Je, yalikuwa mapinduzi ya 'uongo'? Kilicho nyuma ya uvamizi wa kijeshi Guinea-Bissau

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Mapinduzi ya kijeshi si jambo jipya nchini Guinea-Bissau. Taifa hilo la Afrika Magharibi limewahi kupitia majaribio au mafanikio yasiyopungua tisa ya mapinduzi tangu lipate uhuru kutoka Ureno mwaka 1974.
Lakini pale maafisa wa jeshi walipotangaza kuwa walikuwa wametwaa mamlaka ya nchi Jumatano iliyopita, baadhi ya wachambuzi na wanasiasa walionesha shaka.
Dalili zote za kawaida za mapinduzi zilikuwepo: milio ya risasi ilisikika karibu na ikulu ya rais, Rais Umaro Sissoco Embaló alikamatwa, na wanajeshi wakatoa taarifa kupitia televisheni ya taifa.
Hata hivyo, mazingira mengine ya tukio hilo yameibua maswali, huku Waziri Mkuu wa Senegal Ousmane Sonko na Rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan wakiungana na wengine wanaoamini kuwa kutwaa madaraka huko kulipangwa na Embaló mwenyewe.
Zaidi ya hapo, mambo yalizidi kuwa tata wakati jeshi lilipoambia BBC kwamba limetwaa mamlaka ya nchi, lakini likalaani matumizi ya neno "mapinduzi".
Viongozi wa junta walisema walikuwa wakichukua hatua kuzuia njama ya wanasiasa ambao hawakutajwa majina, waliokuwa na "msaada wa mfanyabiashara maarufu wa dawa za kulevya", ya kutaka kuisumbua nchi ambayo kwa muda mrefu imejulikana kama kitovu cha biashara ya dawa za kulevya.
Nini kilitokea katika kipindi kilichosababisha mapinduzi hayo?
Siku tatu tu kabla ya jeshi kutwaa mamlaka, wananchi wa Guinea-Bissau walikuwa wamepiga kura katika uchaguzi wa rais. Embaló, mwenye umri wa miaka 53, alikuwa akigombea muhula wa pili, na mpinzani wake aliyemkaribia zaidi alikuwa Fernando Dias da Costa.
Dias alikuwa akiungwa mkono na Waziri Mkuu wa zamani Domingos Pereira, ambaye awali alitarajiwa kugombea urais kwa niaba ya chama kikuu cha upinzani, PAIGC. Hata hivyo, Pereira alizuiwa kushiriki katika kinyang'anyiro hicho baada ya mamlaka kusema kuwa aliwasilisha nyaraka zake kwa kuchelewa.
Matokeo ya uchaguzi yalipaswa kutangazwa siku ya Alhamisi, siku moja baada ya mapinduzi kutokea.
Nini kilitokea siku ya mapinduzi?
Baada ya milio ya risasi kusikika katika mji mkuu, Bissau, Embaló aliliambia gazeti la Ufaransa Jeune Afrique kwamba alikamatwa na wanaume waliokuwa katika sare katika ikulu ya rais.
Baada ya hapo, maafisa wa jeshi walionekana kwenye televisheni ya taifa, wakitangaza kuwa walimuondoa rais madarakani ili kuzuia njama ya kuharibu utulivu wa nchi. Jeshi lilisitisha mchakato wa uchaguzi na kuzuia kutangazwa kwa matokeo ya kura.
Kupitia mazungumzo mafupi, Embaló aliwaambia wa France 24: "Nimeondolewa madarakani."
Wengine pia walikamatwa, wakiwemo Pereira, Waziri wa Mambo ya Ndani Botché Candé, na mkuu wa jeshi Jen. Biague Na N'tan.
Makao makuu ya tume ya uchaguzi yalishambuliwa na kiongozi mmoja amefichua kuwa wanaume wenye silaha waliovaa balaclava waliharibu karatasi na seva kuu ya kompyuta iliyohifadhi matokeo, ikimaanisha kuwa matokeo ya uchaguzi hayawezi kutangazwa.
Kwa nini kuna shaka kuhusu mapinduzi hayo?
Upinzani, mashirika ya kiraia na wanasiasa kutoka nchi jirani za Afrika Magharibi wameonesha shaka kuhusu tangazo la jeshi.
Embaló aliruka kwenda Senegal jirani kwa ndege ya kijeshi ya Senegal baada ya kuachiliwa huru Alhamisi, jambo ambalo afisa wa PAIGC, Flávio Baticã Ferreira, analiona kuwa na shaka.
"Jinsi alivyotoka Guinea-Bissau, akifuatwa kama mtalii pamoja na familia yake na mizigo, bila kizuizi au upinzani wowote… yote haya yanaonesha kuwa si mapinduzi, kwa sababu sote tunajua jinsi mapinduzi yanavyofanya kazi," alisema Ferreira, ambaye awali alikuwa mbunge, aliiambia BBC.
Katika mlolongo wa mapinduzi yaliyojiri Afrika katika miaka mitano iliyopita, hakuna viongozi waliyoondolewa madarakani walioruhusiwa kuondoka nchini haraka kama Embaló alivyofanya.
Hata hivyo, wachambuzi wawili waliiambia BBC kuwa jeshi la Guinea-Bissau linaweza kuwa kumruhusu Embaló kuondoka haraka lingefanya mchakato wa mpito kuwa laini.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Goodluck Jonathan, rais wa zamani wa Nigeria, pia alionesha shaka kuhusu mapinduzi hayo, akisema kuwa kiongozi wa taifa kawaida haruhusiwi kuzungumza na vyombo vya habari vya kigeni kwa simu wakati wa mapinduzi ya kijeshi.
"Kile kilichotokea Guinea-Bissau si mapinduzi... kwa kutokupata neno bora, ningesema ilikuwa mapinduzi ya tamasha," alisema rais huyo wa zamani, ambaye alikuwa sehemu ya timu iliyoangalia uchaguzi nchini Guinea-Bissau, kwa waandishi wa habari.
Jonathan yuko sahihi, viongozi walioondolewa madarakani kawaida hawajulikani kuwasiliana na ulimwengu wa nje wakati wako kizuizini. Lakini kuna matukio tofauti, rais wa zamani wa Gabon alirekodi video akiwahimiza "marafiki zake kote duniani" kwa msaada baada ya kuondolewa madarakani mwaka 2023.
Uteuzi wa Jen. Horta N'Tam kuwa kiongozi mpya wa kijeshi wa Guinea-Bissau pia umeibua shaka, kwani jenerali huyo alionekana kuwa mshirika wa karibu wa Embaló.
Embaló hajajibu madai kwamba yeye ndiye aliyetengeneza mapinduzi hayo.
Kwa nini mtu huigiza mapinduzi?
Wakosoaji kwa muda mrefu wamekanusha kuwa Embaló ameigiza jaribio la mapinduzi ili kuwapiga marufuku wapinzani wake, madai ambayo kiongozi huyo wa zamani anayakanusha.
Alisema kuwa amekwepa mapinduzi matatu kwa jumla. Mnamo Desemba 2023, baada ya moja ya njama za mapinduzi, Embaló alivunja bunge lililoongozwa na upinzani. Tangu wakati huo, Guinea-Bissau haijakuwa na bunge.
Baadhi ya mashirika ya kiraia yamekanusha Embaló kuandaa mapinduzi ya wiki iliyopita ili kuzuia matokeo yoyote mabaya ya uchaguzi kutangazwa.
Mchambuzi wa siasa, Ryan Cummings, alisema matendo ya rais hapo awali, kama vile kuchelewesha uchaguzi kwa mwaka mmoja, yamezidisha mashaka kama haya.
Pia inawezekana sana kuwa vikosi vya silaha vilichukua hatua kwa uhuru ili kuzuia msukosuko wa kisiasa, kwani Embaló na Dias wote walidai walishinda uchaguzi huu, Bw. Cummings aliiambia BBC.
Beverly Ochieng, mchambuzi wa Afrika Magharibi katika kampuni ya ujasusi Control Risks, pia alikubaliana na mashaka yanayoelezwa kuhusu mapinduzi hayo.
Hata hivyo, alisema kuwa mvutano miongoni mwa wanasiasa wakuu, pamoja na uamuzi wa kumzuia Pereira kushiriki uchaguzi wa urais, "huenda umechangia kuingilia kati kwa jeshi".
Nani anaiongoza Guinea-Bissau sasa?

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Jenerali N'Tam, ambaye zamani alikuwa mkuu wa majeshi, ameapishwa kuwa rais na anatarajiwa kubaki madarakani kwa kipindi cha mpito cha mwaka mmoja.
Jenerali huyo ameteua baraza jipya la mawaziri, likiwa na mawaziri 23 wa serikali.
Kwa upande mwingine, Embaló ameondoka Senegal kuelekea Congo-Brazzaville.
Kulingana na vyanzo vya habari nchini Senegal na Guinea-Bissau, aliondoka huku akikasirika kwamba waziri mkuu wa Senegal alikuwa ameyaita mapinduzi hayo "uongo".
Dias, ambaye alisema alikwepa kukamatwa siku ya mapinduzi, amepewa hifadhi ya ukimbizi na Nigeria.
Rais wa Guinea Bissau wanasema nini?
Siku ya Jumamosi, mamia ya waandamanaji waliandamana mitaani, wakidai Pereira aachiliwe huru. Pia walitaka mamlaka kuchapisha matokeo ya uchaguzi.
Zaidi ya hayo, vikundi vitatu vya asasi za kiraia vimeitisha mgomo mkuu na kampeni ya kutotii sheria za kiraia ili kurejesha "ukweli wa uchaguzi".
Lakini hisia ziko za mchanganyiko, huku baadhi ya wakazi wakisifu jeshi na kutumaini mabadiliko ya utaratibu.
"Sipingi utawala wa kijeshi mradi tu wanaboresha hali ya maisha nchini," Suncar Gassama aliiambia BBC.
Mbunge wa zamani Ferreira alielezea hali ya nchini kama "ya wasiwasi".
"Hakuna anayejua mustakabali wa Guinea-Bissau," alisema.












