Kwanini Trump anakoleza vita vya kibiashara na China?

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, John Sudworth
- Nafasi, Senior North America correspondent
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Ghafla, vita vya kibiashara vya Donald Trump viko katika mwelekeo mwingine. Amehamisha vita vyake dhidi ya ulimwengu, na sasa inaonekana vita vyake zaidi ni dhidi ya China.
Trump amesitisha kwa siku 90 ushuru wa juu kwa nchi kadhaa na kuacha ushuru wa jumla wa 10%.
Lakini China - ambayo husafirisha kila kitu kwenda Marekani, kuanzia iPhone hadi vifaa vya kuchezea vya watoto na husafirisha karibu 14% ya bidhaa zote za Marekani kutoka nje - imetengwa na kuwekewa ushuru wa kiwango kikubwa zaidi wa 125%.
Trump amesema ongezeko hilo linatokana na Beijing kulipiza kisasi kwa ushuru wake wa 84% kwa bidhaa za Marekani, hatua ambayo rais huyo alieleza inaonyesha "kutokuwa na heshima."
Lakini kwa mwanasiasa ambaye aliingia Ikulu ya White House nyuma ya kauli za kupinga China, kuna mengi zaidi kuliko kulipiza kisasi.
Uhasama wa Trump kwa China
Kwa Trump, hili linahusu mambo aliyoyaacha kiporo katika muhula wa kwanza madarakani.
"Hatukuwa na muda wa kufanya jambo sahihi, na sasa tunafanya," aliwaambia waandishi wa habari.
Lengo lake ni kupindua mfumo wa biashara ya kimataifa ambapo China ni kama kiwanda cha ulimwengu, na mtazamo wa wengi kuwa biashara na China ni jambo zuri.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ili kuelewa jambo hili katika fikra za rais wa Marekani, ni lazima urudi wakati ambao Trump hata hakufikiriwa kuwa mgombea, achilia mbali kuwa rais.
Mwaka 2012, niliripoti kwa mara ya kwanza kutoka Shanghai - mji mkuu wa biashara wa China – kuongezeka kwa biashara ya nchi kulionekana na karibu kila mtu – wafanya biashara wa kimataifa, maafisa wa China, maafisa wa kigeni, waandishi wa habari wa kigeni na wanauchumi wenye ujuzi - kama ni jambo rahisi.
Ilikuwa ikikuza uchumi wa kimataifa, ikisambaza bidhaa za bei nafuu, kuimarisha viwanda katika minyororo ya usambazaji wa kimataifa, na kutoa fursa kwa mashirika ya kimataifa.
Ndani ya miaka michache ya kuwasili kwangu, China iliipita Marekani na kuwa soko kubwa zaidi duniani la Rolls Royce, General Motors na Volkswagen.
Sera yake iliyochapishwa mwaka 2015, yenye kichwa Made in China 2025 - iliweka maono makubwa ya kuwa kiongozi wa kimataifa katika sekta kadhaa muhimu za utengenezaji; anga hadi ujenzi wa meli na magari ya umeme.
Na hivyo ndivyo ilivyokuwa mwaka mmoja tu baadaye, na hapo ndipo Trump akaibuka akiwa nje ya siasa, na kuanza kusema mara kwa mara kwamba kupanda kwa China kumeharibu uchumi wa Marekani, kumesababisha kudorora kwa viwanda na kuwagharimu wafanyakazi wa Marekani riziki zao na utu wao.
Vita vya kibiashara vya Trump vya muhula wa kwanza vilivunja ukungu na kuvunja makubaliano. Mrithi wake, Rais Joe Biden, aliweka kiasi kikubwa cha ushuru kwa China.
Ingawa wameisababishia China maumivu, lakini hawajafanikiwa kubadilisha mtindo wa uchumi.
China sasa inazalisha 60% ya magari yanayotumia umeme duniani - sehemu kubwa ya magari hayo yanatengenezwa na kampuni za nyumbani – na hutengeneza 80% ya betri zinazoyaendesha.
Kwa hivyo, sasa Trump amerejea, na ongezeko hili la nipe nikupe kwenye ushuru.
Kipi kifuatacho?
Kitakachotokea baadaye kinategemea mambo mawili muhimu. Kwanza, ikiwa China iko tayari kufanya mazungumzo.
Na pili, ikiwa itakubali kufanya mazungumzo. Je, iko tayari kufanya makubaliano makubwa ambayo Marekani inayataka, ikiwa ni pamoja na marekebisho ya mtindo wake wa kiuchumi unaoendeshwa na mauzo ya nje.
Kuyajibu haya, jambo la kwanza ni kuelewa kuwa tuko katika eneo ambalo halijashughulikiwa kabisa, kwa hivyo tunapaswa kuwa waangalifu na mtu yeyote anayesema anajua jinsi Beijing itakavyo fanya.
Mtazamo wa China juu ya nguvu zake za kiuchumi – moja ni mauzo ya nje na na pili, ni soko la ndani linalolindwa sana.
Kuna swali la tatu, na hili Wamarekani ndio wanapaswa kulijibu.
Je, Marekani bado inaamini katika biashara huria? Donald Trump mara nyingi husema ushuru ni jambo zuri, sio tu kama njia ya kufikia malengo, lakini nalo ni lengo lenyewe.
Anazungumza juu ya umuhimu wa kuilinda Marekani, ili kuchochea uwekezaji wa ndani, kuhimiza kampuni za Marekani kurudisha minyororo hiyo ya ugavi nyumbani, na kuongeza mapato.
Na ikiwa Beijing inaamini hilo ndilo dhumuni la msingi la ushuru huo, inaweza kuamua kuwa hakuna cha kujadili.
Badala ya kutetea wazo la ushirikiano wa kiuchumi, mataifa haya makubwa mawili duniani yanaweza kujikuta katika mapambano ya kushinda ukuu wote wa kiuchumi.
Ikiwa ndivyo hivyo, hilo litasambaratisha maelewano ya zamani, na kuleta mustakabali mbaya sana.
Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi












