Je, Manchester United iko tayari kupigania taji la ligi baada ya matokeo mabaya dhidi ya wapinzani?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Simon Stone
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Manchester United ilikamilisha ziara yake ya mechi tatu nchini Marekani, kwa kuchapwa mabao 3-0 na wapinzani wao wa muda mrefu Liverpool huko South Carolina.
Vijana wa Erik ten Hag walirejea nyumbani na ushindi mmoja tu, dhidi ya Real Betis ya Uhispania. Walipoteza dhidi ya Arsenal na Liverpool, zote za Uingereza.
Ligi Kuu ya Uingereza ya 2024-25, itaanza baada ya wiki mbili kutoka sasa. BBC Sport imeifuatilia United kwenye safari yao.
Ten Hag hakuwa na wasiwasi baada ya michezo hiyo wala hakukumbana na ukosolewaji mkubwa kutoka kwa mashabiki wa United, amesisitiza tu umoja ndani ya kambi ya Old Trafford.
Lakini anaelewa kama meneja wa klabu kubwa, ikiwa United hawataimarika na kumaliza vizuri katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Uingereza, basi atakuwa na hatima mbaya.
Jukumu lake la kwanza sasa litakuwa ni kukusanya kikosi chake, baada ya mashindano ya Euro 2024 na Copa America, kikosi kitakachokuwa imara vya kutosha kucheza Ngao ya Jamii dhidi ya Manchester City ambao bado wako imara.
Tatizo la United

Chanzo cha picha, Getty Images
Jeraha la msuli wa paja alilopata Rasmus Hojlund muda mfupi baada ya kufunga bao zuri la kwanza katika kipindi cha kwanza dhidi ya Arsenal kwenye Uwanja wa SoFi mjini Los Angeles, lilikuwa baya kwa mchezo.
Mchezaji mpya Joshua Zirkzee, aliyekuwa kwenye majukumu ya timu ya taifa ya Uholanzi kwenye Euro 2024, ni mchezaji ambaye bado hajafanya mazoezi na kikosi kikuu.
Kocha aliweka kando wazo la msimu uliopita la kumuweka Marcus Rashford katikati, akisema anapendelea Muingereza huyo acheze upande wa kushoto na kuingia ndani.
Jadon Sancho, amerejea kwenye kikosi, lakini bado hachezi vizuri kwenye nafasi ya kati.
Kuna uwezekano mkubwa, Ten Hag kumtumia nahodha Bruno Fernandes kucheza namba tisa, hasa kwa vile wachezaji wawili, Mason Mount na Scott McTominay, wamecheza vyema namba kumi katika ziara hiyo.
Amass ameibuka, lakini Shaw anahitajika

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika uwanja wa Williams-Brice huko Columbia, uchezaji wa chipukizi Harry Amass upande wa beki ya kushoto alipokuwa akipambana na Mo Salah, ulivutia sana.
Amass mwenye umri wa miaka kumi na saba anaweza kuwa mchezaji mzuri kwa United, ikiwa Luke Shaw atawekwa benchi katika msimu mgumu na kalenda ngumu ya klabu hiyo.
Amass alifanya vyema dhidi ya Salah. Hatukutarajia chipukizi huyo wa zamani wa Watford kushinda kila zuio dhidi ya nyota huyo mzoefu na wa kiwango cha kimataifa, lakini alifanya kazi nzuri na kuonyesha kwamba anaweza kumdhibiti. Hata hivyo, United - na Ten Hag – bado wanamuhitaji Shaw akiwa imara.
Onana ataimarika msimu huu?
Bao la tatu la Liverpool la Jumamosi usiku limewatia wasiwasi mashabiki wa United kwa sababu lilihusisha makosa ya upangaji ya kipa Andre Onana, makosa ya aina hiyo yalitokea mara nyingi wakati wa mechi zake za awali.
Mipango ya uhamisho

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Sir Dave Brailsford, Omar Berrada, Dan Ashworth na Jason Wilcox hawataichezea Manchester United msimu huu.
Hawakumnunua Casemiro, lakini wanatakiwa kukabiliana na hali halisi ya kifedha ya Mbrazil huyo kuwa atalipwa mshahara mkubwa kwa miaka mingine miwili huku akicheza ovyo na kumruhusu Fabio Carvalho kumpita ndani ya eneo la hatari kwa bao la kwanza la Liverpool siku ya Jumamosi.
Ni bahati mbaya kwa Leny Yoro kupata jeraha ndani ya wiki mbili baada ya kuwasili kutoka Lille kwa pauni milioni 52, akiwa na umri wa miaka 18.
United inahitaji kuleta beki mwingine wa kati. Lakini kufanya hivyo, ni lazima kumuuza Victor Lindelof, na labda Harry Maguire, jambo ambalo sio rahisi.
Ndivyo ilivyo pia kwa beki wa kulia, kwani huenda Aaron Wan-Bissaka akampisha beki Noussair Mazraoui wa Bayern Munich.
Tatizo la United ni la kikosi kizima, kuna wachezaji wenye mikataba mikubwa, na ambao hawajaonyesha kiwango kizuri kwa thamani ya pesa walizonunuliwa.
Muulize meneja yeyote wa kiwango chochote, ufunguo wa mafanikio ni nini, atasema kuajiri.
Muundo mpya wa United unajumuisha wajumbe wa bodi, mtendaji mkuu mpya, mkurugenzi wa michezo na mkurugenzi wa kiufundi.
Ni kazi yao kwa pamoja kuhakikisha makosa ya zamani hayarudiwi tena.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












