Zelensky amtaka Trump kuzuru Ukraine kabla ya kufanya mazungumzo na Urusi
Shambulio la kombora la Urusi katika mji wa Sumy wa Ukraine siku ya Jumapili linatajwa kuwa baya zaidi dhidi ya raia wa nchi hiyo
Muhtasari
- Afrika Kusini yateua mjumbe maalum wa kurahisisha uhusiano wake na Marekani
- Rais wa Togo Faure Essozimna Gnassingbé kuwa mpatanishi mpya kati ya DRC na M23
- Trump atishia kutoza ushuru mpya kwa simu za mikononi siku chache baada ya kuondoa
- Vita vya Sudan: Wanamgambo wa RSF wakiri kudhibiti kambi ya Zamzam
- Afrika kununua mashine ya Playstation 5 kwa bei ya juu - Sony
- Zelensky amtaka Trump kuzuru Ukraine kabla ya kufanya mazungumzo na Urusi
- Daktari wa dharura wa Gaza aliyepotea anazuiliwa na Israel- Msalaba Mwekundu
- Algeria kuwatimua maafisa 12 wa ubalozi wa Ufaransa
- Katy Perry kusafiri anga za mbali na wanawake wengine watano
- Trump alitaja shambulio dhidi ya Sumy kuwa la kutisha, lakini akataa kuitaja Urusi
- Trump: Nitafanya uamuzi kuhusu Iran hivi karibuni
- Kijana aliwaua wazazi wake kama sehemu ya njama ya kumuua Trump - FBI
- Kiongozi wa mapinduzi Gabon ashinda uchaguzi kwa wingi wa kura
- Ushuru mpya: Trump asema hakuna mtu "atakayenusurika " huku akipendekeza ushuru mpya dhidi ya Uchina
- Washirika wa Ukraine wailaani Urusi kwa shambulio baya la kombora
Moja kwa moja
Abdalla Seif Dzungu na Mariam Mjahid
Rais wa Togo Faure Gnassingbé kuwa mpatanishi mpya wa DRC na M23

Chanzo cha picha, Getty Images
Umoja wa Afrika (AU) umemteua rasmi Faure Essozimna Gnassingbé, Rais wa Jamhuri ya Togo, kuwa mpatanishi mpya katika mchakato wa amani wa kutatua mzozo unaoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Uteuzi huu umefanyika baada ya Rais wa Angola ambaye alikuwa akiendesha mchakato huu kutangaza kujiondoa.
Lakini raia wengi wa DRC waliozungumza na BBC wanahisi mpatanashi huyu mpya hatafanikiwa.
Haya yakijiri, vikosi vya Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo FARDC vimekanusha madai ya kuhusika na shambulio dhidi ya jiji la Goma mwishoni mwa wiki iliyopita, likieleza kuwa taarifa zilizotolewa na waasi wa M23 ni “za kupikwa kwa makusudi ili kuficha na kuhalalisha mauaji wanayoyatekeleza kila siku dhidi ya raia katika jiji la Goma.”
Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi, kundi la waasi la M23 lililaani kile ilichokiita msururu wa mashambulizi haramu yaliyofanyika mjini Goma, likidai kuwa yalitekelezwa na wanajeshi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SAMIDRC), kwa kushirikiana na majeshi ya serikali (FARDC), kundi la waasi la FDLR, pamoja na vuguvugu la Wazalendo.
M23 ilieleza kuwa tukio la hivi karibuni lililotokea tarehe 11 Aprili lilizua wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya usalama na ustawi wa raia, na kudai kuwa kumekuwa na juhudi kadhaa—zilizoshindwa—za kutaka kuikomboa tena Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.
Kwa mujibu wa vyanzo vya kuaminika, wiki iliyopita kulifanyika mazungumzo ya ana kwa ana kati ya wawakilishi wa serikali ya DRC na waasi wa M23 mjini Doha, Qatar, chini ya usuluhishi wa serikali ya nchi hiyo.
Hata hivyo, hakuna taarifa rasmi iliyotolewa kuhusu maendeleo ya mazungumzo hayo.
M23 imesema kuwa licha ya kuwa na subira, mashambulizi yanayodai kufanywa na FARDC pamoja na washirika wake yamewalazimu kutathmini upya msimamo wao ili kuweka mbele usalama wa raia na wa majeshi ya SAMIDRC waliopo katika maeneo wanayoyadhibiti.
Pia unaweza kusoma:
Afrika Kusini yamteua mjumbe maalum kushughulikia uhusiano wake na Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Mcebisi Jonas amewahi kuwa mjumbe wa uwekezaji wa Afrika Kusini Afrika Kusini imeteua mjumbe maalum kwa Marekani katika juhudi za kupunguza hali ya wasiwasi kati ya nchi hizo mbili, ambayo imekuwa mbaya zaidi tangu kurejea kwa Donald Trump kama Rais.
Rais Cyril Ramaphosa alitangaza uteuzi wa Mcebisi Jonas, akiongeza kwamba "atakabidhiwa kuendeleza vipaumbele vya kidiplomasia, biashara na nchi mbili za Afrika Kusini".
Jonas, aliyekuwa Naibu Waziri wa fedha, aligonga vichwa vya habari alipotoa tuhuma za ufisadi dhidi ya familia tajiri inayohusishwa na aliyekuwa Rais Jacob Zuma.
Marekani mwezi uliopita ilimfukuza balozi wa Afrika Kusini, Ebrahim Rasool, kutokana na matamshi aliyotoa kuhusu utawala wa Trump.
Ofisi ya Ramaphosa ilisema Jonas "atahudumu kama mwakilishi rasmi" wa Rais na Afrika Kusini.
"Ataongoza mazungumzo, atakuza ushirikiano wa kimkakati na kushirikiana na maafisa wa serikali ya Marekani na viongozi wa sekta binafsi ili kukuza maslahi ya taifa letu."
Uhusiano kati ya Marekani na Afrika Kusini, ambao umekuwa wa kupanda na kushuka kwa miaka mingi, uligonga mwamba mapema mwaka huu, ambapo Trump alifuta misaada kwa nchi hiyo, akitolea mfano Sheria mpya ya Unyakuzi, ambayo inaruhusu serikali kutaifisha ardhi bila kulipwa fidia katika mazingira fulani.
Trump, katika chapisho mwishoni mwa juma, alisisitiza nia yake ya kususia Mkutano ujao wa G20 2025 utakaofanyika nchini Afrika Kusini baadaye mwaka huu, akitaja sera ya ardhi yenye utata kama sababu kuu.
Trump pia ameilaani Afrika Kusini kwa kuipeleka Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, akiituhumu kufanya mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza, jambo ambalo Israel imekanusha.
Soma pia:
Trump atishia kutoza ushuru mpya kwa simu za mikononi siku chache baada ya kuondoa

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Donald Trump anashikilia chati ya ushuru kwa bidhaa zinazoingizwa Marekani Rais Donald Trump anasema simu za mikononi zilizotengenezwa na China na vifaa vingine vya kielektroniki havitaondolewa kwenye ushuru - badala yake vimehamishiwa kwenye fungu tofauti ya ushuru.
Masoko ya hisa ya Ulaya yaliimarika Jumatatu asubuhi baada ya tangazo rasmi la Ijumaa kwamba baadhi ya bidhaa hizi zingeweza kuepuka ushuru wa hadi asilimia 145%.
China imetoa wito kwa Donald Trump "kufuta kabisa" utawala wake wa ushuru, na "kurejea njia sahihi ya kuheshimiana".
Hata hivyo maafisa wa Marekani walisema Jumapili kwamba bidhaa zitakazotozwa ni vimashine vidogo vya kielektroniki, huku Trump akitarajiwa kufichua maelezo zaidi baadaye.
Tishio hili la hivi punde kutoka kwa Trump linajiri siku chache baada ya Idara ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka ya Marekani, kutangaza simu za mikononi na vifaa vya kielektroniki zimeondolewa kwenye orodha ya ushuru wa asilimia 10 uliokuwa ukiathiri nchi nyingi duniani, pamoja na ule wa juu zaidi dhidi ya bidhaa kutoka China.
Ikulu ya White House imesema kuwa inatumia ushuru kama mbinu ya mazungumzo kupata masharti mazuri ya kibiashara kutoka kwa mataifa mengine.
Trump amesema sera yake itarekebisha ukosefu wa haki katika mfumo wa biashara wa kimataifa, pamoja na kurejesha ajira na viwanda nchini Marekani.
Hata hivyo, uingiliaji kati wake umeona mabadiliko makubwa katika soko la hisa na kuibua hofu ya kupungua kwa biashara ya kimataifa ambayo inaweza kuwa na athari kwenye ajira na uchumi wa mtu binafsi hasa raia wa Marekani.
Pia unaweza kusoma:
Vita vya Sudan: Wanamgambo wa RSF wakiri kudhibiti kambi ya Zamzam

Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Kambi ya Zamzam iliyoko karibu na El Fasher inafadhili maelfu ya watu, wanaoishi katika hali ya makali ya njaa Kufuatia mapigano makali nchini Sudan, wanamgambo wa RSF wamesema wamedhibiti kambi ya wakimbizi ya ZamZam, ambayo imehifadhi watu waliokimbia makwao Darfur Kaskazini.
Mamia ya familia wanaotoroka kambi ya ZamZam wamewasili eneo la Tawila.
Wakati huohuo, Waasi wa RSF wametangaza kuwa wanakaribia kudhibiti kikamilifu eneo la El Fasher, mji muhimu wa Darfur wakiendelea kupigana na wanajeshi wa Sudan.
Mashambulizi mabaya kwenye kambi inayohifadhi mamia kwa maelfu ya watu waliokimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan yameendelea kwa siku ya tatu, wakaazi wameiambia BBC.
Mtu mmoja katika kambi ya Zamzam alielezea hali hiyo kuwa ya "janga" huku mwingine akisema mambo ni "mabaya".
Zaidi ya raia 100, miongoni mwao wakiwa watoto 20 na timu ya madaktari, wameuawa katika mfululizo wa mashambulizi yaliyoanza mwishoni mwa juma lililopita katika jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan, Umoja wa Mataifa umesema.
Siku ya Jumapili kundi hilo lilisema limechukua udhibiti wa Zamzam lakini likakanusha ripoti za ukatili.
Kambi hizo, Zamzam na Abu Shouk, zinatoa makazi ya muda kwa zaidi ya watu 700,000, ambao wengi wao wanakabiliwa na njaa.
Habari za mashambulizi hayo zinakuja katika mkesha wa kuadhimisha mwaka wa pili wa kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya RSF na jeshi la Sudan.
El-Fasher ni mji mkuu wa mwisho huko Darfur chini ya udhibiti wa jeshi la Sudan na umekuwa ukizingirwa na RSF kwa mwaka mmoja.
Pia unaweza kusoma:
Afrika kununua mashine ya Playstation 5 kwa bei ya juu - Sony

Chanzo cha picha, Getty Images
Huku ushuru wa kimataifa wa Trump kwa bidhaa za mataifa zaidi ya 60 ukiendelea kutekelezwa, Shirika la Sony limetangaza kuongeza bei ya Playstation 5 katika masoko ya Ulaya, Uingereza, Australia na New Zealand.
Muungano wa teknolojia na burudani nchini Japani unasema "mazingira yenye changamoto ya kiuchumi" yanachangia hatua hiyo, ikitoa mfano wa mfumuko wa bei na viwango vya kubadilisha fedha vinavyobadilikabadilika.
Bei ya PlayStation 5 bila diski imepanda hadi euro 499.99 (US$569.59), kampuni hiyo inasema.
Kifaa hicho kitagharimu £429.99 (US$566.90) nchini Uingereza.
Kulingana na Reuters, hii ni 11% na 10% ya kupanda kwa bei hiyo.
Wateja nchini New Zealand na Australia wataona kupanda kwa bei ya mashine hiyo, pamoja na PS5 ya kawaida yenye kiendeshi cha Blu-ray.
Kampuni hiyo inasema kutakuwa na ongezeko la bei katika eneo la Mashariki ya Kati na Afrika, bila kutoa maelezo.
Michezo ya PS5 huendeshwa kwa njia ya diski au kwa kupakuliwa kutoka kwenye duka la mtandaoni la PlayStation Network.
Inaweza kutumika kwa kucheza michezo ya video, kutazama video, na kutumika kama kituo cha burudani cha nyumbani.
Ni mojawapo ya vituo vya michezo ya video vya kizazi kipya kinachopatikana sokoni.
Soma pia:
Zelensky amtaka Trump kuzuru Ukraine kabla ya kufanya mazungumzo na Urusi

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Rais wa Ukriane, Volodymyr Zelensky Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amemwalika Donald Trump kuzuru nchi yake kabla ya makubaliano yoyote na Urusi yakumaliza vita.
"Tafadhali, kabla ya aina yoyote ya maamuzi, aina yoyote ya mazungumzo, njoo uone watu, raia, wapiganaji, hospitali, makanisa, watoto walioharibiwa au waliokufa," Zelensky alisema katika mahojiano ya programu ya Dakika 60 ya CBS.
Mahojiano hayo yalirekodiwa kabla ya kombora la Urusi kushambulia mji wa Sumy, na kuua watu 34 na wengine 117 kujeruhiwa.
Urusi haijatoa maoni.
Trump alisema alikuwa ameambiwa kuwa ilikuwa ni shambulizi la kimakosa, bila kutaja kama kauli hii imetolewa na Moscow.
Kaimu Kansella wa Ujerumani, Friedrich Merz, aliishutumu Urusi kwa kufanya uhalifu wa kivita.
Hapo awali, mjumbe maalum wa Trump nchini Ukraine, Luteni Jenerali mstaafu Keith Kellogg, alisema shambulio hilo limevuka "mstari wowote wa adabu".
Walakini, inabakia kuonekana ikiwa Trump atakubali mwaliko wa Zelensky.
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alisema "amefadhaika sana na kushtushwa" kujua kuhusu shambulio hilo la kombora.
"Mashambulizi dhidi ya raia yamepigwa marufuku chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu, na kwamba mashambulizi yoyote kama hayo, popote yanapotokea, lazima yakomeshwe mara moja", aliongeza.
Guterres alisisitiza uungwaji mkono wa Umoja wa Mataifa kwa "juhudi za maana kuelekea amani ya haki, ya kudumu na ya kina ambayo inasimamia kikamilifu uhuru wa Ukraine, kama taifa".
Shambulio la mara mbili la makombora la Jumapili lilikuwa shambulio baya zaidi dhidi ya raia nchini Ukraine mwaka huu.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa karibu watu milioni saba wa Ukraine wanaishi kama wakimbizi.
Soma pia:
Daktari wa Gaza aliyetoweka anazuiliwa na Israel- Msalaba Mwekundu

Chanzo cha picha, PRCS
Maelezo ya picha, Shirika la Red Crescent la Palestina lilisema Assad al-Nassasra "alitekwa nyara kwa nguvu" na wanajeshi wa Israel mwezi uliopita na kutaka aachiliwe huru. Daktari wa dharura wa Kipalestina, Assad al-Nassasra, ambaye alikuwa hajulikani alipo tangu shambulio la anga la Israel lilillouwa wahudumu wengine 15 wa huduma za dharura kusini mwa Ukanda wa Gaza takriban wiki tatu zilizopita, sasa anazuiliwa na mamlaka za Israel.
Taarifa hii imethibitishwa na Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (ICRC).
Kupitia taarifa rasmi, ICRC imesema imepokea taarifa kuwa Bw. al-Nassasra, ambaye ni mfanyakazi wa Shirika la Red Crescent la Palestina (PRCS), anashikiliwa katika kituo cha kizuizi cha Israeli.
PRCS kwa upande wake imesema daktari huyo “alitekwa kwa nguvu” na wanajeshi wa Israel baada ya shambulio hilo na imetoa wito wa kuachiliwa kwake mara moja.
Hadi sasa, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) halijatoa uthibitisho rasmi kuhusu kuzuiliwa kwa daktari huyo. Msemaji wa jeshi hilo amesema wanatambua taarifa zinazodai mahali alipo, lakini hawajathibitisha chochote hadharani.
Maiti za wahudumu wanane wa PRCS, wapokeaji huduma sita wa Ulinzi wa Raia, na mfanyakazi mmoja wa Umoja wa Mataifa zilipatikana katika makaburi ya juujuu kandokando ya mji wa Rafah, wiki moja baada ya msafara wao kushambuliwa na vikosi vya Israel tarehe 23 Machi.
Daktari mmoja pekee wa PRCS alinusurika katika shambulio hilo na baadaye alieleza kuwa alitekwa na kuzuiliwa na vikosi vya Israel kwa takribani saa 15 kabla ya kuachiliwa.
Shirika la PRCS limetaja tukio hilo kama “uhalifu wa kivita”, likiituhumu Israel kwa mfululizo wa mashambulizi yaliyolengwa dhidi ya wafanyakazi wa afya na magari ya wagonjwa walipokuwa wakijibu wito wa kutoa msaada kwa waliojeruhiwa.
PRCS linasisitiza haja ya kufanyika kwa uchunguzi huru wa kimataifa kuhusu tukio hilo, na kuchukuliwa hatua za kuwawajibisha waliohusika.
“Tunaomba jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti na kuishinikiza Israel kumuachilia mara moja mwenzetu, daktari Assad, ambaye alitekwa akiwa anatekeleza wajibu wake wa kibinadamu.” Msemaji wa PRCS ameieleza New York Times
Jeshi la Israel, katika taarifa yake ya awali iliyotolewa Jumatatu iliyopita, lilisema uchunguzi wa ndani ulionesha wanajeshi walifyatua risasi wakidhani ni tishio, kufuatia tukio jingine katika eneo hilo, na kwamba watu sita waliouawa walihusishwa na kundi la Hamas.
Hata hivyo, halikutoa ushahidi wowote kuthibitisha madai hayo.
Bw. al-Nassasra amehudumu ndani ya shirika hilo kwa zaidi ya miaka 16, na ni baba wa watoto sita.
Jeshi la Israel lilianzisha kampeni dhidi ya Hamas kufuatia shambulio la kuvuka mpaka la tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo watu takriban 1,200 waliuawa na zaidi ya 250 kutekwa nyara.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas, zaidi ya watu 50,940 wameuawa katika Ukanda wa Gaza tangu kampeni hiyo ianze.
Soma pia:
Algeria kuwatimua maafisa 12 wa ubalozi wa Ufaransa

Chanzo cha picha, AFP
Maelezo ya picha, Bendera za Ufaransa na Algeria zikipepea kabla ya ziara rasmi ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron nchini Algeria mnamo 2022. Algeria imewataka wafanyakazi 12 wa ubalozi wa Ufaransa kuondoka nchini humo ndani ya saa 48, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amesema.
Jean-Noel Barrot aliongeza kuwa hatua hiyo inahusishwa na kufunguliwa mashitaka dhidi ya Waalgeria watatu nchini Ufaransa siku ya Ijumaa, mmoja wao akiwa afisa wa ubalozi.
Wanatuhumiwa kuhusika katika tukio la mwaka jana la utekaji nyara wa Amir Boukhors, 41, mkosoaji wa serikali ya Algeria, ambaye inasemekana alipewa hifadhi nchini Ufaransa mwaka 2023.
Barrot aliitaka Algeria "kuachana" na kufukuzwa na akasema Ufaransa iko tayari "kujibu mara moja" ikiwa wataendelea.
Boukhors, anayejulikana pia kama Amir DZ, ameishi Ufaransa tangu 2016 na aliripotiwa kupata hifadhi ya kisiasa mnamo 2023.
Alitekwa nyara mnamo Aprili 2024 katika vitongoji vya kusini mwa Paris na kuachiliwa siku iliyofuata, kulingana na wakili wake Eric Plouvier.
Plouvier aliiambia shirika la habari la AFP kwamba Boukhors "amekabiliwa na mashambulizi mawili makubwa, moja mnamo 2022 na lingine jioni ya Aprili 29 2024".
Vyombo vya habari vya Ufaransa viliripoti kuwa alilazimishwa kuingia kwenye gari lililokuwa na watu waliodaiwa kuwa "maafisa bandia wa polisi", kisha akaachiliwa siku iliyofuata bila maelezo.
Pia unaweza kusoma:
Mwanamuziki Katy Perry kusafiri anga za mbali na wanawake wengine watano

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwanamuziki wa Pop Katy Perry na wanawake wengine watano wanatazamiwa kuelekea anga za juu kwenye chombo cha angani cha utalii kinachomilikiwa na Jeff Bezos.
Mwimbaji huyo ataungana na mchumba wa Bezos Lauren Sánchez na mtangazaji wa CBS Gayle King.
Chombo hicho kwa jina New Shepard ikinatarajiwa kupaa angani kutoka kwa shina lake magharibi mwa Texas na kinatarajiwa kuzinduliwa saa 08:30 saa za ndani (14:30 BST).
Safari hiyo itachukua takriban dakika 11 na kuwapeleka watalii hao zaidi ya 100km (maili 62) juu ya Dunia, kuvuka mpaka wa amgani unaotambuliwa kimataifa na kuwapa watalii hao dakika chache za kutokuwa na uzito.
Wengine ndani ya ndege ni mwanasayansi wa zamani wa roketi ya Nasa Aisha Bowe, mwanaharakati wa haki za kiraia Amanda Nguyen, na mtayarishaji wa filamu Kerianne Flynn.
Chombo hicho kinajiendesha kikamilifu, hakihitaji marubani, na watalii hawataendesha gari hilo wenyewe.
Chombo hicho baadaye kitarudi duniani kwa urahisi kwa kusaidiwa na parachuti, huku kiboreshaji cha roketi kitatua chenyewe umbali wa maili mbili kutoka eneo la uzinduzi.
"Iwapo ungeniambia kuwa ningekuwa sehemu ya watalii wa kwanza kabisa wa kike angani, ningekuamini.
Hakuna kitu ambacho kilikuwa zaidi ya mawazo yangu nikiwa mtoto. Ingawa hatukukua na mengi, sikuacha kuitazama dunia kwa maajabu yenye matumaini!" Bi Perry alisema katika chapisho la mtandao wa kijamii.
Blue Origin inasema kwamba anga ya mwisho ya wanawake wote ilikuwa zaidi ya miaka 60 iliyopita wakati Mwanaanga wa Soviet Valentina Tereshkova alipokuwa mwanamke wa kwanza kusafiri angani kwa safari ya pekee ndani ya chombo cha Vostok 6.
Habari za hivi punde, Trump alitaja shambulio dhidi ya Sumy kuwa la kutisha, lakini akataa kuitaja Urusi

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Marekani Donald Trump ametaja shambulio la Urusi dhidi ya mji wa Sumy nchini Ukraine kuwa la kutisha, lakini hakuitaja Urusi moja kwa moja.
"Nadhani ni baya. Ninaambiwa walifanya makosa. Lakini nadhani ni baya. Nadhani vita vyote ni jambo baya," Trump aliwaambia waandishi wa habari ndani ya Air Force One akielekea Washington, kwa mujibu wa CNN, AFP na Reuters.
Alipoulizwa kufafanua alichomaanisha kuwa "kosa" la Urusi, rais wa Marekani alisema: "Walifanya makosa. Nadhani ilikuwa makosa ... Tazama, ungewauliza."
Sio Trump wala Ikulu ya White House, katika taarifa iliyotolewa awali, iliyotaja Urusi kuwa wahusika wa shambulio hilo, ingawa Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio alitoa rambirambi kwa "waathiriwa wa shambulio hilo la kombora la Urusi dhidi ya Sumy," AFP inabainisha.
Shambulio la kombora katika mji wa Sumy lililotekelezwa na Urusi Jumapili asubuhi liliua watu 34, wakiwemo watoto wawili, na kujeruhi 117.
Urusi haijatoa maoni rasmi kuhusu shambulio hilo au idadi kubwa ya raia waliouawa.
Makombora ya Urusi yaliwashambulia wakaazi waliokusanyika kwa ibada ya Jumapili, shambulio baya zaidi mwaka 2025, CNN inaripoti.
Trump: Nitafanya uamuzi kuhusu Iran hivi karibuni

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kwamba anatarajia kutoa uamuzi kuhusu Iran hivi karibuni.
Maoni hayo yanajiri baada ya nchi zote mbili kuripoti mazungumzo "chanya" na "ya kujenga" huko Oman siku ya Jumamosi na kukubaliana kuanza tena mazungumzo wiki hii.
Trump, ambaye hapo awali alitishia kuchukua hatua za kijeshi ikiwa makubaliano ya kuzuia mpango wa nyuklia wa Iran hayatafikiwa, aliwaambia waandishi wa habari ndani ya Air Force One Jumapili usiku, saa za Mashariki, kwamba amekutana na washauri wake kuhusu Iran na anatarajiwa kufanya uamuzi hivi karibuni, Hakutoa maelezo zaidi.
Haya ni maoni mafupi ya pili ya Bw. Trump tangu mazungumzo na Abbas Araqchi na Steve Whittaker siku ya Jumamosi.
Lakini Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei hadi sasa hajatoa tamko lake Katika maoni yake ya kwanza kwa waandishi wa habari, Trump alikuwa amesema: "Nadhani mazungumzo yanaendelea vyema.
Hakuna muhimu kusema hadi yatakapokamilika. Kwa hivyo sipendi kulizungumzia. Lakini sio mabaya.
Nadhani yanakwenda vizuri kiasi. Katika mkutano na makamanda wa kijeshi siku ya Jumapili, Ayatollah Khamenei alisisitiza kwamba lazima wawe na "maandalizi ya hali ya juu na tahadhari za vifaa na programu."
Kijana aliwaua wazazi wake kama sehemu ya njama ya kumuua Trump - FBI

Mwanafunzi wa shule ya upili kutoka Wisconsin aliwaua wazazi wake kama sehemu ya njama kubwa ya kumuua Rais wa Marekani Donald Trump, FBI imesema.
Nikita Casap, 17, ameshtakiwa kwa mauaji ya mama yake, Tatiana Casap, 35, na baba yake wa kambo Donald Mayer, 51, ambao walipatikana wamekufa nyumbani kwao mnamo 28 Februari.
Hati mpya ya upekuzi ambayo haijafungwa pia inadai kuwa simu ya mshukiwa ilikuwa na nyenzo zinazohusiana na kikundi cha Nazi kiitwacho Order of Nine Angles na sifa kwa Adolf Hitler.
Wachunguzi pia waligundua maandishi ya chuki dhidi ya Wayahudi ambapo mshtakiwa alidaiwa kuelezea mipango yake ya kumuua Trump kama sehemu ya lengo pana la kupindua serikali, kulingana na hati ya mahakama.
Mshukiwa huyo anatuhumiwa kwa mauaji ya kukusudia ya daraja la kwanza na makosa mengine saba ya uhalifu, ikiwa ni pamoja na kuficha maiti na wizi.
Wazazi hao walipatikana wakiwa wamekufa wakati viongozi wa eneo hilo walipotembelea nyumba yao katika kijiji cha Waukesha, karibu na Milwaukee, baada ya mvulana huyo kukosa kuhudhuria shule kwa wiki mbili.
Bw Mayer alikufa kutokana na jeraha la risasi kichwani, huku Bi Casap akifariki kutokana na majeraha mengi ya risasi mnamo Februari 11, kulingana na malalamiko ya uhalifu kuhusu kijana huyo.
Siku hiyo hiyo miili yao ilipogunduliwa, mshtakiwa alikamatwa na polisi katika jimbo la Kansas alipokuwa akiendesha Volkswagen Atlas ya 2018 mali ya Bw Mayer, wachunguzi walisema.
Ndani ya gari hilo kulikuwa na bastola ya Bw Mayer's Smith & Wesson .357, kadi nne za pesa za wanandoa hao, "vipande vingi" vya vito vya thamani, sefu ya bei ya juu na sarafu ya $14,000 (£10,700), nyingi zikiwa ndani ya Biblia, yalisema malalamiko ya uhalifu.
Katika maandishi yaliyopatikana na wachunguzi, mshukiwa alionyesha imani ya wazungu na kutaka mauaji ya Trump yaanze mapinduzi ya kisiasa, kulingana na hati ya upekuzi.
Madai ya mauaji ya watu wawili "yalionekana kuwa juhudi za kupata njia za kifedha na uhuru muhimu kutekeleza mpango wake," wachunguzi waliandika.
Nyaraka za mahakama zinadai mshukiwa alikuwa akizungumza na watu nchini Urusi kuhusu mipango ya kuwaua wazazi wake.
Mamlaka ilisema kijana huyo alilipia ndege isiyo na rubani na vilipuzi kutumia katika shambulio - na alikuwa na mipango ya kutorokea Ukraine.
Kiongozi wa mapinduzi Gabon ashinda uchaguzi kwa wingi wa kura

Chanzo cha picha, AFP
Kiongozi wa kijeshi wa Gabon, Jenerali Brice Oligui Nguema - ambaye mwaka 2023 aliongoza mapinduzi yaliyomaliza utawala wa familia moja wa takriban miaka 60 - ameshinda uchaguzi wa rais wa Jumamosi kwa zaidi ya 90% ya kura, matokeo ya muda yanaonyesha.
Kabla ya upigaji kura, wakosoaji walidai kuwa katiba mpya na kanuni za uchaguzi zilibuniwa kumpa Oligui Nguema njia rahisi ya kushinda uchaguzi.
Baadhi ya vigogo wa upinzani ambao wangeweza kutoa changamoto kubwa ya kisiasa walitengwa kwenye kinyang'anyiro hicho.
Ushindi wake katika uchaguzi unaimarisha kushikilia kwake mamlaka, karibu miaka miwili baada ya kupanga mauaji ya Rais Ali Bongo, ambaye familia yake ilikuwa madarakani nchini Gabon tangu 1967.
Oligui Nguema, 50, alikabiliana na wagombea wengine saba, akiwemo Waziri Mkuu wa zamani Alain Claude Bilie-by-Nze, ambaye alihudumu chini ya utawala wa Bongo, na vinara wawili wa chama tawala cha zamani cha PDG, Stéphane Germain Iloko na Alain Simplice Boungouères.
Ushuru mpya: Trump asema hakuna mtu "atakayenusurika " huku akipendekeza ushuru mpya dhidi ya Uchina

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Marekani Donald Trump amepuuzilia mbali madai kwamba usitishaji wa utekelezaji wa ushuru mpya ulilenga kuzinusuru baadhi ya nchi.
Akiandika kwenye mtandao wa kijamii Trump alisema: "Hakukuwa na ubaguzi wa ushuru uliotangazwa Ijumaa."
Rais alisisitiza kuwa bidhaa za kielektroniki kutoka Uchina bado zilikuwa chini ya ushuru wa 20% unaohusiana na dawa ya fentanyl - lakini sasa walikuwa kwenye "kikapu tofauti cha ushuru".
Kwa muda mrefu Marekani imekuwa ikishutumu mashirika ya Kichina kwa kusambaza kwa makusudi vikundi vilivyohusika katika uundaji wa opioid ya syntetisk ambayo ilizua shida ya dawa nchini.
Trump alisema kuwa uchunguzi ujao kuhusu ushuru na usalama wa taifa utaangalia bidhaa za elektroniki kama vile semiconductors na "msururu mzima wa usambazaji wa vifaa vya elektroniki".
Alirejelea nia yake ya kurudisha viwanda Marekani, akiandika "Kilichofichuliwa ni kwamba tunahitaji kutengeneza bidhaa nchini Marekani".
Trump alisema hii ni ili kuepuka "kudhibitiwa" na nchi, ikiwa ni pamoja na China ambayo alielezea kama "taifa la kibiashara lenye uadui"
Washirika wa Ukraine wailaani Urusi kwa shambulio baya la kombora

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Watu walionekana kukumbatiana na kulia katika eneo la shambulio huko Sumy Shambulio la kombora la Urusi katika mji wa Sumy wa Ukraine, ambalo liliua watu 34 - ikiwa ni pamoja na watoto wawili - na kujeruhi wengine 117, limelaaniwa vikali na washirika wa Magharibi wa Kyiv.
Makombora mawili ya balistiki yalipiga katikati mwa mji Jumapili asubuhi, na kulipuka karibu na chuo kikuu cha serikali na kituo cha Congress, na kuacha miili iliyojaa damu kutawanyika mitaani.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio amelitaja shambulizi hilo kuwa "la kuogofya" huku kansela mtarajiwa wa Ujerumani, Friedrich Merz, akiishutumu Urusi kwa kufanya uhalifu wa kivita.
Hakukuwa na maoni rasmi ya mara moja kuhusu shambulio hilo kutoka Urusi, ambayo vikosi vyake katika mpaka wa karibu vinasemekana kujiandaa kwa mashambulizi makubwa.
Shambulio hilo limetokea wakati Marekani, mshirika mkubwa zaidi wa kijeshi wa Ukraine, imekuwa ikitafuta suluhu ya vita - sasa katika mwaka wake wa nne - kupitia mazungumzo chini ya Rais Donald Trump.
Kiongozi wa Ukraine Volodymyr Zelensky amemtaka Trump mwenyewe kutembelea Ukraine na kuona uharibifu uliosababishwa na shambulio la Urusi.
"Tafadhali, kabla ya aina yoyote ya maamuzi, aina yoyote ya mazungumzo, njoo uone watu, raia, wanajeshi, hospitali, makanisa, watoto walioharibiwa au waliokufa," alisema Jumapili katika mahojiano ya kipindi cha Dakika 60 cha CBS.
Akitoa salamu zake za rambirambi kwa wapendwa wa waathiriwa, Rubio, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, alisema shambulio hilo ni "kumbukumbu ya kusikitisha" kwa nini utawala wa Trump "unaweka muda mwingi na juhudi kujaribu kumaliza vita hivi".
Hapo awali, mjumbe maalum wa Trump nchini Ukraine, Luteni Jenerali mstaafu Keith Kellogg, alitumia lugha kali zaidi, akisema shambulio hilo limevuka "mstari wowote wa adabu". Merz, ambaye anatarajiwa kuchukua wadhifa wa kansela mpya wa Ujerumani mwezi ujao, aliliambia shirika la utangazaji la Ujerumani ARD kwamba shambulio dhidi ya Sumy lilijumuisha "uhalifu mkubwa wa kivita".
"Kilikuwa kitendo cha kihuni.. na ni uhalifu mkubwa wa kivita, wa makusudi na uliokusudiwa," mwanasiasa huyo wa kihafidhina alisema.
Natumai hujambo na karibu katika habari zetu za moja kwa moja hii leo ikiwa siku ya Jumatatu tarehe 14.04.2025
