Uchaguzi Kenya 2022:Siku moja kabla ya uchaguzi fahamu kinachofanyika Kenya ikiwemo matayarisho ya IEBC

th

Siku moja kabla ya Wapiga kura Zaidi ya milioni 20 kuwachagua viongozi wao katika uchaguzi mkuu unaofanyika kesho Jumanne,shughuli za matayarisho ya uchaguzi huo zimenoga kote nchini .

Tume Huru ya Uchaguzi na mipaka IEBC imekuwa ikiendelea kusafirisha vifaa vya kupigia kura katika vituo vya kupigia kura kabla ya zoezi hilo linalotarajiwa kuanza saa kumi na mbili alfajiri hadi saa kumi na moja jioni .

Usafiri

th

Chanzo cha picha, AFP

Kampuni za usafiri nchini Kenya zimeshuhudia ongezeko idadi ya Wakenya wanaokata tiketi dakika za mwisho ili kabla ya uchaguzi mkuu wa kihistoria wa Jumanne.

Tathmini ya BBC Magharibi mwa Kenya ilipata mamia ya abiria wakijaribu kurudi nyumbani kwenye vituo vyao vya kupigia kura walikosajiliwa . Katika baadhi ya maeneo, nauli za mabasi zimekaribia kuongezeka maradufu kutokana na mahitaji ya watu wengi kutaka kusafiri .

Eneo la magharibi ni nyumbani kwa jamii ya pili kwa idadi nchini Kenya na inaonekana kama eneo lenye umuhimu mkubwa kuamua mshindi wa kura ya urais. Ina jumla ya wapiga kura milioni 2.6 waliosambaa katika kaunti tano.

"Hapa Bungoma sote tuko sawa. Tumeona wasafiri wengi wakipitia hapa wakielekea katika mji wa Busia [mpakani na Uganda] ambako walijiandikisha kama wapiga kura," alisema wakala wa usafiri Kennedy Ajimbi.

Katika mji wa Eldoret, wapiga kura pia wamekuwa wakithibitisha ikiwa wako kwenye sajili ya mwisho ya uchaguzi.

Eldoret , katika eneo la Bonde la Ufa nchini Kenya inaonekana kama ngome ya Naibu Rais William Ruto ambaye Jumanne atapiga kura katika mji aliozaliwa wa Sugoi.

"Ndiyo, tutakuwa na mchakato huru wa haki na uwazi na wa kuaminika, msimamizi wa uchaguzi wa eneo hilo Irene Mutahi alisema

Mkanganyiko wa dakika za mwisho mwisho

th

Katika harakati za kusambaza vifaa vya kura katika maeneo mbali mbali ya nchi pia kumetokea visa vya mkanganyiko huku Karatasi za Kura za kaunti ya Garissa kaskazini mashariki mwa Kenya zikipatikana katika eneo la Chuka kati kati mwa nchi hiyo huku za Kilifi zikipatikana katika kaunti jirani ya Mombasa katika eneo la Pwani.

Afisa wa uchaguzi kaunti ya Kakamega Joseph Ayatta amethibitisha kuwa karatasi za kupigia kura kaunti ya Kirinyaga ,Kati mwa Kenya zimepatikana katika kaunti ndogo ya Mumias Mashariki,magharibi mwa nchi

'Kitambulisho changu kiko wapi?'

th
Maelezo ya picha, Kitambulisho ni lazima iwapo mpiga kura ataruhusiwa kupiga kura endapo alikitumia kama stakabadhi ya kujitambua

Ili kupiga kura Kenya lazima mpiga kura awe na stakabadhi ya kujitambulisha kama vile kitambulisho ama paspoti.

Ni kwa ajili ya hilo ambapo leo foleni ndefu zimeonekana katika vituo vya Huduma jijini Nairobi huku Wakenya waliokuwa wametuma maombi ya kupata kadi za vitambulisho walienda kuzichukua saa chache tu kabla ya kupiga kura.

Mkurugenzi katika Kituo cha Huduma cha Kibera anasema "Nilikuja asubuhi hii na nikashtuka, watu hawa wote wamekuwa wapi?"

th
Maelezo ya picha, Foleni ya watu wakitaka kuchukua vitambulisho vyao kabla ya upigaji kura kesho Jumanne

Usalama Rift Valley

th

Usalama umeimarishwa katika eneo la Bonde la Ufa nchini Kenya kabla ya uchaguzi. Maandamano yamepigwa marufuku wakati wa upigaji kura katika eneo hilo na Wakenya wametakiwa kupiga kura na kurudi nyumbani au kurejea kwenye biashara zao. Eneo la bonde la ufa linatambulika kama mojawapo ya maeneo yenye hatari ya kuathiriwa na machafuko ya uchaguzi.

Akizungumza na BBC, Mkuu wa eneo la Bonde la Ufa Mohamed Maalim ameonya yeyote anayenuia kuvuruga uchaguzi huo atakabiliwa na nguvu kamili ya sheria. Hakutakuwa na maandamano na watu kutembeatembea katika vituo vya kupigia kura. Anasema kuwa polisi wamejipanga vya kutosha kuweka ulinzi katika vituo zaidi ya 12300 vya kupigia kura katika eneo hilo zima wakitoa askari polisi wasiopungua 2 katika kila kituo.

Juu ya taarifa za vijikaratasi vya chuki vinavyosambazwa katika maeneo ya eneo hilo watu 9 wamekamatwa na kufikishwa mahakamani, na kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni 1 za Kenya (kama dola 8,000) au dhamana ya pesa taslimu ya shilingi 500,000 za Kenya (takriban 4000 USD). )

Ujambazi katika Bonde la Kerio umekuwa sababu kuu ya ukosefu wa usalama katika eneo hilo kwa muda, hivyo watu wengi wamepoteza maisha yao na mali kuibiwa.

Eneo la Bonde la ufa ambalo lina kaunti 14 limesalia na idadi kubwa zaidi ya wapiga kura kuwa milioni 5.34.

th

Pia unawezakusoma:

th