Neuralink: Chipu za ubongo zinazoundwa na Elon Musk ni nini?

Chanzo cha picha, Reuters
Kampuni ya chipu ya ubongo ya Elon Musk imesema imepokea kibali kutoka kwa Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani (FDA) kufanya uchunguzi wake wa kwanza kwa binadamu.
Kampuni ya bilionea huyo ya kupandikiza chipu ya Neuralink katika ubongo inataka kusaidia kurejesha uwezo wa kuona na kutembea kwa watu kwa kuunganisha ubongo na kompyuta.
Inasema haina mipango ya haraka ya kuanza kuajiri washiriki. Matarajio ya hapo awali ya Bw Musk kuanza majaribio yaligonga mwamba.
Mdhibiti mwenyewe bado hajatoa tamko.
Jitihada za awali za Neuralink kupata kibali cha FDA zilipingwa kwa misingi wa kiusalama, kulingana na ripoti ya Machi ya shirika la habari la Reuters ambayo ilitaja wafanyakazi wengi wa sasa na wa zamani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Neuralink ni nini?
Neuralink inatarajia kutumia chipu ndogo kutibu hali kama vile kupooza na upofu, na kusaidia watu fulani walemavu kutumia kompyuta na teknolojia ya simu.
Chipu - ambazo zimejaribiwa kwa nyani - zimeundwa kutafsiri mawimbi yanayotolewa kwenye ubongo na kupeleka habari kwa vifaa kupitia Bluetooth.
Bw Musk pia hapo awali alipendekeza kwamba teknolojia iliyopendekezwa inaweza kusaidia kupunguza wasiwasi kuhusu akili bandia AI kuchukua nafasi ya wanadamu .
Akitangaza habari hizo siku ya Alhamisi katika mtandao wa Twitter, Neuralink ilizungumzia "hatua muhimu ya kwanza ambayo siku moja itaruhusu teknolojia yetu kusaidia watu wengi".
Idhini hiyo ilikuwa "matokeo ya kazi ya ajabu ya timu ya Neuralink kwa ushirikiano wa karibu na FDA", ilisema.
Kampuni hiyo iliahidi habari zaidi "hivi karibuni" juu ya mipango ya kusajili washiriki wa majaribio.

Chanzo cha picha, Getty Images
Je ni salama?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tovuti yake inaahidi kwamba "usalama, ufikiaji na kutegemewa" yote ni vipaumbele wakati wa mchakato wake wa uhandisi.
Wataalamu wametahadharisha kuwa vipandikizi vya ubongo vya Neuralink vitahitaji majaribio ya kina ili kushinda changamoto za kiufundi na kimaadili ikiwa vitapatikana kwa wingi.
Kampuni hiyo - ambayo ilianzishwa na Bw Musk mnamo 2016 - imekadiria mara kwa mara kasi ambayo inaweza kutekeleza mipango yake.
Lengo lake la awali lilikuwa kuanza kupandikiza chipu katika ubongo wa binadamu mwaka wa 2020, ili kuheshimu ahadi iliyotolewa mwaka uliopita. Baadaye iliapa kuanza mnamo 2022.
Biashara hiyo ilikabiliwa na msukosuko mwingine Desemba mwaka jana, baada ya kuripotiwa kuchunguzwa kwa madai ya ukiukaji wa ustawi wa wanyama katika kazi yake. Hapo awali ilikanusha madai kama hayo.
Tangazo lake kuhusu idhini ya FDA kwa vipimo vya binadamu linafuatia habari za hivi punde za mafanikio sawa na yale yanayohusisha vipandikizi vya ubongo na watafiti wa Uswizi.
Mtu aliyepooza kutoka Uholanzi aliweza kutembea kwa kufikiria tu – kutokana na mfumo wa vipandikizi ambavyo husambaza mawazo yake kwa miguu bila waya.












