Moja kwa moja, Marekani na Iran zashindwa kufikia makubaliano

Nchi hizo, zilfanya mazungumzo marefu ya saa 21 huko Islamabad, Pakistan, lakini kwa mujibu wa Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, pande hizo mbili hazikuweza kukubaliana juu ya masharti ya mwisho.

Moja kwa moja

Na Yusuph Mazimu

  1. Watu 30 wahofiwa kufariki dunia kwa kukanyagana Haiti

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Watu wasiopungua 30 wanahofiwa kufariki dunia kwa kukanyagana katika eneo maarufu la utalii nchini Haiti siku ya Jumamosi.

    Tukio hilo lilitokea wakati wa mkusanyiko wa kila mwaka wa Pasaka katika sehemu inayoitwa Citadel ya Laferrière, eneo la urithi wa dunia linalotambulika na UNESCO. Jean Henri Petit, mkuu wa ulinzi wa kiraia katika idara ya Nord nchini Haiti, alisema idadi ya vifo huenda ikaongezeka zaidi.

    Waziri Mkuu Alix Didier Fils-Aimé alisema tukio hilo lilitokea “wakati wa tukio la utalii lililohudhuriwa na vijana wengi” katika eneo hilo, katika mji wa kaskazini wa Milot.

    Alisema uchunguzi umeanzishwa na “mamlaka zote husika” zimehamasishwa kusaidia walioathirika.

    “Serikali inatoa pole za dhati kwa familia zilizoathirika,” Fils-Aimé alisema katika taarifa.

    Eneo hilo lilikuwa limejaa wanafunzi na wageni baada ya tukio hilo la uzinduzi wa ngome hiyo ya karne ya 19.

    Inaelezwa kuwa mkanyagano huo ulianza karibu na lango la kuingilia eneo hilo na ukachangiwa zaidi na kuanza kwa mvua kubwa.

  2. Hali ya afya ya kiongozi mpya wa Iran Mojtaba yatia shaka baada ya taarifa za majeraha makubwa

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Kiongozi mpya wa Iran, Mojtaba Khamenei, mtoto wa pili wa aliyekuwa kiongozi mkuu wa taifa hilo, Ayatollah Ali Khamenei, akihudhuria moja ya vikao mjini Tehran, Iran, Oktoba 13, 2024.

    Kiongozi mpya wa juu wa Iran, Mojtaba Khamenei, mtoto wa aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa zamani Ayatollah Ali Khamenei, anaripotiwa kuendelea kuuguza majeraha makubwa usoni na kwenye mguu aliyoyapata kufuatia shambulio la anga lililotokea mwanzoni mwa vita, na kumuua baba yake, inaripoti Reuters.

    Kwa mujibu wa watu watatu wa karibu na mazingira yake, shambulio hilo lililolenga makazi ya uongozi wa juu wa Iran katikati ya Tehran lilisababisha uso wake kuharibika vibaya pamoja na majeraha makubwa kwenye mguu mmoja au yote mawili.

    Licha ya majeraha hayo, Khamenei mwenye umri wa miaka 56 anaendelea kupona na anadaiwa kuwa bado yuko imara kiakili.

    Anashiriki mikutano ya viongozi waandamizi kupitia mawasiliano ya sauti na anahusika katika maamuzi muhimu ya serikali, ikiwemo masuala ya vita na mazungumzo ya kidiplomasia na Marekani.

    Hata hivyo, hali yake halisi ya kiafya na uwezo wake wa kuongoza bado haijathibitishwa hadharani, kwani hakuna picha, video au sauti yake iliyotolewa tangu shambulio hilo na baada ya kuchukua nafasi ya uongozi.

    Serikali ya Iran haijatoa taarifa rasmi kuhusu kiwango cha majeraha yake, huku hali ya usiri ikiendelea kuzunguka uongozi wake.

  3. Mazungumzo yaligubikwa na “kutoaminiana, mashaka na wasiwasi" - Iran

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema mazungumzo ya amani yaliyofanyika Islamabad, Pakistan, yalifanyika katika mazingira yaliyojaa mashaka, kutoaminiana na tahadhari kubwa kati ya pande zilizohusika.

    Msemaji wa wizara hiyo, Esmaeil Baghaei, amesema haikutarajiwa kwamba Iran na Marekani zingefikia makubaliano ya haraka katika kikao kimoja tu cha mazungumzo.

    Ameeleza kuwa kutokana na historia ya mvutano na kile alichokiita “vita vilivyowekwa kwa muda wa zaidi ya siku 40”, hali ya mazungumzo ilikuwa tayari imeathiriwa na ukosefu wa uaminifu kati ya pande hizo mbili.

    Baghaei amesisitiza kuwa hakuna mtu aliyekuwa na matarajio ya kufikia makubaliano ya haraka, akibainisha kuwa mchakato wa mazungumzo ya aina hiyo huhitaji muda na hatua nyingi.

    Hata hivyo, ameongeza kuwa diplomasia bado haijafungwa mlango wake, akisisitiza kuwa mazungumzo yanaweza kuendelea licha ya changamoto zilizopo.

  4. Pakistan yataka Marekani na Iran kuheshimu usitishaji mapigano baada ya kushindwa kukubaliana

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Moja ya vikao vya kutafuta suluhu ya mzozo Mashariki ya kati

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan imetoa wito kwa Marekani na Iran kuendelea kuheshimu makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano kufuatia mazungumzo ya amani yaliyofanyika Islamabad.

    Katika taarifa iliyotolewa, Pakistan imesisitiza kuwa ni “muhimu sana” kwa pande zote mbili kuendelea kusimamia ahadi yao ya kusitisha mapigano, licha ya kushindwa kufikia makubaliano ya mazungumzo kuhusu mzozo wao.

    Taarifa hiyo imeeleza matumaini kuwa Marekani na Iran wataendeleza mazungumzo kwa nia njema ili kufikia amani ya kudumu na ustawi si tu katika eneo la Mashariki ya Kati bali pia kimataifa.

    Pakistan, ambayo imekuwa mpatanishi mkuu wa mazungumzo hayo, imesema itaendelea kuwezesha mazungumzo kati ya pande hizo mbili katika siku zijazo, ikilenga kusaidia kupunguza mvutano na kusaka suluhisho la kudumu.

    Nchi hizo zilikaa kwa saa 21 usiku wa kuamkia leo kwa saa za Afrika Mashariki, lakini zilishindwa kufikia makubaliano ya kusitisha vita kutokana na kila upande kusema masharti ya mwezie hayakuwa yanakubalika.

  5. Marekani na Iran zashindwa kufikia makubaliano baada ya mazungumzo ya kihistoria Pakistan

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Marekani na Iran zimeshindwa kufikia makubaliano ya kumaliza vita baada ya mazungumzo ya ngazi ya juu yaliyofanyika Islamabad, Pakistan.

    Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, amesema licha ya mazungumzo marefu yaliyodumu kwa saa 21, pande hizo mbili hazikuweza kukubaliana juu ya masharti ya mwisho.

    Amesema Iran “haikukubali masharti ya Marekani”, huku akisisitiza kuwa Washington inahitaji kuona dhamira ya wazi kutoka Tehran ya kuacha kabisa mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia.

    Kwa upande wake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema mazungumzo hayo yalikuwa “ya kina”, lakini ikaishutumu Marekani kwa kutoa “matakwa makubwa na yasiyo halali”.

    Mazungumzo hayo yalikuwa yakisimamiwa na Pakistan, huku Waziri Mkuu wake, Shehbaz Sharif akitajwa kupongezwa kwa juhudi za upatanishi.

    Licha ya kushindwa kufikia makubaliano, Donald Trump amesema matokeo hayo “hayajaleta tofauti” kwa Marekani, akisisitiza kuwa nchi yake bado ipo katika nafasi ya ushindi.

    Mazungumzo hayo yalikuwa yakilenga kufikia makubaliano ya kusitisha vita vinavyoendelea huko Mashariki ya Kati, lakini hadi sasa hatma ya mgogoro huo bado haijulikani.

  6. Hujambo na karibu katika habari zetu za moja kwa moja leo April 12, 2026