Mchezaji wa Benfica anayevutia klabu kuu za Ulaya

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Joao Neves
Muda wa kusoma: Dakika 4

Ikiwa klabu yako itakuwekea kipengele cha kuachiliwa cha zaidi ya £100m, kwa kawaida ni ishara kuwa wewe ni mchezaji maalum. Hiyo inaweza kuwa hivyo kwa mchezaji Joao Neves, kiungo wa kati wa Benfica ambaye anatarajiwa kuhamia klabu kubwa msimu huu.

Neves, 19, ameripotiwa kuvutiwa na Manchester United na Arsenal, lakini ni Paris St-Germain ambayo inazungumziwa kuwa klabu anayoelekea kujiunga nayo zaidi.

Kijana huyo tayari ameisaidia klabu yake ya utotoni kutwaa taji la ligi na kucheza michuano ya Uropa kabla ya kufikisha miaka 20.

Je, Neves atafuata nyayo za wachezaji maarufu kama vile Bernardo Silva, Ruben Dias na Enzo Fernandez na kuwa mchezaji anayelekea kujiunga na klabu kubwa kutoka Lisbon?

Neves, mhitimu wa akademi ya klabu ya Benfica, alipata nafasi yake katika kikosi cha kwanza kutokana na kuondoka kwa Fernandez.

Kinda huyo alicheza mechi yake ya kwanza tarehe mosi mwezi Januari 2023 kabla ya Chelsea kutumia kitita kikucha cha fedha kilichovunja rekodi ya Uingereza kumleta kiungo wa kati wa Argentina Fernandez kwenye Ligi ya Premia siku ya mwisho ya uhamisho baadaye mwezi huo.

"Bila Enzo ubora wetu ulipungua," anaelezea Filipe Ingles, kutoka podcast Benfica FM, ambaye alihofia kuwa taji linaweza kupotea kutoka kwa mikono ya Eagles.

Bosi Roger Schmidt alimgeukia Neves miongoni mwa wachezaji wake na kiungo huyo alilipa imani hiyo kwa kufunga bao katika sare ya 2-2 dhidi ya wapinzani wao Sporting ambayo ilionekana kuwa muhimu katika kushinda ligi kwa mara ya kwanza baada ya miaka minne.

"Mchezo uliofuata tulishinda, tulikuwa mabingwa na Joao Neves alikuwa shujaa aliyeokoa siku katika dakika za mwisho," anasema Ingles.

Neves amecheza mechi 50 za Primeira Liga, akianza mara 33 kati ya hizo, huku akifunga mara nne na kusajili moja.

"Alikua kiungo kikuu katika kikosi cha kwanza na pengine alikuwa mchezaji wetu bora msimu mzima," anaongeza Ingles. "Kulikuwa na mechi ambapo meneja na timu alizomewa, lakini sio yeye kamwe. Kwa sababu mashabiki wa Benfica wanamuona kama mmoja wao na huwa anacheza vizuri na kujitolea."

Kiungo huyo pia alifanikiwa kimataifa na hadi sasa ameichezea Ureno mara tisa, ikiwa ni pamoja na katika mechi zao mbili za Euro 2024.

Nini cha kutarajia kutoka kwa Joao Neves?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Neves mara nyingi hutumika kama kiungo ambaye ni wa nne kwa kusaidia kutoa pasi za ufungaji wa magoli mbali na kuweza kuzuia mipira na kuwakaba wapinzani.

"Watu wengi nchini Ureno wanamlinganisha na Joao Moutinho," anasema Ingles, ambaye pia anafananisha mtindo wake na Xavi au Andres Iniesta.

"Ni aina ya kiungo wa kati anayeonekana kufanya kila kitu vizuri - pasi, nafasi, mguso wa kwanza, usawa wa timu.

"Unaona kwamba kila mara anakimbia na kufikiria kuhusu mchezo, halegei hata dakika moja, hatoki kwenye nafasi yake. Na anapkkuw na mpira hana wasiwasi."

Neves ana umri wa miaka 19 pekee na hajacheza hata misimu miwili kamili ya soka la daraja la juu, lakini Ingles anasema amethibitisha kuwa "amekomaa sana".

"Aliingia kwenye kikosi cha kwanza kwenye mechi zenye mvutano zaidi," anaongeza. "Na ilionekana kama alikuwa katika nafasi hiyo kwa miaka 10.

"Mama yake alikufa miezi michache iliyopita na siku kadhaa baadaye alikuwa akicheza, licha ya Benfica kumwambia anaweza kumuomboleza."

Neves pia alikuwa mchezaji aliyetumika baada ya kile Ingles wanachokiita "kukumbatia" kichapo cha 5-0 kutoka kwa Porto mapema msimu ulipoanza

"Yeye ndiye aliyekuja na kuzungumza na mashabiki baada ya mchezo," anasema. "Si [Nicolas] Otamendi, si [Angel] Di Maria. Yeye ndiye aliyekuja kuzungumza na waandishi wa habari."

Je, huu ndio wakati mwafaka wa kuhama?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Joao

Rais wa Benfica, Rui Costa, alithibitisha kuwa ofa ilikuwa imetolewa kwa Neves alipozungumza na gazeti la Ureno la A Bola, lakini hakufichua ni nani aliyewasilisha ombi.

"Kuna ofa mezani ambayo inatathminiwa na inajadiliwa," gwiji huyo wa Ureno alisema.

"Lakini kwa wakati huu, Joao Neves anasalia kuwa mchezaji wa Benfica. Sio kwamba nataka kuficha anayeingia na anayetoka sababu ninaelewa kwamba mashabiki wa Benfica wanataka kujua kama Joao ataondoka au la."

Kujibu ripoti kwamba Neves angeondoka tu kwa kifungu chake cha kuachiliwa kwa pauni milioni 101, rais aliongeza: "Sikusema kamwe kwamba Joao Neves angeondoka tu kwa kifungu chake cha kuachiliwa na kwa hivyo, madai hayo ni ya uwongo."

Ingles anahofia hatua yoyote pia inaweza kuja mapema sana kwa mchezaji huyo - lakini anaamini inaweza kuwa ni rahisi kwake kutulia katika Ligue 1 ya Ufaransa kuliko Ligi ya Premia.

"Licha ya ukomavu wake, nadhani anafanya makosa sawa na Joao Felix, Goncalo Ramos au Renato Sanches: anaondoka haraka sana," anasema.

"Sijui kama yuko tayari. Na kama ilivyo kwa Darwin Nunez, ni jambo moja kuwa mzuri kwenye ligi ya Ureno, ni jambo lingine katika ligi tano bora.

"Hapa kama wewe ni mzuri, unajitokeza. Uingereza, kila mtu karibu nawe ni mzuri au bora, kwa hivyo unajitahidi. Yeye ni mdogo sana na sijui kama angeweza kukabiliana na ufahamu wa Ligi Kuu."

Kwa hiyo amepangiwa kwenda ligi ya juu kabisa?

"Ningecheza kamari kuwa atakuwa mchezaji mzuri sana, atafanya kazi nzuri sana, lakini hatakuwa mchezaji wa kiwango cha kimataifa," anaongeza Ingles. "Lakini nani anajua, ana miaka 19 tu."

Imetafsiriwa na Seif Abdalla na kuhaririwa na Yusuf Jumah