Ndani ya kundi la chuki dhidi ya wageni Afrika Kusini

Na Ayanda Charlie huko Johannesburg & Tamasin Ford huko London
BBC Africa Eye
Kundi la chuki dhidi ya wahamiaji nchini Afrika Kusini Operesheni Dudula limefahamika kwa kuvamia biashara za raia wa kigeni na kulazimisha maduka kufunga. BBC Africa Eye imepata fursa nadra ndani ya shughuli za wanachama wa vuguvugu maarufu zaidi la kupinga wahamiaji nchini humo
Katika jikoni ya shule huko Kwa Thema, kitongoji kilicho mashariki mwa Johannesburg, Dimakatso Makoena anashughulika kutengeneza mkate wa sandwichi. Mzazi huyo asiye na mwenzi mwenye umri wa miaka 57 wa watoto watatu amekuwa mpishi huko kwa zaidi ya miaka 10.
"Kusema ukweli, ninachukia wageni. Jinsi ninavyotamani wangepakia na kuondoka katika nchi yetu," anasema, akizuia machozi.
Ni vigumu kuelewa nguvu ya chuki hii hadi Bi Makoena anapochomoa simu yake kuonyesha picha ya mwanawe. Akiwa amekonda ,makovu ya moto ya hasira yalienea mwilini mwake, juu ya mikono yake na usoni mwake.
“Alianza kutumia dawa za kulevya akiwa na umri wa miaka 14,” asema, akieleza jinsi mtoto wake anavyotoka kwenda kuiba vitu ili kutosheleza uraibu wake. Siku moja alikuwa amejaribu kuchukua nyaya za umeme ili kuuza ndipo aliponaswa na umeme na kuungua.

Mwanawe anatumia crystal meth na nyaope, dawa za kulevya za mitaani ambazo zimeharibu jamii kote Afrika Kusini . Ni hadi anapowalaumu wageni kwa kuuza dawa hizo ndipo hoja yake na kuunga mkono Operesheni Dudula inakuwa wazi.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Dudula, hicho ndicho kitu pekee kinachonifanya niendelee," anaiambia BBC.
Operesheni Dudula ilianzishwa Soweto miaka miwili iliyopita, kundi la kwanza kurasimisha yale yaliyokuwa mawimbi ya mara kwa mara ya mashambulizi ya chuki dhidi ya wageni nchini Afrika Kusini ambayo yalianza muda mfupi baada ya utawala wa wazungu wachache kumalizika mwaka 1994. Linajiita kuwa ni la kiraia,harakati, inayoendeshwa kwenye jukwaa la kupinga wahamiaji, na neno "dudula" linamaanisha "kulazimisha kutoka" kwa Kizulu.
Soweto ilikuwa mstari wa mbele katika upinzani dhidi ya ubaguzi wa rangi na nyumbani kwa Nelson Mandela, rais wa kwanza wa Afrika Kusini kuchaguliwa kidemokrasia. Sasa, kitongoji hicho kimekuwa makazi ya kikundi maarufu zaidi cha kupinga wahamiaji nchini.
Huku mwananchi mmoja kati ya watatu wa Afrika Kusini akiwa hana kazi katika mojawapo ya jamii zisizo na usawa duniani, wageni kwa ujumla wamekuwa walengwa rahisi.
Lakini idadi ya wahamiaji wanaoishi Afrika Kusini imetiwa chumvi kupita kiasi. Kulingana na ripoti ya mwaka 2022 ya Taasisi ya Mafunzo ya Usalama (ISS) , shirika huru la utafiti lenye makao yake makuu katika mji mkuu, Pretoria, kuna wahamiaji wapatao milioni 3.95 nchini Afrika Kusini, ambao ni asilimia 6.5 ya watu wote, idadi inayolingana na kanuni za kimataifa. Idadi hii inajumuisha wahamiaji wote, bila kujali hali ya kisheria au wapi wanatoka.
Maneno ya chuki dhidi ya wageni yanayotumiwa na baadhi ya viongozi wa umma, wanasiasa na makundi yanayopinga wahamiaji yamesaidia kuchochea imani potofu kwamba nchi imejaa wahamiaji. Utafiti wa Mtazamo wa Kijamii wa Afrika Kusini wa mwaka 2021 uligundua kuwa karibu nusu ya watu milioni 60 waliamini kuwa kuna wahamiaji kati ya milioni 17 na 40 nchini humo.
Kura za maoni za hivi sasa zinaonyesha uungwaji mkono kwa chama tawala cha African National Congress (ANC), chama kilichokuwa kikiongozwa na Mandela, unaweza kushuka chini ya 50% kwa mara ya kwanza.
Operesheni Dudula ina matamanio ya kujaza pengo hilo na sasa imejigeuza kutoka kundi la wenyeji la kupinga wahamiaji na kuwa chama cha kisiasa cha kitaifa, kikieleza malengo yake ya kuwania uchaguzi mkuu mwaka ujao.

Zandile Dabula, ambaye alipigiwa kura kama rais wa Operesheni Dudula mnamo Juni 2023, ni mtulivu, mwenye haiba na msisitizo kuhusu ujumbe wa kikundi: "wageni" ndio sababu kuu ya matatizo ya kiuchumi ya Afrika Kusini.
Inapoelezwa kwamba kampeni hii inategemea chuki pekee, anaiambia BBC: "Lazima tuwe wakweli hapa kwamba matatizo mengi tuliyo nayo yanasababishwa na kufurika kwa raia wa kigeni.
"Nchi yetu ni ya fujo. Raia wa kigeni wanafanyia kazi mpango wa miaka 20 wa kuchukua Afrika Kusini."
Alipohojiwa kuhusu ukweli wa mpango huu wa miaka 20, anakubali kuwa ulikuwa uvumi lakini anasema anaamini kuwa ni kweli.
"Unaona madawa ya kulevya kila mahali na wengi wa waathirika wa madawa ya kulevya ni wa Afrika Kusini kuliko raia wa kigeni. Kwa hiyo, nini kinatokea? Je, wanawalisha ndugu zetu wenyewe ili iwe rahisi kwao kuchukua?" anasema.
Hata hivyo hasira zinazotolewa kwa wahamiaji zinaweza kuwa kwa wale ambao wako nchini kihalali na wanaofanya kazi kisheria. Mfanyabiashara wa kutoka Nigeria, ambaye alikuwa mlengwa wa uvamizi wa wanachama wa Operesheni Dudula huko Johannesburg mapema mwaka huu, aliambia BBC kwamba wanawake wawili waliomtia doa na kuharibu nguo zake kwa kuzitupa kwenye mfereji wa maji hawakuacha kuuliza maswali.
Walipokuwa wakimpiga risasi anasema walimtukana, wakisema: "Lazima uende Nigeria… Sisi ni Dudula, sisi ni Afrika Kusini."
Akiwa hana bidhaa za kuuza, sasa analala mitaani: "Ninapiga kura katika nchi hii. Mimi ni raia wa hapa. Sijawahi kuona nchi ikiwatendea watu hivi. Ikiwa ninafanya jambo lisilo halali, sawa. Nifukuze. Lakini sifanyi chochote kinyume cha sheria. Sasa unafanya maisha yangu kuwa duni, siwezi kulipa kodi yangu. Nataka kwenda, haya yamezidi."
Operesheni Dudula inashikilia kuwa ni wasiwasi juu ya uwepo mkubwa wa madawa ya kulevya katika jamii zilizotengwa zaidi nchini Afrika Kusini ambalo ndio malalamiko yao makubwa, lakini hakuna data ya kuunga mkono madai kwamba watu wanaouza madawa ya kulevya si raia wa Afrika Kusini.
Takwimu linganishi hazipatikani kwa uhalifu wa dawa za kulevya, ingawa ripoti ya ISS inamnukuu waziri wa sheria akisema kuwa wahamiaji ni 8.5% ya kesi zote zilizopatikana na hatia mnamo 2019 na 7.1% mnamo 2020. ISS inaongeza kuwa 2.3% ya wafungwa wanaofungwa kila mwaka hawana hati za kuwa nchini humo .
Huko Diepkloof, mashariki mwa Soweto, BBC inajiunga na kile kinachoitwa kikosi kazi cha Dudula. Wanaume wakiwa kwenye malori wanaenda kukabiliana na muuza duka wa Msumbiji ambaye mama mwenye nyumba kutoka Afrika Kusini anadai kuwa hajalipa kodi yake.
Inadaiwa kuwa ni mazungumzo lakini haraka hali inageuka na kuwa mzozo ambapo mmoja wa wanaume hao, Mandla Lenkosi, anatishia kumpiga. Wakati BBC inawauliza kuhusu tabia zao za kijambazi, wanashikilia kuwa wanatekeleza sheria.
Bw Lenkosi, pia kutoka Soweto na asiyekuwa na kazi, anashiriki katika uvamizi wa nyumba za wahamiaji na maeneo ya kazi, watu ambao wanashukiwa kwa chochote kuanzia biashara ya dawa za kulevya hadi kusalia nchini humo vila stakabadhi zifaazo

"Tulikulia katika nyakati za ubaguzi wa rangi, ambapo mambo yalikuwa mazuri zaidi kuliko ilivyo sasa," anasema, akionyesha matatizo ya madawa ya kulevya. "Sheria ilikuwa sheria [wakati huo]."
Mfuasi mwenzake wa Dudula, Cedric Stone, anakubali: "Afrika Kusini inahitaji kurejea Afrika Kusini ya zamani ambayo tunaijua.
"Baba zetu walianzisha vioski vya mitaani lakini leo zote ni wageni, hasa, Bangladesh, Somalia na Ethiopia. Kwa nini?"
Rais Cyril Ramaphosa amezungumza dhidi ya maandamano ya kuwapinga wahamiaji, na kulaani makundi kama hayo kwa kuwanyanyasa na kuwashambulia wahamiaji. Amefananisha tabia zao na mikakati iliyopitishwa na utawala wa kibaguzi kukandamiza jamii za watu weusi.
Mnamo 2019 alizindua Mpango Kazi wa Kitaifa wa kupambana na ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya wageni , lakini wanaharakati wanataka serikali kufanya zaidi.
Annie Michaels, mwanaharakati kutoka Jopo la Ushauri la Wahamiaji la Johannesburg, anasema Waafrika Kusini wanalaumu watu wasio sahihi kwa matatizo yao na wanapaswa kuwastahi wahamiaji kutokana na ujuzi wao wa kuishi.
"Acha kukaa na kulalamika na kufa katika kona hiyo na kusubiri serikali ambayo inashindwa kila siku," anaiambia BBC.
"Wahamiaji... ndio maskini zaidi ya maskini. Afadhali waende kwao na kuwachezea, badala ya kuwavalia njuga watu wanaoishi kwenye nyumba za vioo."
Kwa upande wake, Bi Dabula anasema wakosoaji wa Operesheni Dudula ambao wanadumisha kuwa ni mkusanyiko wa walinzi wenye jeuri ni makosa.
"Hatuendelezi vurugu na hatutaki watu wahisi kunyanyaswa," lakini anaongeza: "Hatuwezi kupitwa na raia wa kigeni na kufanya chochote kuhusu hilo."
Mamia ya wafuasi walisafiri kuhudhuria mkutano wake wa kwanza wa kitaifa mjini Johannesburg mwezi Mei, ambapo wanachama walipiga kura kusajili kundi hilo kama chama cha kisiasa.

Kupeperusha bendera za Afrika Kusini, kucheza na kuimba barabarani hadi Ukumbi wa Jiji, inahisi kama sherehe.
Hata hivyo, nyimbo wanazoimba zina ujumbe wa kutisha: "Mchome mgeni. Tutaenda kwenye karakana, kununua petroli na kumchoma mgeni."
Mavazi ya kijeshi yanaleta kumbukumbu za wakati wa mapambano ya ukombozi wa Afrika Kusini. Yote huwasilisha utayari wa vita.
Bi Makoena pia yuko pale, akitabasamu na amevalia T-shirt ya sherehe yake. "Operesheni Dudula itaweka historia leo," anasema.
Akiwa jukwaani, Isaac Lesole, mshauri wa kiufundi wa Operesheni Dudula, ana swali kwa wafuasi wanaoshangilia: "Je, tunataka amani na wageni haramu?"
"Hapana," watazamaji wanapiga kelele kwa pamoja.
Kulingana na sheria ya Afrika Kusini, kusajili chama haimaanishi kuwa kitafuzu moja kwa moja kugombea uchaguzi - ina misururu ya hatua za kupitia.
Operesheni Dudula haina ilani au sera yoyote isipokuwa msimamo wake kuhusu wageni, ingawa Bi Dabula anashikilia kuwa ina uwepo katika kila mkoa isipokuwa Cape Kaskazini.
Wafuasi wa chama hicho kipya waliozungumza na BBC wanaonekana kutaka mambo yarekebishwe katika jamii zao. Inaonesha mabadiliko ya hali ya hewa katika mazingira ya kisiasa ya Afrika Kusini na watu waliochoshwa na hali ilivyo.
Hata hivyo, mchanganyiko wa umaskini, madawa ya kulevya na hofu imesababisha mchezo wa lawama ambapo wahamiaji wamekuwa kisingizio cha kutwikwa lawama
Unaweza kutazama filamu kamili ya BBC Africa Eye 'Fear and Loathing in South Africa' hapa kwenye idhaa ya YouTube ya BBC Africa.















