Wataalamu: Si kweli mbegu za kiume huogelea katika safari ya utungaji mimba

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Wengi wetu tumejifunza kuhusu mchakato wa kutungisha mimba kwa binadamu kana kwamba ni simulizi.

Hadithi hii inasema kwamba mamilioni ya viluwiluwi wenye vichwa vikubwa na mikia miembamba huogelea kwa furaha katika mazingira ya kuwa na lengo moja: kufikia yai ambalo linangoja wao kuwasili.

Mbegu ya haraka zaidi na nyepesi inayofaulu kukamilisha mbio hizi za marathon hushinda tuzo.

Inashinda yai, hupenya ndani yake, na hivyo kiinitete huanza kuchukua kujitengeneza.

Ama kuwe na maneno zaidi ya haya au machache, hii ni simulizi ambayo kawaida huambatana na mchakato wa utungishaji mimba.

Hata hivyo, hadithi hii inayowasilisha manii kama wakala kamilifu katika upinzani dhidi ya yai, ambalo jukumu lake linachukuliwa kuwa tulivu, halionyeshi kwa usahihi jinsi tukio hili linavyotokea.

Zote—na hasa njia ya uzazi ya mwanamke—hutimiza jukumu muhimu katika uzazi.

‘Vituo vya ukaguzi’

Simulizi hii huanza na kumwaga manii.

Mara tu inapozalishwa, makumi ya mamilioni ya manii huwekwa kwenye uke (inakadiriwa kwamba wastani wa shahawa kutoka inaweza kuwa na karibu mbegu milioni 250).

Wakishafika hapo, lazima kwanza washinde kizuizi cha mlango wa kizazi, Kristin Hook, mwanabiolojia wa mageuzi kutoka timu ya sayansi, tathmini ya teknolojia na uchambuzi wa Ofisi ya Uwajibikaji ya Serikali ya Marekani, anaelezea BBC Mundo.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

‘’Ndani ya njia ya uzazi kuna mfululizo wa kile ninachoweza kuita, kwa mtazamo wa kike, ‘vituo vya ukaguzi’ ambavyo shahawa lazima ipitie ili kufikia eneo la utungisho, ambalo ni mbali kabisa na mahali pa kuingia.’’

Isipokuwa mbegu ziko katika hali nzuri (nyingi zina uharibifu wa DNA au kasoro nyingine), hazitaweza kupita kwenye kizuizi hiki.

‘’Huu ni mchakato muhimu sana wa uteuzi,’’ anasema Daniel Brison, mkurugenzi wa kisayansi wa Idara ya Tiba ya Uzazi katika Chuo Kikuu cha Manchester nchini Uingereza.

‘’Kati ya mbegu milioni kadhaa ambazo hutolewa kwa kumwaga manii, ni mia chache tu zitafikia yai.’’

Mshindo na umajimaji

Hata hivyo, manii haiwezi kufikia mwisho wa mirija ya uzazi peke yake, ambapo mimba hutokea, kwa sababu hazina nguvu za kutosha.

Harakati ambayo manii hufanya katika sehemu za upande ina nguvu mara kumi zaidi kuliko ile ambayo hufanya mbele.

‘’Mbegu za manii haziogelei, lakini zinasukumwa zaidi na mikazo ya tumbo la uzazi,’’ anaelezea Brison.

‘’Kuogelea ni sehemu ndogo tu na hiyo hutokea tu manii inapofikia yai,’’ anaongeza mtafiti.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kuna wanaoeleza kuwa kilele cha mwanamke, kwa kusababisha mshindo, kunaweza kusaidia harakati za mbegu za kiume
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa upande mwingine, umajimaji ndani ya tumbo la uzazi na mirija ya uzazi pia kunaweza kubadilisha njia ya manii, kukuza au kuzuia harakati zao, kubadilisha msimamo wao.

Kwa kifupi, ‘’ni hatua ya mirija ya uzazi, pamoja na mchakato unaoendelea - iwe ina maji ya chumvi au mazito yenye kunatanata, au aina fulani ya asidi yaani pH - vyote vinadhibitiwa na njia ya uzazi wa kike, ambayo itadhibiti jinsi mimba itatokea.

Hiyo ni kusema: ni mbegu gani ya manii itaruhusiwa kukutana na yai la uzazi’’, Virgina Hayssen, profesa wa Biolojia katika Chuo cha Smith huko Marekani, aliambia BBC Mundo.

‘’PH au asidi ya mazingira ya uke iko chini kuliko inavyofaa kwa manii, lakini asidi hii ni muhimu (...) kwa mfululizo wa mabadiliko kutokea katika utando na umeng'enyaji wa manii, ambayo itawawezesha kupata uhamaji zaidi, metaboliki ya haraka, na pia uwezo wa kupenya safu ya nje ya protini ya oocyte (yai lisilokomaa), ambalo ni vigumu sana kupenya,” anaeleza Filippo Zambelli, mtafiti katika Kikundi cha Eugin nchini Hispania, kinachojishughulisha na usaidizi wa uzazi.

Watafiti wengine wanashikilia kuwa kilele cha mwanamke kinaweza pia kuchangia safari hii ya manii kwa kusababisha mishindo ya ndani ya misuli, lakini wengine wanasisitiza kuwa tafiti zaidi zinahitajika ili kudhibitisha nadharia hii.

Safari fupi ya yai

Yai, wakati huo huo, halingojei tu kuwasili kwa manii iliyofaulu kupenya.

Ingawa yai halina uwezo wa kujisogeza lenyewe, silia (aina ya nywele) ndani ya mirija hulisaidia kuelekea chini katika safari fupi inayoanzia kwenye tumbo la uzazi.

‘’Yai husogea kwenye mrija ya uzazi kuelekea kwenye tumbo la uzazi, na kutoa majimaji molekuli za kemikali ambazo huvutia manii na kuziongoza kwa bidii kuelekea huko,’’ anasema Zambelli.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kile tulichojifunza kuhusu utungaji mimba hakilingani kabisa na ukweli.

Yai linaweza kutumia molekuli hizi ‘’kuvuta au kurudisha nyuma, na pia kurekebisha mahali ambapo kila manii huenda,’’ Hayssen anakamilisha.

Kufafanua kukutana kati ya shahawa na yai kuwa tendo la kupenya pia hakuonyeshi kwa usahihi kile kinachotokea, kwa kuwa yai ndilo linalovutia manii na kudhibiti—mara nyingi—kwamba shahawa moja ndiyo inayounganisha.

Muungano huo kwa hakika ni mchakato wa mwingiliano wa pande zote mbili ambapo pande zote mbili huchukua jukumu la utendaji na ambapo mfululizo wa vipokezi na dutu za kemikali huhusika.

Mazingira magumu

Je, mazingira ambayo mbegu za kiume hukua ni ya uadui, kama wanasema?

Kwa maoni ya Hayssen, hili ten ani jingine kwa sababu linaelezea tukio kwa mtazamo wa kiume.

“Ni uadui ukiwa utachukulia kama ushindani na si ushirikiano,” anasema.

‘’Mazingira yanakuza kizazi cha watoto wanaoweza kuishi, hivyo sio uadui kwa lengo, ambalo mwisho wa siku, mtoto anapatikana.’’

Picha: ‘’Mazingira yanajaribu kuzalisha mtoto bora zaidi, ambayo yanaweza kuwezesha watoto wengi, kwa hiyo mazingira hayawezi kuwa na uadui.

Ukiiangalia ‘’ kwa mtazamo wa kike, tumbo la uzazi linafanya kile kinachohitajika kufanywa ili kumnufaisha mama katika kupata watoto bora.

Teknolojia mpya, mawazo ya zamani

Ingawa baadhi ya maelezo ya mchakato wa utungaji mimba yamejulikana hivi karibuni kutokana na kuendeleza utafiti wa kisayansi, habari nyingi, kama vile umuhimu mdogo wa uhamaji wa mbegu za kiume, zimejulikana kwa miongo kadhaa.

Mwanaanthropolojia wa Kimarekani Emily Martin alikuwa mmoja wa watu wa kwanza kuelekeza fikira kwenye lugha inayotumiwa kuzungumzia utungisho, na kuona jinsi maadili ya kitamaduni kwa ujumla yanavyoingia katika jinsi wanasayansi wanavyoelezea uvumbuzi wao kuhusu ulimwengu kiuhalisia.

Maandishi yake ya kitaaluma - yaliyochapishwa mwanzoni mwa miaka ya 1990 - ambayo yanachambua kwa undani mila potofu ya kijinsia iliyofichwa katika maandishi ya kisayansi juu ya mada hiyo, ikawa sehemu ya kumbukumbu ya suala la usawa wa kijinsia.

Wataalamu hao waliozungumza na BBC Mundo pia wanataja ukosefu wa uwakilishi wa wanawake katika sayansi na pia katika maeneo ya kufanya maamuzi katika elimu.

‘’Kuendelea kukosekana kwa uwakilishi katika sayansi ya watu wenye mitazamo tofauti kutaathiri aina ya maswali unayouliza na maelezo utakayopata,’’ anasema Kristin Hook.

Hayssen anasisitiza haja ya kuhoji istilahi tunazotumia na kutumia lugha isiyoegemea upande wowote: tunapaswa kutumia ‘’mimba na si utungishaji’’, kwa mfano.

Lakini kuondoa upendeleo wa kijinsia katika ufahamu wetu wa utaratibu wa utungaji mimba si lazima tu kusahihisha taarifa potofu za kisayansi na kueleza kwa usahihi michakato ya kibiolojia.

Pia ni hatua ya kimsingi ya kuboresha matibabu yaliyopo ya kusaidiwa ya uzazi na kutoa nafasi kwa teknolojia mpya.

Pia unaweza kusoma: