Utata unaomzunguka mfadhili wa mbegu za kiume aliyezalisha 'watoto 1,000'

Chanzo cha picha, NETFLIX
Baadhi ya familia zinasema zilidanganywa, lakini yeye anasema kwamba hakufanya chochote kibaya, akiongeza kuwa kutoa mbegu zake kuliwapa faraja mamia ya watu.
Jonathan Jacob Meijer mwenye umri wa miaka 43 ambaye alipata umaarufu mwaka wa 2017 baada ya mahakama ya Uholanzi kumwamuru kuacha kutoa mbegu kwa kliniki za uzazi, baada ya kuzaa zaidi ya watoto 100 nchini humo pekee, ambapo sheria inaweka kikomo shughuli hiyo kwa watoto 25.
Kesi yake iliangaziwa tena mwaka wa 2023, ilipobainika kuwa hakufuata amri ya Mahakama.
Meijer aliendelea kuuza mbegu zake za kiume, na mamlaka ya Uholanzi ilikadiria mwaka huo kwamba huenda alizaa hadi watoto 1,000 kote ulimwenguni.

Chanzo cha picha, Getty Images
Sasa wanawake kadhaa ambao walitumia mbegu zake wameshiriki katika makala mapya yaliyoonyeshwa siku chache zilizopita kwenye Netflix, ambapo wanaelezea jinsi walivyodanywa.
Mmoja wao alisema alihisi "kusalitiwa, huzunika na kuwa na hasira" baada ya kugundua Meijer ana watoto wangapi.
Ingawa hakushiriki katika uandalizi wa makala hiyo, alikanusha shutuma dhidi yake katika mahojiano na BBC na kutetea hatua yake akisema kwamba watu wengi waliopokea mbegu zake "wana furaha."
Mchango wa Meijer
Meijer alichangia mbegu zake kwa takribani miaka 17. Mara nyingi, alifanya hivyo kwa faragha, akishughulika na familia moja kwa moja badala ya kupitia kliniki ya uzazi.
Nchini Uholanzi yeye ni baba wa watoto 102, waliozaliwa kutokana na michango iliyotolewa katika kliniki 11.
Kwa kuwa alikuwa amepigwa marufuku kuendelea kuchangia katika nchi hiyo tangu 2017, aliamua kutuma mbegu zake nje ya nchi hadi 2023.
Mwaka huo, mwanamke mmoja na taasisi iliyomuunga mkono walifungua kesi dhidi yake, wakidai kwamba vitendo vyake viliongeza hatari ya kufanya ngono na watoto wao.
Akijitetea mahakamani, Meijer alikiri kuwa na watoto kati ya 550 na 600.
Hata hivyo, mahakama ilisema huenda alizaa watoto 1,000 waliotokana na mchango wa mbegu zake katika mabara kadhaa.
Hatimaye hakimu alimpiga marufuku kutoa mbegu za kiume kwa wazazi wapya, ikisema atatozwa faini ya $100,000 kwa kila mchango.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Baba wa watoto 1,000"
Makala ya Netflix iliyopewa jina "The Man of 1,000 Children," inaangazia mahojiano na familia na wanawake kadhaa ambao waligundua Meijer alikuwa na mamia ya watoto, jambo ambalo inadaiwa hakufichua wakati wa akitoa mbegu zake.
"Nimesikitishwa kwa sababu wakati huo aliniambia alikuwa akichangia familia tano," alisema mmoja wa akina mama hao, ambaye jina lake la kwanza ni Natalie, ambaye pia alihojiwa na BBC.
Natalie aliongeza kuwa alibaini kile alichofanya mfadhili wake kupitia vyombo vya habari.
"Hofu yangu ni kwamba watoto hawa watakutana na kupendana, kwa sababu hawajui ukweli kwamba wanatoka kwa mzazi mmoja," alisema.
Lakini Meijer anasema makala inaangazia wale ambao "hawajafurahishwa" na michango, badala ya familia nyingi anazosema zinashukuru.

Chanzo cha picha, NETFLIX
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Waliita [makala hiyo] 'The Man of 1,000 Children', wakati ilistahili kuwa mchangia mbegu za kiume aliyesaidia familia 550 kupata watoto'," aliiambia BBC.
"Kwa hiyo kuanzia mwanzo wanadanya na kutotosha kimakusudi," aliongeza.
Mwanamume huyo pia aliiambia BBC kwamba "haoni chochote kibaya" kuwa na mamia ya watoto. Alipinga uwezekano wa ndugu wawili wa kambo kuwa na uhusiano wa kimapenzi, kwa sababu yeye si mfadhili asiyejulikana.
“Niwahakikishia kwamba sasa hivi kuna vipimo vya bei nafuu vya chembe chembe za vinasaba yaani DNA na nimeweka yangu kwenye kanzidata ya DNA ili mpate kujua,” alisema.
Meijer alisema itaishtaki Netflix. Lakini mtandao huo wa utiririshaji filamu ulikataa kutoa maoni.
Natalie Hill, mtayarishaji mkuu wa makali hiyo, alisema alitumia miaka minne kutafiti matukio na alizungumza na takriban familia 50 zilizoathirika.
"Familia hamsini zilitoa taarifa za kushtua mahakamani kuhusu uwongo wake na kumsihi hakimu amzuie kutoa michango. Kwa hivyo tuko tayari kuangazia kauli ya Jonathan," alisema.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Seif Abdalla












