Uchaguzi Afrika Kusini: Jacob Zuma- rais aliyeondolewa madarakani sasa kuamua mustakabali wa uongozi wa nchi

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Nomsa Maseko
- Nafasi, BBC News
- Akiripoti kutoka, Durban
Miaka sita iliyopita, Jacob Zuma, rais wa zamani wa Afrika Kusini mwenye umri wa miaka 82, alikuwa mfuasi wa kisiasa na chapa iliyoharibika alipolazimishwa kujiuzulu kama rais.
Lakini amerejea kwa kishindo katika ulingo wa siasa katika kile kinatajwa kuwa ‘tsunami ya Zuma’.
Pamoja na hayo, Zuma anasalia kuwa na utata kama zamani. Hii kwa kiasi fulani inatokana na mtindo wake wa kupendwa na watu wengi, lakini pia uhusiano wake unaodaiwa kuwa wa kifisadi na familia tajiri ya Gupta.
Matokeo rasmi ya uchaguzi mkuu wa Afrika Kusini yanaonyesha chama chake kilichoanzishwa hivi karibuni cha Umkhonto weSizwe, kinachojulikana kwa ufupisho wa MK, kilishinda zaidi ya 14% ya kura.

Chama chake kilipata jumla ya kura milioni 2.3 kati ya zaidi ya kura milioni 16.2 zilizopigwa, kikishika nafasi ya tatu nyuma ya chama cha mrengo wa kati cha Democratic Alliance (DA) na chama tawala cha African National Congress (ANC).
Watu wengi wamelinganisha kupanda na kushuka kwa Zuma na kule kwa Donald Trump, ambaye wiki hii alikua rais wa kwanza wa Marekani kuwahi kuhukumiwa kwa uhalifu.
Miaka mitatu iliyopita, Zuma alipelekwa jela baada ya kupatikana na hatia ya kudharau mahakama kwa kushindwa kutoa ushahidi katika uchunguzi wa mahakama kuhusu rushwa katika kipindi chake cha miaka tisa kama rais.
Kukamatwa kwake Julai 2021 kulizua ghasia mbaya zaidi tangu mpito wa Afrika Kusini kuelekea demokrasia, na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 300.

Chanzo cha picha, Reuters
Hadhi ya mtu Mashuhuri
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wiki chache zilizopita, Zuma kwa mara nyingine tena alionekana kutokuwa na bahati baada ya kuzuiwa kisheria kugombea ubunge kutokana na kutiwa hatiani.
Lakini, uamuzi huo haukuathirichama chake ikizingatiwa jinsi ilivyofanya katika uchaguzi mkuu. Inaonekana wapiga kura hawakukatishwa tamaa kwa kuona uso wa Zuma kando ya alama ya chama chake kwenye karatasi za kupigia kura.
Zuma ametiwa moyo na matokeo hayo.
"Hakuna mtu anayepaswa kutangaza matokeo, usituchokoze, usianzishe vurugu," Zuma alisema katika mkesha wa matokeo ya mwisho ya uchaguzi katika kile kilichoonekana kuwa tishio lililofichwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi ya nchi hiyo (IEC), baada ya MK. na vyama vingine 25 vya upinzani kuishutumu IEC kwa wizi wa kura.
Licha ya MK kupata idadi kubwa zaidi ya kura katika jimbo analotoka Zuma la Kwa-Zulu Natal na kushika nafasi ya tatu kitaifa, chama hicho kinadai kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na si wa kuaminika.
IEC imekanusha vikali madai haya.
Kuwasili kwa Zuma ambako hakutarajiwa katika kituo cha matokeo ya uchaguzi huko Johannesburg Jumamosi usiku - usiku wa kuamkia kutangazwa kwa matokeo rasmi - kuliibua msisimko katika jengo hilo, kana kwamba nyota wa muziki wa Amapiano au Afropop ilikuwa ikiingia jukwaani.
Kurejea kwake kumetambuliwa na washirika wa zamani na hata wapinzani wa sasa kutoka chama cha ANC.
"Jacob Zuma ni kiongozi anayepaswa kuzingatiwa katika siasa za Afrika Kusini ... hatukuwahi kumdharau," alisema Katibu Mkuu wa ANC Fikile Mbalula, alipokuwa akitafakari juu ya utendaji dhaifu wa uchaguzi wa chama chake.

Chanzo cha picha, Reuters
Uhusiano ya ANC
Licha ya kusimamishwa uanachama wa ANC, Zuma bado ni mwanachama wa chama kilichokomesha ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.
Alipozindua chama chake kipya cha MK mwezi Desemba, Zuma alitangaza kwamba atakuwa mwanachama wa ANC daima. Lakini wakati huo huo, aliwataka wafuasi wa ANC kukiacha chama.
Umaarufu wa Zuma bila shaka unanaikosesha usingizi ANC.
Uhusiano kati ya chama hicho na Zuma uemeanza mbali tangu zama zile ambapo kilikuwa shirika haramu chini ya mfumo wa ubaguzi. Kwa kutokuwa na shule rasmi na malezi ya kawaida, harakati za Zuma za kupinga ubaguzi wa rangi hatimaye zilimfanya kufungwa kwa miaka kumi katika Kisiwa cha Robben pamoja na Nelson Mandela.
Baada ya marufuku dhidi ya ANC kuondolewa na serikali ya ubaguzi wa rangi mwaka 1990, Zuma alirejea kutoka uhamishoni na kupanda vyeo vya kisiasa. Mwaka 1999 aliteuliwa kuwa naibu rais wa nchi.
Muda wake madarakani uliisha ghafla mwaka 2005 alipofutwa kazi na Thabo Mbeki baada ya kuhusishwa na tuhuma za ufisadi zilizohusisha mkataba wa silaha.
Mshauri wake wa zamani wa masuala ya fedha Shabir Shaik alipatikana na hatia ya kuomba hongo kutoka kwa kampuni ya silaha ya Ufaransa kwa niaba yake. Baadaye mwaka huo huo, Zuma mwenyewe alikabiliwa na mashtaka ya rushwa. Haya yalitupiliwa mbali na kurejeshwa mara kadhaa huku Zuma akidai kuwa madai hayo yanatokana na hujuma ya kisiasa dhidi yake.
Mnamo Desemba 2005, Zuma, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 63, alishtakiwa kwa ubakaji na binti wa mshirika wa chama. Alikuwa na umri wa miaka 31 wakati huo na alilazimika kuficha utambulisho wake baada ya yeye na mamake kukashifiwa na wafuasi wa Zuma.
Maelfu ya wafuasi walikusanyika nje ya mahakama wakati wa kesi ya Zuma ya ubakaji. Alikiri kufanya mapenzi bila kinga na mshtaki huyo mwenye Virusi Vya Ukimwi(VVU) lakini akasema kukutana kwao kulikuwa kwa makubaliano. Mwaka uliofuata, aliondolewa mashtaka yote.
Uwezo wa Zuma kuungana na maskini na waliotengwa katika jamii ya Afrika Kusini ndio unaomtofautisha na wanasiasa wengi. Kuondolewa kwa mashtaka ya ubakaji dhidi yake kulisababisha mzozo wa uongozi wenye utata katika historia ya ANC.
Mwaka 2005, jaji alisema mashtaka ya rushwa na ulaghai dhidi ya Zuma yalionyesha ushahidi wa kuingiliwa kisiasa na rais wa zamani Thabo Mbeki au wafuasi wake.
Mbeki aliombwa na ANC kujiuzulu kama rais siku chache baadaye. Zuma, ambaye alisalia kuwa maarufu katika chama, alichaguliwa kuwa rais wa ANC katika kongamano la uchaguzi la chama mwaka 2007 mjini Polokwane.
Mwaka 2009, Zuma alichaguliwa kuwa Rais wa Afrika Kusini. Alidumu katika nafasi hiyo hadi alipolazimika kujiuzulu mwaka wa 2018 baada ya shinikizo kubwa kutoka kwa chama chake.
Licha ya malumbano makali yaliyosababisha Zuma kuondolewa madarakani, ANC haijaopinga uwezekano wa kubuni muungano na chama cha MK.
"Tunazungumza na kila mtu ambaye yuko tayari kuunda serikali nasi," Katibu Mkuu wa ANC Fikile Mbalula alisema.
MK imesema itakuwa tayari kuingia katika ushirikiano na ANC, lakini uungwaji mkono wao una masharti ya Rais Cyril Ramaphosa kujiuzulu.
ANC imesema hitaji hili halina mjadala. Lakini ukweli ni kwamba Zuma atakumbukwa kama mchezaji wa mchezo wa chess ambaye aliipandisha daraja ANC katika chaguzi zisizotabirika nchini humo.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Yusuf Jumah












