Dudula: Jinsi hasira za wazawa wa Afrika Kusini zilivyowalenga wageni

Watu wakiwa kwenye maandamano

Chanzo cha picha, AFP

Polisi nchini Afrika Kusini wako katika hali ya tahadhari iwapo kutakuwa na makabiliano mapya kati ya wakazi wa kitongoji cha Alexandra mjini Johannesburg na wachuuzi wa mitaani wa kigeni.

Alexandra ni mojawapo ya maeneo maskini zaidi nchini Afrika Kusini lakini kutoka kwenye vibanda vyake, wakazi wanaweza kuona kwa urahisi majumba marefu ya Sandton, mojawapo ya wilaya tajiri zaidi za kibiashara katika bara zima, kilomita chache tu kutoka hapo. Matokeo yake watu kutoka kote Afrika Kusini na nchi jirani humiminika katika kitongoji hicho ili kuutumia kama msingi wa kujipatia riziki.

Makundi mawili yenye utata - Vuguvugu la Alexandra Dudula na Operesheni Dudula - ambayo yanafanya kampeni dhidi ya raia wa kigeni wasio na vibali yameibuka hivi karibuni na uungwaji mkono

unaonekana kuongezeka miongoni mwa jumuiya za Afrika Kusini ambazo zinahisi kutengwa.

Kuna wasiwasi kwamba kampeni zao zinaweza kusababisha kuzuka tena kwa ghasia za chuki dhidi ya wageni nchini humo.

Je, makundi haya yanataka nini?

Umaskini ndio chanzo kikuu cha mvutano kama wakazi wa Afrika Kusini wanavyoamini - iwe sawa au vibaya - kwamba wageni ndio sababu ya shida zao nyingi.

Dudula ni neno katika lugha ya Kizulu ambalo linamaanisha "kusukuma" au "kurudisha nyuma" - hii inatoa picha kuhusu kile wanachotaka.

Ingawa makundi hayo mawili ni tofauti, yametiwa moyo na sababu moja - wote wanatumai kuwafukuza wahamiaji Waafrika wasio na vibali kutoka katika jumuiya zao.

Wanaamini kwa kufanya hivi wanaweza kuhakikisha kuwa ajira na fursa za biashara zinakwenda kwa Waafrika Kusini.

Kuna tofauti gani kati ya vikundi hivyo viwili?

Alexandra Dudula Movement ilianzishwa mwaka jana. Watu nyuma yake walidai kuwa raia wa kigeni walikuwa wakimiliki kinyume cha sheria nyumba zilizotolewa na serikali huko Alexandra, ambazo zinapaswa kuwa za raia masikini.

Maandamano

Chanzo cha picha, AFP

Lakini kampeni hiyo imepanuka na kujumuisha wito kwa wahamiaji wote wa Kiafrika wasio na vibali kuacha kufanya biashara huko Alexandra. Mwezi uliopita, vuguvugu hilo lilifunga vibanda vyote vinavyomilikiwa na raia wa kigeni ambao hawakuweza kuonesha karatasi sahihi za kuendesha biashara hiyo au pasi halali za kuafiria.

Kisha waliwapa vibanda Waafrika Kusini, kama vile mkazi wa Alexandra Wendy Sithole, ambaye alianza kuuza mboga wakati wageni hao walilazimishwa kuacha.

"Sisi kama Waafrika Kusini hatuna ajira na tuna njaa. Tunachotaka ni kupata kazi pia," aliiambia BBC. "Wanatarajiaje sisi kuishi katika nchi yetu wenyewe?"

Sio hatua zote za kikundi zimekuwa za kisheria na mamlaka inachunguza kesi za machafuko ya umma na vitisho.

Operesheni Dudula iko katika kitongoji cha Soweto cha Johannesburg - zaidi ya kilomita 25 (maili 16) upande wa pili wa jiji.

Ilianzishwa na Nhlanhla Lux Dlamini mwenye umri wa miaka 33, ilikuja kujulikana Juni mwaka jana wakati wakazi wa Soweto waliandamana katika kitongoji hicho kwa kile kilichoitwa "operesheni ya kusafisha".

Iliwalenga washukiwa wa uuzaji wa dawa za kulevya na watu ambao walidaiwa kumiliki mali ya serikali kinyume cha sheria.

Lakini kama vile Alexandra, wigo wa maslahi ya kikundi umeongezeka.

Operesheni Dudula jijini Soweto

Chanzo cha picha, AFP

Wanachama sasa wanataka wamiliki wengi wa maduka ya kigeni nchini Afrika Kusini kufunga biashara zao na kuondoka nchini humo.

Pia wanataka biashara ndogo ndogo, kama vile migahawa na maduka, kuajiri raia wa Afrika Kusini pekee. Hii ni kwa sababu wanakampeni wanaamini kuwa maeneo haya hayawaangalii Waafrika Kusini na kuajiri wahamiaji wasio na vibali badala yake kwa sababu wanaweza kuwalipa chini ya kima cha chini cha mshahara.

Mamlaka zimesema ingawa hili linaweza kutokea katika baadhi ya maeneo sio tatizo lililoenea.

Makundi yote mawili yamekanusha kuwa nia zao ni chuki dhidi ya wageni na wanadai kuwa wanalinda tu maisha ya Waafrika Kusini, jambo ambalo wanasema serikali ya African National Congress (ANC) inashindwa kufanya.

Wanasema hawafungwi na chama chochote cha siasa.

Je, majibu yamekuwa nini?

Kutoka kwa wageni kuna hisia kwamba wanalaumiwa kwa matatizo makubwa zaidi.

"Hatuchukui kazi ya mtu yeyote, tunaunda fursa zetu wenyewe, hatuzuii Waafrika Kusini kufanya vivyo hivyo," Sam Manane, raia wa Msumbiji ambaye amekuwa akiuza vitafunwa huko Alexandra kwa miaka 10 iliyopita, aliiambia BBC.

"Tunalengwa tu."

Wafanyabiashara wakifunga duka

Chanzo cha picha, AFP

Serikali ya kitaifa bado haijajibu lakini Waziri Mkuu wa jimbo la Gauteng, linalojumuisha Johannesburg, David Makhura wa ANC, amesema ana wasiwasi kuhusu ghasia za hivi majuzi dhidi ya raia wa kigeni huko Alexandra. Ametoa wito kwa mashirika ya kiraia kushirikiana na serikali katika kuendeleza amani na uvumilivu.

Lakini baadhi ya vyama vya upinzani vinajaribu kutafuta mtaji wa kisiasa kutokana na suala hilo.

Moja ambayo inachukua mtazamo mkali ni Muungano mpya wa Patriotic Alliance (PA) unaoongozwa na mfungwa wa zamani Gayton McKenzie. PA, ambao una baadhi ya viti vya udiwani lakini bado haujashiriki katika kura ya kitaifa, inataka wahamiaji wote wasio na vibali kuondoka nchini.

Mapema mwaka huu, wanachama wa chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters bila kutarajia walitembelea migahawa mjini Johannesburg "kukagua" uwiano wa wafanyakazi wa kigeni walioajiriwa na kuweka shinikizo kwa wafanyabiashara kuajiri Waafrika Kusini zaidi.

Kuhusu suala la kuangalia hadhi ya watu, serikali imesema kuwa inafanya juhudi zaidi kuhakikisha watu wanakuwa na nyaraka sahihi - lakini hiyo itachukua muda.

Kwa nini yanatokea sasa?

Hii si mara ya kwanza kumekuwa na ongezeko la chuki dhidi ya wageni nchini Afrika Kusini.

Mwaka 2008, kulikuwa na wimbi la mashambulizi nchini kote dhidi ya wakimbizi na wahamiaji - zaidi ya watu 60 waliripotiwa kuuawa na maelfu kuyahama makazi yao.

Kulikuwa na milipuko zaidi ya ghasia dhidi ya watu wasiokuwa Waafrika Kusini mwaka 2015, hasa katika miji ya Durban na Johannesburg, ambayo ilisababisha kutumwa kwa jeshi kuzuia machafuko zaidi.

Na miaka mitatu iliyopita ongezeko jingine la mashambulizi dhidi ya wageni lilisababisha mamia ya Wanigeria kuondoka nchini humo.

Haijabainika ni kwa nini hasa suala hilo linakuja tena lakini matatizo mengi ya kiuchumi ya Afrika Kusini yamezidishwa na athari za hatua za kukabiliana na Covid-19 ambazo zilisababisha kupotea kwa kazi nyingi na kuongezeka kwa gharama ya maisha.