Je, Zirkzee ndiye mshambuliaji ambaye Man Utd imekuwa ikimtafuta?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Joshua Zirkzee

Manchester United lazima ijifunze kutokana na uzoefu wao wa hivi majuzi wa kusajili wachezaji wa Uholanzi baada ya kuwasili kwa Joshua Zirkzee, BBC Sport imeambiwa.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23 alijiunga na klabu hiyo kutoka Bologna ya Italia Jumapili kwa mkataba wa thamani ya £36.54m.

Kuwasili kwa Zirkzee kunajiri baada ya kuondoka kwa Muholanzi mwenzake Donny van de Beek, ambaye alinunuliwa na Girona kwa pauni 420,600 wiki iliyopita baada ya kuhangaika kujiimarisha Old Trafford tangu uhamisho wa pauni milioni 35 Septemba 2020.

Mshambuliaji wa Uholanzi Memphis Depay alikuwa mwingine ambaye alitatizika, akaondoka 2017 baada ya kufunga mabao saba pekee ndani ya misimu miwili.

"Natumai Manchester United, kama klabu, imejifunza kutokana na kile kilichotokea na Memphis Depay," mwandishi wa habari wa soka wa Uholanzi Marcel van der Kraan alisema.

"Alikuja akiwa na umri mdogo sana - matarajio makubwa, ada kubwa ya uhamisho. Alikuwa mchezaji aliyejiimarisha katika ligi ya Uholanzi, lakini hiyo haiwezi kulinganishwa na Ligi Kuu au ukubwa wa klabu kama Manchester United.

"United bado wana matarajio sawa na mojawapo ya klabu tano bora duniani - na hii ni kubwa. Ndiyo maana [Erik] Ten Hag atamleta Zirkzee hatua kwa hatua na kumruhusu kujua soka la Uingereza. Wachezaji wa Uholanzi wanahitaji muda.

"Tumeona wengi wameshindwa - Donny van de Beek, Davy Klaassen na Daley Blind hawakuwa na mchezo mzuri. Inahitaji muda lakini uwezo upo."

Zirkzee anaweza kucheza kama nambari tisa au 10, anaweza kushindana na mshambuliaji Rasmus Hojlund katika nafasi ya kuanzia Old Trafford.

Van der Kraan anaamini kuwa Zirkzee atafaidika kwa kucheza chini ya Ten Hag, lakini akaongeza: "Awache kumtegemea Ten Hag na wachezaji wa Uholanzi, kwa sababu kuwa Mholanzi sio hakikisho la mafanikio.

"Unahitaji kuelewa utamaduni wa Ligi Kuu na matarajio makubwa ya Ligi Kuu - na lazima ubadilike na kuwa Muingereza kidogo kwa mtindo wako kama mwanasoka.

"Tempo ya juu na kasi kubwa - kimwili ni ngumu na kiasi cha mechi ni nyingi. Natumai Ten Hag anaweza kumuongoza kidogo kutokana na uzoefu wake wa misimu miwili ya kwanza."

Je, Zirkzee anasemaje?

Joshua Zirkzee anasema yuko "tayari kuleta mabadiliko mara moja" Old Trafford.

"Ninajua jinsi siku za usoni zitakavyokuwa hapa na siwezi kusubiri kucheza sehemu yangu," alisema mchezaji huyo wa kimataifa wa Uholanzi mwenye umri wa miaka 23.

"Mimi ni mchezaji ambaye siku zote nimejitolea kila kitu kushinda. Niko tayari kwa changamoto hii ijayo - kwenda ngazi nyingine katika maisha yangu ya soka na kushinda mataji zaidi."

Mkurugenzi mpya wa michezo wa United Dan Ashworth amesema kuongeza mshambuliaji kwenye kikosi ni "lengo kuu la msimu huu wa joto".

"Tunafuraha kwamba tumefanikiwa kusajili mchezaji wa kiwango cha Joshua mapema katika dirisha la uhamisho.

"Uwezo wake na hamu yake ya kukua na kuwa mchezaji wa kiwango cha kimataifa inamaanisha kuwa atakuwa nyongeza kubwa."