‘Niligundua kuwa mwanangu amefariki kwenye mitandao ya kijamii’

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Khadidiatou Cissé
- Nafasi, BBC News
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Huku idadi kubwa ya vijana wa Kiafrika wakihatarisha maisha yao kujaribu kufika Visiwa vya Canary, Waziri Mkuu wa Uhispania anaanza mazungumzo ya mgogoro na Senegal, Mauritania na Gambia ili kukabiliana na uhamiaji haramu.
Lakini hii itakuja kama faraja kidogo kwa Amina.
"Niligundua kuwa mtoto wangu amefariki kwenye mtandao wa kijamii," anaiambia BBC akiwa nyumbani kwake karibu na mji mkuu wa Senegal.
"Tulikuwa tukizungumza kila mara na aliniambia anataka kuenda Morocco," mama huyo wa miaka 50 anasema.
"Hakuwahi kusema kwamba alikuwa akipanga kupanda mashua."
Mara ya mwisho aliwasiliana na mtoto wake, Yankhoba, ilikuwa mwezi Januari mwaka huu. Juhudi za miezi sita za kumtafuta fundi cherehani aliyejitolea mwenye umri wa miaka 33 hazikuzaa matunda.
Lakini, mapema Agosti, wavuvi walipata mwili wake upande wa Bahari ya Atlantiki, karibu kilomita 18 kutoka pwani ya Jamhuri ya Dominica.
Takriban miili 14 iliyokuwa ikioza ilipatikana kwenye mashua hiyo ndogo ya mbao, wanasema polisi wa eneo hilo. Simu za rununu na hati za kibinafsi zilizopatikana kando yao zilionyesha kuwa wengi walikuwa kutoka Senegal, Mauritania na Mali.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Miongoni mwa vitu vilivyokuwemo ndani ni kitambulisho cha Yankhoba.
Mamlaka ya Dominica pia iliripoti uwepo wa vifurushi 12 vyenye dawa.
Uchanguzi unafanywa ili kubaini chanzo cha vifo hivyo, ingawa inakisiwa kuwa abiria hao walipotea walipokuwa wakijaribu kufika Visiwa vya Canary. Mashua yao ilikuwa mfano wa boti za uvuvi za mbao ambazo mara nyingi hutumika kusafirisha wahamiaji haramu kutoka Afrika Magharibi kuelekea Ulaya.
Yankhoba alikuwa mtoto wa kwanza wa mama yake na mwana pekee. Ni nafasi ambayo inakuja na wajibu mkubwa katika jamii ya Senegal.
Mshonaji cherehani huyo mchanga ameacha mke na watoto wawili wachanga, akiwemo mmoja ambaye hakuishi muda wa kutosha kumuona.
Kabla ya Amina kujua kuhusu kifo cha mwanawe, aliomba usaidizi kutoka kwa kurasa za watu waliopotea kwenye Facebook na kuwataka washawishi wa mitandao ya kijamii wenye wafuasi wengi kuangazia hali yake.
"Nilikuwa imani kwamba Yankhoba anaweza kuwa amefungwa katika gereza mahali fulani huko Morocco au pengine hata Tunisia," anasema, sauti ya huzuni.
Vijana wahamiaji wa Afrika Magharibi wanaojaribu kufika Ulaya wanazidi kutumia njia ya Visiwa vya Canary badala ya Bahari ya Mediterania.
Licha ya hatari, inahusisha hatua moja tu, badala ya changamoto ya kuvuka Jangwa la Sahara na Mediterania.
Mwaka jana pekee nidadi ya wahamiaji wanaotumia njia ya Atlantiki iliongezeka kwa 161% ikilinganishwa na mwaka uliopita, linasema shirika linalosimamia masuala ya mpaka wa Umoja wa Ulaya, Frontex.
Uhispania ni mojawapo ya nchi za Ulaya zinazopokea wahamiaji wengi zaidi.
Kuhusu watu wanaoondoka Senegal, idadi inayoongezeka kati yao ni wafanyakazi wa tabaka la kati wanaoweza kumudu safari ya gharama kubwa ya kwenda Marekani badala ya Ulaya.
Hivyo ndivyo Fallu alivyofanya.
Licha ya kuendesha ufugaji wenye mafanikio wa kondoo na ndege huko Dakar kwa karibu muongo mmoja, alikuwa akijitahidi.
“Nilihisi kukwama. Juu ya kuendesha biashara yangu, nilikuwa pia nikifanya kazi katika kiwanda, lakini nilitatizika kupata riziki,” anakumbuka.
Kwa hiyo, alipokuwa na umri wa miaka 30, aliuza kila kitu alichokuwa nacho na kununua tikiti ya ndege ya kwenda Nicaragua huko Amerika ya Kati. Kutoka hapo, angejaribu safari ya nchi kavu kuelekea Marekani.
Fallou alihimizwa kuondoka na kaka yake mkubwa, ambaye tayari yuko Marekani, na kwa picha na video nyingi za watu wa Senegal kwenye TikTok wakishiriki safari yao kupitia Amerika ya Kati.
"Mama yangu hakutaka niende, lakini nilikuwa tayari kukabiliana na kifo," anasema.
Fallou alisafiri kwa siku 16, akipitia Nicaragua, Honduras, Guatemala na Mexico, kwa usaidizi wa wasafirishaji haramu. Kwa jumla alitumia zaidi ya dola 10,000 za Kimarekani katika safari hiyo.
Hata hivyo, wahamiaji maskini zaidi walio na azma ya kufika Ulaya huamua hutumia mashua kutoka Senegal hadi Visiwa vya Canary na kwa kawaida hulipa wasafirishaji haramu karibu dola 450.

Chanzo cha picha, AFP
Fallou anasema kwambajuhudi zake izilikumbwa na matukio ya kutisha.
"Watu kadhaa walikufa mbele ya macho yangu," asema.
“Lakini niliwaona baadhi ya wanawake ambao waliendelea na safari, hata wakiwa na watoto wao migongoni, nikajipatia moyo: ‘Lazima nibaki imara.’”
Baada ya kuzuiliwa katika kambi ya Marekani kwa siku chache, hatimaye Fallou alipewa ruhusa ya kubaki kama mtafuta hifadhi. Tangu wakati huo ameunganishwa tena na kaka yake na sasa anafanya kazi kama mekanika.
Fallou alikuwa na bahati, lakini wahamiaji wengi wa Kiafrika kwenda Marekani hawana
Septemba iliyopita, zaidi ya watu 140 wa Senegal walirudishwa nyumbani baada ya kuvuka mpaka wa Mexico na Marekani.
Makundi ya haki za binadamu na jumuiya za watu wanaoishi nje ya nchi zinazounga mkono wahamiaji hao wapya zinaripoti kwamba makazi mara nyingi hulemewa na visa kama hivyo.
Baadhi ya wahamiaji hawana chaguo ila kulala mitaani. Wengine wanaweza kuruhusiwa kukaa kwa muda misikitini.
Licha ya kuongezeka kwa hamu ya Waafrika Magharibi katika njia mbadala za uhamiaji, bado wahamiaji wengi wa Kiafrika wanajaribu kufika Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania.
Katika muongo uliopita, shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa (IOM) linasema zaidi ya wahamiaji 28,000 wamezama katika eneo hilo moja la maji pekee.
Ahadi za kisiasa
"Watu wanaondoka [Afrika Magharibi] kwa sababu wanakabiliwa na mlipuko wa matatizo ya usalama, taasisi, lishe, usafi, baada ya Covid-19 na mazingira," anasema mtaalamu wa uhamiaji Aly Tandian.
Idadi ya watu wanaoondoka Senegal haswa inaongezeka, licha ya kuwa nchi yenye amani na rais mpya ambaye anaahidi kubuni nafasi za ajira kwa vijana.
Tangu serikali mpya ilipochaguliwa mwezi Machi, imefanikiwa kupunguza bei ya baadhi ya mahitaji ya kimsingi, ikiwa ni pamoja na mafuta, mkate na mchele – hivyo kurahisisha ubanaji wa gharama za maisha.
Lakini haitoshi.
"Sote tulifikiri kwamba matumaini yaliyoletwa na mabadiliko ya serikali yangesitisha kuibuka tena kwa mmiminiko huu wa wahamaji, lakini kwa bahati mbaya hali haijawa hivyo," anasema Boubacar Sèye, mkuu wa shiŕika lisilo la kiseŕikali, Horizon Without Borders.
"Kukata tamaa na mashaka kumeingia katika mazingira yetu ya kijamii, hadi kufikia hatua ambapo watu hawaamini tena kwamba hatima yao inaweza kutimizwa hapa," anaongeza.

Chanzo cha picha, Getty Images
Bw Sèye ameandika barua rasmi kwa mamlaka ya Senegal, akiomba uchunguzi ufanyike kuhusu kilichotokea kwa mashua iliyopatikana katika Jamhuri ya Dominica.
Anasema ripoti zinaonyesha "kuna uchumi wa uhalifu unaozunguka uhamiaji huu usio wa kawaida. Usafirishaji wa dawa za kulevya, silaha, binadamu na pia viungo”.
Mwezi Julai, baada ya miili 89 kupatikana katika mashua nje ya pwani ya Mauritania, Waziri Mkuu wa Senegal Ousmane Sonko alitoa ombi la hadharani kwa vijana wasichukue njia ya hatari ya Atlantiki kuelekea Ulaya.
"Mustakabali wa dunia uko barani Afrika, na ninyi, vijana mnapaswa kufahamu hilo," alisema.
Hata hivyo, kwa idadi kubwa ya vijana wa Kiafrika ambao bado wanahatarisha maisha yao ili kufika Ulaya na Marekani, mustakabali huo hauko popote isipokuwa nyumbani.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi












