Jambazi wa zamani ambaye sasa ni waziri wa michezo Afrika Kusini

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Rafieka Williams
- Nafasi, BBC News, Johannesburg
Gayton McKenzie, mwanasiasa wa upinzani ambaye safari yake ya maisha yalizungukwa na matukio kadha wa kadha kuanzia kuwa jambazi sugu hadi mmiliki wa klabu ya burudani yenye utata, sasa ameteuliwa kuwa waziri wa michezo, sanaa na utamaduni wa Afrika Kusini.
Rais Cyril Rampahosa alimteua Bw McKenzie - kiongozi wa Muungano wa Patriotic (PA) - kwenye wadhifa katika serikali ya vyama vingi ambayo aliitangaza Jumapili baada ya chama chake cha African National Congress (ANC) kupoteza wingi wake wa wabunge katika uchaguzi wa Mei 29.
Mtumiaji huyo mahiri wa mtandao wa X, (zamani Twitter), mwenye umri wa miaka 50, alifurahia uteuzi wake, akituma picha yake akiwa amevaa viatu vya soka, kwa ucheshi, aliandika: "Asanteni kwa umbe wenu wa heri, nitajibu hivi karibuni. Niko mbioni kujiandaa, nina kazi ya kufanya 🥅 ⚽️."
Kwa wandani wa Bw McKenzie, uteuzi wake ni ishara ya hivi punde ya jinsi alivyoshinda dhiki ili kupata mafanikio. Aliiba benki mara ya kwanza kabla ya kufikisha umri wa miaka 16, kisha akawa jambazi kamili. Alisema hayo alipokuwa akihojiwa na kituo cha redio, alikaa gerezani kwa miaka saba, na akaapa kubadilika baada ya kuachiliwa.
"Ningeweza kuwa na randi 12 mfukoni mwangu lakini nilikuwa na randi bilioni moja akilini mwangu. Na hilo ndilo watu hawaelewi - wanazingatia kile wanachokosa badala ya jinsi ya kupata kile wanachokosa," alisema katika mahojiano ya 2013 na shirika la utangazaji la SABC.
Alikua mzungumzaji wa kutia motisha anayelipwa sana, akachapisha vitabu kuhusu maisha yake, ikiwa ni pamoja na A Hustler's Bible, na kujitosa katika biashara mbalimbali - kutoka uchimbaji madini nchini Zimbabwe hadi vilabu vya burudani nchini Afrika Kusini - akiwa na Kenny Kunene, mwandani wake kutoka gerezani.
Bw Kunene alijipatia jina la utani la "Sushi King" baada ya kuomba kuandaliwa mlo wa sushi kwenye miili ya wanawake wakiwa wamevalia nguo ya ndani pekee kwenye tafrija ya kutimiza miaka 40 ya kuzaliwa kwenye klabu ya usiku ya Zar Lounge, jijini Johannesburg.

Chanzo cha picha, Getty Images
Klabu hiyo ya usiku ilifungwa, pamoja na tawi la Cape Town iliyosajiliwa kwa jina la Bw McKenzie kufuatia hatua za kisheria kuhusu madai ya kutolipa ada ya nyumba na bili ya umeme, kulingana na tovuti ya habari ya IOL.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Sina nia ya kufanya biashara ya klabu. Sina muda kwa sababu nina miradi mingine. Tuliangamiza chapa ya Zar - hakuna mipango ya siku zijazo [ya Zar]," Bw McKenzie alinukuliwa akisema wakati huo .
Siku hizi, Bw McKenzie anajulikana zaidi kama mwanasiasa, baada ya kuzindua PA mnamo 2013, na Bw Kunene, kama naibu wake.
Zaidi ya muongo mmoja baadaye, chama hicho kilipata asilimia mbili ya kura za kitaifa na kufanya vyema katika uchaguzi wa serikali ya mkoa wa Cape Magharibi, na kupata asilimia nane.
Uungwaji mkono wake ulitoka kwa watu wa rangi mchanganyiko kama wanavyoiulikana nchini Afrika Kusini.
Kauli mbiu ya saini ya PA ni "Ons baiza nie", maneno ya Kiafrikana ambayo yanatafsiriwa kama "Hatuogopi". Kiafrikana kinazungumzwa sana katika jamii ya watu waliochanganya damu, ambayo inakadiria karibu asilimia nane ya watu wa Afrika Kusini.
"Kwa mara ya kwanza kuna watu jamii hiyo wanaowakilishwa bungeni kupitia Muungano wa Patriotic. Sisi ndio chama pekee kinachopeleka mbio zote bungeni," Bw McKenzie alisema, baada ya matokeo kutangazwa.
Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Kagiso Pooe aliambia BBC kwamba Bw McKenzie alikuwa na mtindo wa "ushujaa", ambao unavutia eneo bunge lake.
"Watu wanvutiwa zaidi na mtu anayeelewa maisha yao kwa kuwa alilelewa miongoni mwao na kupambana hadi kufikia ufanisi naishani na haoni haya kusema, 'Hivi ndivyo nilivyo.' Kadhia hii inajitokeza kwa watu kama vile marais wa zamani Jacob Zuma, Donald Trump na watu wengine kama hao," alisema.
Kampeni ya Bw McKenzie dhidi ya wahamiaji wasio na vibali ilipatia kura nyingi, mchambuzi aliongeza.
"Kwa bahati mbaya, wanasiasa wa kawaida na vyama vimekwepa hili na anakabiliana nalo moja kwa moja."
Wakosoaji wa Bw McKenzie walishutumu kampeni yake kama chuki dhidi ya wageni. Aliiendesha chini ya kauli mbiu "Mabahambe", ambayo kwa Kizulu inamaanisha "Lazima waondoke" - na, katika hatua ya kuhimiza hilo, alitembelea mpaka na Zimbabwe kuwafukuza watu wanaojaribu kuingia Afrika Kusini.
Pia alishutumiwa kwa unafiki, kwani wakosoaji wake walieleza kuwa katika mahojiano na SABC 2013 aliwataja wahamiaji kutoka sehemu nyingine za Afrika, ikiwa ni pamoja na Zimbabwe, kama sehemu muhimu ya uchumi wa Afrika Kusini, wakati "tatizo kwetu ni watu ninaowazungumzia hapa, sisi ni wavivu".
Bw Ramaphosa alipoanza mazungumzo kuhusu kubuniwa kwa serikali ya mseto, Bw McKenzie alisema hadharani kwamba anataka naibu wake asimamie wizara ya maswala ya ndani, ambayo inasimamia uhamiaji.
Alijitafutia wizara ya polisi kwani alisema maisha yake ya awali kama jambazi yalimaanisha kuwa alikuwa katika nafasi nzuri ya kukabiliana na kiwango kikubwa cha uhalifu nchini Afrika Kusini.
"Hakuna hata mmoja wao [wanasiasa wengine] aliye na vifaa vya kukabiliana na mafia, kwa viwango vya mauaji tunayoyaona. Afrika Kusini inanihitaji," alinukuliwa akisema na tovuti ya habari ya TimesLive.

Chanzo cha picha, Getty Images
Hakushangazwa aliposhindwa kupata wadhifa huo, akisema kwamba aliomba wizara ya michezo katika mazungumzo ambayo "hayakurekodiwa" na ANC.
“Michezo inaweza kutumika kubadili maisha ya watoto," alisema.
"Kuna ahadi moja ambayo nimetoa: nitafanya spinning [kuendesha gari kwa mduara] kuwa moja ya michezo mikubwa zaidi nchini," aliongeza kwenye chapisho la moja kwa moja la Facebook.
Spinning ni mchezo unaotambulika nchini Afrika Kusini - unahusisha magari yanayoendeshwa kwa miduara na dereva kupanda juu na kufanya vituko.
Lakini kuna matukio mengi ambayo hayajadhibitiwa na kama mwanahabari wa michezo wa IOL John Goliath alivyoandika , unyanyapaa bado ungalipo kwani watu wengi katika vitongoji vya Wahindi na Waafirka mara nyingi huzozana mitaani, jambo ambalo linaonekana kuwa hatari.
Uamuzi wa Bw Ramaphosa kumpa Bw Mckenzie kiti katika baraza lake la mawaziri ni hatari kisiasa, kwani anakabiliwa na uchunguzi ulioamriwa na serikali ya Western Cape, ambayo inadhibitiwa na chama cha Democratic Alliance (DA), mpinzani mkali wa kisiasa wa PA.
Hadi mwaka jana, Bw McKenzie alikuwa meya wa Central Karoo, na alishutumiwa kwa kushindwa kukadiria rand milioni tatu sawa na dola 161 elfu za Kimarekani zilizokusanywa katika dhifa ya glitzy gala mwaka wa 2022 ili kuboresha huduma za umma, ikiwa ni pamoja na kukarabati mabwawa ya kuogelea na kubadilisha vyoo vya ndoo. .
Kulingana na vyombo vya habari vya ndani, mahakama ilimuamuru mwezi uliopita - wiki chache tu kabla ya kupandishwa cheo kwenye baraza la mawaziri - kutangaza rekodi fulani za kifedha kwa wachunguzi.
Wakati PA ikielezea uamuzi huo kuwa "una dosari", DA iliikaribisha, ikisema Bw McKenzie "atafahamu hivi karibuni kwamba rushwa haina faida" .
DA iliendelea na shinikizo wiki iliyopita katika mji mdogo wa Beaufort West, ambao ni sehemu ya Karoo ya Kati, kutaka majibu kuhusu pesa hizo.
Bw McKenzie alisema kwenye chapisho kwenye X kwamba alinuia kuzuru eneo hilo ili kutoa "maoni".
"Ukweli utadhihirika. Sina la kuficha," alisema na kuongeza: "Uongo una miguu mifupi."
Maelezo zaidi kuhusu uchaguzi wa Afrika Kusini:
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Yusuf Jumah












