Hakuna kitakachotokea hadi mimi na Putin tutakapokutana, Trump asema
Rais wa Marekani Donald Trump amedokeza kwamba hakuna hatua itakayopigwa katika mazungumzo ya amani ya Ukraine hadi atakapokutana ana kwa ana na mwezake wa Urusi Vladmir Putin.
Muhtasari
- Rigathi Gachagua: Aliyekua naibu Rais wa Kenya azindua chama kipya cha siasa
- Mfadhili wa mbegu za kiume 'baba wa watoto -180' anyimwa haki ya kuwa mzazi
- Hakuna kitakachotokea hadi mimi na Putin tutakapokutana, Trump asema
- Kwanini PSG na Mbappe wanakabiliana mahakamani?
- Haya ndio majina maarufu zaidi waliyopewa watoto wa 2024
- Rwanda: Kituo cha tiba ya bangi Rwanda mbioni kukamilika
- Marekani na Iran ziko karibu kufikia makubaliano ya nyuklia, Trump anasema
- Mashambulizi ya anga ya Israel yawaua watu zaidi ya 100, huku mashirika yakionya kuhusu njaa
- Lineker aomba radhi kwa kutumia picha ya Panya kudhalilisha Uzayoni
- Polisi wanatembea nyumba hadi nyumba kutafuta wazazi wa watoto waliotelekezwa kupitia DNA
- Rais wa zamani wa Mauritania ahukumiwa miaka 15 jela baada ya kukata rufaa kifungo cha miaka 5
- Mashambulizi ya anga ya Israel yaua watu 40 Gaza - Hospitali
- Mashambulizi ya droni yanaongezeka katika awamu mpya ya vita vya Sudan
- Rais wa Afrika Kusini kukutana na Trump wiki ijayo
- Mshawishi wa mitandao ya kijamii Mexico auawa akiwa mubashara kwenye TikTok
- Watu 21 wamepoteza maisha katika ajali iliyotokea Mexico - afisa amesema
- Putin hatahudhuria mazungumzo ya amani ya ana kwa ana Uturuki.
Moja kwa moja
Na Asha Juma & Dinah Gahamanyi
Rigathi Gachagua: Aliyekua Naibu Rais wa Kenya azindua chama kipya cha siasa

Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Tangu kuondolewa madarakani mwaka jana, Bwana Rigathi Gachagua amegeuka kuwa mkosoaji mkubwa wa Rais Ruto. Aliyekuwa naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua Alhamisi amezindua chama kipya cha kisiasa kiitwacho Democratic Citizen Party DCP ambacho anakinadi kuwa kitajikita katika msingi wa kuwasikiliza Wakenya.
Katika hafla ya kuzindua chama cha DCP, Bwana Gachagua amesema chama chake kitafufua matumaini ya Wakenya waliovunjwa moyo na uongozi ulioko madarakani unaoongozwa na Rais William Ruto wa chama cha UDA.
Tangu kuondolewa madarakani mwaka jana, Bwana Rigathi Gachagua amegeuka kuwa mkosoaji mkubwa wa Rais Ruto.
Naibu huyo wa zamani wa Rais William Ruto katika uchaguzi uliopita alitimuliwa na bunge la Kenya mapema mwezi Oktoba, 2024 , kwa kile kilichoelezewa kama kuhujumu idara ya ujasusi na mahakama, kukiuka kiapo chake na Katiba na kuchochea siasa za ukabila, shutma ambazo alizikana.
Unaweza pia kusoma:
Mfadhili wa mbegu za kiume 'baba wa watoto -180' anyimwa haki ya kuwa mzazi

Chanzo cha picha, Instagram/Robert Albon
Maelezo ya picha, Jaji wa Mahakama Kuu alitilia shaka motisha ya Robert Albon ya kuzaa watoto wengi Mwanaume aliyetoa ufadhili wa mbegu za kiume ambaye anadai kuzaa zaidi ya watoto 180 duniani kote, amenyimwa haki za uzazi kwa mtoto aliyemzaa kama mfadhili kwa njia ya asili.
Robert Albon, ambaye alichapisha sampuli za mbegu za kiume zilizopakiwa na kugandishwa ili kuziweka katika hali ya ubaridi, alitaka kuwa na udhibiti wa mzazi wa mtoto wake na kuwasiliana na msichana , aliyezaliwa mnamo 2023.
Jaji wa Mahakama ya Juu Bw. Jaji Poole alikataa ombi la Bw Albon, akidai mfadhili huyo "anataka kudhibiti wengine" na anaweza kuhamia familia nyingine "kama alivyofanya hapo awali".
Alisema: "Ushahidi ulio mbele ya mahakama unaonyesha kwamba Bw Albon atafanya ngono na, au kutoa mbegu zake kwa ajili ya upandikizaji wa bandia, kwa mtu yeyote anayeuliza."
Mzee huyo mwenye umri wa miaka 54 badala yake alimuomba hakimu kumpa jukumu la mzazi pamoja na kuwasiliana ana kwa ana.
Mahakama pia ilisikiliza kesi ya msichana mwingine aliyezaa na Bw Albon mnamo 2022 na anayejulikana kama CB.
Unaweza pia kusoma:
Hakuna kitakachotokea hadi mimi na Putin tutakapokutana, Trump asema

Rais Donald Trump anamesema kuwa maendeleo makubwa katika mazungumzo ya amani ya Ukraine hayawezekani hadi yeye na Rais Putin watakapokutana ana kwa ana.
Kama mwandishi aliyeeambatana naye kwenye ndege ya Air Force One, nilimuuliza Trump ikiwa alikatishwa tamaa na kiwango cha ujumbe ambao Urusi imetuma Uturuki.
"Angalia, hakuna kitakachotokea hadi mimi na Putin tutakapokutana. Sawa?" Trump anasema.
"Na ni wazi hangeenda. Alikuwa anataka kwenda, lakini alifikiri ninakwenda pia.
"Hangeenda ikiwa sikuwepo na siamini kuwa chochote kitatokea, iwe unapenda au la, hadi mimi na yeye tutakapokutana, lakini tutahitaji kulitatua hili kwasababu watu wengi wanakufa.
Unaweza pia kusoma:
Kwanini PSG na Mbappe wanakabiliana mahakamani?

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Uamuzi kuhusu mzozo kati ya Kylian Mbappe na PSG unatarajiwa tarehe 26 Mei Wakati Kylian Mbappe hatimaye alipoondoka Paris St-Germain majira ya kiangazi yaliyopita, wengi walitarajia pande zote mbili zingesonga mbele haraka baada ya sakata moja ya uhamisho iliyodumu kwa muda mrefu katika soka hatimaye kukamilika.
Mzozo unaoendelea wa kisheria, hata hivyo, umeendelea kuharibu uhusiano kati ya mshambuliaji huyo na klabu yake ya nyumbani kwa kipindi kikubwa zaidi cha mwaka.
Mshambuliaji huyo wa Real Madrid anadai euro 55m (£46.3m) kama mshahara ambao haujalipwa kutoka kwa mabingwa hao wa Ligi 1.
Kiasi hiki, pamoja na ushuru, kilizuiliwa kutoka kwenye akaunti za klabu na mahakama ya Paris kufuatia ombi la timu ya wanasheria ya Mbappe mwezi uliopita.
Kiini cha mzozo huo ni kuongezwa kwa kandarasi mbaya kwa mshambuliaji huyo wa Ufaransa mnamo 2022 ambayo ilimhusisha ambapo alionekana akiwa amepiga picha pamoja na rais wa klabu Nasser Al-Khelaifi kwenye uwanja wa Parc des Princes, akionyesha shati yenye "2025" mgongoni.
Hata hivyo, Mfaransa huyo alikuwa ametia saini mkataba wa miaka miwili na msimu wa ziada wa hiari, jambo muhimu ambalo lingejitokeza hadharani baadaye.
Mwaka mmoja baadaye, barua kutoka kwa Mbappe ikionyesha kwamba hakuwa na nia ya kuanzisha chaguo hilo iliibuka.
Ingawa ilifika tu kwa usimamizi wa PSG mnamo Juni 2023, hati hiyo iliwekwa chini ya miezi miwili baada ya kusaini mkataba msimu wa majira ya kiangazi uliopita.
Unaweza pia kusoma:
Haya ndio majina maarufu zaidi waliyopewa watoto wa 2024

Chanzo cha picha, Getty/SDI Productions
Unaweza kutambua majina bora 20 ya watoto maarufu zaidi ya 2024 ?... huenda karibu yote umewahi kuyasikia.
Liam na Olivia walikuwa majina maarufu zaidi ya watoto mnamo 2024, nafasi ambayo majina yote yameshikilia tangu 2019, kulingana na taasisi ya Utawala wa Usalama wa Jamii au Social Security Administration (SSA) ambayo hunatoa viwango vya umaarufu wa majina ya kila mwaka.
Taasisi hiyo pia iliushirikisha umma majina yasiyo ya kawaida ambayo umaarufu wake ulipanda zaidi mwaka wa 2024. Mwaka huu, majina hayo ni pamoja na Truce, Halo na Azaiah kwa upande wa wavulana na Ailany, Scottie na Analeia kwa upande wa wasichana.
Majina 10 bora ya wasichana 2024
- 1. Olivia
- 2. Emma
- 3. Amelia
- 4. Charlotte
- 5. Yangu
- 6. Sophia
- 7. Isabella
- 8. Evelyn
- 9. Ava
- 10. Sofia
Majina 10 bora ya wavulana 2024
- 1. Liam
- 2. Nuhu
- 3. Oliver
- 4. Theodore
- 5. Yakobo
- 6. Henry
- 7. Mateo
- 8. Eliya
- 9. Lucas
- 10. William
Rwanda: Kituo cha tiba ya bangi Rwanda mbioni kukamilika

Maelezo ya picha, Rwanda inalenga kuuza bangi zaidi nje Mradi wa Rwanda wa zao la bangi kwa ajili ya matibabu ya thamani ya Juu (HVTC) unapiga hatua kubwa, huku mradi wa miundombinu ya matibabu ya zao hilo ukiwa umekamilika kwa asilimia 83, kulingana na Bodi ya Maendeleo ya Rwanda (RDB).
Mradi wa bangi ni sehemu ya hatua ya Rwanda katika tasnia ya matibabu na dawa, kwa lengo la kuchangia utafiti wa afya ulimwenguni na uchumi.
Kampuni tanzu ya KKOG Global - King Kong Organics (KKOG), ilikwa ni kampuni ya kwanza kupata leseni ya miaka mitano kutoka kwa Bodi ya Maendeleo ya Rwanda (RDB) kuendesha uzalishaji wa bangi.
Kampuni hiyo hapo awali ililiambia gazeti la The New Times nchini humo kwamba ilikuwa imefanya uwekezaji wa dola milioni 10 katika mashine, ujenzi wa kituo, malipo ya ada katika upatikanaji wa ardhi na wakandarasi, pamoja na kuagiza mbegu za bangi zilizobadilishwa vinasaba.
Kukamilika kwa shughuli za ujenzi wa kituo cha uzalishaji wa bangi, kilichoko katika Wilaya ya Musanze katika Mkoa wa Kaskazini, hapo awali kilikuwa kimepangwa kuhitimishwa ifikapo Mei mwaka jana kabla ya kuongezwa hadi Septemba mwaka huo huo.
Kulingana naye, mchakato wa uzalishaji ambao unahusisha uukamuliwaji wa mafuta ya bangi ambayo yatasafirishwa kwa masoko yaliyolengwa utawezekana kwa ushirikiano wa serikali ya Rwanda itakayochangia takriban dola milioni 3 katika mradi huo.
Rwanda tayari imetenga hekta 134 kwa kilimo cha bangi ya kimatibabu, hasa ikilenga mauzo ya nje.
Soma zaidi:
Marekani na Iran ziko karibu kufikia makubaliano ya nyuklia, Trump anasema

Chanzo cha picha, Reuters / Getty Images
Maelezo ya picha, Rais wa Marekani Donald Trump (kulia) na Kiongozi Mkuu wa Iran Ali Khamenei (kulia) Rais wa Marekani Donald Trump anasema kuwa Iran "imekubali" masharti ya mkataba wa nyuklia na Marekani.
Trump alielezea mazungumzo ya hivi punde kati ya nchi hizo mbili, ambayo yalimalizika Jumapili, kama "mazungumzo mazito" ya "amani ya muda mrefu".
Hapo awali, mshauri wa kiongozi mkuu wa Iran aliiambia NBC News kwamba Tehran iko tayari kufanya makubaliano kuhusu mpango wake wa nyuklia ili badala yake iondolee vikwazo.
Marekani imesisitiza kuwa Iran lazima isitishe urutubishaji wa madini ya uranium ili kuzuia nchi hiyo kutengeneza silaha za nyuklia - ingawa Iran inasisitiza kuwa shughuli zake za nyuklia ni za amani kabisa.
Akizungumza siku ya Alhamisi nchini Qatar, katika kituo cha pili cha ziara yake ya siku nyingi ya Ghuba, Trump alisema kuwa makubaliano yamekaribia kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran na kuongeza kuwa shambulio la kijeshi katika maeneo ya Tehran linaweza kuepukwa.
"Hatutatimua vumbi lolote la nyuklia nchini Iran," Trump alisema baada ya mkutano huko Doha na viongozi wa biashara.
"Nadhani tunakaribia labda kufanya makubaliano bila kufanya hivi.
"Labda umesoma leo taarifa kuhusu Iran. Ni aina fulani ya kukubaliana na masharti."
Unaweza pia kusoma:
Mashambulizi ya anga ya Israel yawaua watu zaidi ya 100, huku mashirika yakionya kuhusu njaa

Chanzo cha picha, Reuters
Mashambulizi ya anga ya Israel yawaua takriban watu zaidi ya 100, huku mashirika yakionya kuhusu njaa, ulilinzi wa raia unasema.
Mashirika mashirika ya kibinadamu pia yanaonya kuhusu njaa kutokana na ukosefu wa chakula
Israel imezidisha mashambulizi yake ya kulipua Gaza huku mazungumzo ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka yakiendelea na Donald Trump yuko safarini Mashariki ya Kati.
Duru za hospitali za eneo hilo zinasema zaidi ya watu 40 wameuawa katika mashambulizi ya hivi karibuni ya anga ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza.
Ripoti zinasema kuwa takriban miili 36 imefikishwa katika hospitali za Khan Younis, kusini mwa Gaza, ambako Israel ilishambulia kwa mabomu makubwa jana usiku.
Wakati huo huo, Israel imewaamuru watu kuondoka katika eneo hilo, jambo ambalo limeongeza hofu zaidi miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.

Chanzo cha picha, Reuters
Haya yanajiri wakati ambapo Israel imekuwa ikizuia misaada ya kibinadamu ikiwemo chakula na vifaa vya matibabu kufika Gaza tangu mwanzoni mwa mwezi Machi. Jumuiya ya kimataifa imelaani vizuizi hivyo, na Umoja wa Mataifa umeonya kuwa zaidi ya Wapalestina milioni mbili wanaoishi huko wanakabiliwa na "hatari kubwa" ya njaa.
Lakini Israel inakanusha kuwa mtu yeyote huko Gaza anakabiliwa na njaa.
Unaweza pia kusoma:
Lineker aomba radhi kwa kutumia picha ya Panya kudhalilisha Uzayoni

Chanzo cha picha, PA Media
Gary Lineker "ameomba radhi" baada ya kukosolewa kwa kuweka ujumbe kwenye mtandao wa kijamii kuhusu Uzayoni uliojumuisha picha ya panya.
"Kwenye mtandao wa Instagram nilichapisha tena ujumbe ambao nimegundua kuwa uilikuwa na maudhui ya kuudhi," alisema katika taarifa. "Najutia sana marejeo haya.
"Siwezi kamwe kushirikisha kitu chochote cha chuki kwa kujua. Kinakwenda kinyume na kila kitu ninachoamini." Mtangazaji wa kipindi cha Match of the Day alisema nilifuta ujumbe huo "mara tu nilipofahamu suala hilo".
Kihistoria panya amekuwa akitumiwa kama tusi dhidi ya Wayahudi, akimaanisha lugha iliyotumiwa na Ujerumani ya Nazi kuwatambulisha Wayahudi.
"Wakati ninaamini sana umuhimu wa kuzungumza juu ya masuala ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na janga linalotokea Gaza, najua pia jinsi tunavyofanya hivyo ni muhimu," Lineker aliendelea.
"Nachukua jukumu kamili kwa kosa hili. Picha hiyo haiakisi maoni yangu.
"Lilikuwa kosa kwa upande wangu ambalo ninaomba msamaha kwa kumaanisha."
Pia unaweza kusoma:
Polisi wanatembea nyumba hadi nyumba kutafuta wazazi wa watoto waliotelekezwa kupitia DNA

Chanzo cha picha, PA
Polisi wanawasaka wazazi wa watoto watatu waliotelekezwa dakika chache baada ya kuzaliwa mashariki mwa London, na wamesema kuwa sasa wanachunguza takriban nyumba 400 zilizo karibu.
Mtoto Elsa aliachwa kwenye begi la kubebea viatu karibu na njia ya kutembea kwa miguu huko Newham mnamo 18 Januari 2024, kabla ya kugunduliwa na mtu mmoja aliyekuwa anatembea na mbwa wake.
Vipimo vya DNA alivyofanyiwa vilithibitisha kwamba alikuwa ndugu wa watoto wengine wawili, mvulana na msichana, kila mmoja akiwa amepatikana katika hali kama hiyo mnamo mwaka 2017 na 2019.
Licha ya polisi kufungua mashtaka, wazazi wa watoto hao watatu bado hawajatambuliwa.
"Walituruhusu kuwafuata maafisa waliokuwa wakienda nyumba hadi nyumba wakiwataka wakazi kutoa sampuli za DNA ili kuona ikiwa zinafanana na watoto hao," BBC imesema.
Pia wanawasiliana na watu ambao sampuli zao za DNA zinaendana na mama huyo baada ya kupata taarifa zao kutoka kwenye hifadhidata ya kitaifa ya DNA.
Pia unaweza kusoma:
Rais wa zamani wa Mauritania ahukumiwa miaka 15 jela baada ya kukata rufaa kifungo cha miaka 5

Chanzo cha picha, AFP
Mahakama ya rufaa nchini Mauritania imetoa hukumu ya kifungo cha miaka 15 jela na faini ya dola milioni 3 kwa Rais wa zamani Mohamed Ould Abdel Aziz baada ya kukata rufaa dhidi ya kifungo cha miaka mitano.
Aziz alisaidia kuongoza mapinduzi mawili kabla ya kuhudumu kwa mihula miwili kama rais wa nchi hiyo ya kaskazini magharibi mwa Afrika na kuwa mshirika wa kukabiliana na ugaidi katika mataifa ya Magharibi.
Alihukumiwa mwaka wa 2023 baada ya kupatikana na hatia ya utakatishaji fedha na kujitajirisha. Kulingana na wachunguzi, alikusanya mali yenye thamani ya zaidi ya dola milioni 70 akiwa madarakani. Amekuwa kizuizini tangu kutolewa kwa uamuzi huo.
Kesi hiyo ilikuwa tukio la nadra ambapo kiongozi wa Kiafrika alishtakiwa kwa ufisadi. Mawakili wa Aziz wamesema kesi hiyo imechochewa kisiasa.
Uamuzi huo wa Jumatano uliwaondolea kesi maafisa sita wakuu kutoka kwa utawala wa rais huyo wa zamani, lakini ukamhukumu mkwe wa Aziz kifungo cha miaka miwili jela kwa kosa la ushawishi.
Mauritania ina utajiri mkubwa wa maliasili ikijumuisha madini ya chuma, shaba, zinki, fosfeti, dhahabu, mafuta na gesi asilia.
Lakini bado karibu 60% ya watu wanaishi katika umaskini, kulingana na Umoja wa Mataifa, wakifanya kazi kama wakulima au waajiriwa.
Mashambulizi ya anga ya Israel yaua watu 40 Gaza - Hospitali

Chanzo cha picha, Reuters
Zaidi ya watu 40 wameuawa katika mashambulizi ya hivi punde ya Israel katika Ukanda wa Gaza, kulingana na vyanzo vya hospitali.
Kuna ripoti kwamba takriban miili 36 ilipelekwa katika hospitali za kusini, ambazo zilishuhudia mashambulizi makali ya Israel usiku kucha.
Israeli imeongeza mashambulizi yake huko Gaza huku Rais Donald Trump akiendelea na ziara yake eneo la mashariki ya kati katika juhudi za kusitisha mapigano na kufufa mpango wa kuachiliwa kwa mateka.
Zaidi ya watu 52,000 wameuawa na mashambulizi ya Israel, kulingana na wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas, na wale ambao wamenusurika wako katika hali mbaya.
Tangu katikati ya mwezi Machi, Israel imezuia chakula cha msaada, dawa na misaada mingine kuingia Gaza.
Kumekuwa na shutuma za kimataifa kuhusu kizuizi hicho, ikiwa ni pamoja na kutoka kwa Umoja wa Mataifa, ambayo imesema kwamba wakazi wa Gaza wapatao milioni 2.1 wako katika "hatari kubwa" ya njaa na wanakabiliwa na "kiwango kikubwa cha uhaba wa chakula".
Mashirika ya misaada yameambia BBC kwamba watu wana njaa, wanaugua kutokana na maji machafu, na kwamba wanaugua magonjwa yanayotibika.
Israel haiwaruhusu waandishi wa habari wa kimataifa kuingia Gaza, kwa hivyo tunategemea ujumbe, maelezo ya sauti na picha zinazotumwa kwetu na Wagaza moja kwa moja.
Soma zaidi:
Mashambulizi ya droni yanaongezeka katika awamu mpya ya vita vya Sudan

Chanzo cha picha, Reuters
Wapiganaji wa Rapid Support Forces (RSF) wanaonekana kuanza awamu mpya ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan baada ya kufurushwa kutoka mji mkuu, katika hatua ambayo baadhi ya wataalam wameitaja kuwa "mkakati wa kufikia utawala haraka".
Wiki chache tu baada ya jeshi kusherehekea kutwaa tena mji wa Khartoum, adui wake Rapid Support Forces (RSF) wameanzisha mfululizo wa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani katika Bandari ya Sudan mashariki mwa nchi hiyo.
Mashambulizi hayo yamesababisha hali ya kukatika kwa umeme kuwa mbaya zaidi, huku wakaazi wa jiji hilo wakikumbwa na uhaba wa maji.
"Ni hali ya kukatika kwa umeme katika eneo hili ambayo hatujawahi kushuhudia," alisema Alan Boswell, mtaalam wa Pembe ya Afrika wa Kundi la Kimataifa la Migogoro.
Msururu wa mashambulizi kwenye mji mkuu na kitovu cha shughuli za kibinadamu kunaashiria kwamba RSF imedhamiria na inaweza kuendelea na vita licha ya hasara kubwa za kimaeneo.
Na imeonyesha kuongezeka kwa vita vya droni barani Afrika.
Ndege zisizo na rubani zimechangia kuongezeka kwa mzozo huo, ambao umeingia mwaka wake wa tatu.
Vita hivyo vilianza kama vita vya kuwania madaraka kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na RSF na vimevutia makundi mengine yenye silaha ya Sudan na waungaji mkono wa kigeni, na kuitumbukiza nchi hiyo katika kile ambacho Umoja wa Mataifa unakiita mgogoro mbaya zaidi wa kibinadamu duniani.
Katika miezi ya hivi karibuni RSF wameongeza mashambulizi ya ndege zisizo na rubani kwenye miundombinu muhimu ya kiraia katika maeneo yanayodhibitiwa na jeshi, kama vile mabwawa na vituo vya umeme.
Soma zaidi:
Rais wa Afrika Kusini kukutana na Trump wiki ijayo

Chanzo cha picha, AFP
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa atasafiri kwenda Marekani kwa ziara ya kikazi wiki ijayo na atakutana na Rais wa Marekani Donald Trump Mei 21, ofisi ya Ramaphosa ilisema katika taarifa yake siku ya Jumatano.
"Rais Ramaphosa atakutana na Rais Donald Trump katika Ikulu ya Marekani huko Washington DC kujadili masuala ya maslahi ya pande mbili, kikanda na kimataifa," ofisi ya rais wa Afrika Kusini ilisema.
"Ziara ya rais nchini Marekani inatoa fursa ya uwepo wa uhusiano mpya wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili," iliongeza taarifa hiyo.
Uhusiano kati ya Afrika Kusini na Marekani umedorora sana tangu Trump arejee Ikulu ya Marekani mnamo mwezi Januari.
Trump amekata misaada yote ya kifedha ya Marekani kwa Afrika Kusini, akitaja kutoridhishwa kwa sera yake ya mageuzi ya ardhi na kesi yake ya mauaji ya kimbari katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki dhidi ya mshirika wa Marekani, Israel.
Wiki hii utawala wa Trump ulikaribisha wazungu 49 wa Afrika Kusini ambao umewapa hadhi ya ukimbizi, baada ya kuwachukulia kuwa wahanga wa ubaguzi wa rangi.
Soma zaidi:
Mshawishi wa mitandao ya kijamii Mexico auawa akiwa mubashara kwenye TikTok

Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Valeria Marquez alikuwa na jumla ya wafuasi 200,000 kwenye TikTok na Instagram Mshawishi wa mitandao ya kijamii wa Mexico mwenye umri wa miaka 23 ameuawa kwa kupigwa risasi akiwa anazungumza na mashabiki zake moja kwa moja kwenye TikTok, ofisi ya mwendesha mashtaka wa serikali ilisema.
Valeria Marquez aliuawa wakati mwanamume mmoja alipoingia kwenye saluni yake katika jiji la Guadalajara "na kumfyatulia risasi", kulingana na ofisi ya mwendesha mashtaka wa jimbo la Jalisco.
Sababu ya shambulio hilo baya haijatambuliwa lakini kesi hiyo inachunguzwa kama mauaji dhidi ya wanawake - wakati wanawake na wasichana wanauawa kwa sababu ya jinsia zao, mwendesha mashtaka wa serikali alisema.
Unyanyasaji wa kijinsia ni jambo la kawaida sana nchini Mexico ambapo Umoja wa Mataifa unaripoti wanawake au wasichana 10 wanauawa kila siku na wapenzi au wanafamilia.
Soma zaidi:
Watu 21 wamepoteza maisha katika ajali iliyotokea Mexico - afisa amesema

Chanzo cha picha, Reuters
Takriban watu 21 wamefariki katika ajali ya barabarani katikati mwa Mexico, kulingana na afisa wa eneo hilo.
Ajali hiyo ya magari matatu ilitokea kwenye barabara kuu kati ya Cuacnopalan na Oaxaca katika jimbo la Puebla Jumatano asubuhi, alisema Samuel Aguilar Pala, afisa wa serikali ya mtaa.
Bw Pala alisema watu 18 walifariki katika eneo la tukio na wengine watatu walifariki baadaye hospitalini.
Wengine kadhaa walijeruhiwa na wanapokea matibabu, aliandika kwenye mtandao wa X.
Kulingana na vyombo vya habari vya eneo hilo, ajali hiyo ilihusisha lori, basi na gari dogo.
Gazeti la Mexico la La Jornada linaripoti kwamba ajali hiyo ilitokea wakati lori la saruji lilipojaribu kulipita gari dogo.
Lilipokuwa likivuka kuelekea upande wa pili, lori hilo liligonga basi na kisha kugongana na gari la usafiri uso kwa uso kabla ya kuangukia kwenye bonde lililokuwa chini na kuwaka moto, La Jornada alisema.
Putin hatahudhuria mazungumzo ya amani ya ana kwa ana Uturuki.

Chanzo cha picha, EPA
Rais wa Urusi Vladimir Putin hatahudhuria mazungumzo ya amani kwa ajili ya vita huko Ukraine yatakayofanyika Istanbul Alhamisi, licha ya wito kutoka kwa Volodymyr Zelensky wa Ukraine.
Ujumbe wa Urusi badala yake utaongozwa na msaidizi wa rais Vladimir Medinsky, kulingana na taarifa ya Kremlin.
Zelensky hapo awali alisema kuwa atahudhuria mazungumzo hayo na kukutana ana kwa ana na Putin iwapo rais wa Urusi atakubali, na akasema atafanya kila awezalo kuhakikisha mkutano huo unafanyika.
Rais wa Marekani Donald Trump pia hatahudhuria, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, licha ya awali kudokeza angehudhuria iwapo Putin angekuwepo.
Soma zaidi:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 15/05/2025.
