Je, ajali ya Titan na kuzama wahamiaji Ugiriki vinatwambia nini kuhusu thamani ya maisha?

.

Chanzo cha picha, Greek Coast Guards

Mamilioni ya watu ulimwenguni wamefuatilia operesheni ya kujua ilipo nyambizi ya kitalii iliobeba watu watano, iliopotea ikielekea kutalii mabaki ya meli maarufu ya Titanic.

Picha za abiria waliolipa dola za kimarekani 250,00 kila mmoja kuabiri nyambizi ya Titan zimesambaa mitandaoni. Watu wanafuatilia taarifa mpya kutoka kwa walinzi wa pwani ya Marekani, na kuperuzi taarifa mubashara katika kurasa zinazoelemewa na wingi wa watu.

Awali mahojiano katika vyombo vya habari vya kimataifa, yalionyesha chombo hicho kidogo kinacho milikiwa na OceanGate kikoje ndani.

Ila kwa nini taarifa hii imevutia wengi kuliko taarifa nyingine za watu kuzama baharini?

Mwandishi wa BBC Urdu, Saher Baloch akiwa Islamabad, amefuatilia utata unaoendelea katika mitandao ya kijamii nchini Pakistan kuhusu jambo sawa na hilo.

Taarifa za kupotea nyambizi zilipoibuka, watu katika mitandao ya kijamii nchini Pakistan walielewa tofauti ya ushughulikiaji wa taarifa hiyo ukilinganisha na ajali nyingine za baharini.

Rejelea boti ya uvuvi iliobeba watu wanaokisiwa kuwa 700, ilizama katika bahari ya Kusini mwa Ugiriki Juni 14, likiwa ni moja ya janga baya la wahamiaji wanaoelekea Ulaya

Manusura wanasema hadi watoto 100 wanaamini walikuwemo katika boti na watu takribani 78 wamethibitishwa kufariki. Lakini mamia wamepotea baharini.

Walinzi wa pwani ya Ugiriki wanadai boti ilikuwa ikielekea Italy na haikuwa na uhitaji wa kuokolewa, lakini BBC imepata ushahidi unatia shaka madai hayo.

Uchambuzi wa mwenendo wa meli nyingine katika eneo hilo, unaonesha chombo hicho kilicho jazana watu hakikuwa kinatembea kwa masaa saba kabla ya kupinduka. Mamlaka ya Ugiriki bado haijajibu matokeo ya uchunguzi wa BBC.

Katika taarifa ya Mwenyekiti wa Seneti ya Pakistan, anasema Wapakistan 300 wamefariki kwa kuzama, na imekuwa ni habari kubwa nchini humo.

.

Chanzo cha picha, Mean PA

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa upande mwingine, Titan iliyokuwa na watu watano ilipoteza mawasiliano na meli ya usaidizi saa moja na dakika 45 tangu ipige mbizi. Walinzi wa pwani ya Marekani wanasema - walitaarifiwa kuhusu tatizo hilo masaa nane baadaye, na operesheni kubwa ya utafutaji ikaanzishwa, ikihusisha mamlaka nyingine ikiwemo Canada, Ufaransa, Uingereza na kampuni binafsi.

Ingawa Titan ilipiga mbizi ikiwa na oksijeni ya dharura ya kudumu kwa siku nne. Juhudi kubwa zilifanyika kujua ilipo nyambizi hiyo, na mitandao ya kijamii ikatawaliwa na maoni na kauli kuhusu ajali zote mbili. Na maoni mengi yalizingatia tofauti iliyokuwepo ya ushughulikiaji wa ajali hizo.

Mkurugenzi wa Human Rights Commission, ya Pakistan Farah Zia, “ulimwenguni msiba wa matajiri unabeba umuhimu mkubwa, kwa sababu watu huvutiwa na maisha yao. Hivyo ni kawaida kwa vyombo vya habari kuripoti kwa wingi,” ameiambia BBC.

Lakini anadhani mjadala huu unaweza kutoa fursa kwa vyombo vya habari ulimwenguni kujitathmini na kutafuta sauti za waliotengwa.

Wazungumzaji wengine wamekosoa mwitikio wa matukio haya mawili.

Mtumiaji wa Twitter Maryam ameandika, “tofauti ya operesheni ya kimataifa sanjari na ufuatiliaji wa vyombo vya habari kwa watalii matajiri katika nyambizi ya matembezi, na kukosekana hayo kwa wahamiaji masikini walio katika boti iliyopinduka, inasema mambo mengi kuhusu dunia tunayoishi.”

Mtoa maoni na mwandishi habari, Zarrar Khuhro anafikra tofauti.

“Nafikiria kila baada ya janga lolote, kifuatacho ni kuona ubora na vilevile ubaya ambao ubinadamu unaweza kuonyesha.”

Akizungumza kuhusu kuzama kwa boti la wahamiaji katika pwani ya Ugiriki, anasema, “tunaona tabia ya kuwakemea ikielekezwa kwa walinzi wa pwani ya Ugiriki. Lakini wakati huo huo maelfu ya watu wanaandamana Athents. Labda ndio kwa mara ya kwanza tunaona maandamano makubwa yakilaani vifo vya wahamiaji.”

Pia, kuna ripoti boti ya kifahari katika bahari ya Mediterrean ambayo ilikimbilia kutoa msaada baada ya kupata ishara ya hatari.

Kuna mjadala katika mitandao ya kijamii kuhusu mgawanyiko wa kitabaka, lakini mazungumzo yanarudi katika mjadala kuhusu maisha ya binadamu.

Mtumiaji mmoja wa mtandao wa Twitter ameandika, “tofauti iko wazi lakini misiba inafanana.”

Mtumiaji mwingine ameandika, “wakati Kanisa Kuu lilipoungua moto Ufaransa, ukarabati wake ulichangiwa kutoka duniani kote. Je, hilo linatokea pale majanga ya asili yanapotokea katika dunia inayoendelea? Hapana. Tunapaswa kujisikia vibaya kuhusu jambo hilo? Ndio. Je, kuna kitakacho badilika? Hapana.”