weibo.

Mtumiaji mmoja alikuwa akiomba usaidizi baada ya kukosa ajira kwa muda mrefu na kuwa na deni. Chapisho lingine lilikuwa kuhusu kupoteza pesa kwenye soko la hisa.

Lakini maoni mengi yalifutwa baadaye, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Magharibi.

Lynn Song, mchumi katika benki ya Uholanzi ya ING, anasema ''China ni tofauti na nchi nyingi, haikuwa imetumia sera kali ili kuchochea ukuaji."

A bar chart showing GDP per capital and GDP growth rate of China, US, Japan, Germany and India in 2022
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Song anaeleza: “Sera ya uchumi ya China imepoa. Mfumuko wa bei haujawa tatizo nchini China, lakini uchumi unaimarika polepole mno.”

Wang Tao wa benki ya uwekezaji ya UBS anaeleza sababu nyingine juu ya ufufuaji dhaifu wa uchumi:

"Zaidi ya 60% ya utajiri wa China uko kwenye makazi na ardhi. Bei za nyumba zinaposhuka, watu hawatumii sana pesa, hasa watu wa tabaka la kati. Kwa mfano, matumizi ya vifaa vikubwa yamepungua sana," aliongeza.

Matatizo katika soko hilo yana athari kubwa kwani sekta hiyo inachangia theluthi moja ya uchumi.

Sekta hiyo imekuwa ikikabiliwa na mkwamo mkubwa wa kifedha tangu 2021, wakati China ilipoanzisha hatua za kupunguza kiwango cha kukopa kwa kampuni kubwa za majengo.

Kwa miaka mingi, sekta hii imechangisha fedha kwa ajili ya miradi mipya kwa kukopa kutoka benki, kutoa dhamana na kuuza nyumba mpya kwa wanunuzi.

Serikali za mitaa, ambazo zimekopa mabilioni ya fedha kwa ajili ya kujenga miundombinu na kutegemea mauzo ya ardhi kuleta mapato, pia zimekuwa kwenye matatizo yanayoongezeka.

Hata hivyo, kwa Tianchen Xu, mwanauchumi katika taasisi ya Economist Intelligence Unit, anasema, "kwa hakika uchumi wa China hauko katika shida."

Uchumi wa China utaipiku Marekani?

China ilipokuwa nchi ya pili kwa uchumi mkubwa mwaka 2010, kwa ukubwa wa Pato la Taifa, ilitabiriwa itazidi uchumi wa Marekani, huku wengi wakiamini ni suala la muda tu kabla hilo kutokea.

Kabla ya kushuka, makadirio ya China kuipiku Marekani yalikuwa yatokee 2028, wengine wakiamini itakuwa ni 2032.

Lakini sasa China inabakiliwa na hali ya kutokuwa na uhakika juu ya uchumi wake. Je, bado inaweza kuipiku Marekani?

Overgrown grass in front of a few unfinished residential blocks in Hebei Province in China [February 2024]

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Wachina wengi wamelipia makaazi ambayo bado hayajajengwa au kumalizwa

"Ndiyo, lakini si kwa miaka ya hivi karibuni," Prof Li Cheng, mkurugenzi mwanzilishi wa kituo cha Contemporary China and the World (CCCW) katika Chuo Kikuu cha Hong Kong.

Xu anatoa jibu la moja kwa moja, anasema ni mwaka 2040.

Prof Li anaeleza kuwa Marekani inakabiliwa na hali ya sintofahamu, ikiwa ni pamoja na matokeo ya uchaguzi wake wa urais baadaye mwaka huu.

"Lakini habari mbaya kwa China ni jamii yake inayozeeka. Kwa kulinganisha, Marekani ina kiwango cha juu cha vijana kuliko China na Marekani ina idadi ya wahamiaji ambayo huongeza nguvu kazi.

Uchumi wa China na mvutano na Taiwan

Song anaamini mtazamo hasi unashusha uchumi - ukosefu wa imani hupunguza uwekezaji na matumizi, pia hupunguza faida kwa kampuni.

Wengine wanahofia kwamba Rais Xi Jinping wa China anaweza kuivamia Taiwan. China inaiona Taiwan inayojitawala kama jimbo lililojitenga ambalo hatimaye litakuwa chini ya udhibiti wa Beijing.

Prof Li anaseme “mtu yeyote anayetaka vita dhidi ya Taiwan, iwe watunga sera nchini China, Marekani au Taiwan, anapaswa kufikiri kwa makini, vita hivi vitakuwa tofauti na Ukraine".

A line chart showing China's annual GDP growth rate from 1978 to 2023

"Hii vinaweza kuwa vita vya kwanza vya akili bandia. Itakuwa vita vya teknolojia ya hali ya juu na silaha nzito nzito.

"Taiwan ni suala muhimu kwa China, lakini uongozi wa China pia unatambua kuwa vita ni suluhisho la mwisho kabisa - na kudorora kwa uchumi sio sababu ya kutosha ya kuingia vitani."

Kudorora kutaathiri vipi uchumi wa dunia?

Xu anaamini itaathiri dunia kwa njia tatu; bidhaa, utalii wa China na siasa za kijiografia.

"Kwanza, kwa kuwa China ni muagizaji mkuu wa bidhaa, kushuka kwake kunamaanisha upatikanaji wa bidhaa utakuwa mdogo hasa zile zinazotumika katika ujenzi.

"Pili, kupungua kwa watalii nchini China itakuwa hasara kwa maeneo ya utalii.

"Tatu, kushuka uchumi - haswa ikiwa kunaambatana na shida ya kifedha nyumbani - kutazuia ushawishi wa China katika siasa za jiografia kupitia misaada na ukopeshaji."

Katika muongo uliopita, China ilianzisha uwekezaji na miradi ya miundombinu. Ilitia saini mikataba na nchi 152 na kuwekeza katika miradi zaidi ya 3,000.

Lakini wakosoaji wameeleza kuwa miradhi hiyo ilisababisha "mitego ya madeni," na China ikawa mkopeshaji mkuu kwa nchi nyingi za kipato cha chini au cha kati.

Ripoti ya Benki ya Dunia mwaka 2022 ilisema China ndiyo nchi inayokopesha zaidi nchi za Maldives, Pakistan na Sri Lanka.

Ahadi ya hivi karibuni ya Xi Jinping ya uwekezaji, kama ilivyoripotiwa wakati wa vikao vya Bunge la Wananchi (NPC) mwezi Machi, imepunguzwa kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na hapo awali.

Inaeleza kuwa uwekezaji mkubwa wa nje hauwezi kudumu ikiwa kuna hali ya kuzorota kwa uchumi wa China.

Lakini Song anasisitiza hata kwa kudorora, ukubwa wa uchumi wa China bado utairuhusu kuwa mchangiaji mkubwa wa ukuaji wa kimataifa.

"China bado ina uwezo wa kuchangia 20% au zaidi ya ukuaji wa kimataifa katika miaka mitano ijayo."

China ifanye nini kurudi kileleni?

Song anaamini awamu inayofuata, baada ya mpito wake wa kiuchumi China itapanda na kuwa na ukuaji ubora, na kupanda ongezeko la thamani.

"Vikao vya watunga sera vilizingatia vipaumbele vya muda mrefu. Ni muhimu kwa China kushughulikia mzozo wa ardhi na nyumba. Pili, inapaswa kuelekeza nguvu kwenye mahitaji.

"China inapaswa pia kutoa nafasi zaidi kwa makampuni binafsi na ya kigeni, na kuwa na mageuzi ya fedha ambayo yanahakikisha uendelevu wa muda mrefu wa fedha za umma," anasema Xu.

Song anaamini uongozi wa China utajikita kufikia lengo la ukuaji wa Pato la Taifa la 5% lililowekwa ndani ya mwaka 2024.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Jason Nyakundi na kuhaririwa an Ambia Hirsi