Tshisekedi na Kagame wakutana na kukubaliana kusitisha vita DRC

Chanzo cha picha, The New Times/Rwanda
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame walikutana nchini Qatar Jumanne hii kwa mazungumzo yao ya kwanza ya ana kwa ana tangu waasi wa M23 waanze mashambulizi mashariki mwa Kongo mwezi Januari, taarifa ya pamoja ya serikali tatu ilisema.
Mkutano huo uliosimamiwa na Amir wa Qatar, unakuja siku moja baada ya kundi la M23 kujitoa kwenye mazungumzo mengine ya Angola, ikiwa tayari imeteka miji miwili mikubwa mashariki mwa Kongo.
Kongo inaishutumu Rwanda kwa kutuma silaha na wanajeshi wa Rwanda kuwaunga mkono waasi hao, ambao mashambulizi yao yameitumbukiza mashariki mwa Kongo katika mzozo wake mbaya zaidi katika miongo kadhaa.
Rwanda imesema kuwa vikosi vyake vinafanya kazi ya kujilinda dhidi ya jeshi la Kongo na wanamgambo wanaoishambulia Kigali., ikikana kuiunga mkono M23.
Nchi jirani zimekuwa zikifanya kazi ya kusuluhisha usitishaji mapigano lakini jaribio la kuileta serikali ya Kongo na viongozi wa M23 pamoja katika mkutano nchini Angola siku ya Jumanne lilishindikana wakati M23 ilipojiondoa Jumatatu mchana.
"Wakuu wa nchi walithibitisha kujitolea kwa pande zote kusitisha vita mara moja na bila masharti," serikali tatu zilisema katika taarifa ya pamoja.
"Wakuu wa nchi kisha walikubaliana juu ya haja ya kuendelea na majadiliano yaliyoanzishwa Doha ili kuweka misingi imara ya amani ya kudumu."
Mwanadiplomasia aliyefahamishwa kuhusu mazungumzo hayo alisema mkutano huo haukuwa rasmi na haukusudiwa kuchukua nafasi ya juhudi zozote zilizopo na zinazoendelea za kutatua mzozo wa DRC.
Mzozo wa mashariki mwa Kongo umedumu kwa muda sasa, madini yakitajwa kama kichochea kikubwa. Mzozo umeongezeka haraka tangu Januari 2025, na maelfu ya watu waliuawa na mamia ya maelfu kulazimishwa kuyakimbia makazi yao.
Nchi ya Ghuba ya Kiarabu ya Qatar imekuwa kama mpatanishi katika mizozo kadhaa ya kimataifa, hivi karibuni ikifanya kazi na Misri na Marekani katika mazungumzo ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas huko Gaza, ambayo yalivunjika mapema Jumanne.















