Siri ya mafanikio ya Zuma Afrika kusini

DC

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

    • Author, Nomsa Maseko
    • Nafasi, BBC

Alituhumiwa kwa ufisadi - alifukuzwa kazi, alishtakiwa kwa ubakaji - aliachiliwa huru, alichaguliwa kuwa rais, alishtakiwa kwa ufisadi tena, alifukuzwa uraisi, alifungwa kwa kudharau mahakama - aliachiliwa huru, alizuiwa kuwa mbunge.

Kwa wanasiasa wengi, lolote kati ya hilo lingewaletea shida katika maisha yao ya kisiasa, lakini si kwa Jacob Zuma wa Afrika Kusini.

Rais huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 82, kufuatia matokeo ya kura za wiki iliyopita yanaonyesha bado ana ushawishi mkubwa.

Yuko kwenye usukani wa chama kipya kilichopambana na chama tawala African National Congress (ANC), akipata 15% ya kura.

Matokeo yamekuwa ya kufedhehesha kwa ANC, chama cha ukombozi ambacho Zuma aliwahi kukiongoza, kimepoteza idadi kubwa ya wabunge kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30 - na "tsunami ya Zuma," kama ilivyoitwa, inahusika kwa kiasi fulani.

Katikati ya jiji la pwani la Durban, jiji kuu katika jimbo la KwaZulu-Natal, uso wa tabasamu wa Zuma unang'aa kwenye mabango ya kampeni ya kijani-nyeusi ya chama chake kilichoanzishwa hivi karibuni, uMkhonto weSizwe (MK) au Mkuki wa Taifa.

Hakuna shaka ushawishi wake hapa ni mkubwa, anaheshimiwa kwa kushikilia tamaduni na jadi za Kizulu.

Pia anasifiwa kwa jukumu lake kama wakala wa amani wakati wa ghasia za kisiasa mwanzoni mwa miaka ya 1990, ambazo nusura zivuruge mpito wa nchi kuelekea demokrasia.

Zaidi ya miaka 20 iliyopita, alipewa sifa ya kuleta wapiga kura wa KwaZulu-Natal kutoka chama cha Zulu cha Inkatha Freedom Party hadi ANC.

CX

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Rais huyo wa zamani aliweza kuchukua wafuasi wake waaminifu hadi Mkhonto weSizwe
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mwaka huu aliweza kuwachukua wafuasi wake waaminifu hadi MK. Chama hicho kimepewa jina la wanamgambo wa zamani wa ANC, ambao wana alama kubwa ya kisiasa kwa sababu ya jukumu lao katika kupigania kukomesha utawala wa wazungu wachache.

Kuzinduliwa kwa ilani ya MK, wiki moja kabla ya uchaguzi wa tarehe 29 Mei katika uwanja uliojaa watu 40,000, ilikuwa ishara tosha kwamba “uBaba” (baba), kama anavyojulikana Zuma, amerejea.

Umati wa wafuasi wake wakistahimili joto kali waliimba: “Zuma! Zuma!”

Mmoja alipiga kelele: "Uyinsizwa nxamala", ambayo inatafsirika kutoka Kizulu kama "shujaa asiye na woga ambaye harudi nyuma."

Siku ya uchaguzi, alipofika katika kituo chake cha kupigia kura, shule ya msingi isiyo na vyoo vya kusukuma, kiongozi huyo wa chama cha MK alilakiwa na mamia ya watu walioita majina ya ukoo wake: “Msholozi, Nxamalala, Maphum’ephethe.”

Rais huyo wa zamani aliwapungia mkono na kutabasamu kabla ya kuingia darasani kupiga kura.

Alipokuwa akiondoka kwenye kituo cha kupigia kura, wafuasi wake waliimba wimbo wa kumuunga mkono Zuma kwa lugha ya Kizulu ambao ulivuma miaka kadhaa iliyopita wakati rais huyo wa zamani aliposhutumiwa kwa ufisadi.

Wimbo mmoja ambao walijizuia kuuwimba, ni ule: “Zuma amefanya nini? Umeathiriwa na propaganda kutoka mji mkuu wa ukiritimba wa wazungu.”

Wanasiasa wengi hutegemea uungwaji mkono kutoka kwa wafuasi wao waaminifu, lakini uwezo wa Zuma wa kuungana na watu maskini na waliotengwa ndio unaomtofautisha.

Na hilo linaeleza juu ya umaarufu wake wa muda mrefu, licha ya kukabiliwa na kashfa nyingi na shutuma kali.

Miaka sita iliyopita, ilionekana kuwa maisha yake ya kisiasa yamekwisha baada ya kuondoshwa katika urais, kufuatia msururu wa madai ya ufisadi, ambayo aliyakanusha.

Cyril Ramaphosa alichukua nafasi yake kama rais na Zuma akatengwa kisiasa na sifa yake ikaharibika.

FGVC

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Wakati rais, Jacob Zuma alikabiliwa na hoja za kutokuwa na imani naye na tuhuma za ufisadi dhidi yake

Kisha miaka mitatu iliyopita, mambo yalizidi kuwa mabaya; alipelekwa jela baada ya kupatikana na hatia ya kudharau mahakama kwa kushindwa kutoa ushahidi katika uchunguzi wa kimahakama kuhusu ufisadi katika kipindi chake cha miaka tisa kama rais.

Kukamatwa kwake Julai 2021 kulizua ghasia mbaya zaidi tangu kumalizika kwa utawala wa wazungu wachache mwaka 1994 na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 300.

Alihukumiwa kifungo cha miezi 15, lakini Rais Ramaphosa alimwachilia huru baada ya kuhudumu miezi mitatu pekee, katika jaribio la kumtuliza yeye na wafuasi wake waliokuwa na hasira.

Wiki chache tu zilizopita, Zuma alipata pigo jingine baada ya kuzuiwa kisheria kuwa mbunge kwa sababu ya kutiwa hatiani. Lakini hayo yote hayakuwarudisha nyuma wafuasi wake.

Licha ya kusimamishwa kwake kutoka ANC, Zuma anasalia kuwa mwanachama wa chama kilichokomesha ubaguzi wa rangi.

Hakuenda shule na hakulelewa katika malezi ya kawaida, harakati zake za kupinga ubaguzi wa rangi zilimfanya kufungwa miaka 10 katika gereza maarufu la Robben Island pamoja na Nelson Mandela.

Baada ya marufuku dhidi ya ANC kuondolewa na serikali ya wazungu mwaka 1990, Zuma alirejea kutoka uhamishoni na kupanda vyeo vya chama hicho. Mwaka 1999 aliteuliwa kuwa naibu rais wa nchi.

Alihusishwa na tuhuma za rushwa mwaka 2005, ambazo alikanusha, zikihusisha mkataba wa silaha mwaka 1999 na alifutwa kazi na Rais wa wakati huo Thabo Mbeki. Kesi hii inaendelea - na bado anakabiliwa na mashtaka juu ya kashfa ya mabilioni ya dola.

Desemba mwaka huo, alishtakiwa kwa kumbaka binti wa mwanachama wa ngazi ya juu wa chama hicho. Alikiri kufanya mapenzi na mwanamke huyo, ambaye alikuwa na VVU, lakini akasema kulikuwa na makubaliano.

Zuma alitoa dhihaka aliposema alioga baada ya kujamiiana ili kuzuia maambukizi ya VVU na aliamini mwanaume mwenye afya hawezi kupata VVU kutoka kwa mwanamke.

Mwaka uliofuata, aliachiliwa kwa kosa la ubakaji.

C

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Kesi ya ubakaji ilifanyika miaka michache kabla ya kuwa rais

Alipambana kurejea kileleni mwa ANC na kuwa rais mwaka 2009.

Zuma alisalia katika nafasi hiyo hadi alipolazimika kujiuzulu 2018 baada ya shinikizo kubwa kutoka chama chake.

Hii ilikuja baada ya kushutumiwa kuhusika katika mchakato ulioruhusu familia ya wafanyabiashara matajiri - Guptas - kuwa na ushawishi mkubwa wa kisiasa.

Zuma na ndugu wa Gupta wamepuuzilia mbali madai ya ufisadi na kusema kuwa ni uzushi. Rais huyo wa zamani na wafuasi wake wanamlaumu mrithi wake, Ramaphosa, kwa kuanguka kwake.

Na sasa anaweza kutaka kusuluhisha uhasama na mpinzani wake.

Huku mazungumzo ya muungano yakiendelea, chama cha MK kimeweka wazi kuwa kitaunda ushirikiano na ANC iwapo rais atajiuzulu.

Akiwa ametiwa moyo na utendaji wa chama chake, Zuma alirusha ngumi ya kwanza Jumamosi, akidai kulikuwa na kasoro katika uchaguzi.

"Usituchokoze, usianze matatizo," alisema katika mkesha wa kutangazwa matokeo ya mwisho ya uchaguzi.

Tume ya uchaguzi imekanusha vikali madai haya.

Polisi sasa wako macho kwa sababu ya hatari ya kutokea machafuko kufuatia madai ya Zuma.

Hata hivyo licha ya uhusiano mbaya na ANC, chama hicho tawala hakijaondoa uwezekano wa kuungana MK.

"Tunazungumza na kila mtu ambaye yuko tayari kuunda serikali nasi," amesema katibu mkuu wa ANC, Fikile Mbalula.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi