Greenland, Bodi ya Amani ya Trump na Ukraine - kinachoendelea

Chanzo cha picha, EPA
Alhamisi ilikuwa siku nzito ya diplomasia huko Davos, Uswisi, ambako viongozi wa dunia wamekuwa wakikutana wiki hii kwa ajili ya Jukwaa la Kiuchumi la Dunia (World Economic Forum) la kila mwaka.
Hapa kuna muhtasari wa mambo makuu ya jana:
Greenland
Kulikuwa na hali ya nafuu barani Ulaya kufuatia matamshi ya Trump aliyotoa usiku uliotangulia, ambapo alionekana kuachana na msimamo wake kwamba Marekani lazima ipate umiliki wa Greenland. Alitangaza kuwa kulikuwa na “mfumo wa makubaliano ya baadaye” na Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte.
Hata hivyo, tangu Jumatano, maelezo machache sana yameibuka kuhusu mfumo huo unahusisha nini hasa. Mwenyekiti wa Kamati ya Kijeshi ya NATO, Admirali Giuseppe Cavo Dragone, alisema makubaliano hayo yako katika “hatua ya awali kabisa”, akiongeza kuwa “bado tunasubiri mwelekeo.”
Katika mahojiano na Fox Business, Trump alisema makubaliano hayo yataruhusu “ufikiaji ulio kamili,” na kwamba “tunapata kila kitu tunachotaka bila gharama.”
Bodi ya Amani
Trump alizindua rasmi Bodi yake mpya ya Amani katika hafla ya kutia saini pamoja na viongozi wa kimataifa.
Awali, bodi hiyo ilibuniwa kama njia ya kutekeleza sehemu ya mpango wa kusitisha mapigano huko Gaza. Lakini Trump na maafisa wake walisema sasa itashughulikia masuala mbalimbali ya kimataifa, huku rais wa Marekani akisema ina uwezo wa kuwa “moja ya taasisi zenye athari kubwa zaidi kuwahi kuanzishwa.”
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Yvette Cooper, alisema Uingereza haitajiunga kwa sasa, kutokana na wasiwasi kuhusu ushiriki wa Rais wa Urusi, Vladimir Putin. Hakuna hata mmoja wa wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, China, Ufaransa au Urusi, ambaye ameahidi kushiriki hadi sasa.
Ukraine
Baadaye, rais wa Marekani alikutana na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky. Baada ya mkutano huo, Zelensky aliwaambia waandishi wa habari kuwa wamekubaliana kwamba hati kuhusu dhamana za usalama ilikuwa “tayari”, lakini bado inahitaji kutiwa saini na kupelekwa kwa mabunge ya kitaifa.
Katika hotuba kali kwa wajumbe wa Davos, Zelensky alisema Ulaya mara nyingi huepuka “kuchukua hatua”, na akaitaka kufanya zaidi ili “kujilinda yenyewe.”
Unaweza kusoma;





