Uchaguzi Kenya 2022: Je Kenya iko tayari kwa uchaguzi mkuu?

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Caro Robi
- Nafasi, BBC Swahili
Uchaguzi mkuu wa Kenya unaotarajiwa mwezi Agosti 2022, utakuwa ukurasa wa kupisha uongozi mpya utakaochukua usukani kutoka kwa utawala wa Rais Uhuru Kenyatta ambaye ameiongoza Kenya tangu mwaka 2013 kwa kipindi cha mihula miwili madarakani kupitia chama cha Jubilee.
Viongozi kadhaa wameonesha nia ya kutaka kuwania urais akiwemo naibu wa rais William Ruto ambaye anatarajiwa kuwania wadhifa huo sio kupitia chama kilichomuingiza madarakani cha Jubilee bali chama kipya cha United Democratic Alliance UDA kinachonadi sera zake kama chama kinachojali maslahi ya Wakenya wa tabaka la chini,wanaohangaika kila siku kusaka tonge ili angalau wapeleke mkono kinywani.
'Wahusika wakuu'
Bwana Ruto aneyejiita 'Hustler' ni naibu rais wa Kenya tangu mwaka 2013 mpaka sasa katika serikali ya Rais Uhuru Kenyatta chini ya chama tawala cha Jubilee.
Uhusiano kati yake na Rais umedorora na umezidi kuwa mbaya kila uchao, chanzo cha mkwaruzano huo hakijulikani wazi lakini inakumbukwa maji yalianza kuzidi unga punde baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuafikia makubaliano ya kuleta maridhiano ya kitaifa na kiongozi wa upinzani Raila Odinga lengo likiwa kutuliza uhasama wa kisiasa nchini.

Chanzo cha picha, AFP
Mwingine anayetafuta kuliongoza taifa la Kenya ni kiongozi huyo wa muda mrefu wa upinzani Raila Odinga wa chama cha Orange Democratioc Movement ODM ambaye hivi karibuni amezindua rasmi azma yake ya kuwania urais kwa mara ya tano.
Katika miaka ya hivi karibuni, Bwana Raila Odinga almaarufu 'Baba' kama anavyoitwa na wafuasi wake, amekuwa na uhusiano wa karibu kisiasa na Rais Uhuru Kenyatta ambaye zaidi ya mara moja amedokeza hadharani ni upande gani kisiasa anaegemea kati ya Raila Odinga na naibu wake William Ruto bila ya kutaja jina la yeyote.
Mshirika wa Bwana Odinga kisiasa katika uchaguzi uliopita Musalia Mudavadi wa chama cha Amani National Congress ANC pia ashadokeza mapema nia ya kuwa rais wa tano wa Kenya katika uchaguzi huo wa Agosti 2022.

Chanzo cha picha, Getty Images
Si hao tu kuna gavana wa Makueni Profesa Kivutha Kibwana, Makamu wa rais wa zamani Kalonzo Musyoka, mwimbaji wa miziki ya injili Reuben Kigame miongoni mwa wengine wengi.
Hiyo ni katika ngazi ya urais, lakini uchaguzi huo utakuwa pia wa kuchagua viongozi wa nyadhifa nyingine ambazo ni Ugavana wa kaunti zote 47, maseneta, wabunge,wawakilishi wa wanawake na wawakilishi wa wodi.
Lakini huku macho yakielekezwa kwa uchaguzi huo, maswali ni mengi hasa kuhusiana na maandalizi na mazingira ya kuandaliwa kwake.
Sauti za washikadau
Je washikadau mbali mbali wako tayari kuhakikisha uchaguzi mkuu wa Kenya utakuwa sio tu wa huru na haki bali wa amani, jumuishi na wa wazi?
Kuna muda wa kutosha kuhakikisha mfumo mzima unaendeshwa kwa njia inayostahili? Hasa ikizingatiwa kuwa taifa hilio la Afrika Mashariki limeshuhudia machafuko na ghasia katika baadhi ya chaguzi zilizopita?
Mchambuzi wa siasa za Kenya Dr Alutalala Mukhwana anasema imekuwa desturi sio tu kwa Kenya bali mataifa mengi ya Afrika kufanya uchaguzi kama ambao wameshitukizwa. Naye mtaalam wa masuala ya utawala bora Stella Agara anahisi bado tume ya uchaguzi IEBC bado haijajiandaa ipasavyo lakini ana matumaini bado wana muda wa kutosha kugeuza hali kabla ya uchaguzi huo .
Tangu kuanzishwa kwa siasa za vyama vingi nchini Kenya mnamo mwaka 1992, vyama chungu nzima vimejitokeza kushiriki katika uchaguzi unaofanyika kila baada ya miaka mitano kwa ngazi zote toka urais hadi udiwani.
Vingi ya vyama hivi vinaegemea katika misingi ya kikabila au kikanda na ni vichache mno ambavyo vimedumu zaidi ya miaka kumi bila ya kumezwa na vyama vikubwa au hata kupooza kwa kutoshiriki katika siasa za siku baada ya siku.
Ili siasa ziwe siasa sharti kuwe na asasi nyingine zinazoshiriki au kushirikishwa kwa mchakato mzima kuanzia usajili wa vyama, uangalizi wa kampeini na uchaguzi, kuripotiwa kwa matukio yenyewe na wanaotwishwa jukumu la kusimamia,kuhesabu na kutangaza matokeo.
Lakini je uchaguzi Kenya unatizamwa kwa jicho lipi kama mfumo endelevu au tukio la kukumbukwa tu baada ya miaka mitano.
Matayarisho yamekamilika au muda umepita?
Kuna muda wa kutosha kuhakikisha mchakato mzima unazingatia uwazi,uwajibikaji ujumuisha na uadilifu kuanzia uchaguzi mmoja unapokwisha hadi mwingine? Na je nini mchango wa asasi za kiraia katika kuboresha demokrasia?
Mule Musau mratibu wa kitaifa Wa muungano wa waangalizi wa uchaguzi kutoka asasi za kiraia ELOG anasisitiza kuwa kuna haja kubwa ya kuweka mambo sawa ikiwemo kuainisha mchango wa asasi za kiraia katika utoaji wa hamasisho kwa umma, kupitishwa kwa sheria kwa wakati ufaao kuhusu ufadhili wa kampeini na hata kuheshimiwa kwa kipindi rasmi cha kuanza na kumalizika kwa kampeini

Chanzo cha picha, AFP
Mbali na mchango wa asasi za kiraia katika kuhakikisha uchaguzi unaendeshwa ipasavyo mchangiaji mwingine mkuu katika uchaguzi wowote ule ni vyombo vya habari.
Ripoti, taarifa,na chambuzi katika mchakato mzima husaidia wapiga kura kuelewa, kufuatilia, na hata kufanya maamuzi kutokana na wanachokisikia,kukisoma au kukiona katika vyombo hivyo. Kwa hivyo swali bila shaka vyombo hivyo vinautizama vipi mchakato wa kisias Kenya.
Mkurugenzi mkuu mtendaji wa baraza la vyombo vya habari David Omwoyo ana imani na jinsi vingi ya vyombo vya habari vilivyojiandaa kuuangazia uchaguzi huo na kusema wameshatoa muongozo wa jinsi wanahabari wanapaswa kujiendesha katika kipindi hiki huku wakiwa na mipango ya kuwapa mafunzo hasa waandishi habari chipukizi ambao wengi wao hawakushiriki katika uchaguzi uliopita wa 2017.
Bwana Omwoyo anasema mojawapo ya changamoto wanazokumbana nazo hivi sasa ni kuwafuatilia waandishi wa habari amabo wametangaza azma ya kuwania nyadhifa mbali mbali katika uchaguzi wa 2022 wakati mpaka sasa hawajajiuzulu.
Makundi muhimu ya wapiga kura
Ikiwa imesalia miezi minane kuelekea uchaguzi wa Kenya, jambo moja ambalo bado halitafutiwa ufumbuzi mpaka sasa licha ya kuwepo juhudi nyingi iwe za kisheria, kibunge na hata muhimili wa rais katika kulishughulikia ni utekelezaji wa usawa wa kijinsia ambapo kuambatana na katiba ya Kenya iliyopitishwa mwaka 2010, uwakilishi wa kijinsia unapaswa kuwa thuluthi moja.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kuna muongozo bayana wa kuhakikisha kuwa bunge lijalo litafikia hilo, lakini pia je wanawake wenyewe wamejitokeza kimasomaso kuonesha azma ya kuwania nyadhifa za juu kisiasa na iwapo sivyo kwanini? Bi Charity Ngilu mwanasiasa mkongwe aliyewahi kuwania uraia hivi sasa ni gavana wa kaunti ya Kitui anaelezea nafasi ya mwanamke katika siasa za Kenya kwa kusema kizingiti kikubwa kinachowakabili wanawake ni kukosa nguvu ya kifedha kufanya kampeini kote nchini. Lakini anasema kuanzia mwaka 1992, wamepiga hatua kubwa ya kuwa na uwakilishi katika bunge na kwingineko.
Mojawapo pia ya makundi muhimu yatayaoamua mustakabali wa uchaguzi ujao ni nafasi ya vijana katika siasa za Kenya. Tume ya uchaguzi IEBC ilinuia kusajili zaidi ya wapiga kura wapya milioni sita ambao watashiriki kwa mara ya kwanza uchaguzi.
Kundi hili ni vijana wa kati ya umri wa miaka 18 hadi 35. Wanasiasa bila shaka wanategemea kupata uungwaji mkono kutoka kwa vijana hawa ili kujihakikishia idadi ya kutosha ya kura kuwapa ushindi.
Licha ya hilo kuna wasiwasi kuwa wengi wao hawana msukumo wa kushiriki katika uchaguzi kwa kuzingatia, zoezi la hivi karibuni na kuwasajili wapiga kura wapya, ni milioni moja na laki tano tu waliojitokeza kati ya zaidi ya milioni sita waliotarajiwa. Na hili bila shaka linazua wasiwasi.
Vijana wengi wanasema wanahisi kwa miaka mingi kuelekea uchaguzi masuala yao hasa kubwa ukosefu wa ajira limepuuzwa na wanasiasa na wanahisi wanatumika tu kuendeleza ajenda binafsi za viongozi.
Bila shaka kuna masuala mengi na wachangiaji chungu nzima katika kuhakikisha uchaguzi wa 2022 una utofauti ikilinganishwa na uliopita kwa misingi ya kudumisha amani, ujumuishi, uadilifu,uwazi, haki na uhuru.
Huku macho yote yakielekezwa kwa miezi michache ijayo, jinsi Kenya itakavyojiendesha, matumaini ya wengi ni kuwa ukomavu wa demokrasia na kuheshimu utawala wa sheria vitatamalaki katika siasa za taifa hilo la Afrika Mashariki linalotizamwa kama kielelezo katika nyanja nyingi.
Je Kenya iko tayari kwa uchaguzi wa 2022? Hilo ni swali lisilohitaji mate bali wino kulijibu.













