Mchezaji gani atashinda tuzo ya Ballon d'Or 2024?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Emlyn Begley
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Walioteuliwa kuwania tuzo ya mchezaji bora wa dunia watatangazwa tarehe 4 Septemba. Msimu wa 2023-24 na mashindano makubwa ya msimu huu wa kiangazi ni mambo yatakayozingatiwa.
Vinicius Junior wa Real Madrid na Jude Bellingham, wameshindwa mtawalia kushinda mashindano yao ya makombe ya bara wakiwa na Brazil katika Copa America na England katika Euro 2024, bila shaka hilo limefungua mlango kwa wachezaji wengine pia.
BBC Sport inawaangazia wachezaji sita wenye uwezo wa kushinda tuzo hiyo tarehe 28 Oktoba mjini Paris, Ufaransa.
Vinicius Junior (Real Madrid, Brazil)

Chanzo cha picha, Getty Images
Amecheza michezo 49, amefunga mabao 26, amepiga pasi za mwisho 11, makombe ni La Liga, Champions League na Spanish Super Cup.
Winga wa Real Madrid Vinicius, 24, amekuwa akitajwa kuwania tuzo ya Ballon d'Or kwa muda mrefu baada ya kuisaidia timu yake kushinda La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Alimaliza msimu akiwa mfungaji bora wa Real Madrid kwa mabao 24 na pasi za mabao 11.
Kama Brazil ingeshinda Copa America pengine angekuwa na uhakika wa kutwaa tuzo hiyo - lakini walitolewa katika robo fainali kwa mikwaju ya penalti na Uruguay, mchezo ambao Vinicius aliukosa kwa sababu ya kufungiwa baada ya kupewa kadi mbili za njano katika hatua ya makundi.
Mbrazil wa mwisho kushinda Ballon d'Or alikuwa Kaka mwaka 2007, na Neymar pekee ndiye aliyemaliza katika nafasi tatu za juu tangu wakati huo.
Rodri (Manchester City, Uhispania)

Chanzo cha picha, Getty Images
Amecheza michezo 63, amefunga mabao 12. Ametoa pasi za mwisho za magoli 14. Makombe aliyobeba ni Premier League, Uefa Super Cup, Club World Cup, Euro 2024.
Kiungo wa kati Rodri, 28, ana mataji manne Ligi Kikuu ya Uingereza, Uefa Super Club na Kombe la Dunia la Klabu akiwa na Manchester City, na kisha Euro 2024 akiwa na Uhispania.
Alitoka nje ya uwanja akiwa ameumia wakati wa mapumziko kwenye fainali ya Euro dhidi ya England lakini tayari alikuwa amefanya vya kutosha kutangazwa mchezaji bora wa michuano hiyo.
Hakuna mchezaji wa Manchester City ambaye amewahi kushinda Ballon d'Or akiwa na klabu hiyo.
Jude Bellingham (Real Madrid, Uingereza)

Chanzo cha picha, PA
Michezo aliyocheza ni 54. Mabao kafunga 27. Katoa pasi za mwisho 16. Makombe aliyoshinda ni La Liga, Champions League, Spanish Super Cup.
Kiungo wa kati wa Uingereza Bellingham, 21, alikuwa na msimu mzuri akiwa na Real Madrid kufuatia uhamisho wa msimu uliopita wakati wa kiangazi kutoka Borussia Dortmund.
Alimaliza akiwa na mabao 23 - ikiwa ni pamoja na ushindi wa dakika za lala salama katika mechi zote mbili za La Liga akiwa na Barcelona - na pasi za mwisho 13 kwa klabu yake waliposhinda ligi ya Uhispania na Ligi ya Mabingwa.
Wakati wake wa kuvutia zaidi kwenye Euro 2024, ulikuwa mpira wa juu wa dakika za majeruhi, bao lililopelekea mchezo wa 16 bora wa England dhidi ya Slovakia kwenda muda wa ziada.
Kama angeiwezesha Uingereza kushinda katika fainali dhidi ya Uhispania, huenda angekuwa mshindi wa kwanza wa Ballon d'Or kutoka Uingereza tangu Michael Owen mwaka 2001.
Dani Carvajal (Real Madrid, Uhispania)

Chanzo cha picha, Getty Images
Michezo aliyocheza ni 54. Mabao aliyofunga ni 7. Pasi za mwisho alizotoa ni 8. Makombe ni La Liga, Champions League, Spanish Super Cup, Euro 2024.
Beki wa kulia Carvajal, 32, ni mmoja wa wachezaji 12 waliocheza na kushinda fainali za Ligi ya Mabingwa na Ubingwa wa Ulaya katika msimu mmoja.
Aliifungia Real Madrid bao la kwanza katika ushindi wa fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Borussia Dortmund - na pia aliifungia Uhispania dhidi ya Crotia katika mechi ya makundi ya Euro 2024 .
Kama atashinda atakuwa beki wa pembeni wa kwanza kushinda Ballon d'Or.
Lamine Yamal (Barcelona, Hispania)

Chanzo cha picha, fcbarcelona.com
Michezo aliyocheza ni 64. Mabao aliyofunga ni 10. Pasi za mwisho alizotoa ni 14. Kombe ni Euro 2024.
Winga wa Barcelona Yamal tayari alikuwa na msimu mzuri kwa kijana mwenye umri wa miaka 16 wakati akicheza mechi 50 za klabu, akafunga mabao saba na pasi za mwisho saba.
Kwenye Euro 2024 aliufanya msimu wake kuwa wa kuvutia zaidi kwa mchezaji yeyote wa umri wake.
Pasi za mwisho nne nchini Ujerumani zilikuwa muhimu kwenye rekodi ya michuano hiyo ya Ulaya - na alifunga bao zuri katika ushindi wa nusu fainali dhidi ya Ufaransa ambalo liliingia kwenye historia.
Mchezaji mwenye umri mdogo zaidi, mfungaji mabao na mshindi katika michuano ya Ulaya - alitimiza umri wa miaka 17 siku moja kabla ya fainali - alitajwa kuwa mchezaji bora kwa mchanga wake katika mashindano hayo.
Gwiji wa Brazil Ronaldo, akiwa na umri wa miaka 21 mwaka 1997, ndiye mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kushinda Ballon d'Or.
Lionel Messi (Inter Miami, Argentina)

Chanzo cha picha, Getty Images
Michezo 39 amecheza. Mabao 28 amefunga. Amepiga pasi za mwisho 17. Kombe amechukua Copa America.
Messi mwenye umri wa miaka 37, ndiye mchezaji aliyefanikiwa zaidi katika historia ya Ballon d'Or, akishinda mara nane - ikiwa ni pamoja na mwaka jana, baada ya kuiongoza Argentina kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia.
Alifunga bao moja pekee katika ushindi wa Argentina msimu huu wa joto, dhidi ya Canada katika nusu fainali ya Copa America, alitoka nje baada ya jeraha kwenye fainali. Kwa ujumla alicheza chini ya kiwango chake.
Messi hajashinda taji lolote akiwa na Inter Miami hadi sasa.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla












