Ukweli kuhusu kufa kwa ubongo na kisa cha mchuuzi aliyepigwa risasi Kenya

Chanzo cha picha, Familia ya Boniface Kariuki
- Author, Na Ambia Hirsi
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Kifo cha Bonface Mwangi Kariuki, mchuuzi aliyepigwa risasi kwa karibu wakati wa maandamano ya Juni 17 jijini Nairobi, Kenya kimeibua maswali kadhaa huku baadhi ya Wakenya wakihoji hali yake alipofikishwa hospitali.
Hii ni baada ya madakari waliokuwa wakimhudumia katika hospitali ya Rufaa ya Kenyatta alikokuwa amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kwa majuma mawili kuiambia familia yake siku ya Jumapili kuwa ubongo umekufa na saa kadhaa baadaye kuwathibitishia kuwa amefariki dunia.
Kufa kwa ubongo kunatambuliwa kisheria na kiafya kama kifo nchini Kenya.
Inaashiria mwisho usioweza kubadilishwa wa shughuli zote za ubongo. Ingawa mashine zinaweza kufanya mapigo ya moyo na mapafu kufanya kazi kwa muda, hali hiyo inachukuliwa kuwa ya mwisho.
Mjadala wa ubongo kufa kama ilivyotokea kwa marehemu Boniface Kariuki pia uliibuka nchini Uganda mapema mwaka huu wakati Mbunge wa Kawempe Kaskazini Mohammed Ssegirinya alipofariki baada ya kuthibitishwa kuwa ubongo wake umekufa huku wataalam wakielezea kuwa hali hiyo huenda ilitumiwa kutoa matumaini ya uwongo na kuvutia gharama zisizo za lazima.
Kufa kwa ubongo hata hivyo ni hali ambayo hata wataalamu wenyewe wanasema vigumu sana kwa mtu wa kawaida kuelewa. Hii ni kwa sababu anajiuliza maswali kama vile... vipi ubongo unaweza kufa na mwathirika awe hai?
Tunajibu baadhi ya maswali hayo na mengine katika taarifa hii kwa usaidizi wa mtaalamu.
Kufa kwa ubongo ni nini?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kufa kwa ubongo kulingana na wataalamu wa nurolojia ni pale ambapo ubongo wa mtu unapoacha kufanya kazi kabisa lakini mwili unabaki ukiwa hai kwa mashine za kupumua na dawa. Vigezo vinavyoashiria kuwa ubongo wa mwathirika hauwezei tena kufanya kazi kabisa ni pale ambapo:
- Mtu ambaye ubongo wake umekufa hatambui chochote na hafikirii wala kuhisi
- Hawawezi kujisogeza wala kupumua
- Ubongo wake huacha kudhibiti shughuli za mwili zisizo za hiari kama vile mapigo ya moyo na shinikizo la damu
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hii ndio sababu mtu ambaye ambaye ubongo wake umekufa kisheria, anachukuliwa kuwa wameaga dunia.
Dk Erasmus Okello, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Makerere na Daktari anayewahudumia wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum baada ya kufanyiwa upasuaji wa kichwa wa kutishia maisha anaeleza kuwa uharibifu wa shina la ubongo, eneo dogo katika ubongo ambalo hudhibiti utendaji kazi muhimu wa maisha, hauwezi kurekebishwa na hakuna uwezekano wa mtu kufufuliwa hata kama anaweza kuwa na viungo vyake muhimu kama vile moyo au figo kwa muda mfupi sana.
''Mashine zinaweza kupumua kwa niaba ya mtu ambaye ubongo wake umekufa na dawa zinaweza kufanya moyo uendelee kudunda kwa muda mfupi,'' alisema katika mahojiano na The Uganda Radio Network, wakati mjadala ulipoibuka nchini humo kuhusu kifo cha Mbunge wa Kawempe Kaskazini Mohammed Ssegirinya ambaye madaktari walisema kuwa ubongo wake umekufa.
Dk Okello pia anongeza kuwa hakuna mtu ambaye ubongo wake ulikufa aliyewahi kupona. ''Kufa kwa ubongo ni tofauti na kupoteza fahamu. Mtu ambaye amepoteza fahamu, ubongo wake una kiasi fulani cha utendaji kazi na wakati mwingine hupata afueni.''
Je, nini husababisha kufa kwa ubongo?
Kufa kwa ubongo husababishwa na uharibifu mkubwa wa ubongo ikiwa ni pamoja na:
Jeraha la kichwa- Hii ni mojawapo ya sababu kuu za kifo cha ubongo.
Jeraha kali la kichwa linaweza kusababisha uharibifu mkubwa wa ubongo, uvimbe, na kutokwa na damu, ambayo inaweza kusababisha kifo cha ubongo.
Ukosefu wa oksijeni kwenye ubongo unaotokana na mshtuko wa moyo pia unaweza kusababisha kufa kwa ubongo.

Kulingana na utafiti ulifanywa nchini Marekani wataalamu walibaini kuwa kuwa vifo vya ubongo vilichangia 2% ya vifo vyote nchini humo
Madaktari hujuaje kama ubongo wa mtu umekufa?
Kwanza madaktari huwa wanahakikisha kuwa mtu huyo hana tatizo lolote la kiafya ambalo linasababisha kupoteza fahamu kabisa sawa na kufa kwa ubongo. Matatizo hayo yanajumuisha:
Kuzidisha kiasi kinachohitajiwa cha dawa fulani
Joto la chini sana la mwili (hipothemia)
Ikiwa mgonjwa hana mojawapo kati ya hayo matatizo, madaktari hufanya uchunguzi wa kimwili ili kubaini uwepo wa dalili za shughuli za ubongo ikiwemo:
- Kujaribu kupumua kwa kuzima mashine ya kupumua na kuona kama mtu anaweza kupumua peke yake
- Kushtuka au kusogeza mwili mtu atakapofinywa au kuchomwa kwa sindano
- Kugandamizwa au kukakamaa kwa misuli ya shingo wakati kifaa kidogo kinapoingizwa nyuma ya koo
- Kupepesa jicho ili kuona kama jicho linajibu linapoguswa
- Mwanga wa tochi kuchoma mboni ya jicho na kuona kama mboni inasinyaa
Ikiwa hakuna dalili za shughuli za ubongo, wakati mwingine madaktari hurudia vipimo baada ya saa 6 hadi 24 ili kuhakikisha kwa mara nyingine tena kuwa mtu huyo haonyeshi kuitika. Baada ya kumpima mara mbili bila kuitikia, madaktari wanajua ya kwamba ubongo wa mtu huyo umekufa.
Madaktari hufanya nini mtu akiwa na hali ya kufa kwa ubongo?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa sababu kufa kwa ubongo kisheria humaanisha kuwa mtu amekufa, viungo vya mtu huyo vinaweza kutolewa kwa mtu ambaye ana uhitaji wa upandikizaji wa kiungo. Sheria za uchangiaji wa viunga hata hivyo hutofautiana kutoka nchi moja hadi nyingine.
Uchangiaji hauhitaji kusubiri hadi moyo wa mtu huyo uache kudunda. Viungo huchukuliwa ikiwa mtu huyo au familia yake inataka kuvitoa.
Mashine ya kumsaidia kupumua au mashine za usaidizi huendelea kufanya kazi hadi mchakato huo ukamilishwe. Viungo huondolewa kwa umakini, na mwili hushughulikiwa kwa heshima kubwa. Kisha madaktari:
Huzima mashine ya kumsaidia kupumua, Kusitisha dawa zozote alizokuwa akipewa
na hatimaye kupeleka mwili kwenye ofisi ya afisa mchunguzi wa vifo au mochwari.

Licha ya maelezo hayo dhana inayosalia vichwani mwetu ni kwamba binadamu akiacha kupumua, moyo unaacha kupiga. Hata hivyo madaktari huenda wanavuka mstari kati ya maisha na kifo.
Huduma ya kisasa ya tiba kwa wagonjwa mahututi inatia ukungu mstari huo. Sasa, tiba inayohusisha vifaa kama ventilator zinaweza kudumisha upumuaji na mapigo ya moyo kwa muda ili wahudumu wa afya waweze kutambua na kutibu tatizo. Kwa hiyo, inaweza kuwa vigumu kukubali kwamba mtu anayeonekana kuwa anapumua na ana mapigo ya moyo, kwa kweli, amekufa.
Imehaririwa na Yusuph Mazimu












