Beijing yajibu -Je, China na Marekani zinaweza kuepuka kuongezeka kwa vita vya biashara?

Trump anasema amekuwa akizungumza na Xi wa China kupitia wasaidizi wake tangu kuchaguliwa kwake

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Trump anasema amekuwa akizungumza na Xi wa China kupitia wasaidizi wake tangu kuchaguliwa kwake
    • Author, Laura Bicker
    • Nafasi, Mwandishi China
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Beijing imefanya maamuzi yake.

Baada ya kutoa tahadhari ya kukabiliana na mikakati mipya ya Trump ya kufanya mazungumzo, imeamua kujibu mapigo kwa kutangaza ushuru mpya dhidi ya bidhaa za Marekani.

China imesema itatekeleza asilimia 15 ya ushuru kwa mkaa wa mawe na gesi asilia pamoja na ushuru wa asilimia 10 kwa mafuta ghafi, nyenzo za kilimo na mashine za gari zinazoagizwa kutoka Marekani kuanzia tarehe 10 mwezi Februari.

Hata hivyo kabla ya tarehe hiyo kutimia huenda mataifa haya mawili yaliyo na uchumi mkubwa kufikia maelewano ya kuepusha mzozo wa kibiashara.

Viongozi wa mataifa hayo mawili wanatarajiwa kukutana wiki hii na kuna dalili maamuzi haya yanaweza kubatilishwa, China wakionekana kuwa tayari kwa mazungumzo yakuleta muafaka.

Kwanza, China haina mikakati ya kutosha ya kuingia katika vita vya kiuchumi ukilinganisha na ushuru wa asilimia 10 unaotozwa na Trump kwa bidhaa za China zinazoingia Marekani.

Marekani ndiyo muuzaji mkuu wa gesi asilia duniani kote, lakini Uchina inachangia karibu asilimia 2.3% tu ya mauzo hayo na uagizaji wake mkuu wa magari hutoka Ulaya na Japan.

Hatua ya Beijing kuchagua bidhaa wanazotaka kuzitoza ushuru wa juu ni njia moja ya kujitafutia umuhimu pindi watakapoingia mezani na Marekani.

Rais wa Marekani Donald Trump alisema alifanya mazungumzo ya faragha kwa njia ya simu na rais wa China Xi siku chache baada ya kuapishwa kwake, ambapo sherehe hiyo ilihudhuriwa na wajumbe wa haiba ya juu kutoka Uchina.

Pia Trump alisema anatumai atajadiliana na Rais wa China namna ya kumaliza vita vya Urusi katika taifa la Ukraine.

Rais Xi huenda hatapendelea kuanzisha mkwaruzano na Trump kwani anakabiliwa na kibarua cha kuimarisha uchumi wa taifa lake unaodidimia.

Mkawruzano wa kiuchumi baina ya mataifa haya mawili sio jambo geni kwao lakini wawili hao huenda wakaepuka kujipata katika vita hivi ambavyo viliwahi kutokea hapo awali.

Kulikuwa na uhusiano mwema kati ya China na Marekani wakati wa muhula wa mwisho wa Trump, kabla ya uhusiano huo kuwa chachu.


Magari yakiendeshwa wakati wa msongamano wa asubuhi huko Beijing

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Gari zinazotumia injini kubwa ni miongoni mwa bidhaa zinazoagizwa kutoka Marekani ambazo Beijing zimeapa kuzitoza ushuru wa juu

Kuafikiana au kutoafikiana

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Itakuwa vigumu zaidi kwa Trump kuafikia makubaliano na China kuliko ilivyokuwa kwa Mexico na Canada, na mengi yatategemea kile anachotaka kutoka Beijing.

China ni mshindani mkuu wa kiuchumi wa Washington, na kutenganisha nchi hiyo na usambazaji mkubwa wa bidhaa imekuwa lengo la utawala wa Trump.

Ikiwa Trump atadai mengi zaidi, Xi anaweza kuhisi kuwa anaweza kujiondoa, na kutakuwa na mipaka juu ya jinsi anavyoweza kushinikizwa.

Rais wa Marekani anaingia mazungumzo na China ambayo ina kiwango kikubwa cha kujiamini kuliko ilivyokuwa zamani.

Beijing imetanua mawanda yake duniani kote, na sasa ni mshirika mkuu wa kibiashara wa zaidi ya nchi 120.

Katika miongo miwili iliyopita, China pia imejaribu kupunguza umuhimu wa biashara kwa uchumi wake na kuongeza uzalishaji wa ndani.

Leo, bidhaa zinazouzwa nje na zile zinazozalishwa nchini zinachangia takribani asilimia 37% ya Pato la Taifa la China, ikilinganishwa na zaidi ya asilimia 60% mwanzoni mwa miaka ya 2000, kulingana na Baraza la Mahusiano ya Nje.

Kodi ya asilimia 10 itakuwa na madhara, lakini Beijing inaweza kuhisi kuwa inaweza kuvumilia pigo hilo - kwa sasa.

Hofu itakuwa kama Rais Trump anamaanisha kuongeza asilimia hiyo hadi asilimia 60% aliyoahidi wakati wa kampeni yake au kama ataendelea kutumia tishio la kodi kama chombo cha kidiplomasia cha kudumu dhidi ya utawala wa Xi.

Ikiwa hiyo itatokea, Beijing itataka kuwa tayari, na hiyo inamaanisha kuwa na mkakati wazi endapo hali hii itazidi kuwa mbaya.

Kujifunza baada ya matukio ya zamani

Mara ya mwisho viongozi hawa wawili walipotia saini makubaliano, hayakumalizika vizuri.

Nchi hizi mbili zilianzisha kodi za kisasi kwa bidhaa za thamani ya mabilioni ya dola kutoka mwaka 2018.

Mgogoro huu ulidumu kwa zaidi ya miaka miwili hadi mwishowe China ilikubali kutumia dola bilioni 200 zaidi ($200bn) kila mwaka kununua bidhaa za Marekani mwaka 2020.

Washington ilitumai kuwa makubaliano hayo yangepunguza pengo kubwa la biashara kati ya China na Marekani, lakini mpango huo ulipunguzwa na janga la Covid, na sasa pengo hilo linafikia dola bilioni 361 ($361bn), kulingana na takwimu za forodha za China.

China pia inakutana na changamoto kubwa kwa kuwa inawaza hatua zaidi katika majadiliano yoyote.

Beijing bado inanunua bidhaa nne zaidi kutoka Marekani kuliko inavyouza, na wakati wa utawala wa Trump, ilikosa bidhaa za kumlenga kwa kodi.

Wataalamu wanaamini kuwa China sasa inatafuta mikakati mipana kando na ushuru kama njia ya kujibu ikiwa vita vya biashara vitaongezeka.

Muda unazidi kuyoyoma.

Huu ni mwanzo tu wa vita vya kiuchumi baina ya mataifa haya mawili ambayo yanajivunia ubabe wa kiuchumi duniani.

Biashara duniani kote zitakuwa zikifuatilia kuona kama viongozi hawa wawili watafanikiwa kufikia makubaliano mwishoni mwa juma hili.

Mada zinazofanana:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi