Hofu na chuki nchini Afrika Kusini ambako wageni wanaishi katika hatari

Chanzo cha picha, BBC/Shiraaz Mohamed
Waafrika wengi wanaokimbia ghasia na umaskini huja Afrika Kusini kutafuta maisha bora. Lakini mara nyingi wanajikuta katika hatari katika makazi yao mapya, wakishutumiwa kwa kuchukua kazi kutoka kwa Waafrika Kusini.
Mpiga picha Shiraaz Mohamed alikutana na baadhi ya watu wanaoishi katika kitongoji cha Alexandra cha Johannesburg na Hillbrow, kitongoji cha ndani ya jiji, kuhusu jinsi ilivyo kukabiliana na chuki dhidi ya wageni na uhalifu kila siku.

Chanzo cha picha, BBC/Shiraaz Mohamed
Mmiliki wa maduka ya jumla Getachew Desta (juu) alitoroka Ethiopia mwaka wa 2010 baada ya kushukiwa kuunga mkono chama cha upinzani na sasa anaishi nyuma ya ngome ya chuma na milango ya kuzuia wizi huko Alexandra.
Anasema anayapata maisha bora hapa, lakini analalamika kuhusu uhalifu.
"Niko sawa kufungiwa nyuma ya ngome kwani hatujui wahalifu wakuja lini. Wakati wowote wanaweza kukutokea, kukuelekezea bunduki na kukuibia pesa zako. Pia wanaweza kukuua."

Chanzo cha picha, BBC/Shiraaz Mohamed
Alikuwa mwathirika wa mashambulizi ya chuki dhidi ya wageni mwaka wa 2016, wakati umati ulipovamia duka lake na kuachwa bila chochote.
Na tena mwezi Julai mwaka huu katika machafuko yaliyozuka baada ya kufungwa kwa aliyekuwa Rais Jacob Zuma kwa kukaidi mahakama. Ghasia hizo zilikumba majimbo mawili na kuua takriban watu 340, huku uharibifu ukizidi 50bn randi ($3.2bn, £2.4bn).
"Ilitokea usiku sikuwepo, nilipiga simu polisi kuwatahadharisha lakini hawakufanya lolote, nilipoteza kila kitu na kulazimika kukopa pesa kwa familia ili nianze upya lakini hazikutosha nikaishia kununua vifaa vyangu kwa mikopo."

Chanzo cha picha, BBC/Shiraaz Mohamed
Pia ametekwa nyara mara mbili - mnamo 2016 na 2019 - hadi fidia ya zaidi ya $ 3,000 ililipwa kwa kila tukio
Mwenye duka huyo bado anapendelea maisha ya hapa kuliko kurejea Ethiopia, lakini amezidi kukata tamaa kuhusu polisi kwani kesi za uhalifu hazifuatiliwi. "Polisi hawawezi kufanya lolote kwa wageni hapa. Ni kana kwamba hawatujali

Chanzo cha picha, BBC/Shiraaz Mohamed
Mmiliki mwenzake wa duka kuu ambaye pia anatoka Mulugeta Negash (juu), ambaye amekuwa Alexandra kwa miaka 13, anasema hatari ni kubwa sana anaweza kufikiria kurudi nyumbani.
"Hatuwezi kupata hati za utambulisho. Matokeo yake hatuwezi kufungua akaunti za benki na kulazimika kubeba pesa taslimu kununua bidhaa za kuuza . Wezi wanafahamu hili, jambo ambalo linatuweka hatarini," kijana huyo mwenye umri wa miaka 34 anasema.
Pia alikuwa mwathirika wa mashambulizi dhidi ya wageni baada ya kupigwa na kundi la watu na kupoteza mali yake yote muda mfupi baada ya kuwasili kwa mara ya kwanza.
"Ninaishi kwa hofu kila siku," anasema

Chanzo cha picha, BBC/Shiraaz Mohamed
Mwanamume mwenye umri wa miaka 43 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (hapo juu) anayeishi Hillbrow anasema anahisi mwenye bahati kuwa hai: "Rafiki yangu alishambuliwa asubuhi moja [katika ghasia za chuki dhidi ya wageni mwaka wa 2008].
"Alipigwa mawe hadi kufa kama mbwa.
"Fikiria mtu anakimbia kutoka katika ardhi yake na kuja hapa kupata amani lakini anaishia kuuawa."
Akiomba asitajwe jina ili kulinda utambulisho wake, alieleza jinsi alivyosafirishwa hadi Afrika Kusini kwa lori miaka 20 iliyopita wakati wamishonari wa Kikatoliki walipomsaidia kutoroka jela baada ya kupata matatizo kwa kumkosoa rais wa Congo wakati huo.
Ilikuwa vigumu kwake kupata kazi mwanzoni kwani hakuweza kuzungumza Kiingereza, lakini baada ya kupewa hadhi ya ukimbizi mwaka 2008 aliweza kupata mafunzo ya afisa usalama - na sasa ameoa na ana familia na raia mwenzake wa Congo.
Licha ya hofu yake anasema anashukuru kwamba ana uwezo wa kulisha familia yake - masikitiko yake ni kwamba ameshindwa kuwasiliana na wazazi wake na hajui kama wako hai.

Chanzo cha picha, BBC/Shiraaz Mohamed
Raia wa Msumbiji Nelfalda Dule (juu) pia anajivunia kwamba anaweza kujikimu yeye na familia yake nchini Afrika Kusini. Anaendesha saluni ya nywele kando ya lami kwenye barabara yenye shughuli nyingi huko Alexandra.
Lakini hii pia inamweka katika hatari katika kitongoji ambacho ujambazi ni jambo la kila siku. Anaishi ndani ya jamii kubwa ya Msumbiji na wana tabia ya kushikamana kwa sababu za usalama.

Chanzo cha picha, BBC/Shiraaz Mohamed
Bi Dule anasema jambo la kuumiza zaidi ni matusi ambayo Waafrika Kusini mara nyingi humtupia, wakitumia neno "kwerekwere", neno la dharau kwa wahamiaji wa Kiafrika.
"Hili ni jambo ambalo linanifanya kuwa na huzuni," anasema.

Chanzo cha picha, BBC/Shiraaz Mohamed
Msumbiji mwenzake Mateu Madjila, ambaye ameishi Alexandra kwa muongo mmoja uliopita akiendesha biashara ya ushonaji , anasema pia huitwa "kwerekwere", licha ya kumuoa mwanamke wa Afrika Kusini ambaye ana watoto watatu.
"Watu wote wanaoishi Afrika Kusini wanawadharau watu kutoka Msumbiji, Zimbabwe au nchi nyingine yoyote - maisha si rahisi," anasema.

Chanzo cha picha, BBC/Shiraaz Mohamed
Kwa Philimon Gwetekwete mwenye umri wa miaka 41, ambaye alikuja Alexandra kutoka Zimbabwe mwaka 2016, fursa za Afrika Kusini ndizo muhimu.
Anazikarabati televisheni pamoja na vifaa vya elektroniki - kazi aliyojifunza nyumbani.
"Ilikuwa ngumu huko Zim, sikuwa na kazi na nina watoto sita. Maisha ni bora hapa lakini natatizika kwa sababu hakuna kazi nyingi za ukarabati. Napata pesa lakini haitoshi kwa sababu lockdown iliharibu mambo. ."
Wazimbabwe wengine wanaonekana kutojali kuhusu hali yao, wakikubali kwamba maisha ni magumu lakini bora kuliko nyumbani.

Chanzo cha picha, BBC/Shiraaz Mohamed
Mfanyakazi wa nyumbani mwenye umri wa miaka 40 (hapo juu), ambaye alihamia Afrika Kusini kutoka Zimbabwe na familia yake akiwa kijana, anasema dawa za kulevya ndiyo zinazomsumbua zaidi.
Akiomba jina lake lisitajwe, mama huyo wa watoto watatu alisema kuwa Hillbrow ilikuwa maarufu kwa magenge yake ya dawa za kulevya yanayoaminika kuhusisha wageni: "Maisha ni magumu sana hapa. Tunaishi chini ya wauzaji wa dawa za kulevya. Ninaogopa kwamba watoto wangu wanaweza kuingizwa. "

Chanzo cha picha, BBC/Shiraaz Mohamed
Mzimbabwe mwenye umri wa miaka 51 Jafter Ndlovu pia amekuwa nchini Afrika Kusinikwa muda mrefu ,alifika miaka 30 iliyopita kutafuta kazi na kuanza kuwa mhudumu.
Alihifadhi pesa za kutosha kununua gari la mitumba ili kuanzisha biashara ya teksi inayofanya kazi karibu na Hillbrow.
Kero yake kuu ni kwamba kampuni yake ya teksi imeathiriwa pakubwa na kampuni maarufu ya teksi ya Uber.

Chanzo cha picha, BBC/Shiraaz Mohamed
Helder Massinge, raia wa Msumbiji mwenye umri wa miaka 27, amekuwa nchini Afrika Kusini kwa miaka 10. Anatatizika kupata riziki kwa kuuza mboga huko Hillbrow - inamgharimu $30 kwa siku kununua mazao ambayo yanaweza kuharibika.
Pia yuko chini ya tishio la mara kwa mara kutoka kwa polisi, kwani maafisa wanaweza kumpokonya bidhaa zake kwa vile haruhusiwi kuuza kutoka kwa lami.

Chanzo cha picha, BBC/Shiraaz Mohamed
"Unapokuwa mgeni huna kitambulisho hivyo huwezi kupata kazi nzuri. Lakini ninaendelea kujaribu kwa sababu sitaki kujihusisha na uhalifu."
Kama wahamiaji wengi, anasema ni suala la kuishi kwani anahitaji kupata pesa kwa ajili ya mama yake na bintiye ambao wamesalia nchini Msumbiji.
Picha zote chini ya hakimiliki














