Idjwi: Kisiwa katikati ya uwanja wa vita DRC, lakini ndicho salama zaidi

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Marina Daras
- Nafasi, BBC News
- Author, Catherine Heathwood
- Nafasi, BBC News
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Kisiwa cha Idjwi nchini Kongo ni eneo lililosahaulika ambalo limeishi kwa miongo kadhaa ya vita bila kuathirika.
Kisiwa cha pili kwa ukubwa kilichoko ziwani barani Afrika, Idjwi, kipo katika sehemu ya kusini ya Ziwa Kivu, kikizungukwa na nchi mbili ambazo zimekuwa katika vita kwa karibu miongo mitatu: DRC na Rwanda.
"Hatuna wanajeshi hapa, kutoka upande wowote. Hatujawahi kusikia milio ya bunduki au mabomu, lakini tunahisi athari za vita," anasema Yves Minani, mjasiriamali na mkurugenzi wa kituo cha redio cha ndani.
Maisha kwenye Idjwi yanaelezwa kuwa ya amani, na mazuri. Ni tofauti kabisa na sehemu za bara ambako waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wameteka miji miwili mikuu ya mkoa, Goma na Bukavu.
"Tangu mwanzo hapa, hakujawahi kuwa na vita," anasema Mustafa Mamboleo, msimamizi wa eneo la Idjwi na afisa wa Kivu Kusini.
"Lakini hofu inaenea miongoni mwa wakazi kwani kufungwa kwa benki na mizozo sehemu za bara kunamaanisha bidhaa muhimu pia hazitufikii."
Kisiwa hicho ni makazi ya watu wapatao 300,000: Wengi wao, wahavu, wameishi hapa kwa miongo kadhaa.
Hakuna umeme au maji ya bomba na huduma za afya ni ngumu kupatikana. Hata hivyo, watu wanaokimbia vita katika Mashariki ya DRC wanaona ni mahali salama.

Chanzo cha picha, AFP
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kufuatia mapigano makali katika mji mkuu wa Kivu Kaskazini, Goma, na maendeleo yasiyo ya kawaida ya waasi wa M23 katika mkoa wa Kivu Kusini, makumi ya maelfu ya Wakongo waliokimbia makazi yao wamekimbilia Idjwi.
Sasa wanalala katika kambi za wakimbizi zisizo rasmi kaskazini mwa kisiwa hicho, wakitegemea tu ukarimu wa wenyeji kwa msaada.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, kuna angalau watu 42,000 wanaoishi katika kambi za muda, lakini hakuna rekodi rasmi kwa wale waliokolewa na familia za wenyeji. Wenyeji wanakadiria kuwa kunaweza kuwa na wakimbizi wengi kama 60,000 wanaoishi Idjwi.
"Hukuna kaya hapa ambayo haijammpokea mwanafamilia, rafiki, au jamaa wa mbali aliyekimbia vita," anasema Yves Minani.
Vituo vya wakimbizi vimeanzishwa katika makanisa, shule na majengo yaliyotelekezwa. Mbali na jenereta chache, hakuna umeme au maji ya bomba.
Kuna hospitali kuu moja tu, na kuna magari machache tu, mara nyingi haiwezekani kwa wale walio katika maeneo ya mbali kupata matibabu.
"Wakati mwingine tunalazimika kutembea kilomita 10 na mgonjwa kwenye machela," anasema Yves. "Wakati mwingine wanakufa njiani kwa sababu hatuwezi kufika kwa haraka vya kutosha."
Licha ya kuwa na rasilimali chache, hii sio mara ya kwanza kwa wakaazi wa kisiwa hicho kufungua milango yao kwa wale watu wenye shida. Katika miaka ya 1990, wimbi la wakimbizi wa Rwanda lilifika Idjwi kukimbia maafa ya mauaji ya kimbari nyumbani kwao.
"Hiyo ndiyo Idjwi, hatuna makubwa watu, lakini tunakaribisha," anasema Yves.
Wakati wa Vita vya Kwanza na vya Pili vya Kongo vilivyoharibu eneo hilo katika miaka ya 1990, pia vinajulikana kama Vita vya Dunia vya Afrika, Idjwi ilikuwa sehemu salama.
Wenyeji wanasema mfululizo wa mazungumzo na vikundi vya waasi na vikosi vya jeshi viliwazuia kuingia kwenye mzozo.
"Tulisikia tu kuhusu vita kwenye redio au mara kwa mara wakati sauti ilivuka ziwa," anasema Yves.
Ardhi iliyosahaulika

Chanzo cha picha, AFP
Wenyeji wanasema wanahisi wametelekezwa kabisa na serikali kuu iliyo umbali wa kilomita 1,545.
Mpango wa kitaifa wa kuleta umeme Idjwi ulianza mwaka 2006, lakini vifaa vilivyosafirishwa hadi kisiwani havikuwahi kufungwa.
"Vimeachwa tu vioze," anasema Yves. "Utafiti wote muhimu ulifanywa, pamoja na tafiti za topografia."
Lakini, licha ya kuonekana kama wamekwama katika wakati, Idjwi imevutia wengi wa wajasiriamali wanaojaribu kuboresha maisha ya wakaazi wa kisiwani.
Mnamo 2017, mradi kabambe ulileta mtandao wa kwanza wa WiFi (internet) kisiwani, unaoendeshwa na umeme wa jua (sola). Uliongozwa na Patrick Byamungu kutoka shirika linaloitwa 'La Différence.
Mtandao ulijengwa kwa kutumia miundombinu na vifaa vya ndani na unafadhiliwa kwa sehemu na biashara za ndani zinazolipa kutumia mtandao kabla ya saa 12 jioni, baada ya hapo ni bure kwa wakaazi wengine kutumia.
"Jioni, unaona kweli vijana, walimu, madaktari, wote wakikusanyika karibu na sehemu ya muunganisho ili kupata intaneti, mitandao ya kijamii, au kupiga simu tu kwa familia zilizo mbali," anasema Patrick.
Hii pia imesaidia kuunganisha wakaazi wa Idjwi wenyewe kwa wenyewe na pia kwa ulimwengu wa nje. Kama matokeo, ushirika unaokuza kahawa umeweza kusafirisha mazao yake kwa mashirika makubwa ya kimataifa kama Starbucks.
La Différence pia imefanya kazi na mamlaka za kisiwa kwenye miradi ya kijamii kama usajili wa kuzaliwa kidijitali na mpango wa uzazi wa mpango unaohusisha vikundi vya wanawake na watoa huduma za afya wa ndani. Hiyo ni njia nyingine ya kuleta msaada.
Maisha mengine

Chanzo cha picha, Véronique Oberli
Wananchi wa Idjwi wanaishi kwa kutegemea ardhi. Kilimo cha ushirika cha mananasi, kahawa, na mihogo kimetengeneza ajira na fursa, na kuwapa wakazi wanaoongezeka njia ya kuishi.
Hata hivyo, takriban 80% ya wakaazi wa kisiwa hicho wanaishi chini ya dola moja kwa siku, maisha bado ni magumu. Biashara na sehemu za bara ni chanzo muhimu cha mapato.
"Biashara kati ya kisiwa hiki na Rwanda ni ya muda mrefu sana," anasema Padri Adrien Cishugi, ambaye ana nyumba kisiwani na anatumia muda mwingi huko kusaidia jamii ya Wapigmi.
Anasema kwamba katika baadhi ya sehemu za kisiwa, hasa kusini, watu hutumia zaidi faranga ya Rwanda kuliko faranga ya Kongo kwa sababu biashara yote inafanywa na Rwanda.
Kuna safari za mara kwa mara zinazounganisha miji ya Goma na Bukavu na Idjwi, na safari inachukua saa mbili hadi tatu.
Mwishoni mwa Januari, mapigano kati ya M23 na jeshi la Kongo yalisimamisha safari hizi, na kukinyonga kisiwa.
"Bila boti, maisha hayapo hapa," anasema PadreiAdrien Cishugi.
Bandari ya Goma ilipofungwa Januari baada ya wanajeshi wa M23 kuuteka mji, safari zote za boti zilisimamishwa. Lakini "walifanya msamaha maalumu kwa kisiwa kwa sababu kilikuwa matatizoni," anasema Padri Adrien.
Urithi wa kiasili
Biashara pia ndiyo inayowapa jamii ya Wapigmi wa Idjwi njia ya kujikimu.
Waliishi kama wawindaji katika misitu ya kisiwa hicho kwa maelfu ya miaka lakini walifukuzwa kutoka ardhi yao ya asili ili kutoa nafasi kwa ongezeko la idadi ya watu wa kabila la Bantu. Wengi walipoteza riziki zao kutokana na hilo, wakisukumwa kuishi pembezoni mwa jamii.
Kundi la kiasili la Wapigmi wa Idjwi, Bambuti, ni miongoni mwa watu wa kiasili wa zamani zaidi wa Afrika ya kati, lakini mara nyingi wametengwa na kutengwa na elimu ya kawaida.

Chanzo cha picha, Véronique Oberli
Tangu miaka ya 1990, Padri Adrien Cishugi amefanya kazi kwa pamoja na jamii hiyo kutengeneza fursa na kuboresha viwango vya chini vya kusoma na kuandika.
Amesaidia kuanzisha shule kwa watoto wa Wapigmi nje ya mfumo wa elimu wa kawaida.
Watoto huhudhuria masomo siku za Jumapili badala ya Alhamisi, ambayo kiasili ni siku ya soko kwa jamii yao. Ili kuwahimiza wabaki shuleni, wanapewa mlo kila siku na nguo safi.
Watoto hujifunza masomo ambayo Padri Cishugi anasema, "yanaendana na falsafa yao", kama vile dawa za kiasili, ufinyanzi, na usukaji wa vikapu.
"Katika programu za elimu za kitaifa, kuna masomo ya TEHAMA, lakini unawezaje kumfundisha TEHAMA mtu ambaye hajawahi hata kuona simu?" anasema.












