'Nyota ya Mbappe ilizima ilipohitajika kung'aa' - Fahamu kwanini Real Madrid wapo mashakani

Chanzo cha picha, Getty Images
Jess Anderson
Mwandishi wa BBC Sport
Kupoteza mara tatu katika mechi tano na kukabiliwa na kibarua kigumu kufuzu kwa awamu inayofuata ya Ligi ya Mabingwa, ndio masaibu yanayoikumba Real Madrid.
Hiyo si nafasi ambayo mabingwa mara 15 wa Uropa, Real Madrid wanatarajiwa kuwa.
Wakiwa katika nafasi ya 24 kwenye jedwali kufuatia kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Liverpool siku ya Jumatano, wababe hao wa Uhispania wanajikuta kwenye matatizo makubwa katika michuano hiyo ambayo kwa muda mrefu wametangazwa kuwa vigogo.
Katika muundo mpya wa shindano hili, timu nane bora hutinga hatua ya 16 moja kwa moja huku zile za tisa hadi 24 zikiingia hatua ya mtoano kwa mikondo miwili.
Mabingwa hao watetezi kwa sasa wako nafasi ya 24 na wanakabiliwa na kisirani cha kutofika awamu inayofuata.
Nyota Kylian Mbappe na Jude Bellingham hawakuwa na ushawishi mkubwa au athari nzuri kwenye mchezo huo, huku mkwaju wa penalti wa Mbappe ukiwa ni donda wanalotaka kusahau kwa haraka.
Kiungo wa kati wa Uingereza, Bellingham alisema Liverpool "wapo vizuri" zaidi kuliko timu yake huku wachambuzi wakisema mchezo wa sasa wa Real "unatisha".
Huku wakiwa wamepoteza mara tatu katika mechi zao tano za Ligi ya Mabingwa Ulaya, zaidi ya mechi 24 zilizopita, nini kinaendelea vibaya kwa Real Madrid? Je, kweli wanaweza kuondolewa kwenye shindano ambalo wamekuwa wakitawala?
Mbappe na 'matarajio mazito ya ufanisi'
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Uhamisho wa Mbappe kwenda Real Madrid ulitawala vichwa vya habari kutoka mwanzo.
Miezi kadhaa ya uvumi, ukweli kwamba Paris St-Germain ililazimika kumwacha aende bure, mishahara ya juu, mbwembwe na matarajio.
Na sasa, pambano la fowadi huyo wa Ufaransa kutulia katika timu hii ya nyota.
"Hatujaona ubora wa Mbappe usiku wa leo," kiungo wa zamani wa Real Steve McManaman alisema kwenye TNT Sports.
"Walimhitaji Mbappe usiku wa leo na 'alijipendekeza kwa kudanganya'. Waandishi wa habari wa Madrid watakuwa wakatili kwake kwa sababu hakutoa mchezo ufaao alipohitaji.
"Madrid inapitia hali mbaya na wachezaji wakubwa hawafanyi vizuri.Matatizo yote yanayomzingira Mbappe yanalifanya jambo hilo kuwa kubwa. Mwaka huu wanatatizika kweli kweli."
Mbappe hajapata makali yake na maswali yanabaki juu ya nafasi yake na jinsi ya kupata ubora kutoka kwake na Vinicius Jr, ambaye anacheza nafasi sawa, katika timu moja.
Kutokana na kukosekana kwa Vinicius Jrkwa ajili ya jeraha, Mbappe bado alishindwa kufanya vyema. Lakini wachezaji wenzake wanabaki na imani kwamba anaweza kuleta mafanikio.
"Kylian ni mchezaji mzuri lakini shinikizo ni kubwa," alisema Bellingham.
"Penati sio sababu ya sisi kupoteza . Kylian anaweza kuweka kichwa chake juu na najua kwa hakika atatoa dakika nyingi muhimu kwa klabu hii."
Bellingham, majeraha, Ancelotti - ni nini kingine kinachoendelea?
Ni rahisi kutaja kukosa penalti ya Mbappe na ukosefu wake wa athari kwenye mchezo kama sababu zilizoifanya Real kupoteza.
Lakini ukweli ni kwamba Mbappe hakuwa peke yake aliyehangaika. Bellingham bado hajafunga katika kampeni hii ya Ligi ya Mabingwa na katika maandalizi ya mechi hii mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 alisema anahisi alitumiwa kama "kisingizio" katika michuano ya Euro msimu huu wa kiangazi, ambapo Uingereza ilimaliza washindi wa pili kwa Uhispania.
"Kuingia kwenye Euro kila mtu alifurahishwa sana na kiwango cha mchezo wa Bellingham na alizama kidogo, kama walivyofanya wachezaji wengi wa Uingereza," alisema mshambuliaji wa zamani wa Blackburn Chris Sutton kwenye BBC Radio 5 Live.
"Unapokuwa mchezaji wa hadhi ya juu kama yeye basi unakuja kuhukumiwa kutokana na uchezaji wako na labda hakufikia kiwango ambacho watu walitarajia."
Labda jambo linalotia wasiwasi zaidi ni orodha ya majeruhi ya Ancelotti inayozidi kuongezeka.
Kiungo Eduardo Camavinga alitoka uwanjani Anfield akishukiwa kuwa na tatizo la msuli wa paja na kuungana na beki wa pembeni Dani Carvajal, washambuliaji Rodrygo na Vinicius Jr, kiungo Aurelien Tchouameni na mabeki David Alaba na Eder Militao kwenye orodha ya majeruhi ya Real.

Shinikizo nchini Uhispania pia ni kwa bosi Ancelotti.
Licha ya kuwaongoza kutwaa ubingwa wa La Liga na Ligi ya Mabingwa msimu uliopita, Muitaliano huyo amekabiliwa na shutuma kutoka kwa vyombo vya habari.
Lakini mtaalam wa kandanda wa Uhispania Guillem Balague anasema tamko lililotolewa na Ancelotti katika mkutano na waandishi wa habari Jumanne ambapo alisema "hakuna mtu anayeweza kunipa ushauri kuhusu mabadiliko - nimesimamia michezo 1,300, nimeunda vikosi 1,300 na kufanya mabadiliko ya wachezaji zaidi ya 4,000" h halikulenga vyombo vya habari lakini maafisa wa juu wa Real.
"Ni kwa sababu anahisi watu katika klabu wanatilia shaka uwezo wake wa kubadilisha hali hii," alisema Balague.
“Anahisi mashaka yataongezeka kwa kila mchezo kwa sababu anashindwa kuitoa timu kwa sasa ambayo inafahamu soka, mambo haya yanahitaji muda.
"Lakini anajua si muda mwingi unaruhusiwa Real Madrid na shaka ya iwapo yeye ndiye mtu wa kazi hiyo katika siku za usoni inatoka ndani."
Shinikizo linaendelea kwa 'kutisha' Real
Real Madrid haijawahi kutolewa katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ingawa mfumo mpya wa mwaka huu unawapa neema ya kujirejesha katika nafasi iliyopotea.
Lakini wakati kiwango cha mchezo wa Liverpool msimu huu kinaonyesha kuwa kuna kitu maalum kinaweza kutetemeka, hii ilikuwa mara ya kwanza kuwafunga Real katika mechi nane za Ligi ya Mabingwa, zikiwemo fainali mbili.
Kawaida timu hiyo huwa moto kama pasi katika mashindano haya, beki wa zamani wa Manchester United na England Rio Ferdinand alisema hali ya sasa ya Real "inatisha".
"Unapokuwa na wachezaji nyota, unaweza kubadilisha msimu wako wakati wowote," alisema.
"Mchezo wao ni jambo la kusumbua sana. Unapaswa kuwathibitishia wachezaji wenzako kuwa wewe ndiye - Mbappe atakuwa anataka kuwathibitishia wachezaji wenzake 'Mimi ni galactico, mimi ndiye kijana(Mahiri).'
"Wakati huo utakuja tena hivi karibuni. Ni lazima, wanaweza kuwa wanatoka."
Lakini Real wamepitia kila kitu kwenye shindano hili na ujumbe kutoka kwa Ancelotti kufuatia kushindwa ulikuwa wazi.
"Tutafuzu kwa raundi inayofuata na tutashindana kama kila mwaka. Utaona. Tutafuzu."
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah na kuhaririwa na Seif Abdalla












