Kuna mifupa ya watu katika mpaka hatari wa Afrika Kusini

Chanzo cha picha, BBC/Ed Habershon
- Author, Jenny Hill
- Nafasi, BBC News, Musina
Wahamiaji wengi wanahatarisha maisha yao kufika Afrika Kusini, wakifanya safari ya hatari kuvuka mpaka kutoka Zimbabwe. Hukimbia umaskini na kukata tamaa katika nchi zingine za Afrika - hujihisi hawana chaguo.
Lakini Afrika Kusini kwenyewe hisia za chuki dhidi ya wageni zinaongezeka na serikali iko chini ya shinikizo la kuongeza ulinzi mpakani.
Wanaume waliombaka Portie Murevesi hawakujali kwamba alikuwa mjamzito. Walimshambulia kwa chupa za glasi pia, alituambia, huku akionyesha kovu kubwa kwenye paji la uso wake.
Sasa anakaribia kujifungua, amepata hifadhi katika makazi ya kanisa katika mji wa mpakani wa Afrika Kusini wa Musina.
"Ninapojaribu kulala wakati mwingine, naona walichonifanyia wanaume hao," aliiambia BBC.
Musina inajulikana kuwa ni mahali pa kukimbilia wahamiaji ambao huingia kinyume cha sheria kama vile Bi Murevesi.

Chanzo cha picha, BBC/Ed Habershon
Wahamiaji wanaofanikiwa kupita hufanya safari ngumu ya kupitia vichaka. Ni eneo lisilo na sheria na ni hatari. Wanyama wa porini na magenge ya wahalifu ni tishio la wakati wote.
Visa vya wizi, kupigwa, ubakaji na hata mauaji hutokea mara kwa mara.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Ni hatari sana," mwanamume mmoja wa Zimbabwe, anayejiita tu George, alituambia.
"Unaona mifupa, unaona mtu tayari ameuawa miezi miwili au mitatu iliyopita."
Mmoja alieleza: "Hatuwezi kurejea Zimbabwe kwa sababu hakuna kitu huko. Tunakufa njaa. Hakuna chakula."
Hakuna anayejua kwa uhakika ni wahamiaji wangapi wasio na vibali wanaishi nchini Afrika Kusini, yenye uchumi wa juu zaidi barani humo.
Sensa ya mwisho iligundua kulikuwa na zaidi ya wageni milioni 2.4 - karibu nusu yao Wazimbabwe - wanaoishi nchini humo, wakichukua zaidi ya 3% ya watu wote.
Lakini hakuna makadirio rasmi ya idadi ya wale ambao wameingia kinyume cha sheria.
Na huku uchaguzi mkuu ukipangwa kufanyika mwishoni mwa Mei, uhamiaji limekuwa suala la mjadala mzito wa kisiasa.
Serikali ya Afrika Kusini inasema inaimarisha usalama wa mpaka.
Kwenye mto wa mpakani kumekauka. Na hivyo katika joto kali, makumi ya watu wanatembea kuingia na kutoka kuvuka mpaka.
Mikokoteni ya punda, iliyosheheni bidhaa, huvuka mto. Wanawake na vifurushi kwenye vichwa vyao, hutembea haraka kuvuka.
Walituambia inachukua kama dakika tano kutembea kutoka kijiji cha karibu cha Zimbabwe hadi Afrika Kusini.
Na hakuna kitu - hakuna uzio, hakuna walinzi - kuwazuia.
John - ambaye aliomba jina lake libadilishwe ili kulinda utambulisho wake – akiwa juu ya mkokoteni wake, mara kwa mara akiwapiga mjeledi punda wake waliobeba matikiti.

Chanzo cha picha, BBC/Ed Habershon
Ana familia nyumbani Zimbabwe, alituambia. Lakini hakuna kazi huko, hakuna chakula cha kutosha. Kwa hivyo sasa analima matikiti na huyaleta ili kuyauza nchini Afrika Kusini, ambako yana bei ya juu zaidi.
"Ninafanya hivi ili kuishi," anasema.
Ni soko linalostawi, haramu, la kuvuka mpaka. Wakati wahamiaji wanaovuka hapa wanakabiliwa na safari ya kuchosha hadi Musina, bidhaa nyingi husafirishwa kwa mkokoteni au gari.
John alituambia, mara kwa mara askari hufika na kukamata watu. Lakini kwa kawaida kuna onyo la mapema, aliongeza, na ni rahisi - ingawa ni hatari - kujificha kwenye kichaka.
Lakini serikali ya Afrika Kusini inataka kurudisha udhibiti. Mwaka jana Rais Cyril Ramaphosa alizindua kikosi kipya cha mpakani.
Mike Masiapato, kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mipaka (BMA), alituambia anatuma mpakani maafisa wapya 400 waliofunzwa na kununua ndege zisizo na rubani, kamera za mwili na pikipiki ili kuboresha ufuatiliaji.
"Ninaweza kukuhakikishia uongozi wa sasa wa nchi unaelewa umuhimu wa kazi hii."

Chanzo cha picha, AFP
Lakini hata Masiapato anakubali kwamba itachukua muda kuulinda mpaka wa nchi hiyo.
"Tumeanza kuimarisha mazingira. Tunatumai katika miaka michache ijayo tutaweza kufanikiwa."
Chama tawala nchini humo, African National Congress (ANC), baada ya miongo mitatu madarakani, ANC inaongoza nchi ambayo haina nishati ya kutosha na usambazaji wa maji.
Raia wake wanakumbwa na viwango vya juu vya ukosefu wa ajira na uhalifu.
Huku Afrika Kusini ikielekea kwenye kile ambacho kura za maoni zinatabiri kuwa uchaguzi mchungu kwa ANC, haishangazi kwamba baadhi ya wapinzani wa kisiasa - kama vile chama kinachopinga wahamiaji cha Operesheni Dudula - wanalaumu waziwazi wahamiaji kwa masaibu ya nchi.
Na maneno ya chuki dhidi ya wageni yameenea, huku wahamiaji pia wakilaumiwa kwa kuchukua kazi kutoka kwa wenyeji.
Hata Rais Ramaphosa amesema kuwa raia wa kigeni wasio na hati wanazidisha matatizo ya kijamii na kiuchumi ya Afrika Kusini.
Na vyama vingine vya upinzani vinataka ulinzi mkubwa wa mipaka, ikiwa ni pamoja na ActionSA, ambayo kilichoundwa miaka minne iliyopita na Herman Mashaba, mwanasiasa na meya wa zamani wa Johannesburg.
"Serikali ya ANC imeshindwa," anasema Malebo Kobe, msemaji wa kanda wa ActionSA.
Bi Kobe, ambaye tulikutana nae katika wa Zimbabwe, anasema uhamiaji haramu ndio unaoongoza mjadala katika masuala ya wapiga kura katika eneo hili.
Anasema hospitali za ndani na huduma zingine zimezidiwa na wahamiaji wasio na hati ambao huja hapa kutafuta huduma za afya au faida zingine.
"Itakuwa ni ajabu tusipozungumza kuhusu ukweli wa kile kinachotokea kwa mifumo yetu ya umma - watu wasiolipa kodi, wanatarajia kuishi na kufaidika na bidhaa na huduma ambazo serikali yetu hutoa."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












