Mapinduzi ya kijeshi Gabon hayataondoa utawala wa ukoo wa Bongo

Chanzo cha picha, AFP
Jeshi kufanya mapinduzi na kuchukua mamlaka nchini Gabon kutasababisha kuendelea tu kwa utawala wa ukoo wa Bongo ambao umekuwa madarakani kwa miaka 55, chanzo kilicho karibu na rais aliyeondolewa madarakani kimeiambia BBC.
Jenerali Brice Oligui Nguema ni zao la moja kwa moja la ukoo wa Bongo,” kilisema chanzo hicho ambacho kilitaka jina lake lihifadhiwe kwa sababu za kiusalama.
Aliwaonya wanaosherehekea mapinduzi hayo wasitarajie mengi sana kubadilika.
Wanajeshi walipotwaa mamlaka waliapa kukomesha utawala wa Bongo pindi watakaponyakua madaraka.
Walitangaza kutwaa mamlaka ya kijeshi muda mfupi baada ya Rais Ali Bongo kutangazwa mshindi wa uchaguzi uliokuwa na utata. Kwa sasa rais huyo amewekwa kizuizini nyumbani kwakwe.

Chanzo cha picha, Reuters
Jeshi siku ya Jumamosi lilisema kuwa mipaka ya nchi hiyo itafunguliwa tena baada ya kufungwa kufuatia mapinduzi ya Jumatano.
Matamshi ya chanzo chetu yanafanana na ya kiongozi wa upinzani Albert Ondo Ossa, ambaye aliliambia shirika la habari la Associated Press kwamba mapinduzi hayo yalikuwa "mapinduzi ya Ikulu", yaliyobuniwa na familia ya Bongo ili kuendelea kuhodhi madaraka yao.
Muungano unaomuunga mkono Bw Ossa, Alternance 2023, ambao unasema ndiye mshindi halali wa uchaguzi wa Jumamosi iliyopita, umehimiza jumuiya ya kimataifa kushinikiza kurejeshwa kwa utawala wa kiraia.
"Tulifurahi kwamba Ali Bongo alipinduliwa lakini...tunatumai kwamba jumuiya ya kimataifa itasimama kuunga mkono jamhuri na utaratibu wa kidemokrasia nchini Gabon kwa kuomba wanajeshi kurudisha mamlaka kwa raia," msemaji wa Bw Ossa. , Alexandra Pangha, aliambia BBC.
Aliongeza kuwa mpango wa Jenerali Nguema kuapishwa kama rais wa mpito siku ya Jumatatu ni "upuuzi".

Chanzo cha picha, Getty Image
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Omar Bongo alikuwa madarakani kwa miaka 41 kabla ya mwanawe Ali Bongo kumrithi kufuatia kifo chake mwaka 2009.
Inasemekana kuwa kabla ya kifo cha Omar Bongo mwaka 2009, Gen Nguema alimuahidi kuwa ataitunza familia yake. Hata hivyo, Ali Bongo alipochukua hatamu, mwanajeshi huyo alipelekwa kwenda kuhudumu kama mwanzilishi wa balozi za Gabon nchini Morocco na Senegal.
"Aliporejea mnamo 2019, Jenerali Nguema aligundua kuwa mzunguko wa mamlaka ulikuwa umeenda mbali zaidi ya watu wa karibu wa familia na kwamba udhibiti wa serikali ulikuwa ukitoka mikononi mwa ukoo wa Bongo," kinaeleza chanzo chetu. Hii ilikuwa baada ya Ali Bongo kuugua ugonjwa wa kiharusi ambao ulimweka kando kwa muda wa mwaka mmoja na kumtaka ajiweke kando.
Muda mfupi baada ya mapinduzi hayo kutangazwa, washirika kadhaa wa rais aliyepinduliwa walitiwa mbaroni, akiwemo mtoto wake wa kiume Noureddin Bongo Valentin mwenye umri wa miaka 31, ambaye amekuwa akituhumiwa kwa uhaini mkubwa na ufisadi. Televisheni ya Taifa imeonyesha picha zake na washirika wengine wa karibu wa Bongo wakiwa mbele ya masanduku ya pesa ambayo ilisema yamekamatwa kutoka kwenye nyumba zao. Wao wenyewe hawajazungumzia tuhuma hizo.
Lakini chanzo chetu kinasema hii ni kwa ajili ya maonyesho.
“Anataka kutuma ujumbe mzito kwa wananchi kwa kumkamata mtoto wa rais.
"Kila mtu anasherehekea sasa lakini hatupaswi kusahau kwamba kiongozi wa mpito alikula kwenye meza moja ya familia ya Bongo kwa miongo kadhaa. Ana uzoefu mkubwa na aliweza kurudisha matumaini, lakini watu wa Gabon lazima wakae macho".












