Kinyang'anyiro cha kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa Kenya unaotarajiwa Agosti 9, mwaka huu, kilivutia takriban wawaniaji hamsini.
Lakini ilipowadia muda wa wagombea hao kuwasilisha maombi yao kwa Tume huru ya uchaguzi IEBC ili kuona iwapo wametimiza yote yalioanishwa kuchambua nani ni Mtia nia na nani anastahili kuwa mgombea urais, orodha hiyo ndefu ilisalia na majina manne tu!
Nao ni mgombea wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga, anayewania urais kwa mara ya tano tangu kuanzishwa kwa mfumo wa siasa za vyama vingi nchini Kenya., naibu rais William Ruto anayewania kupitia tiketi ya chama cha UDA.
Wengine ni George Wajackoyah ,aliyezua mjadala katika mitandao ya kijamii kutokana na azma yake ya kutaka bangi ihalalishwe na mwisho David Mwaure wa chama cha Agano .
Wafahamu viongozi hao kwa ufupi.
Je Raila Odinga ni nani?
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Raila Odinga
Bwana Odinga anaonekana kuwa mrithi wa kisiasa wa baba yake, Jaramogi Odinga. Alikuwa makamu wa kwanza wa rais wa Kenya baada ya uhuru, lakini aliondoka serikalini mwaka wa 1966 baada ya kutofautiana na kiongozi wa wakati huo, Jomo Kenyatta, baba yake na rais wa sasa, Uhuru Kenyatta.
Jaramogi Odinga aliunga mkono ushirika na uhusiano wa karibu na nchi za Umoja wa Kisovieti na China, huku Jomo Kenyatta akiunga mkono ushirika wa Marekani na mataifa mengine yenye nguvu ya Magharibi.
Tofauti zao zilizidi kuwa mbaya, ambapo Jaramogi Odinga alifungwa kwa miezi 18 hadi alipoachiliwa huru mnamo mwaka 1971. Raila Odinga pia ni mfungwa wa zamani wa kisiasa, na anashikilia rekodi ya kuwa mfungwa wa kisiasa aliyetumikia kifungo cha muda mrefu zaidi nchini Kenya.
Maelezo ya video, Uchaguzi Kenya 2022: Wafahamu wagombea hawa wanne wa uchaguzi
Mapambano yake dhidi ya udikteta wa chama kimoja yalimfanya awekwe kizuizini mara mbili (kutoka 1982 hadi 1988 na 1989 hadi 1991) wakati wa utawala wa mrithi wa Jomo Kenyatta na Daniel Arap Moi.
Hapo awali alifungwa kwa kujaribu kufanya mapinduzi mwaka wa 1982.
Mpinzani wake wa karibu ni William Ruto, wa Chama cha United Democratic Alliance UDA Naibu wa sasa wa Rais anayejinadi kwa misingi ya kutetea maslahi ya wananchi wa tabaka la chini waliobandikwa jina 'Hustler'.
Nani yuko kwenye kinyang'anyiro cha kuiongoza Kenya ?
Fahamu zaidi kuwahusu wagombea urais wa Kenya
Chagua mgombea ili kutazama wasifu wake
Raila Amollo Odinga
Muungano wa Azimio la Umoja
Mgombea huyo mwenye umri wa miaka 77 ni mhandisi aliyesomea Chuo Kikuu cha Ufundi cha Magdeburg (sasa kinajulikana kama Chuo Kikuu cha Otto-von-Guericke Magdeburg) nchini Ujerumani.
Anawania kiti cha urais kwa tikiti ya Azimio la Umoja One Kenya Coalition Party.
Hili litakuwa jaribio lake la tano baada ya kugombea katika: 1997, 2007, 2013 na 2017.
Bw Odinga alikuwa mmoja wa wapiganiaji wa demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya. Alikamatwa, akafungwa na wakati fulani akaenda uhamishoni kwa sababu ya kupigania haki hiyo
Aliwahi kuwa Waziri Mkuu, kuanzia 2008-2013.
Odinga alihusika kufanikisha miradi mikubwa iliyotekelezwa na serikali ya Kibaki, kama vile miradi ya umeme vijijini na barabara.
Kuafikia ukuaji wa uchumi wa tarakimu mbili kupitia uwekezaji katika biashara ndogo ndogo na sekta ya viwanda.
Utoaji wa huduma bora za afya kwa wote.
Utoaji wa vifaa vya michezo na burudani kwa ukuaji wa kimwili, kiakili, kijamii, kimaadili na maendeleo ya watu.
Kufuatia jaribio la mapinduzi ya Agosti 1, 1982, Raila Odinga alikamatwa na kukabiliwa na mashtaka kadhaa, yakiwemo ya uhaini ambayo alizuiliwa bila kufunguliwa mashtaka. Tume ya Ukweli ya Haki na Maridhiano iliambiwa mwaka 2011 kwamba Odinga alikuwa na mawasiliano na mpangaji mkuu wa mapinduzi hayo. Odinga amekana kuhusika kila mara. - Makavazi ya Kitaifa ya Kenya.
William Samoei Ruto
Muungano wa Kenya Kwanza
Mgombea huyu mwenye umri wa miaka 55 ana Shahada ya Uzamifu/PhD katika Ikolojia ya Mimea na BSc katika Botany na Zoology kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.
Anawania kiti cha urais kwa tikiti ya chama cha United Democratic Alliance ( chenye mafungamano na Kenya Kwanza).
Aliongoza Vuguvugu la vijana la Youth for Kanu '92 (YK'(92).
Wizara yake iliorodheshwa kama inayofanya bora zaidi serikalini alipokuwa Waziri wa Kilimo.
Alihudumu kama Naibu Rais wa kwanza wa Kenya chini ya katiba mpya ya 2010.
Alihudumu kama mbunge wa eneo bunge la Eldoret Kaskazini kuanzia 1997-2007.
Kutenga $424 milioni kila mwaka kwa biashara ndogo ndogo za kati.
Kuanzisha mfuko wa elimu wa kitaifa ili kukidhi gharama zisizo za masomo.
Tekeleza kikamilifu sheria ya usawa wa kijinsia ya thuluthi mbili katika uteuzi wa kisiasa na kutenga nusu ya baraza lake la mawaziri kwa wanawake.
Mnamo 2008, Mahakama Kuu ya Kenya iliamuru Naibu Rais William Ruto kusalimisha shamba la ekari 100 na kulipa $ 62,500 kwa Adrian Muteshi, mkulima ambaye alimshtaki kwa kuchukua mali hiyo baada ya uchaguzi wa 2007. - Kenya Law
Mnamo 2011, Bw Ruto alikabiliwa na kesi kwa makosa matatu dhidi ya binadamu: Mauaji, uhamisho wa watu kwa lazima na mateso ya watu katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu. Miaka mitano baadaye mahakama ilisitisha kesi hiyo kwa msingi kwamba - ushahidi wa upande wa mashtaka ulikuwa dhaifu. -ICC
George Wajackoyah
Chama cha Roots
Profesa huyo mwenye umri wa miaka 61 ana shahada ya uzamili katika sheria kuhusu maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Warwick na shahada ya uzamili , sheria (sheria za Marekani kutoka Chuo Kikuu cha Baltimore.
Bw Wajackoyah anawania kiti cha urais kwa tiketi ya Chama cha Roots Party.
Alihudumu kama Inspekta katika idara ya usalama ya Special branch wakati wa utawala wa marehemu Rais Daniel Moi kabla ya kulazimika kutorokea ng'ambo ili kuepuka kufunguliwa mashtaka na mamlaka.
Yeye ni mshirika katika kampuni ya mawakili aliyoianzisha mwaka wa 2018.
Alifunnza somo la sheria na uchumi katika vyuo vikuu vya Marekani, Uingereza na Kenya.
Kuhalalisha matumizi ya kiviwanda ya bangi
Badilisha siku za kazi hadi Jumatatu hadi Alhamisi.
Huduma ya afya ya bure na msaada kwa wazee, walio hatarini na wajawazito
David Mwaure Waihiga
Chama cha Agano
David Mwaure anawania kiti cha urais kwa tiketi ya Chama cha Agano.
Ni kiongozi wa Chama cha Agano.
Alihitimu na shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi na ana Shahada ya Uzamili katika masomo ya uongozi.
Yeye ni wakili mkuu na amehudumu kama mwanasheria kwa zaidi ya miongo mitatu.
Ana kampuni ya uwakili na amewania viti mbalimbali vya kisiasa.
Ilianzishwa chama cha Agano mwaka 2006.
Kupambana na ufisadi uliokithiri.
kuunda nafasi za ajira.
Kurejesha mali ya Kenya iliyofichwa nje ya nchi.
Pata maelezo zaidi kuhusu sera za wagombea urais hapa
Mfahamu William Ruto
Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, William Ruto
Maisha ya utotoni ya William Ruto ni mfano halisi wa maisha ya watoto wengi masikini Wakenya.
Alikwenda shule miguu peku, ambapo alivaa kwa mara ya kwanza viatu akiwa na umri wa miaka 15. Aliuza kuku na karanga kando ya barabara katika maeneo ya kijijini kwao katika mkoa wa Bonde la ufa (Rift Valley).
kwa hiyo sio jambo la kushangaza kwamba anajielezea kama kiongozi wa masikini wakati anapogombea kiti cha urais katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 9 Agosti.
Bw Ruto anawania kiti hicho chini ya Muungano unaofahamika kama Kenya Kwanza, akitoa ahadi ya kukuza uchumi.
Wagombea hao wawili wakuu wamekuwa wakitawala siasa za Kenya katika nyadhifa mbali mbali kwa miongo kadhaa sasa, wakizoeleka machoni na masikioni mwa Wakenya.
Profesa Wajackoyah ni Nani?
Chanzo cha picha, GL Wajackoyah
Lakini ni kujitosa kwa Profesa George Luchiri Wajackoyah katika kinyanganyiro cha uchaguzi wa rais 2022 ambako kumezua gumzo kweli kweli miongoni mwa Wakenya ambapo limeibua shauku hasa miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii na vijana.
Hamu ya kutaka kumfahamu zaidi imeongezeka baada ya Tume ya uchaguzi kumuidhinisha kuwa mgombea rasmi wa urais katika uchaguzi unaokuja ndani ya miezi miwili.
Mgombea huyu alizaliwa magharibi mwa Kenya eneo la Matungu. Ana umri wa miaka 61. Alilelewa katika mazingira magumu baada ya wazazi wake kuachana akiwa na umri mdogo sana.
Kama wasemavyo Waswahili ukikosa ziwa la mama hata la mbwa huamwa, alipata wahisani waliomshika mkono na angalau kumsaidia kupata elimu, akitolewa mfano aliyekuwa waziri wa elimu marehemu Joseph Kamotho aliyeelezewa masaibu ya Wajackoyah na kumsaidia kulipa karo yake ya shule ya upili.
Baadaye alisomea sheria katika vyuo vikuu mbali mbali duniani, akisemekana kuwa na zaidi ya shahada kumi za uanasheria.
Profesa Wajackoyah ni Mwanasheria mwandamizi aliyefunza katika vyuo vikuu mbali mbali ndani na nje ya nchi,akijulikana pia katika tajriba yake kubwa katika sheria za wakimbizi na uhamiaji, akiwakilisha na kuwatetea baadhi ya wanasiasa wa upinzani katika kanda ya Afrika Mashariki waliolazimika kukimbia uhamishoni.
Profesa Wajackoyah ni muasisi wa Chama cha Roots kinachokusudia kuhalalalisha bangi na inadi pakubwa uzalishaji na matumizi ya mmea
Ameahidi iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Kenya, atajenga fursa za kazi hasa kwa vijana kwa kuruhusu uuzaji wa bangi ndani na nje ya nchi, akisisitiza kuwa zao hilo pia litasaidia kupunguza mzigo wa madeni ya Kenya kwani utazalisha mapato makubwa. Bangi imeharamishwa nchini Kenya kuambatana na sheria za sasa.
Aidha ameahidi akiwa Rais, Kenya itakuwa na Mawaziri wakuu wanane kuendesha Serikali yake, atasimamisha Katiba kwa miezi sita na siku rasmi za kufanya kazi zitakuwa Jumatatu hadi Alhamisi badala ya Jumatatu hadi Ijumma.
David Mwaure Waihiga
Chanzo cha picha, Twitter/Waihega Mwaure
Mgombea mwingine katika uchaguzi wa Agosti 2022 ni David Mwaure Waihiga, kiongozi wa Chama cha Agano kilichoanzishwa miaka kumi na sita iliyopita. Ni mwanasheria mwandamizi mwenye tajriba ya kuwa wakili kwa miaka thelathini na tano na pia ni Mhubiri.
Hajaonekana sana hadharani akinadi sera zake lakini katika ruwaza yake amejikita zaidi katika ahadi kuwa akichaguliwa kuwa Mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta anayeondoka madarakani baada ya kukamilisha mihula miwili madarakani, atakabiliana vilivyo na ufisadi.
Kiongozi huyo anasema ufisadi ndiyo jinamizi kubwa linaloizonga Kenya na limetokana na kuwachagua viongozi wafisadi, wasio waadilifu wanaotuhumiwa katika kashfa mbali mbali za uporaji na ubadhirifu wa mali za umma.
Katika manifesto yake ameapa kuleta uongozi mpya Kenya utakaojikita katika misingi ya Usawa,uwazi,uadilifu, Umoja na haki. Bwana Waihiga anasema angependa kukumbukwa kama kiongozi aliyetokomeza ukabila,urasimu, usimamizi mbaya na kurejesha mali iliyofichwa na mafisadi nje ya nchi.
Bwana Waihiga awali mwaka 2011 alijaribu kuwania kiti cha eneo bunge la Kamukunji bila ya mafanikio. Mwaka 2013,aliwania ugavana wa Kaunti ya Lamu na Mnamo mwaka 2021, aliidhinishwa na Chama chake kuwania Ugavana wa Kaunti ya Nairobi kufuatia Gavana Mike Mbuvi kuondolewa madarakani kwa kura ya kutokuwa na imani naye lakini hakukuwa na uchaguzi ulioendeshwa kujaza nafasi hiyo baada ya mahakama kutoa uamuzi naibu gavana Ann Kananu kushikilia ugavana wa Nairobi.
Bwana David Mwaure Mwaiga ana imani ana sifa zote za kustahili kuwa kiongozi ajaye wa Kenya.
Lililosalia ni kujua mbivu na mbichi ifikapo Agosti 9,2022, miezi miwili kutoka sasa. Wapiga kura waamuzi wa nani kati ya wagombea wanne wa urais watampa ridhaa ya kuwaongoza katika kipindi cha miaka mitano ijayo.