Arsenal na Manchester City katika mbio za kipekee za mataji manne

Saliba&Haaland

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Arsenal na Manchester City zinajaribu kufukuzia kushinda mataji manne msimu huu
    • Author, Chris Adams
    • Nafasi, BBC Sport journalist
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Arsenal na Manchester City ziko katika mbio za kipekee msimu huu wakisaka kutwaa mataji manne makubwa kwa wakati mmoja – jambo linalojulikana kama "Quadruple". Haya ni mataji ya Ligi kuu England (EPL), Kombe la FA (FA Cup), Kombe la ligi (EFL Cup) na Ligi ya mabingwa Ulaya (UEFA Champions League), ambayo yanahesabika kuwa mafanikio makubwa zaidi kwa ngazi ya klabu ndani na nje ya England.

Katika makala hii, "Quadruple" inarejelea ushindi wa mataji manne tajwa juu yanayotambuliwa katika soka la England na Ulaya na yaliyo kwenye mtindi wa ligi ama mtoano katika msimu. Mashindano mengine kama FA Community Shield, UEFA Super Cup au Kombe la dunia la vilabu (FIFA Club World Cup) hayahesabiwi katika mazungumzo ya "Quadruple", kwa sababu ni mechi za ufunguzi wa mwanzo wa msimu au mfano Kombe la dunia la vilabu ni mashindano mafupi na yote haya hayana hatua nyingi kwenye msimu wote kama ilivyo kwa mataji manne makubwa yanayozungumziwa.

Sasa kwa mara ya kwanza katika historia ya soka la England, klabu mbili zimeingia mwezi Machi zikiwa bado zinawania mataji yote manne. Arsenal na Manchester City zinaonekana kuwa na uwezo wa kufanya hivyo, kwani zote zinapambana kuwania ubingwa wa ligi kuu, bado zipo katika mashindano ya FA Cup na ligi ya mabingwa, huku pia zikitarajiwa kukutana katika fainali ya EFL Cup baadaye mwezi huu.

Arsenal walifanikiwa kusonga mbele katika mashindano ya FA Cup baada ya kuwachap 2-1 Mansfield Town Jana Jumamosi, wakati Manchester City nao walisonge mbele kwa kuwafunga Newcastle United 3-1. Hii ina maana timu zote mbili zinaendelea kushindania mataji hayo manne, huku droo ya hatua za mtoano ya ligi ya mabingwa ikiashiria kuwa haziwezi kukutana katika hatua za sasa, zinaweza kukutana tu katika fainali mwezi Mei.

Hata hivyo, historia inaonyesha kuwa kushinda mataji manne ndani ya msimu mmoja si jambo rahisi. Klabu pekee iliyowahi kufanya hivyo barani Ulaya ni Celtic F.C., ambao walitwaa mataji yote mwaka 1967. Mafanikio yao yalihitimishwa kwa ushindi dhidi ya Inter Milan katika fainali ya Kombe la Ulaya, huku kikosi chao maarufu cha "Lisbon Lions" kikiwa kimeundwa na wachezaji waliokulia mtaani karibu na uwanja wa Celtic Park. Je kuna timu zilizokaribia kufanya hivyo?

Celtic players celebrate with European Cup trophy after winning final against Inter Milan in Lisbon 25th May 1967

Chanzo cha picha, Mirrorpix via Getty Images

Maelezo ya picha, Magwiji wa Celtic 'Lisbon Lions' wakifurahia taji lao la Ulaya mwezi May 1967 - klabu pekee ya Ulaya iliyofanikiwa kutwaa mataji manne

Timu zilizowahi kukaribia kutwaa makombe manne

Ingawa baadhi ya klabu zimewahi kushinda mataji matatu makubwa, hakuna iliyofanikiwa kufikia Quadruple nchini England. Manchester United walitwaa mataji matatu mwaka 1999, huku Manchester City wakifanya hivyo mwaka 2023. Hata hivyo, timu zote mbili ziliondolewa mapema katika EFL Cup, jambo lililowazuia kupigania mataji yote manne hadi mwishoni mwa msimu.

Klabu nyingine iliyokaribia kufikia rekodi hiyo ni Liverpool F.C. katika msimu wa 2021–22. Liverpool walikuwa tayari wameshinda vikombe viwili vya ndani ya England, lakini walikosa ubingwa wa ligi kwa tofauti ya alama moja tu siku ya mwisho ya msimu. Baadaye walipoteza fainali ya ligi ya mabingwa dhidi ya Real Madrid siku sita baadaye.

Chelsea walikuwa pia katika mbio za mataji manne msimu huo. Hata hivyo walipoteza fainali ya EFL Cup kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Liverpool tarehe 27 Februari, kabla ya Liverpool pia kuwafunga katika fainali ya FA Cup. Kikosi cha kocha Thomas Tuchel, ambacho kilikuwa kinaongoza ligi kuu mwezi Desemba, kilimaliza msimu katika nafasi ya tatu na baadaye kuondolewa katika robo fainali ya ya ligi ya mabingwa Ulaya. Hali hiyo inaonyesha kuwa hata timu ikiwa kwenye mbio za mataji manne inaweza kuishia kukosa yote, ingawa Chelsea walipata faraja ya kushinda UEFA Super Cup na FIFA Club World Cup msimu huo.

Chelsea pia waliwahi kukaribia sana mafanikio hayo katika msimu wa 2006–07, lakini walishindwa kutwaa mataji makubwa mawili yaliyokuwa muhimu zaidi. Kikosi cha kocha José Mourinho, ambacho kilikuwa kinashikilia ubingwa wa Premier League, kiliondolewa katika nusu fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya baada ya kufungwa kwa mikwaju ya penati na Liverpool F.C. Ilikua Mei mosi. Wiki iliyofuata matumaini yao ya kutwaa ubingwa wa ligi yakawa hayawezekani tena kihesabu, huku kombe hilo likichukuliwa na Manchester United.

Hali kama hiyo iliwahi kuwakumba pia Manchester United katika msimu wa 2008–09. Ingawa walionekana kuwa kwenye mbio za mataji manne, walimaliza msimu wakiwa na mataji mawili pekee. Aprili 19 walitolewa na Everton F.C. katika nusu fainali ya FA Cup kwa mikwaju ya penati, kabla ya United kufungwa na FC Barcelona katika fainali ya Ligi ya mabingwa Ulaya iliyochezwa wiki sita baadaye.

Nje ya England hali ikoje?

Katika sehemu kubwa ya Ulaya, mashindano ya aina ya kombe la ligi (League Cup) hayapo, jambo linalofanya jambo la kutwaa mataji manne 'Quadruple' kuwa nadra. Nchini Ufaransa, mashindano ya Coupe de la Ligue yalifutwa mwaka 2020, wakati Hispania na Ujerumani pia waliwahi kuwa na mashindano kama hayo kwa muda mfupi kabla ya kufutwa.

Hata hivyo, baadhi ya klabu zimewahi kushinda mataji manne kwa tafsiri pana zaidi ikiwa ni pamoja na taji la Super Cup. Mfano ni Bayern Munich mwaka 2013 na Paris Saint‑Germain katika misimu ya hivi karibuni.

PSG walikaribia sana kufikia mafanikio makubwa mwaka 2020 waliposhinda mataji matatu ya ndani ya Ufaransa chini ya kocha Thomas Tuchel, lakini walipoteza fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya dhidi ya Bayern Munich.

Paris Saint-Germain coach Thomas Tuchel (L) and forward Kylian Mbappe (C) receive their runner-up medals from Uefa president Aleksander Ceferin (R) after Bayern Munich won the Uefa Champions League final 1-0 at the Luz stadium in Lisbon on August 23, 2020.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Thomas Tuchel's Kylian Mbappe-inspired Paris Saint-Germain team came within a whisker of the Quadruple in 2020

Baada ya Arsenal na City zote kutinga robo fainali ya FA Cup Jumamosi, sasa macho ya mashabiki yanaelekezwa kwenye fainali ya EFL Cup itakayochezwa Wembley tarehe 22 Machi utakaozikutanisha timu hizo. Mchezo huo unaweza kuwa hatua muhimu katika mbio za mataji manne.

Timu hizo pia zitakutana tena katika mchezo wa ligi kuu utakaochezwa kwenye uwanja wa Etihad tarehe 19 Aprili, pambano ambalo pia linaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuamua bingwa wa Ligi kuu msimu huu. Kwa sasa, mbio za kutwa mataji manne 'Quadruple' zinaendelea na msisimko unaongezeka kadiri msimu unavyoelekea katika hatua zake za mwisho.