Ligi Kuu ya England: Timu gani itaizuia Man City kutwaa tena ubingwa?

Chanzo cha picha, Getty Images
Swali la kila mwaka ni hili - kuna timu yoyote inayoweza kuizuia Manchester City kuchukua ubingwa?
Kwa msimu wa tisa mfululizo kikosi hicho cha Pep Guardiola kinapewa nafasi kubwa ya kutwaa taji la Ligi Kuu ya Uingereza.
Wameshinda mataji sita kati ya saba yaliyopita, yakiwemo manne mfululizo.
BBC Sport inazitazama timu saba, wapinzani wa City walio na uwezo pia wa kutwaa taji. Timu zimepangwa kulingana na nafasi zao za kumaliza msimu uliopita.
Arsenal
Mwisho wa msimu uliopita, walikuwa nafasi ya pili, pointi mbili chini ya City. Wamemaliza washindi wa pili chini ya City katika misimu miwili iliyopita.
The Gunners wamefanya mabadiliko makubwa, wamemleta mlinzi wa Italia Riccardo Calafiori kutoka Bologna kwa ada ya pauni milioni 42. Anaweza kucheza beki wa kushoto au wa kati.
Pia wamegeuza mkataba wa mkopo kuwa wa kudumu kwa kipa wa Uhispania, David Raya, ambaye alimpiku Aaron Ramsdale na kuwa nambari moja msimu uliopita.
Winga wao Bukayo Saka ndiye mfungaji wao bora katika misimu miwili iliyopita. Na wanahusishwa kutaka kumnunua mshambuliaji wa Napoli, Victor Osimhen.
“Nahodha wa Arsenal, Martin Odegaard alisema mwishoni mwa msimu uliopita kwamba, wameibadilisha klabu na anaamini Arsenal watashindania taji kwa muda mrefu," anasema mwandishi wa michezo wa BBC, Alex Howell.
Liverpool
Mwisho wa msimu walikuwa nafasi ya tatu, pointi tisa chini ya City. Liverpool wanaanza msimu bila ya meneja Jurgen Klopp kwa mara ya kwanza tangu 2015-16.
Klopp alitangaza ataondoka mwishoni mwa msimu, lakini tangazo lake lilikuja katikati ya msimu uliopita - na nafasi yake imechukuliwa na Arne Slot mwezi Mei.
Mdachi huyo anaonekana kubadilisha mtindo wa uchezaji wa Liverpool kutoka mchezo wa nguvu na haraka hadi ule wa kumiliki mpira.
Liverpool ndio timu pekee mbali na City kushinda taji la Ligi Kuu katika kipindi cha miaka saba iliyopita, bado hawajasajili mtu yeyote msimu huu - lakini Slot anatumai watasajili.
Mwandishi mwandamizi wa kandanda wa BBC Sport, Nizaar Kinsella, anasema: "Liverpool wanatarajia kuleta ushindani katika msimu wa kwanza wa Slot baada ya enzi nzuri chini ya Jurgen Klopp na kuiacha klabu katika nafasi nzuri.”
Aston Villa

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwisho wa msimu uliopita walikuwa nafasi ya nne na pointi 23 chini ya City. Ilifuzu Ligi ya Mabingwa kwa kufanikiwa kumaliza katika nafasi ya nne msimu uliopita.
Unai Emery ameigeuza klabu hiyo kutoka kugombea kutoteremka daraja hadi timu ambayo inazungumzwa kama mshindania taji msimu uliopita - na hata hajaiongoza kwa miaka miwili bado.
Klabu hiyo inalazimika kuuza wachezaji msimu huu wa joto ili kutimiza kanuni za faida na kifedha za Ligi Kuu ya Uingereza.
Lakini wameleta sura nyingi mpya - ikiwa ni pamoja na kiungo wa Everton. Amadou Onana, beki wa kushoto wa Chelsea, Ian Maatsen, kiungo wa kati wa Luton, Ross Barkley - na vijana wa akademi Jaden Philogene na Cameron Archer.
Tottenham Hotspur

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwisho wa msimu uliopita walikuwa watano, wakiwa chini ya City kwa alama 25. Walianza vyema msimu uliopita chini ya Ange Postecoglou na walikuwa nyuma kwa pointi tano kileleni baada ya mechi 10.
Archie Gray, pauni milioni 30 kutoka Leeds, Lucas Bergvall pauni milioni 8.5 kutoka Djurgarden na George Feeney kutoka Glentoran - aliyesajiliwa kwa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 18, ndio pekee waliosajiliwa majira ya joto hadi sasa.
Winga chipukizi wa Korea Kusini, Yang Min-hyuk atajiunga na kikosi hicho mwezi Januari.
Mikey Moore, mshambuliaji wa akademi mwenye umri wa miaka 16, amevutia katika mechi za kirafiki za kabla ya msimu mpya.
Mwandishi wa BBC Sport Nizaar Kinsella anasema: "Meneja Postecoglou ndiye atakayeisukuma Tottenham kushinda kwa mara ya kwanza tangu 2008. Hatataka kuweka kikomo katika malengo ya Spurs lakini kufuzu Ligi ya Mabingwa litakuwa lengo lao kubwa zaidi."
Chelsea
Mwisho wa msimu uliopita ilishika nafasi ya sita na alama 28 chini ya City. Kocha Enzo Maresca, baada ya kuifundisha Leicester na kupanda daraja, alichukua nafasi ya Mauricio Pochettino katika kiti moto cha The Blues.
Wamesajili wachezaji wengi majira ya kiangazi - Kiernan Dewsbury-Hall, Tosin Adarabioyo na Omari Kellyman wote wana uzoefu wa Ligi Kuu.
Beki mkongwe wa kati Thiago Silva, pamoja na Hakim Ziyech, Ian Maatsen, Lewis Hall na Omari Hutchinson - wote walikuwa nje kwa mkopo msimu uliopita – wameondoka moja kwa moja. Na Conor Gallagher anatarajiwa kuhamia Atletico Madrid.
Mwandishi wa BBC Sport Nizaar Kinsella anasema: "Kufuzu Ligi ya Mabingwa na kufanikiwa kupata vikombe yatakuwa ndio matarajio yao, lakini pia kuna matumaini kwamba kikosi hiki cha vijana kinaweza kukua na kuleta ushindani katika misimu ijayo."
Newcastle United
Mwisho wa msimu uliopita ilishika nafasi ya saba na pointi 31 chini ya City. Newcastle walifanya vyema msimu wa 2022-23 kwa kufuzu Ligi ya Mabingwa, lakini kumaliza katika nafasi ya saba msimu uliopita kulionekana kama kushuka chini.
Sasa Newcastle wanatumai watambakiza meneja Eddie Howe, ambaye anapendekezwa kuwa kocha wa England.
Mwandishi wa kandanda wa BBC Sport Simon Stone anasema: "Nilifadhaika kuhusu Newcastle kwamba wanalemewa na sheria za kifedha, ikimaanisha kuwa wanalazimika kuuza wachezaji wakati wanataka kununua.
"Habari njema ni Alexander Isak, Bruno Guimaraes na Anthony Gordon wote bado wako kwenye klabu."
Manchester United

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwisho wa msimu walikuwa nafasi ya nane na pointi 31 chini ya City. Walimaliza vibaya zaidi tangu ligi ya msimu wa 1989-90, walipomaliza katika nafasi ya nane – ingawa msimu huu wameshinda Kombe la FA.
Meneja Erik ten Hag alitarajiwa kupoteza kibarua chake, lakini United waliamua kubaki na Mholanzi huyo ambaye ameshinda mataji katika misimu yake yote miwili klabuni hapo.
Manchester United wametumia pesa kununu vijana wawili msimu huu - mshambuliaji wa Bologna, Joshua Zirkzee kwa pauni milioni 36.5 na mlinzi wa kati wa Lille, Leny Yoro kwa pauni 52.
Hata hivyo, tayari Yoro amejeruhiwa na huenda akakaa nje ya uwanja kwa miezi mingi. Vilevile, wachezaji kadhaa wameondoka kwa uhamisho wa bure akiwemo mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa, Raphael Varane na Anthony Martial.
Mwandishi wa BBC Sport, Simon Stone anasema: "Erik ten Hag lazima aepuke kufanya vibaya msimu huu kwa sababu hawezi kumudu kumaliza nafasi ya nane tena.”
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah












